The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Yaendelea Kujidhatiti Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali 2025/26

Pamoja na bajeti hii kuainisha mipango yenye tija bado ya uhaba wa walimu, kiwango kidogo cha fedha za bajeti kinachotolewa na urejeshaji hafifu wa mikopo vitaendelea kukwamisha upatikanaji wa elimu bora.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Mei 26, 2025, Baraza la Wakilishi liliipitisha bajeti ya Shilingi bilioni 864, fedha ambazo zinatarajiwa kwenda kwenye Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele mbalimbali ikiwa ni sawa na takribani asilimia 17 ya bajeti kuu ambayo Serikali imepanga kutumia.

Baadhi ya vipaumbele vya bajeti hii kwa mwaka 2025/26 ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya elimu, kuimarisha mafunzo ya ualimu na walimu waliopo kazini, kuongeza uwezo wa vyuo vya elimu ya juu, kukuza mafunzo ya amali na elimu mbadala pamoja na kuboresha mafunzo ya TEHAMA.

Vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa ubora wa elimu, kupanua wigo wa utoaji mikopo na ufadhili wa elimu ya juu, pamoja na kuhakikisha utoaji wa elimu bora kwa ujumla.

Katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2023/2024 hadi 2025/2026, bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeendelea kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 457.3 hadi Shilingi bilioni 864.0, sawa na ongezeko la Shilingi bilioni 406.7 ambayo ni sawa na asilimia 88.9.

Kwa mwaka 2023/2024, wizara hiyo ilipatiwa kiasi cha Shilingi bilioni 457.3. Mwaka 2024/2025 bajeti hiyo iliongezeka hadi Shilingi bilioni 830.9, hii ikiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 373.6, sawa na asilimia 81.7.

Mwaka wa fedha 2025/2026, bajeti imeongezeka tena hadi Shilingi bilioni 864.0, sawa na ongezeko la Shilingi bilioni 33.1, ambayo ni sawa na asilimia 3.96.

SOMA ZAIDI: Je, Bajeti ya Wizara ya Kilimo 2025/26 Inaakisi Matarajio ya Wakulima?

Kitendo cha bajeti ya wizara hii kuendelea kuongezeka kadri miaka inavyozidi kwenda inaonesha dhahiri dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha kwamba Wazanzibari wanapata elimu bora na katika mazingira bora.

Jambo ambalo linatutia wasiwasi ni jinsi ambavyo Serikali imekuwa ikipeleka pesa kidogo sana kwenye wizara hii kwa ajili ya kutekeleza mipango yake, tofauti na bajeti yenye kiwango kikubwa cha pesa.

Kwa mfano, hadi kufikia Aprili 2025, miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha wa 2024/2025 kukamilika, jumla ya Shilingi 409,729,646,068 sawa na asilimia 49 ya makadirio ya bajeti zilipatikana. Kati ya fedha hizo, Shilingi 175,967,128,973 sawa na asilimia 82 zimetumika kulipia mishahara ya wafanyakazi.

Kwa upande wa fedha za maendeleo, jumla ya Shilingi 167,272,787,830 sawa na asilimia 32 zilipatikana. Kati ya fedha hizo Shilingi 115,920,114,523 sawa na asilimia 38 ni kutoka Serikali ya Mapinduzi na Shilingi 51,352,673,307 sawa na asilimia 25 ni kutoka kwa wahisani.

Kitendo cha fedha zilizoainishwa kwenye bajeti kutopatikana kwa asilimia 100 kinatia mipango ya kibajeti ya wizara hii kukamilika na kukwamisha adhma ya kufikia kiwango cha juu ya utoaji na upatikanaji wa elimu bora visiwani hapa.

Mipango

Kwa mwaka 2025/2026 wizara imepanga kujenga na kukarabati shule zaidi ya 100 za maandalizi, msingi na sekondari, pamoja na vyuo vya elimu ya juu.

Aidha, ujenzi wa madarasa mapya na miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum umepewa kipaumbele. Ili kutekeleza mpango huu wizara imepanga kutumia Shilingi bilioni 308.79 kutoka Serikali ya Mapinduzi na Shilingi bilioni 209.27 kutoka kwa wahisani.

SOMA ZAIDI: Elimu ya Zanzibar Inavyowaacha Nyuma Wanafunzi Wenye Ulemavu Kwenye Masuala ya Teknolojia

Wizara pia imepanga kuendelea kuimarisha elimu ya msingi na sekondari. Programu hii inalenga kuongeza idadi ya shule, kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani, kusambaza vifaa vya maabara na TEHAMA, na kutoa ruzuku kwa shule. Serikali pia itaendelea kutoa huduma ya lishe kwa wanafunzi wa maandalizi na msingi.

Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza vyuo vikuu pamoja na kutekeleza tafiti na kuanzisha mitaala mipya ya kisasa. Ujenzi wa shule ya tiba, kilimo na kliniki unatarajiwa kuendelea sambamba na matumizi ya mifumo ya TEHAMA.

Wanafunzi zaidi ya 11,000 wanatarajiwa kunufaika na mikopo ya elimu ya juu. Wizara pia itaendelea kufadhili wanafunzi bora kupitia ufadhili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wahisani kutoka nje ya nchi kama China, Uturuki, na Algeria.

Mpango wa mwisho ambao uchambuzi huu umeuangazia ni programu za mafunzo ya ualimu zimeongezwa kutoka saba hadi nane. Wizara itaendelea na mpango wa kufungua chuo kipya cha Ualimu Dole mwaka 2026, huku wakufunzi zaidi ya 3,000 wakitarajiwa kupatiwa mafunzo kazini.

Hii ni mipango ambayo kwa mwaka huu inatoa mwanga kwamba huenda adhma ya kuiboresha elimu ya Zanzibar ikafanikiwa, lakini ni kama haya yote yatatekelezwa kwa asilimia 100.

Changamoto

Licha ya Serikali kuajiri walimu wapya 889 kwa shule za maandalizi na msingi, bado uwiano wa walimu kwa wanafunzi upo juu, hasa katika maeneo ya vijijini. Vilevile, uhaba wa madarasa, madawati, na vyoo unaendelea kuchochea msongamano wa wanafunzi madarasani, hali inayochangia kushuka kwa ubora wa utoaji wa elimu.

Kwa upande wa elimu ya juu, urejeshaji mdogo wa mikopo kwa wanafunzi waliokwishahitimu unaathiri mzunguko wa fedha kwa wanafunzi wapya. Ripoti ya bajeti inaonyesha kuwa hadi Aprili 2025, kiasi cha shilingi bilioni 3.43 pekee ndicho kilichokusanywa kati ya malengo yaliyowekwa, sawa na asilimia 62.

Hali hii inaweza kuathiri uwezo wa Serikali kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji zaidi ya 11,000 waliopangwa kufaidika.

Aidha, ongezeko kubwa la uandikishaji wa wanafunzi linaongeza shinikizo kwa bajeti ya elimu, huku uwezo wa kifedha wa serikali ukibaki kuwa mdogo. Uhitaji huu mkubwa wa huduma unahitaji rasilimali zaidi kuliko uwezo uliopo, hali inayotishia kudhoofisha ubora wa elimu endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar anapatikana kupitia najjatomar@gmail.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×