Leo nataka kuongelea mpira na siasa. Hapana, siyo yale mapambano yasiyoisha kati ya tembo wawili ambao wanachosha majani katika ugomvi wao usioisha. Sisi tunataka kuona mpira jamani! Tunataka kufurahia mapambano uwanjani, si yale ya mezani.
Tunataka kuona ufundi wa wachezaji, si ule wa wanasheria na wengine. Tena ule wa mezani unaua, unaua hata hamu ya kuona mchezo unavyochezwa, kuuona ufundi wa wachezaji wenyewe. Tena nakumbuka wakati fulani wachezaji wa timu moja walipinga viongozi wao, wakaambiwa waondoke, hawahitaji wachezaji. Yaani, klabu ya mpira haihitaji wachezaji wa mpira! Muhimu ni viongozi, si wachezaji, lakini bila wachezaji, klabu ipo kweli? Kweli dunia iko chini juu.
Lakini nataka kuangalia kwa namna tofauti. Tuwaangalie washabiki. Maana bila washabiki pia hakuna timu, hakuna klabu. Na hapo ningependa kutambua washabiki wa aina tatu.
Kwanza kuna washabiki njaa, au tuseme washabiki chawa (maana njaa ya chawa ndiyo inayosababisha tunyonywe damu). Washabiki hawa hawana upendo wa “hadi kifo kitutenganishe.” Thubutu! Watashabikia timu “yao” kwa muda ambao timu inafanya vizuri. Ikianza kuporomoka na wao wanakimbia kama panya anayekimbia boti inayozama na kuhamia timu nyingine inayofanya vizuri.
Unaweza kuamini wengine wanaweza hata kuhama ile United na kuhamia ile City. Hata hivyo, kwa hapa Bongo, nadhani tabia hii inahusu ushabiki wa timu za nje, hatuna uchungu sana nao, si ni za nje! Lakini ukweli ni kwamba, hata kwa timu hizi za nje, kuna ushabiki wa kweli, ushabiki wa damudamu, sembuse wa timu zetu za ndani.
SOMA ZAIDI: Watawala Tanzania Wana cha Kujifunza Kwenye Kisa cha Mfalme Henry II wa Uingereza na Askofu Thomas Becket
Mbili, kuna washabiki vurumai, au tuseme wanazi wa timu. Hawa nitawaongelea hapo baadaye.
Washabiki damudamu
Tatu, tuna washabiki damudamu, washabiki wazalendo wa kukubuhu wa timu zao. Hawa wana tabia gani? Utawaona wakishangilia matokeo mazuri kwa nguvu sana na kusononekea matokeo mabovu. Na daima hawaridhiki. Wanataka timu yao ifanye vizuri zaidi na zaidi. Ndiyo maana, wakiona kocha hafanyi vizuri watakuwa wa kwanza kumlaumu, kumkosoa, hata kumtusi na kudai aondoke wapate kocha mwingine mzuri.
Na wachezaji vilevile. Hata wakati wa mechi, utawasikia washabiki hawa wakipiga kelele kushauri, kulaumu, kushangilia na kuzomea. Ndiyo. Hawajali kama hawasikiki. Au tuseme wanajua hawasikiki, lakini hawawezi kunyamaza. Ni timu yao na wana uchungu nayo.
Tena washabiki hawa wanafanya vivyo hivyo kwa viongozi wao wengine wa klabu. Wakiona viongozi hawapigi tafu wachezaji, hawaleti wachezaji wengine wa kupaisha klabu, wakifuja fedha (fedha ambazo ni zao washabiki kutokana na michango yao, viingilio vyao n.k.) washabiki hawawezi kukaa kimya. Kitu chochote kinachovuruga timu yao hawatakikubali.
Watasema, watapiga mayowe, watalaumu, watazomea, hata kama ni kuandamana wataandamana ili mradi timu yao ipate kinachohitajika ili ifanye vizuri na kushinda. Na isiposhinda, watasononeka, watakasirika, watanuna kweli kweli lakini hoja kuu ni kwamba daima hawataacha timu yao.
SOMA ZAIDI: Kuna Uchaguzi, Uteuzi na Uchafuzi. Hapa Tanzania Tuna Nini?
