Tunapozungumzia maendeleo, ubunifu na teknolojia ni zana muhimu zinazotoa majibu ya changamoto mbalimbali. Majibu haya hutengeneza mustakabali wetu, kijamii na kiuchumi. Hata hivyo, licha ya uwepo wa mambo ya msingi zaidi — linapokuja suala la ubunifu katika jamii yetu — maneno yanayotawala zaidi ni teknolojia, ujasiriamali, na mabadiliko ya kidigiti. Lakini, masuala haya yote yanategemea utayari wa kimfumo.
Nilishiriki Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 iliyoanza Mei 12 hadi 16, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Nilijifunza mengi. Lakini, maswali yaliyonisumbua zaidi ni je, tunajenga mifumo ya ubunifu yenye uhalisia kwa jamii yetu? Je, mifumo hii inawajumuisha vijana wa maeneo ya pembezoni? Au, tunasherehekea tu hadithi za mafanikio zinazoonekana kuvutia, hasa Dar es Salaam?
Taswira iliyojitokeza zaidi kwenye mijadala pale JNICC ilikuwa dhahiri: vijana wana vipaji, ndoto, na ustahimilivu. Kuanzia bunifu zao hadi afua za changamoto mbalimbali — kama vile athari za mabadiliko ya tabianchi. Kimsingi, hakuna tatizo la uhaba wa bunifu. Hata hivyo, vijana hawa kuonekana tu ni suala moja. Lakini ushirikishwaji wao wa kweli katika mchakato mzima wa ubunifu kwa maendeleo ni kitu kingine.
Mara nyingi, ushiriki wa vijana huwa ni wa ishara tu. Utawaona jukwaani, kwenye chemshabongo au mashindano fulani, na hasa zaidi, katika picha ya pamoja. Lakini kwenye meza za maamuzi, mgawanyo wa rasilimali, au usanifu wa sera, vijana wengi hubaki nje ya vyumba vya majadiliano, hususan wale wa maeneo ya pembezoni. Hali hii hugeuza suala la ubunifu kuwa suala lisilo jumuishi na la wachache.
Upatikanaji wa maarifa
Wakati mmoja kwenye Wiki ya Ubunifu, nilikuwa nabadilishana mawazo na kijana mwenzangu mmoja. Alichokoza mada: “Kwa nini tunaonekana kuwa Waingereza kwenye kila kitu? Hata hizi bunifu, Kingereza ni kingi mno!” Swali hili linaweza kuonekana ni la kawaida, lakini lina maana kubwa sana. Kama ubunifu unakusudiwa kulenga watu wetu, basi lugha lazima iwe jumuishi. Kwa Tanzania, Kiswahili sio tu lugha ya mawasiliano. Ni njia sahihi na yenye usawa kwa Watazania karibu wote.
SOMA ZAIDI: ‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’
Takribani asilimia 90 ya Watanzania wanaelewa Kiswahili. Kuanzia vijijini hadi mijini. Lakini, ukizungumzia Kingereza, ambayo ni lugha ya kigeni, kinazungumzwa kwa ufasaha na takribani asilimia 10 tu ya Watanzania wote. Takwimu hizi tu, ni ishara tosha kuwa upatikanaji wa lugha ni muhimu katika umiliki na ushiriki wa afua za changamoto mbalimbali. Kwa mtazamo wangu, ubunifu sahihi ni ule unaoleta majawabu ya changamoto halisi katika jamii husika. Na lugha ni usukani.
Ninamaanisha, kuanzia elimu ya kidigiti, sheria, sera, mikakati, mipango kazi, mafunzo, hadi mashindano ya ubunifu, lazima tuhakikishe suala la upatikanaji wa lugha linakuwa sio jambo la kuwaza baadaye. Lugha inapaswa kuwa msingi wa mwanzo kabisa wakati tunaandaa miradi na programu mbalimbali. Maswali muhimu ya kutafakari: Je, tunabuni kwa ajili ya nani? Nani anatuelewa tunapokuja na hizo bunifu?
Tatizo sio fedha pekee, ni mfumo
Mijadala ya pale JNICC ilionesha bayana changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa miradi ya vijana. Lakini mbali na fedha, kuna tatizo kubwa zaidi: mfumo wa sera na utekelezaji usio na muunganiko. Tuna mikakati mingi na mizuri ya kiwizara, mashirika ya kiraia, wafadhili, na sekta binafsi — yote ikilenga vijana. Hata hivyo, juhudi zote hizi mara nyingi hazina mshikamano — haziko kwenye mstari mmoja — na ni za muda mfupi.
Hali hii inasababisha kujirudia kwa miradi, matumizi mabaya ya rasilimali, na inaharibu kabisa uendelevu wa majawabu ya changamoto halisi kwenye jamii yetu. Kama nilivyobainisha katika jukwaa moja: tunahitaji kuhama kutoka “miradi ya vijana” na kujikita zaidi kwenye “mifumo ya vijana.” Tunahitaji jitihada zinazorandana — ambapo usaidizi, stadi, mafunzo, uwazi, uwajibikaji, na matokeo vinaonekana na vinastawi.
