The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kwa Nini Msimu wa Ligi Uwe Miezi 12 Badala ya Tisa ya Kawaida?

Ratiba isipangwe na kubadilishwabadilishwa kiholela.

subscribe to our newsletter!

Nchi nyingi ambazo msimu wao wa soka ulianza Septemba, zimeshahitimisha ligi zao, zikiwa zimeshapata bingwa, wawakilishi katika mashindano ya kimataifa, na timu zinazoshuka daraja.

Hata zile zenye mashindano zaidi ya mawili, nazo zimeshakamilisha msimu wake, hali inayoziweka klabu na wachezaji katika nafasi nzuri ya kupumzisha miili, kuungana na familia na marafiki zao na pia kufanya maamuzi kuhusu msimu mpya, huku viongozi wakihangaika kujaza nafasi za wanaoondoka, kutathmini kazi za makocha na benchi la ufundi kama kuna haja ya kufanya mabadiliko na mambo mengine mengi.

Timu zilizokwisha kujihakikishia nafasi ya kupanda, ndio wakati wao wa kutafuta wachezaji wa kuongeza nguvu, kuboresha benchi la ufundi na kusaka wadhamini ambao ni rahisi kupatikana timu ikiwa daraja la juu kwenye nchi.

Morocco, Misri, Tunisia na Afrika Kusini ni baadhi ya mataifa ambayo yameshakamilisha ligi zao na kutoa nafasi kwa wadau wake kufanya maandalizi ya msimu ujao.

Ukiangalia mipango ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), utaona bado wako ndani ya muda. Yaani, walipanga kuanza msimu Agosti 16, 2024, na kumaliza Juni 22, yaani bado hatujafikia hiyo tarehe. Lakini, kimahesabu, ni kwamba ligi yetu inachezwa kwa miezi yote 12, badala ya kawaida msimu kuwa na miezi tisa tu.

Si kwamba hakukuwa na ratiba ya msimu mzima, la hasha. Ratiba ilishakuwepo na ilionyesha kuwa mechi za mwisho zingechezwa Mei 24, kwa mujibu wa tovuti ya TPLB. Lakini mazoea ya kuahirisha mechi mara kwa mara, yamesababisha ligi iingie mwezi Juni na inawezekana ikafika mbali zaidi kama sakata la Yanga, Shirikisho la Soka (TFF) na TPLB halitaisha mapema.

SOMA ZAIDI: Sakata la Yanga, Simba Haliwezi Kuisha Kama Kidonda. Viongozi Wawajibike

Sakata hilo lilitokana na kuahirishwa kimazoea kwa mechi baina ya Yanga na Simba iliyopangwa kuchezwa Machi 8, lakini ikaahirishwa baada ya Simba kutangaza kuwa isingepeleka timu uwanjani kutokana na kuzuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla.

Mechi hiyo sasa imepangwa kuchezwa Juni 15, lakini Yanga imesema haiitambui kwa kuwa haifahamu sababu za kuahirisha mechi ya awali.

Kwa hiyo, tukivuka Juni tutakuwa tumeandika historia ya ligi kuchezwa kwa muda mrefu, miezi 13.

Athari kwa soka

Hii haisaidii mchezo wa mpira wa miguu, hasa kama nilivyoeleza awali, afya ya wachezaji ambao baada ya kuishi kambini kwa muda mrefu hustahili muda wa kuupumzisha mwili kabla ya kuanza kujiandaa kwa msimu mpya. 

Ligi inapochezwa kwa muda mrefu, huondoa vipindi vya mapumziko ya kawaida kwa wachezaji katikati ya msimu kwa kuwa kila wakati watatakiwa wawe kambini kujiandaa kwa mchezo wa raundi fulani.

SOMA ZAIDI: Simba Inapaswa Kujiandaa, Ushindi Mnono Si Rahisi Katika Fainali

Na kwa klabu, hali ni mbaya zaidi kwa kuwa msimu mrefu husababisha zitumie fedha nyingi kwa ajili ya kambi za mara kwa mara, safari, posho kwa wachezaji, benchi la ufundi na wengine wanaohusika na maandalizi ya timu, huku viongozi wakiwa na muda finyu wa tathmini na kufanya maamuzi ya msimu unaofuata.

Kampuni kama NBC Bank, ambayo inadhamini ligi nzima, inalazimika kutumia miezi 12 kusisimua udhamini wake kwa kuwa haiwezi kutulia na kusema ilishatoa fedha, bali inakwenda sambamba na matukio ili ipate mwonekano.

Hali kadhalika kwa kampuni zilizoshinda haki ya matangazo kama Azam Media na TBC ambazo ni lazima bajeti zake zinapanuka kutokana na muda wa kucheza kuwa mrefu zaidi.

