The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Betting: Rafiki Mzuri wa Soka Anayehitaji Umakini

Waingereza wameonyesha njia na sisi hatuna budi kuangalia tunawezaje kuingiza hiyo dhana ya kuwajibika katika kubashiri, hasa wakati huu ambao kampuni za ubashiri zinazidi kumiminika.

subscribe to our newsletter!

Ni taswira halisi ya mitaani hivi sasa. Vijiofisi vidogo vyenye runinga vimezagaa mitaani na vina nidhamu ya hali ya juu katika utendaji, yaani wahudumu wa hizo ofisi huwahi pengine hata watoaji huduma nyingine kama maduka ya bidhaa za chakula.

Na ni kawaida kukuta wateja wawili au watatu ndani wakiwa wanajaza karatasi. Hawa ni wabashiri wa mechi za michezo mbalimbali, na hasa mpira wa miguu.

Wale wasioenda kwenye ofisi hizo kujaza kitu kinachoitwa “mikeka,” hufanya hivyo kwa kutumia simu zao.

Huweka dau la kuanzia Shilingi 1,000 hadi kwa wanaoweza Shilingi 200,000 au hata Shilingi 500,000, wakitarajiwa kupata mara mbili au tatu ya kile walichowekeza iwapo ubashiri wao utakuwa sahihi.

Kampuni zinazoendesha michezo hii sasa zimekuwa rafiki mkubwa wa mpira wa miguu kwa kuwa ndio mchezo unaoweza kuwatengenezea mabilioni ya fedha.

SOMA ZAIDI: Kuna Dalili za Soka la Tanzania Kurudi Mahakamani

Kwa kuwa mchezo huo unafuatiliwa na wengi, kampuni hizo zimeona fursa ya kukuza biashara zao. Na fursa kubwa ni kujitangaza kupitia klabu zinazoshiriki ligi ya juu kwa kuwa ndizo zinazofuatiliwa, zinazoonyeshwa moja kwa moja na televisheni na ndizo zenye mashabiki wengi. Kwa hiyo, kuonekana kupitia klabu hizi ni kitu rahisi.

Na uzuri wake hazing’ang’anii klabu kubwa peke yake. Zipo kila sehemu na barani Ulaya zipo kwa klabu ndogo na si kubwa kama Barcelona, Real Madrid, Liverpool, Ajax, Arsenal na Bayern Munich.

Kama zitajihusisha na wakubwa hao, basi si kwa kuwa wadhamini wakuu, bali zitachukua sehemu ya udhamini, siku hizi wanaita “washirika.”

Hapa nyumbani tulianza na SportsPesa, ambayo iliingia kwa kishindo kudhamini klabu vigogo vya Simba na Yanga, kabla ya biashara kupamba moto na Simba kuachana nao na kuingia mkataba na M-Bet.

Ubashiri

Pamoja na kwamba mchezo huu wa kubashiri huhusishwa na magenge ya kamari yaliyozagaa barani Asia, yakifanya njama za kupanga matokeo ili kujivunia mamilioni ya dola, bado mpira wa miguu haujaharamisha ubashiri wa mechi za mashindano yake.

SOMA ZAIDI: TFF Isisubiri CAS, Ianze Kujiwajibisha Sakata la Yanga v Simba

Ubashiri wa mechi bado unaendelea kuwa mchezo halali, unaotambuliwa na mamlaka na unaoendeshwa bila ya mbinu chafu za kukwepa kodi.

Kampuni hizi zimesaidia sana klabu kuimarika kifedha na kuweza kuendesha mambo yake bila ya matatizo.

Kwa sasa, mbali na kampuni kama GSM, inayojihusisha na uuzaji bidhaa mbalimbali, ni kampuni chache zinazouza bidhaa zimeingia katika udhamini mkuu wa klabu za Ligi Kuu.