Kwenye majukumu yangu ya kila siku, ukiwemo ujumbe katika Bodi ya Sauti ya Vijana ya Umoja wa Ulaya Tanzania, ninasisitiza zaidi ushiriki wa vijana kama vinara wenza, na sio washauri tu. Na, Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 ilionesha wazi umuhimu wa wito kama huu. Tunayo majukwaa mengi ya vijana “kutoa mawazo.” Lakini mawazo yoyote bila mamlaka — hususan katika muktadha kama huu — hugeuka masikitiko.
SOMA ZAIDI: Shule, Vyuo Vikuu Viwaelimishe Wanafunzi Badala ya Kuwatahinisha
Taasisi zetu nchini hazipaswi tu kusikiliza, bali zinapaswa kuwa tayari kugawana mamlaka na rasilimali, ili vijana washawishi namna sera, mikakati, na programu mbalimbali zinavyoundwa, kutekelezwa, na kufanyiwa tathmini. Endapo vijana wataonekana kwenye hatua za mwanzo tu, lakini wakapotea wakati wa bajeti kuandaliwa, huo sio ushirikishwaji. Ni ishara tu ya kwamba walikuwepo!
Maarifa yawe mali ya jamii
Somo jingine muhimu, ni jinsi maarifa yatokanayo na programu zetu yanavyokusanywa, kuhifadhiwa, kusambazwa, kutumiwa na hata kufanyiwa tathmini. Vijana, kupitia juhudi zao, hushiriki taarifa na uzoefu kutokana na juhudi zao. Taarifa hizi hutumwa kwa Serikali, watafiti, na mashirika wanayoshirikiana nayo.
Lakini, ni mara ngapi vijana hawa hupokea mrejesho au kuona matumizi au utekelezaji wa maarifa na mapendekezo waliyoyatoa? Kwa hakika, ni nadra. Hali kama hii huondoa motisha na huleta hali ya kuchoka, kudharauliwa, kubaguliwa, na kutengwa.
Usimamizi wa maarifa yanayopatikana kupitia miradi na programu mbalimbali, hasa za vijana, sio tu kwa ajili ya wafadhili au ripoti. Ni wajibu wa kimaadili. Kila mdau, ikiwa ni pamoja na vijana wenyewe, tunapaswa kujifunza kuhusu juhudi zipi zinazaa matunda na wapi panahitaji marekebisho au maboresho.
Tunahitaji mifumo ya mawasiliano ya pande zote — vijana, wadau na Serikali. Tunahitaji mchakato wa kujifunza unaowatambua vijana kama washiriki, na sio walengwa tu wa hizi afua na mikakati.
Tunatokaje hapa tulipo?
SOMA ZAIDI: Kijana wa Miaka 18 Anaweza Kuwa Kiongozi. Tuondokane na Ubaguzi wa Umri
Muhimu zaidi, bunifu zetu zitokane na muktadha na uzoefu wa jamii yetu. Sio kuiga kila bunifu za nje. Bunifu zao zinajibu changamoto za jamii za huko. Lakini pia, tunahitaji kuachana na hadithi za mtu mmoja mmoja. Tunapaswa kujikita katika mabadiliko ya mifumo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uratibu kati ya taasisi na wadau. Na, tuwekeze kwenye mifumo ya maarifa. Vijana wanayo maarifa mengi. Tuwape nafasi mezani, tuwasikilize na tushirikiane nao kama marubani wenza kugeuza mawazo kuwa vitendo.
Kwa sisi vijana, tunapaswa kuja na mikakati ya kidigiti inayojumuisha jamii za pembezoni. Tupime mafanikio ya mikakati na afua tunazokuja nazo, hasa kuhusu namna maisha yetu yanavyoboreshwa na sio tu idadi ya bunifu. Muhimu zaidi, tunapaswa kutambua kuwa upatikanaji wa lugha na muktadha ni chachu muhimu ya ubunifu unaoendana na jamii yetu. Lugha sahihi huchagiza tija, ufanisi, na uendelevu.
Ni muda muafaka tujiulize maswali magumu. Sio tu, “Vijana wanawezaje kubuni?” Bali pia, “Kwa nini mifumo yetu inawazunguka tu vijana, badala ya kushirikiana nao moja kwa moja?” Ubunifu ni zaidi ya bidhaa. Ni uwezo wa kuleta suluhu ya changamoto halisi kwenye jamii, ikiwa ni pamoja na kuziba ombwe la haki za kijamii na kiuchumi. Na uwezo huu, unategemea mifumo iliyotayari kuwezesha harakati hizi muhimu kwa jamii.
Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 ilikuwa ya msisimko, muhimu, na ya matumaini. Lakini kama tunamaanisha kweli kuhusu ushirikishwaji wa vijana, lazima tufanye zaidi ya kuwaalika kwenye makongamano. Lazima tubadilishe kabisa tunavyoweka mikakati, kufadhili, kuwasiliana, na kujifunza. Ubunifu unapaswa kuwa mradi wenye haki. La sivyo, utabaki kuwa maonesho tu. Tunapaswa kuja na mifumo inayowajumuisha vijana kuanzia mwanzoni, na sio kuwapa nafasi tu pale mwishoni.
Venance Majula ni mtaalamu wa sera za kazi na maendeleo na mjumbe wa Bodi ya Sauti ya Vijana ya Umoja wa Ulaya Tanzania, anayejikita katika ujumuishaji wa vijana, mifumo ya maarifa, na mpito wenye haki. Unaweza kumpata kupitia baruapepe majulavefama@gmail.com au X kama @venancemajula. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.