Kuna msemo tuliouzoea katika familia zetu, kwamba “Mtoto kwa mzazi hakui, hata akiwa na mji wake na watoto wake.” Tulipousikia mara ya kwanza, tulitabasamu. Lakini kadri miaka inavyosonga, tunauelewa kwa kina. Tumewalea watoto wetu kwa upendo, tumeona wakikua, wakajitegemea, na hata kuanzisha familia zao wenyewe.
Lakini ndani ya mioyo yetu, bado tunawaona kama “watoto” wetu. Safari yetu ya malezi haikuisha walipofikisha miaka 18. Haikukoma walipohitimu masomo au walipoanza kuishi mbali nasi. Iliendelea, ingawa kwa sura na namna tofauti. Tumeendelea kukua pamoja nao, tukijifunza kuwa wazazi wa watu wazima, na kujifunza kupenda kwa njia mpya.
Lakini kuendeleza uhusiano huu si jambo linalotokea tu. Linahitaji juhudi, uvumilivu, na utayari wa kukubali mabadiliko. Tunapaswa kujifunza kusikiliza hata pale tunapohisi tunajua zaidi.
Tunapowapokea watoto wetu kwa mara ya kwanza, tuliwakumbatia kwa mikono yenye shaka, lakini iliyojaa upendo na matumaini. Hatukuwa na majibu yote, lakini tulijua wanatuhitaji kila saa, kila dakika. Tunajifunza lugha yao kabla hawajaanza kusema.
Tunatambua mahitaji yao kupitia kilio, tabasamu na mitazamo yao. Tukiimba nao, kucheza sakafuni, au kukesha usiku kuwafariji, tunakuwa tunajenga msingi wa usalama wa kihisia sehemu salama ya kwanza wanapoweza kurudi wakijiamini kila walipoogopa au kuchoka.
SOMA ZAIDI: Tuanze Mazungumzo ya Fedha Nyumbani
Kadri walivyokua, tuliona uwezo wao wa kufikiri ukitanuka. Walianza kuuliza maswali ya maana yenye tafakuri zaidi na kuchora ndoto zao kwa kalamu na hata kutushirikisha kwa maneno. Tulihudhuria mikutano yao shuleni, tukashangilia walipoimba au kucheza na kupewa zawadi jukwaani, na tukafanya nao kazi za shule hata pale tulipochoka.
Tulijua huu ndio wakati wa kuwekeza katika maadili, upendo, taaluma, ushirikiano, na kadhalika. Kwa maneno na kwa matendo, tulijitahidi kuwa kielelezo cha uadilifu, heshima na upendo. Walipochokozana au kukosea, tuliwarekebisha na kuwaonesha njia bora.
Kipindi cha ujana kilikuja na changamoto zake. Ghafla, watoto wetu walihitaji faragha zaidi, wakaanza kuwa na marafiki wapya, na wakati mwingine wakawa kimya kiasi cha kututia wasiwasi. Tulijifunza kuwa wavumilivu. Tulijifunza kutowachukulia kama watoto wadogo, bali kama vijana wanaojitafuta.
Tuliacha mlango wa mazungumzo wazi, tukijadili masuala mazito kama mahusiano, ndoto zao, na hofu zao bila kuhukumu, kuwatuhumu wala kuwalaumu. Tulijifunza kuwaamini kuwa hata wakikosea, bado watarudi na kujirekebisa kwakuwa watajifunza kutokana na makosa. Na walirudi.
Walitugeukia walipojeruhiwa na maisha, walipohitaji kusamehewa, au walipotaka kujua kama bado tunawapenda na kuwajali kama zamani. Na jibu letu daima lilikuwa: “Ndiyo, bado tunawapenda na kuwathamini zaidi.” Na kuwakumbusha kuwa tupo kwa ajili ya kuwapa muongozo.
SOMA ZAIDI: Tunawaleaje Wavulana Wetu Kuwa Wanaume Bora wa Baadaye?
Walipoanza maisha yao ya utu uzima na kuanza kujitegemea katika maamuzi mengi, kutafuta ajira, kuanzisha familia, au kuhamia mbali, tulijifunza kuwapa uhuru wao. Si rahisi kumwona mtoto wako akiwa mtu mzima, anayefanya maamuzi yake hata kama huyaungi mkono.
Lakini tulijifunza kupumua, kusikiliza kabla ya kuzungumza, na kuwaheshimu kama watu wazima wanaojitahidi kuishi maisha kwa misingi tuliyowafundisha. Wakati mwingine walitushirikisha mipango yao, wakatutafuta kwa ushauri. Wakati mwingine walinyamaza kwa muda mrefu.
Lakini sisi tulibaki tukipatikana. Tulipokea simu ya usiku wa manane yenye sauti ya wasiwasi au ujumbe mfupi wa: “Nimekumbuka supu ya nyumbani.” Na tuliitikia kwa upendo ule ule wa siku za mwanzo.
Sasa tunaongea nao kama marafiki, na kama wazazi wenzao. Tunawatazama wakileta wajukuu, tukitabasamu kuona maisha yanavyojirudia. Wakati mwingine wanatuuliza, “Na sisi tulikua hivi kweli?” Tunaongeza kwa vicheko: “Na zaidi ya hapo.”
Hata wakiwa na majukumu yao, bado wanatutafuta wanapotutumia ujumbe wa “Shikamoo Baba/Mama,” au wanapokuja kutuona bila taarifa, tunajua uhusiano haukukoma bali umekomaa.
SOMA ZAIDI: Ni Muhimu Wazazi na Walezi Tuanze Kujadili Baleghe na Watoto Wetu Bila Hofu
Na pale wanapotushika mkono hospitalini, wanapotupikia chakula, au kutusindikiza safari, tunajifunza kupokea upendo wao kwa bashasha. Haya ni matunda ya miaka ya uaminifu, mazungumzo ya kweli, na upendo usiokoma.
Tumegundua kuwa kilichotuunganisha na watoto wetu ni upendo wa dhati, uliozaliwa katika mazungumzo ya wazi, uelewa, na moyo wa kutokata tamaa hata pale tulipochoka. Uhusiano huu umebadilika, lakini haujawahi kupungua. Miaka inaweza kupita, sura zao kubadilika, majina yao kuongezeka, lakini mioyo yetu itaendelea kuwa na nafasi yao.
Nasi, tutabaki pale, si kuwachagulia njia, bali kutembea karibu nao hata wanapotuacha nyuma, tukiwatazama kwa fahari. Tuendelee kusimulia hadithi zetu. Je, nawe umelelewa au kulea kwa namna inayofanana na hii?
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.