The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

CCM na Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030: Ushindi Si Swali la ‘Je, Itashinda?’ Bali ‘Itashinda kwa Kiasi Gani?’

CCM inaingia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 ikiwa na silaha tatu kuu: rekodi ya utekelezaji wa Ilani ya 2020–2025, dira ya maendeleo kupitia Ilani ya 2025–2030, na msingi mpana wa wanachama kote nchini.

subscribe to our newsletter!

Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), kinaonekana kukusudia kuingia kwenye kampeni kikiwa kimejizatiti kwa nguvu mpya, mtaji wa wanachama wa kutosha, na rekodi imara ya mafanikio yaliyotokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020–2025. Kikiwa tayari kimetoa mwelekeo mpya kupitia rasimu ya Ilani ya 2025–2030, chama hicho kinaonesha dalili zote za kutaka kushinda tena kwa kishindo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika jijini Dodoma mwezi Januari 2025, chama hicho kimeeleza kwa kina mafanikio ya kisekta yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa mhimili wa utekelezaji huo, na mafanikio hayo sasa yamegeuka kuwa silaha kuu za kisiasa kuelekea uchaguzi ujao.

Miongoni mwa mafanikio haya ni yale yanayoonekana katika sekta ya miundombinu, huku mradi mkubwa wa Reli ya Kisasa (SGR) ukisifiwa kwa kuleta mapinduzi ya kweli katika usafiri wa abiria na mizigo. Safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma zimezinduliwa rasmi, na katika kipindi kifupi cha miezi minne, zaidi ya abiria 1.2 milioni wameshasafirishwa. Hii si tu imerahisisha maisha ya wananchi, bali pia imeongeza mapato ya ndani, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 30 zimeripotiwa kupatikana.

Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ni lango kuu la biashara Afrika Mashariki, imeboreshwa kwa kiwango kikubwa. Gharama za matumizi zimepunguzwa kwa asilimia 47, hali iliyovutia wawekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania. Mapato ya bandari hiyo sasa yamefikia Shilingi bilioni 62.4 kwa mwaka, yakionyesha ongezeko la ufanisi na usimamizi thabiti.

Katika sekta ya maji, zaidi ya miradi 1,600 imetekelezwa kote nchini. Takwimu zinaonesha kuwa upatikanaji wa maji safi na salama vijijini umeongezeka kutoka asilimia 70 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 79.6 mwishoni mwa mwaka 2024. Hili ni ongezeko kubwa linaloashiria dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuondoa kero ya maji vijijini, hasa kwa wanawake na watoto ambao kwa muda mrefu wamekuwa waathirika wakuu wa changamoto hiyo.

SOMA ZAIDI: Nukuu Muhimu Kutoka Kwenye Mahojiano Maalum Kati ya The Chanzo na Ally Salum Hapi, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, CCM 

Sekta ya elimu nayo imepata msukumo mkubwa. Bajeti ya elimu bila ada imeongezeka mara dufu, jambo ambalo limewawezesha zaidi ya wanafunzi milioni 16 kunufaika na fursa ya kusoma bila mzigo wa ada. Madarasa zaidi ya 15,000 yamejengwa kote nchini, na serikali imeanzisha shule maalum za wasichana katika kila mkoa—hatua ya kihistoria ya kuimarisha elimu ya mtoto wa kike.

Katika sekta ya afya, Serikali imefanikiwa kujenga vituo 183 vya kutolea huduma za afya katika maeneo mbalimbali ya nchi. Aidha, idadi ya vitanda vya hospitali imeongezeka hadi kufikia 126,209, kiwango ambacho kipo karibu na viwango vinavyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Hii imesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyoweza kuzuilika na pia kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Kilimo, ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa Watanzania wengi, kimepata msukumo mpya. Bajeti ya sekta hii imeongezeka hadi Shilingi bilioni 954, huku ruzuku ya mbolea ikitolewa kwa thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 150. Hatua hii imeongeza uzalishaji wa chakula na kuinua kipato cha wakulima, ambao sasa wanaona matunda ya sera bora za kilimo.

