Watanzania mitandaoni wameibuka kwa wingi kusambaza ujumbe wa No Reforms, No Election (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi) wa chama cha CHADEMA mitandaoni, hii imefanya kampeni hiyo kuwa jambo pekee linalozungumzwa kwa ujumla katika anga la mitandao ya kijamii Tanzania.
Sehemu kubwa ya watu wanaandika maoni (comment) kwenye kurasa za vyombo vya habari, viongozi, kurasa za serikali, kurasa za taasisi, kurasa za watu maarufu jambo ambalo inafanya kuwa vigumu kuingia katika mtandao wowote wa kijamii Tanzania bila kukutana na jumbe hizo. Hali hii imetoa kazi kubwa kwa waongoza kurasa za viongozi na taasisi mbalimbali za umma kujikita katika kufuta na kuzuia baadhi ya maoni katika kurasa zao.
No Reforms, No Election ni kampeni ya CHADEMA inayohimiza katika kuleta mabadiliko muhimu katika mfumo wa uchaguzi Tanzania. Chama hicho kimekuwa kikitaja matukio ya wanachama wao kuuwawa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, majina ya wagombea wao kuenguliwa, ugumu wanaokutana nao kutangazwa wanaoshinda, na kasoro katika muundo na utendaji wa Tume ya Uchaguzi kama baadhi ya vichocheo vya kuhitaji mabadiliko. Tume ya Uchaguzi ilitangaza kuwa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania kitazuiwa kushiriki katika uchaguzi kwa miaka mitano, kwa kutokusaini fomu za maadili mnamo Aprili 12, 2025, jambo ambalo wanasheria na wachambuzi wameendelea kulikosoa, huku wengine wakienda Mahakamani kutaka ufafanuzi zaidi.
Mrindimo wa No Reforms, No Election mitandaoni umezua mijadala hasa baada ya watumiaji wa mtandao wa Instagram na Tiktok kuanza kusambaza jumbe hizo. Wengi wakihusisha hali hii na chachu aliyotoa mwanaharakati Mange Kimambi, mwenye umaarufu mkubwa katika mtandao wa Instagram. Mitandao hiyo ambayo inafahamika zaidi kwa maudhui ya burudani na watu maarufu, imeendelea kuacha mshangao namna jumbe hizo zilivyoweza kusambaa na kuwa maarufu, huku wengi wanao onekana kutokuwa na kawaida ya kushiriki wazi wazi katika maudhui ya siasa wakishiriki kusambaza jumbe hizo.
“No Reforms, No Election si kauli ya kupinga uchaguzi kwa utashi wa kisiasa bali ni wito wa haki na demokrasia ya kweli. Tunadai marekebisho ya msingi katika mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha kila kura ina thamani, na matokeo yanayoakisi sauti ya wananchi,” alieleza moja ya mwananchi aliyeandika kwenye ukurasa wa msanii maarufu.
Wimbi la No Reforms, No Election lilionekana ia kumfikia msani maarufu kutoka Nigeria Chella Boi, aliyefika Tanzania kwa ajili ya kutumbuiza. “Mimi ni mwanamziki na sijihusishi na siasa, na sijui lolote kuhusu siasa, jumbe zinazoandikwa kwenye ukurasa wangu zinanishtua, no reforms, no election ni nini, Watanzania mnaweza kunielewesha,” alieleza Chellaboi.
Wachambuzi wengi wanaieleza kampeni ya CHADEMA kama kampeni inayotoa uchaguzi wa watu kuamua kutochagua, jambo ambalo linaonekana kuwa jipya Tanzania. Hata hivyo, baadhi ya wadau ikiwemo Jaji Mkuu Msataafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, wameendelea kuonya juu ya changamoto ya uhalali wa kisiasa na mgawanyiko katika jamii ikiwa mamilioni wataachwa nje katika fursa ya kupiga kura.
“Ukiona taasisi hizi zinazosimamia mambo ya siasa hapa wanatazama vyama. Tume inatazama vyama. Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa inatazama vyama lakini hawajui ndani ya vyama hivyo kuna wananchi. Kwa hiyo ukichukua uamuzi unasema unaadhibu chama ni kwamba unaagiza unaadhibu mamilioni wa Watanzania,” alieleza Jaji Joseph Warioba katika mjadala wa Chama cha Mwakili mnamo Mei 03, 2025, akiongelea kuhusu hoja ya CHADEMA kuzuiwa kushiriki uchaguzi mpaka 2030.
“Huko nyuma, sisi tulikataa utaratibu ambao unaweka pembeni watu mpaka hata ukifika Zanzibar, mapinduzi msingi wake ilikuwa ni kwamba watu hawakuwa wamepata haki. Sasa tunakuja tunarudi kule kule, yale yaliyo tuliyowakataa ya 1958 ya 1963 tunarudi kuyafanya haya tukasema inaweza kuleta matatizo,” aliendelea kufafanua zaidi.
Serikali imeendelea kuhamasisha Watanzania kujitokeza kupiga kura, huku Rais Samia akisistiza ni uzalendo kujitokeza kupiga kura na kuchagua.
“Kutokujitokeza kuandikisha ni kukataa mwenyewe haki yako ya kikatiba. Na unapokataa haki ya kikatiba swala unajiuliza je wewe ni mzalendo? Ni mzalendo wa aina gani ambaye katiba imekupa fursa hii? Nenda kaandikishe piga kura weka kiongozi unayehisi atakuja kukuhudumia. wewe unaikataa,” alieleza Rais Samia Mnamo Mei 17, 2025, akiboresha taarifa zake kwenye daftari la wapiga kura.
Na kuongeza: “Ukiikataa wenzio watakwenda kuweka wanayemtaka na unakosa fursa ya kushawishi wengine kuweka yule mnayemtaka. Kwa hiyo unakuwa wewe wa kubabaisha tu na wa kulalamika. Lakini swala kubwa hapa ni uzalendo. Jiulize mwenyewe rohoni kwako uzalendo wangu uko wapi?”
Katika kukabiliana na wimbi kubwa la No Reforms, No Election, wafuasi wa chama tawala, CCM, wameanzisha kampeni ya #OktobaTunatiki, wakiandika jumbe sehemu mbalimbali na kusambaza pia kupitia watu maarufu, hata hivyo bado kampeni hii haijafanikiwa kurindima kama No Reforms, No Election.