Wengi wetu tumekulia kwenye familia ambazo pesa haikuwa mada ya watoto. Tulipokuwa wadogo, tulikuwa tukisikia wazazi wakiongelea hali ngumu ya maisha, madeni, au michango ya ghafla, lakini si kwa njia ya kutufundisha, bali kwa sauti ya hofu, hasira au huzuni.
Tulipojaribu kuuliza, tuliambiwa, “Haya ni mambo ya wakubwa.” Tukaendelea kukua bila kuelewa pesa ni nini, inapatikanaje, inatunzwaje, wala namna ya kuishi nayo kwa mipango thabiti.
Sasa, sisi ndio tunalea kizazi cha sasa. Tuna nafasi ya kubadili historia hiyo, tuanze kuwajengea watoto wetu misingi bora ya kifedha, siyo kwa kuwapa mamilioni, bali kwa kuwapa maarifa, msimamo na maadili yatakayowasaidia dhana ya pesa hata kipindi hiki ambapo kama watoto, hawana chochote mkononi.
Tunaweza kabisa kuwalea watoto wanaojua kupanga pesa zao, kujizuia na tamaa, kusaidia wengine kwa moyo, na kutofautisha mahitaji na matamanio, lakini, kubwa zaidi, kuelewa mchakato wanaoupitia wazazi kuzitafuta, kizisimamia, kuzitunza na kuzitumia pesa.
Tunaweza kuwafundisha kuwa pesa ni rasilimali siyo mzigo, wala si mungu wa kuabudiwa, na wala hazipatikani kwa miujiza bali kwa maarifa na kujituma.
Tubadilike
Hatua ya kwanza ni sisi kubadilika. Tunahitaji kubadili namna tunavyoizungumzia pesa nyumbani kwetu. Watoto wanasikia! Wakiona pesa ni chanzo cha ugomvi kila mara, watadhani ndivyo ilivyo.
SOMA ZAIDI: Tunawaleaje Wavulana Wetu Kuwa Wanaume Bora wa Baadaye?
Wakiona kila mara tunasema “hatuna,” “tumeishiwa,” au tunagombania matumizi, nao watakuwa na hofu na huzuni kila pesa ikitajwa. Badala ya kusema “Hatuna hela,” tunaweza kusema, “Tunaweka akiba kwa ajili ya jambo la muhimu,” au, “Tumeamua kutonunua kitu hiki wiki hii kwa sababu tuna malengo ya baadaye.” Hii inawapa watoto nafasi ya kuelewa kuwa pesa ni jambo la kupangwa, si la kufichwa.
Kuna fursa nyingi za kuwafundisha watoto kuhusu pesa katika maisha ya kila siku. Huhitaji kuwa na elimu ya kifedha, au programu maalum. Unapokuwa sokoni, tunaweza kumuomba mtoto akusaidie kulinganisha bei au kuhesabu chenji.
Anapopokea pesa ya zawadi, sherehe au sadaka, tumsaidie kuigawanya, pesa ya kutumia sasa, ya kuweka akiba, na hata ya kusaidia mtu mwingine. Hili linaweza kufanyika hata kama ni shilingi mia mbili tu. Tunapowashirikisha kwenye maamuzi madogo ya kifedha, tunawajengea msingi wa maamuzi makubwa ya fedha baadaye.
Tusilazimishe
Pia, tunahitaji kutambua kuwa elimu ya kifedha haipaswi kuwa ya kulazimisha, au ya kitaalamu sana. Tunaweza kuanzia na watoto wadogo kwa kuwasaidia kutambua sarafu na noti, kucheza michezo ya “duka-duka,” na kuwaeleza tofauti ya kitu tunachohitaji na kile tunachotamani.
Watoto wakikua, tunaweza kuwaingiza katika mazungumzo ya kuweka akiba kidogo, kupanga matumizi ya hela ndogo wanazopata, na kuwasaidia kuelewa kuwa pesa huisha, hivyo inahitaji kutumia kwa akili.
SOMA ZAIDI: Ni Muhimu Wazazi na Walezi Tuanze Kujadili Baleghe na Watoto Wetu Bila Hofu
Tunapofika katika umri wa balehe, tunaweza kuwatia moyo kufikiria malengo ya kifedha, kuwapa majukumu madogo ya kupanga matumizi yao ya kujikimu, au kuwasaidia kuanzisha mradi mdogo wa biashara. Hii siyo tu inafundisha uwajibikaji bali inawajengea hali ya kujiamini.
Vijana wetu wa kizazi hiki pia wanahitaji kufundishwa kuhusu usalama wa kifedha wa kidigitali, PIN, OTP, na utapeli wa mitandaoni. Lazima tuwafundishe kuwa siyo kila “fursa” inayotangazwa Instagram, au kwenye mitandao ya kijamii, ni ya kweli.
Hali ya kifedha ya familia nyingi Afrika si sawa na ya mataifa ya huko nje. Tunaishi katika jamii zenye mshikamano, ambapo kuchangia harusi, msiba au ada ya ndugu ni kawaida. Hili ni jambo la maana, lakini pia linaweza kuleta mzigo kama halina mipaka.
Tunapaswa kuwaeleza watoto wetu kwa uwazi: kwamba kusaidia ni jambo la muhimu, lakini kujipangia mipaka ni muhimu pia. Tunaweza kusema, “Tulimchangia mjomba kwa sababu tulikuwa na pesa hiyo wakati huo,” au “Kwa sasa hatuwezi kuchangia zaidi kwa sababu fulani inayoeleweka.”
Tuwe kielelezo
Zaidi ya hayo, tunapaswa kuwa kielelezo kwa yale tunayofundisha. Watoto hawaangalii tu wanachosikia, wanaangalia zaidi tunachofanya. Wakituona tukitenga akiba, wakituona tukisema “hapana” kwa matumizi yasiyo ya lazima, wakituona tukitoa kwa moyo bila majivuno, watajifunza hayo kwa haraka zaidi kuliko mawaidha.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Huugua Wote Kwa Wakati Mmoja?
Na wakituona tukifanya makosa ya kifedha na tukakiri, pia watatambua kuwa kukosea ni sehemu ya kujifunza.
Ni muhimu pia tuondoe wazo la kuwa pesa ndio kipimo cha mafanikio, au thamani ya mtu. Watoto wetu wanapaswa kufahamu kuwa mtu mwenye pesa si bora kuliko asiye na pesa. Mafanikio yana maana zaidi ya vitu tunavyomiliki. Tunapaswa kuwafundisha kujitahidi, kuwa na ndoto, lakini pia kujua kuwa thamani yao haitegemei pesa waliokuwa nayo.
Mwisho, tunapaswa kufanya mazungumzo ya pesa kuwa ya kawaida. Yasihusishwe tu na shida au ukali. Tuwe na muda wa kukaa na watoto, kuzungumzia ndoto zao, malengo yao, na hata changamoto wanazopitia kuhusu pesa. Tukubali kuulizwa maswali. Tuwaruhusu kufanya maamuzi, wakosee, wajifunze.
Hatuhitaji kuwa matajiri ili kuwalea watoto wenye maarifa ya kifedha. Hatuhitaji kila kitu kiwe sawa. Tunachohitaji ni kuwa tayari kuzungumza, kufundisha na kujifunza pamoja nao.
Watoto wetu wana uwezo wa kuwa kizazi kinachopangilia maisha yao kwa utulivu, kinachojua kutoa, kuwekeza, na kutumia kwa akili. Kizazi kinachoiheshimu pesa bila kuiabudu.
Na yote haya, yanazaliwa nyumbani. Na nyumbani tupo sisi.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.