Serikali kupitia hotuba ya bajeti imeeleza kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 yanaendelea, ambapo katika kipindi cha miezi 11 yaani kuanzia Julai 2024 mpaka Mei 2025, serikali imeweza kutumia kiasi cha Bilioni 741.5, katika maandalizi ya uchaguzi unatarajiwa mnamo Oktoba 2025.
Taarifa ya hotuba ya bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Dk.Mwigulu Nchemba inaeleza:
“Baadhi ya maeneo yaliyopelekewa fedha katika kipindi cha Julai 2024 hadi Mei 2025 ni pamoja na: ugharamiaji wa deni la Serikali shilingi trilioni 11.16; ugharamiaji wa mishahara ya watumishi wa umma shilingi trilioni 10.27; na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, shilingi bilioni 741.5.”
Vitabu vya matumizi vya bajeti vinaonesha kuwa jumla ya makadirio ya fedha yaliyotengwa kwa ajili ya Tume ya Uchaguzi kwa mwaka 2025/26 ni shilingi Bilioni 378.2, huku bilioni 316.2 zikioneshwa kuwa zinaenda katika uchaguzi. Hii inafanya takribani Trilioni 1 kutumika katika maandalizi na shughuli za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, jumla ya Bilioni 416.8 zilitumika, ambao maandalizi ya uchaguzi yaligharibu Bilioni 154.3 na Tume ikatumia bilioni 262.2 kati ya Bilioni 331.8 zilizotengwa kwa ajili ya uchaguzi.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, jumla ya Bilioni 534 zilitumika katika uchaguzi, ambapo Bilioni 260.8 zilitumika katika maandalizi na Bilioni 273.6 zilitumika katika kuendesha uchaguzi. Serikali imeeleza kuwa, gharama zote za uchaguzi mkuu zitatoka katika fedha za ndani.