Lakini kampuni za ubashiri zinaanza kushamiri baada ya SportsPesa kufungua njia. Hivi sasa kuna kampuni kama 10 Bet, Meridian Bet na M-Beti zilizoingia Tanzania kuchangamkia fursa inayotolewa na Ligi Kuu ambayo ni ya nne kwa ubora barani Afrika kwa sasa.

Nchini Uingereza, hali ni zaidi ya hapa. Kati ya klabu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu ya England, klabu kumi na moja zinadhaminiwa na kampuni zinazoendesha biashara ya ubashiri.

Kwa pamoja, klabu hizi zilikusanya mapato ya Pauni bilioni 15 za Uingereza msimu wa mwaka 2023/24, mapato ambayo ni makubwa. Kwa hiyo, kuna biashara kubwa ndani ya ubashiri, hasa katika soka, na kitu kizuri sehemu ya fedha hizo zinarudi kwenye mchezo huu maarufu duniani.

Ushiriki wa watoto

SOMA ZAIDI: Simba Wameonyesha Njia Ujenzi wa Viwanja

Lakini si kila rika linaweza kushiriki mchezo huu, bali watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 18 kutokana na kuhusishwa na kamari. Watoto, au vijana wadogo, wanatakiwa kukaa mbali na mchezo huu, lakini inaonekana wengi wanavutiwa kutokana na jinsi wanavyoona baadhi ya wabashiri wakitengeneza fedha kirahisi.

Hawa vijana wadogo na watoto huwa hawaoni jinsi hao wabashiri wanavyoathirika pale ubashiri wao unapokwenda mrama, bali huona pale wanapovuna fedha nyingi. Na hii ni hatari kwa kizazi cha baadaye kudhani kuwa maisha ni kubashiri tu na si kufanya kazi.

Kuonekana kirahisi kwa matangazo ya kampuni hizi ndiko kunakoongeza umaarufu wa biashara hii na kuvuta watu wa rika tofauti, na hapo ndipo tatizo linapokuwa kubwa zaidi.

Watoto na vijana wadogo ndio wanaonekana kuwa katika uwezekano mkubwa wa kuathirika na biashara hii.

Nchini England kuanzia msimu ujao, klabu za Ligi Kuu na Championship hazitaruhusiwa kuweka nembo zao kifuani mwa jezi za klabu wanazozidhamini.

Huu ni uamuzi ambao nchi hiyo imeamua kuchukua bila ya kulazimishwa na mashirikisho ya kimataifa kwa lengo la kulinda vijana wadogo na watoto.

Kubashiri kwakuwajibika

Wameachukua uamuzi huo ili kupunguza mwonekano, au visibility kwa kimombo, wa biashara ambayo inaweza kuathiri vizazi vijavyo. Hata mdhamini aliyeingia mkataba na Chama cha Soka cha England (FA), anafanya shughuli zake kwa kaulimbiu ya Responsible Gambling, au kubashiri kwakuwajibika.

Hizi ni juhudi binafsi za kupunguza athari za mchezo wa kubashiri kwa taifa la kesho.

SOMA ZAIDI: Kama Ligi za Wilaya na Mkoa Hazisikiki, Kuna Haja ya Kuwa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es Salaam?

Hivyo, pamoja na ukweli kwamba ubashiri, au betting, ni biashara kubwa inayoingiza fedha nyingi kwa nchi na inayoimarisha uchumi wa klabu za mpira wa miguu, kuna haja ya kuangalia kwa jicho zuri urafiki kati ya betting na mpira wa miguu.

Waingereza wameonyesha njia na sisi hatuna budi kuangalia tunawezaje kuingiza hiyo dhana ya kuwajibika katika kubashiri, hasa wakati huu ambao kampuni za ubashiri zinazidi kumiminika, ofisi zao mitaani zinazongezeka, urahisi wa kubashiri unazidi kuongezwa na wakati ambao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeingia mkataba na kampuni ya ubashiri.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×