Katika utalii, mafanikio ni ya kupigiwa mfano. Idadi ya watalii imeongezeka kutoka 620,867 mwaka 2020 hadi zaidi ya milioni 1.9 kufikia mwishoni mwa mwaka 2024. Mapato kutokana na utalii yamefikia dola za Marekani bilioni 3.3, yakiongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa na kuimarisha ajira kwa vijana na wanawake.

Kwa upande wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), chini ya uongozi wa Rais Hussein Ali Mwinyi, imepiga hatua kubwa. Uchumi wa visiwa hivyo umeendelea kuimarika, kutoka ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2024.

SOMA ZAIDI: CCM Yafanya Mabadiliko Mengine ya Katiba Mei 29, 2025: Vikao vya Kidigitali, Yaongeza Idadi ya Wajumbe Baraza la Wadhamini na Sharti la Ruhusa ya Miradi

Mapato ya Serikali ya Zanzibar yameongezeka na kufikia Shilingi trilioni 6.3. Hii imetokana na usimamizi mzuri wa mapato na kupanuka kwa wigo wa kodi pamoja na uwekezaji wa ndani na wa nje. Ujenzi wa shule mpya 116 umefanyika, na miradi 424 ya uwekezaji imesababisha upatikanaji wa ajira rasmi zaidi ya 22,000 kwa vijana wa Kizanzibari.

Utalii unaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Zanzibar. Mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa la visiwa umefikia asilimia 30. Visiwa 21 vimetangazwa kwa uwekezaji wa kimkakati, na tayari 15 kati yake vina wawekezaji waliothibitishwa.

Miaka mitano ijayo

Katika kuangalia mbele, CCM, kupitia rasimu ya Ilani ya 2025–2030, imejipanga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuongeza nguvu katika maeneo mapya. 

Dira ya chama ni pamoja na kuendeleza uchumi wa viwanda, TEHAMA na biashara ndogo ndogo kwa kuimarisha mazingira ya biashara; kupanua upatikanaji wa maji safi, huduma za afya, elimu bora na nishati vijijini; kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kupanda miti milioni 100 kila mwaka ili kulinda mazingira na kuongeza mvua; pamoja na kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kwa kuongeza ushirikiano wa kimataifa, usalama wa taifa, na uhifadhi wa rasilimali za taifa kama gesi, madini na misitu.

Pia, kwa mara ya kwanza katika historia ya Ilani zake za Uchaguzi, CCM imeweka bayana dhamira yake ya kuongoza mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo (2025–2030). Hii ni hatua ya kihistoria inayojibu kilio cha muda mrefu cha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na Katiba inayozingatia mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kwa zaidi ya muongo mmoja, Watanzania kutoka kada mbalimbali wamekuwa wakitoa wito wa kuwa na Katiba Mpya itakayoweka misingi bora ya utawala wa sheria, mgawanyo wa madaraka, uhuru wa vyombo vya habari, na usawa wa kijinsia. Maandamano, mijadala ya kisiasa, na midahalo ya kitaaluma yamekuwa sehemu ya harakati hizo, zikilenga kuhakikisha kuwa taifa linaongozwa na Katiba inayotokana na matakwa ya wananchi.

SOMA ZAIDI: Historia Mpya Iliandikwa Kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM 2025. Lakini Inaweza Kuwa na Maana Gani kwa Tanzania? 

Katika mwaka 2014, Rasimu ya Katiba Mpya iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba iliibua mijadala mikubwa na matumaini kwa wananchi. Rasimu hiyo ilijikita katika masuala ya msingi kama vile usawa wa Muungano, haki za binadamu, uwajibikaji wa viongozi, na uhuru wa vyombo vya dola. Hata hivyo, mchakato huo haukukamilika kutokana na sababu mbalimbali za kisiasa na kiutendaji.

Kwa sasa, CCM imeonyesha utayari wa kweli wa kurudi kwenye ajenda hiyo. Kupitia Ilani ya 2025–2030, chama kimeweka wazi kuwa kitaongoza mchakato wa kupata Katiba Mpya kwa kushirikisha wananchi, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia na taasisi nyingine za kiraia. Hii inaashiria mwelekeo mpya wa kisiasa unaotambua kuwa maendeleo ya kiuchumi hayawezi kutenganishwa na misingi imara ya kikatiba.