Tunapozungumzia ubora wa ligi, ni pamoja na uimara wa ratiba inayojulikana mwanzo na mwisho wake. Na mwisho unatakiwa uwe wa kusisimua kulingana na msimu ulivyokwenda na wadau walivyoukubali uendeshaji.

Dosari

Ligi Kuu ya NBC inakwenda kuhitimishwa na dosari na kasoro nyingi, ambazo hakukuwa na umuhimu wa kuhalalisha kuwepo kwake, au kudumu kuanzia mwanzo wa msimu hadi mwisho.

SOMA ZAIDI: Betting: Rafiki Mzuri wa Soka Anayehitaji Umakini

Wapo wanaosema kuwa huenda msimu huu ndio umekuwa mbovu kuliko mingine yote ya hivi karibuni kutokana na matukio ya ajabu, uamuzi mbovu na sakata la uahirishaji holela wa mechi za Yanga na Simba na ile la Kagera/Simba ambayo yametokea kwa mara ya tatu ndani ya miaka mitatu.

Si kwamba Bodi ya Ligi hawakujipanga kukabiliana na ratiba za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) na zile za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), la hasha. Bali ni uahirishaji mechi usiozingatia masuala mengine muhimu.

Ratiba inaonyesha kulitakiwa kuwe na mapumziko Septemba 2 hadi 10, 2024, kwa ajili ya kupisha mechi za michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), pia ligi ilitakiwa isimame Oktoba 7 hadi 15, 2024 kupisha tena michuano ya awali ya AFCON.

Mapumziko kama hayo yalihusisha pia mechi za Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho Afrika, Kombe la CRDB, Kombe la Mapinduzi na Kombe la Muungano yalikuwa Oktoba 25 hadi 27, 2024, Novemba mosi hadi 3, 2024, Novemba 8-10, 2024, Novemba 11-19, Novemba 26-27, 2024, Desemba 6-8, 2024, Desemba 13-15, 2025, Januari 1-13, Machi 17-26, Februari 5-7, Aprili 5-6, Aprili 18-20, Aprili 21-27, Aprili 25-27, Mei 10-11, Mei 18-31 na hivyo raundi ya 30 ingeisha Mei 24 kwa timu zote 16 kushuka dimbani.

Fainali ya Kombe la CRDB ilipangwa kufanyika Mei 31, huku mechi za mtoano kwa ajili ya kupata timu mbili zinazoshuka zikipangwa kuchezwa Mei 28 na Juni mosi, huku zile zinazowania kupanda zikipambana na zinazotakiwa kushuka zikipambana Juni7 na 11.

Nini kimezuia?

SOMA ZAIDI: Kuna Dalili za Soka la Tanzania Kurudi Mahakamani

Kwa hiyo, Bodi ya Ligi ilikuwa na zana zote za kutumia kupanga ratiba, yaani kalenda ya FIFA, CAF na Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF) ili iishe mapema. Nini sasa kimezuia isiishe mapema?

Kuahirisha kiholela kwa mechi za wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa na hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa ratiba, hasa timu zinaposonga mbele. Lakini cha ajabu msimu huu ni Simba pekee iliyofikia hatua za juu za mashindano ya Afrika ilipofika fainali ya Kombe la Shirikisho, tofauti na msimu uliopita wakati Simba na Yanga zilipofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Azam FC, iliyoshiriki Ligi ya Mabingwa, na Coastal Union FC iliyoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika, ziliishia raundi za mwanzo wakati Yanga ilityolewa robo fainali ya Ligi ya Bingwa. Haingewezekana Simba pekee isababishe msimu kuchelewa kuisha kwa takriban mwezi mzima. Huu ni ulegevu.

Kama mwakilishi mmoja aliyefika fainali ya Afrika amesababisha ligi ichelewe kwa tarkiban mwezi mmoja, itakuwaje pale wawakilishi wanne kutoka Ligi namba nne Afrika watakapotinga wote hatua za juu za mashindanp hayo?

TPLB haina budi kujiangalia katika suala hilo. Ratiba isipangwe na kubadilishwabadilishwa kiholela. Ungetegemea uahirishaji wa mechi kwa ajili ya kupisha mashindano ya kimataifa ufidiwe haraka ili kutoweka tofauti kubwa ya idadi ya mechi na kuepuka kuchelewesha mechi nyingine bila ya sababu za msingi.

Yale mambo ya kizamani ya kuipa timu mwakilishi wiki moja nzima ya kujiandaa, ni lazima yakome kwa kuwa ndiyo yanachangia msimu kuwa mrefu bila ya sababu.

Tunahitaji kuona timu zetu zikiwa na wachezaji wenye utimamu wa mwili na hivyo ligi kuwa tamu, si timu moja inakuwa iko vizuri na nyingine inacheza na uchovu. Kwa kuendelea kuwa na ligi inayochezwa kwa miezi 12, hatutaweza kupata burudani safi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×