Baada ya mgogoro uliodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja kati ya klabu ya Yanga, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka (TFF), hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, ameamua kutumia busara kuumaliza.
Yanga ilikuwa inapinga kitendo cha Bodi ya Ligi kuahirisha mechi ya Machi 8, 2025, kati yake na Simba bila ya kufuata kanuni, huku chombo hicho kinachosimamia Ligi Kuu kikishindwa kauli ya kutetea uhalali wa uamuzi huo na kupanga tarehe mpya.
Mgogoro huo ulifika hatua ya Yanga kugomea mechi zote za Ligi na kupanua wigo wa madai yake kwa kutishia pia kugomea fainali ya Kombe la CRDB kwa hoja kwamba haijalipwa fedha za zawadi kwa kipindi cha miaka mitatu.
Wakati Bodi ya Ligi inaonekana kuanza kusalimu amri na uwezekano wa kuahirisha mechi kutoka Juni 15 ukionekana dhahiri, Simba, ambayo ilitishia kutocheza mechi ya Machi 8 kwa madai kuwa ilizuiwa kufanya mazoezi mepesi Machi 7, ilitangaza tena kutishia kucheza mechi itakayopangwa tofauti na Juni 15, hali iliyosababisha Rais Samia aingilie kati na hivyo mechi kupangwa Juni 25.
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Steven Mguto, alijiuzulu mara baada ya Rais Samia kukutana na pande zote za mgogorpo, huku rais wa TFF, Wallace Karia, akimsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo.
Kasoro nyingi
Wakati wa mgogoro wote kumeonekana kasoro nyingi kubwa katika muundo, uendeshaji, na ufanyaji maamuzi wa Bodi ya Ligi, hasa uhuru wake katika kuendesha mambo ya kila siku ya Ligi Kuu na mashindano mengine inayosimamia.
SOMA ZAIDI: TFF Ijiepusha na Chaguzi za Wilaya
Yanga iliibuka na hoja ya uhuru wa Bodi ya Ligi, ambao ni wachache tumekuwa tukiupigania kwa muda mrefu. Bodi hiyo inafanya maamuzi kwa maelekezo ya TFF na ndio maana hata sasa Karia ndio amemsimamisha Kasongo na si Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi.
Kwa hiyo, kutokuwepo kwa uhuru wa Bodi ya Ligi kunaonekana dhahiri katika uamuzi huo. Kwamba TFF ndiyo inayoajiri watendaji wa Bodi ya Ligi na si wawakilishi wa klabu katika uongozi wa chombo hicho ambao ni Kamati ya Uongozi ya TPLB.
Maana yake ni kwamba CEO wa Bodi ya Ligi hawezi kufanya uamuzi wowote mkubwa bila ya kupata maelekezo ya wakuu wa TFF, na hata uamuzi wa kuahirisha mechi ulitokana na maelekezo kutoka juu.
Katika mkutano wake na vyombo vya habari baada ya kukutana na viongozi wa Yanga, Kasongo alionyesha udhaifu huo aliposema maamuzi dhidi ya matakwa ya Yanga kutaka ajiuzulu pamoja na mwenyekiti wake na kuvunjwa kwa bodi hiyo, yalitegemea vyombo vya juu, akitaja Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu wa TFF, na si Mkutano Mkuu wa Klabu.
Uwajibikaji
Udhaifu mwingine uliojitokeza ni mfumo wa uwajibikaji. Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, akiwa pamoja na katibu wake.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Msimu wa Ligi Uwe Miezi 12 Badala ya Tisa ya Kawaida?
Huyu ni ngazi ya juu katika uongozi wa bodi hii, lakini anashiriki katika maamuzi ya kila siku, hali inayosababisha asiwepo mtu mwingine wa kuhoji maamuzi ambayo kamati yake imeyafanya.
Kama vile haitoshi, mwenyekiti wa bodi hiyo ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya TPLB, chombo ambacho kingetakiwa kihoji utendaji wa menejimenti inayoongozwa na CEO, lakini mwenyekiti anakuwa ameshashiriki katika shughuli za menejimenti.
Pia, muundo wa Bodi ya Ligi hauakisi chombo kinachoendeshwa kibiashara, kutokana na ukweli kwamba mpira wa miguu sasa ni biashara kubwa inayohitaji utamaduni wa uwajibakaji, uwazi, kusimamia nastadi za kibiashara na masoko.