Kwa kuweka dhamira hiyo ndani ya Ilani yake rasmi, CCM sio tu inajibu sauti ya wananchi, bali pia inaonesha kukomaa kwa demokrasia ya Tanzania. Endapo itatekelezwa kama ilivyopangwa, Katiba Mpya itakuwa msingi wa haki, usawa na maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo.

Namba hazidanganyi

Katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2024, Watanzania wapatao 31,282,331 walijiandikisha kupiga kura. Taarifa za hivi karibuni zinaonesha kuwa hadi kufikia Mei 2025, CCM ina jumla ya wanachama 13,000,670 waliothibitishwa kupitia mfumo wa usajili wa kidigitali. 

Hata hivyo, viongozi wa chama wanasema kuwa idadi kamili ya wanachama wa CCM ni kubwa zaidi ya hiyo, ikihusisha wale ambao bado hawajasajiliwa kidigitali au wale walio vijijini ambako mchakato wa usajili bado unaendelea.

SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi, Kuhusu Kutekwa Kwangu Nikiwa Ndani ya Gari la Mwenyekiti wa UVCCM, Bariadi 

Kwa mantiki hiyo, takwimu hizi zinaonesha kuwa takribani asilimia 42 ya wapiga kura wote waliosajiliwa mwaka 2024 tayari ni wanachama wa CCM walio kwenye mfumo rasmi wa usajili. Kwa mantiki ya kisiasa, hii ni hazina kubwa ya kura za awali kwa chama hicho tawala.

Ikiwa hata asilimia 80 tu ya wanachama wa sasa waliopo kwenye mfumo wa kidigitali watashiriki kupiga kura, CCM ina uhakika wa kuanza kampeni ikiwa na zaidi ya kura milioni 10 mikononi. Hii ni kabla hata ya kufikia wapiga kura wapya, makundi huru, na wafuasi wa vyama vingine.

Tahadhari

Pamoja na takwimu hizi kuipa CCM matumaini makubwa, na lazimika kutoa angalizo kwamba ushindi hauwezi kuchukuliwa kama jambo la moja kwa moja. Kuna changamoto kadhaa ambazo chama lazima kizikabili kwa makini.

Changamoto hizi ni pamoja na kuhamasisha wanachama wote wa CCM kushiriki kikamilifu katika kupiga kura ni kazi kubwa. Pia, CCM haina budi bali kukabiliana na hoja za vyama vya upinzani kuhusu masuala ya uchumi, ajira, uhuru wa vyombo vya habari, na haki za kiraia.

Chama hicho tawala nchini pia hakina budi kuimarisha mahusiano na vijana na makundi ya kisasa ambayo mara nyingi huathiriwa na mitazamo ya kisasa ya siasa na wanamashaka kuhusu siasa za jadi, huku ikiweka wazi mpango wa chama wa kushughulikia changamoto za kila siku za mwananchi wa kawaida, hasa katika maeneo ya bei ya bidhaa, ajira na huduma za kijamii.

SOMA ZAIDI: Makamu Mwenyekiti wa CCM,Abdulrahman Kinana Ajiuzulu

Kwa ujumla, CCM inaingia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 ikiwa na silaha tatu kuu: rekodi ya utekelezaji wa Ilani ya 2020–2025, dira ya maendeleo kupitia Ilani ya 2025–2030, na msingi mpana wa wanachama kote nchini. Haya yote yanaiweka CCM katika nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi mkubwa kama itatumia ipasavyo fursa hii.

Hata hivyo, ushindi huo hautatokana na nguvu ya historia pekee. Unahitaji kuimarisha nidhamu ya kisiasa, mbinu za kisasa za kampeni, na uwezo wa kuwasiliana na wananchi kwa lugha wanayoielewa—lugha ya matokeo na mabadiliko yanayoonekana.

Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au X kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×