Ndio ushabiki ulivyo. Shabiki wa kweli si chawa. Si mtu wa kusifu tu maana anajua kusifu tu si kwa faida ya klabu yao. Kusifusifu tu kutasaidia nini? Kweli watasifia yale mazuri, lakini hakuna timu malaika. Hakuna viongozi miungu. Na kusifusifu huleta hali ya kubweteka, ya kujiachia, ya kupotoka miongoni mwa viongozi, na kocha na wachezaji wenyewe. Na mwisho wa siku, wanajua klabu ni mali yao. Ni kweli, bila wachezaji, hawawezi kujiita klabu, lakini klabu ni mali yao ndiyo maana wanataka wachezaji watakaofanya kazi kufa na kupona kwa ajili ya klabu mali yao.
Na viongozi wazuri wa klabu, kocha mzuri, wachezaji wazuri, wanatambua umuhimu wa washabiki na maoni yao. Si lazima wayakubali yote ya washabiki, na washabiki wenyewe watapingana, lakini viongozi watazingatia, watawajibu washabiki, na kujieleza kwao, kutaka kushirikiana nao katika kupaisha klabu yao.
Hawatataka kumpoteza shabiki hata mmoja. Ndiyo maana utaona kwamba, baada ya mechi, wachezaji wakiwafuata washabiki wao huko waliko na kuwapigia makofi. Mahusiano kati ya wachezaji, kocha, viongozi na washabiki ndiyo gundi la kuunganisha klabu ifanye vizuri.
Uzalendo kwa taifa
Ndipo hapo nalinganisha ushabiki wa klabu na uzalendo kwa taifa. Kama ambavyo washabiki wanashangilia mafanikio na kuchukia wanachoona ni makosa, ni uzembe, ni ubadhirifu unaorudisha nyuma klabu yao, uzalendo ni vilevile. Uzalendo ni ushabiki wa taifa, kutaka taifa lifanikiwe, lipate maendeleo, lishinde ndani ya dunia uwanja wa fujo.
Mzalendo haogopi kutoa maoni yake, tena anasukumwa kabisa kutoa maoni kwa sababu ushindi wa taifa ni ushindi wake. Akili yake iko kwenye mafanikio ya taifa na si vingine. Ushabiki uko kwa taifa si vingine. Unashangilia mafanikio, na hauogopi kutoa maoni kama unaona mafanikio hayapatikani.
SOMA ZAIDI: ‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’
Lakini hapo pia napenda kutofautisha kati ya ushabiki na unazi. Nafananisha unazi na uchawa maana, pamoja na kutaka mafanikio ya timu, mnazi kazi yake ni kutukana, kutusi na hata kupigana na timu nyingine ili mradi awe juu kwa njia halali au haramu wakati shabiki anaweza kutambua kwamba, hata upande wa pili kuna uzuri na ubaya, na kwamba huenda analo la kujifunza kutoka kwa upande wa pili.
Mapenzi ya timu yake hayafanyi awe kipofu kwa klabu nyingine na mafanikio yao. Kwa ujumla, washabiki wa mpira hupenda kuona mpira ukichezwa vizuri apate raha. Na mzalendo vivyohivyo. Ni mshabiki wa maendeleo.
Mwaka mmoja kabla ya kuja Tanzania, timu yangu, Arsenal, iliingia katika fainali ya kombe la FA kushindana na Liverpool, baada ya kushinda tayari ligi hivyo ilikuwa inataka kushinda The Double ya ligi na kombe. Rafiki yangu, ambaye alikuwa shabiki sana wa Liverpool, alifanikiwa kupata tiketi mbili katika bahati nasibu ya timu yake kutokana na kwamba aliendesha timu ndogo ya mtaani kwao huko Liverpool. Alinipatia tiketi moja twende pamoja kwenda kuhudhuria fainali huko Wembley.
Tulikwenda na nikajikuta ni shabiki wa Arsenal peke yangu ndani ya bahari ya washabiki wa Liverpool. Duh! Wangekuwa wanazi ningekoma hasa baada ya Arsenal kushinda. Lakini haikuwa hivyo. Nikashangilia na kutaniana na washabiki wale.
Bila shaka hawakuwa na raha kabisa na walitoa ushauri lukuki kwa timu yao, lakini tulielewana. Tulifurahia mpira pamoja. Walikubali Arsenal siku ile walicheza vizuri zaidi. Ndio ushabiki huo. Kwa wanazi ningepigwa kisu.
Ndiyo hivyo. Hata katika taifa letu, tunataka ushabiki wa aina gani, wa uchawa, wa unazi au wa damudamu?
Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.