Kwenye nchi za wengine, mwenyekiti wa bodi hachaguliwi kwa sifa za elimu ya kidato cha nne kama ilivyo kwa viongozi wa klabu. Viongozi wa klabu walishauriwa wakati wa kuunda TPLB kwamba si lazima mwenyekiti awe na sifa za kiongozi wa ngazi ya klabu kwa kuwa si lazima atoke kwenye klabu. Lakini kwa kuitaka nafasi hiyo, walipinga.
Katika nchi zilizoendelea, mwenyekiti wa chombo kinachosimamia ligi ya juu katika nchi, pamoja na CEO wake, ni lazima wawe ni watu wenye elimu, au stadi za biashara, na wawe wameongoza mashirika makubwa.
SOMA ZAIDI: Sakata la Yanga, Simba Haliwezi Kuisha Kama Kidonda. Viongozi Wawajibike
Hii inasaidia kwa kuwa kanuni za uendeshaji mashirika makubwa zimeweka misingi ya utawala bora, uwajibikaji, viwango na mahitaji ya taarifa za fedha na uwazi.
Ni kwa jinsi hiyo, menejimenti inayoongozwa na CEO huwajibika kwa bodi iliyo na wajumbe wengine ambao hawahusiki kabisa katika uendeshaji shughuli za kila siku, na hivyo kuwa na ujasiri wa kuhoji vitu vinavyoonekana kwenda mrama, au kutofuata miongozo na kanuni za uendeshaji mashirika makubwa.
Isingetokea mwenyekiti wa bodi ahusike katika vyombo vitatu tofauti vya bodi, huku akiwa mwenyekiti sehemu zote.
Hata mahusiano na wadau ni kitu ambacho kimewekwa bayana na mgogoro huo. Uahirishaji mechi ulifanywa kiholela bila ya kujali wadau wangeathirika vipi. Ni ngumu kwa chombo kinachofuata miongozo na kanuni za uendeshaji mashirika makubwa kufikia uamuzi kama huo wa kuahirisha mechi saa mbili kabla ya muda wa kuanza mchezo, wakati mtangazaji, wadhamini, klabu, mashabiki na wengine wengi wameshakamilisha maandalizi na wanasubiri tukio tu.
Hata ushirikishwaji wa wadau muhimu kwa mechi hiyo, ambao ni Simba na Yanga, haukuwepo. Yaani walitangaza tu kujiahirishia mechi bila ya kwanza kuwasiliana na pande hizo mbili kujadili tatizo ili kufikia muafaka. Ni uamuzi wa mchezo wa ridhaa.
Mageuzi
Yapo mengi yaliyojibainisha katika mgogoro huo ambayo yanaweza kuwa chanzo cha mageuzi muhimu ya kuifanya Bodi ya Ligi iwe na muundo wa kisasa, unaoweka uwajibikaji, unaojali ufanisi, unaojali usawa, unaojali maslahi ya wadau na unaoendeshwa kibiashara zaidi.
SOMA ZAIDI: Simba Inapaswa Kujiandaa, Ushindi Mnono Si Rahisi Katika Fainali
Na hii haiwezi kusubiri TFF ndio ifanye mageuzi hayo, bali klabu zenyewe ndizo zinahitaji kukaa chini na kuteua watu ambao watasaidia kufanya utafiti na kuunda mfumo thabiti wa Bodi ya Ligi.
TFF haiwezi kufanya hayo kwa sababu ni lazima itajifikiria kwanza mamlaka yake ambayo yanatoweshwa na uhuru wa TPLB, na hivyo kuweka vizingiti katika mambo yanayoweza kuwa na faida kubwa katika uendeshaji wetu wa ligi.
Ni aibu kusikia viongozi wa klabu eti wakisema Yanga walikuwa wanapigania maslahi yao. Hivi kuna maslahi ya klabu ambayo ni binafsi na hayawezi kuwa ya klabu nyingine?
Hivi Kagera Sugar hawakulalamikia mechi yao na Simba kuahirishwa kiholela mwaka 2024? Hivi hakuna klabu inayolalamikia maamuzi ya kila mara ya kuahirishiwa mechi zao? Hivi klabu ikitwaa kombe isipewe zawadi za fedha, ni tatizo la klabu moja?
Mawazo hayo hayastahili kutamkwa na kiongozi anayejua maslahi ya klabu. Kila klabu moja inapopigania kitu fulani, inapigania maslahi ya wote, hata kama wakati huo ni klabu hiyo pekee itakayonufaika na uamuzi mzuri kwao.
Kwa hiyo, viongozi waache kulala, waache kuangalia malalamiko ya klabu moja kuwa ni maslahi binafsi bali ni jambo ambalo litanufaisha wengine wote likiamuliwa vizuri.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.