Katika kila nyanja, kila sekta, kila taasisi au kampuni ya umma au ya binafsi, wengi wanakubaliana juu ya umuhimu wa mabadiliko. Mabadiliko ni muhimu kwa taasisi, kwa nchi ili iweze kuendelea. Mabadiliko ni jambo jema. Ni jambo la kheri, lina nia ya kuboresha, kuongeza ufanisi na kutatua changamoto zilizopo.
Kwa ufupi sana, nitaje baadhi tu faida za mabadiliko na hasa ya kisiasa: Mabadiliko huimarisha utawala bora na uwajibikaji. Mfano mabadiliko ambayo kila siku wananchi wanayadai kuweza kuimarisha uwajibikaji, demokrasia na kuongeza uwazi ili hatimaye kuondoa rushwa na kuwajibisha viongozi. Haya yote hupelekea kuwa na Serikali inayoaminika na Serikali ambayo ina untendaji mzuri na ufanisi mkubwa.
Kukua kwa Uchumi na maendeleo: Hii pia ni faida nyingine ya mabadiliko. Ni wazi kuwa mabadiliko huweza kufungua masoko, kuchochea uwekezaji, na kuongeza ufanisi ambao mwisho wake huleta ustawi katika maisha ya wananchi maskini na kuzalisha ajira zenye tija.
Kuimarisha utawala wa sheria na haki: Kwa maoni yangu, naamini kuwa mabadiliko ya sheria na hasa Katiba, sheria ya mama huweza kuimarisha tasisi ambazo huwa huru, zenye nguvu na ambazo zitatekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha kuwa sheria inatumika kwa usawa, wakati wote na inalinda haki za wananchi na kuimarisha amani.
Kupanua ushiriki wa kisiasa na uwakilishi: Mabadiliko ya kisiasa huongeza ushiriki wa wananchi katika masuala yote yanayowahusu wananchi. Mabadiliko ya kisiasa yataweza kutengeza mufumo jumuishi, yenye kuruhusu maoni na sauti mbalimbali na hasa hasa, sauti kutoka katika makundi yaliyopo pembezoni kama vile wanawake, vijana, wazee, wenye mahitaji maalumu n.k.
Usawa na ujenzi wa jamii jumuishi: Mabadiliko huweza kuondoa matabaka yaliyopo katika jamii kwa kuhakikisha huduma bora za jamii kama vile elimu, afya, na ajira zinapatikana kwa wote bila ubaguzi na hili hupelekea kupungua kwa umaskini na kuleta ustawi kwa wote bila kumwacha yoyote nyuma.
Uchumi wa kisasa na unyumbufu: Mabadiliko husaidia sana taasisi na sera mbalimbali kuweza kuendana na kasi ya mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia na hifanya nchi iweze kushindana kimataifa. Hivyo, mabadiliko ni muhimu sana katika kuiwezesha nchi iweze kushindana na mataifa mengine na iweze kutumia vizuri fursa ilizo nazo.
Kupunguza migogoro na misuguano ya kijamii: Hii nayo ni faida nyingine ya mabadiliko kwani mabadiliko hujikita katika kutafuta chanzo cha tatizo kama vile rushwa, kusekana kwa kwa usawa, na ubaguzi. Hivyo, mabadiliko huchangia kwa kiasi kikubwa sana katika kudumisha amani na upendo kwa miongo mingi ijayo. Mabadiliko yataweza kutusaidia kupunguza urasimu na kuleta ufanisi na kuboresha huduma za jamii na kuzifanya ziwe rafiki kwa wananchi wote.
SOMA ZAIDI: Yanayokera Kuhusu Katiba ya 1977 na Haja Yakuwa na Katiba Mpya Sasa
Hizi ni baadhi ya faida chache za kufanya mabadiliko katika katika Nyanja mbalimbali za jamii. Licha ya faida hizi, watawala katika nchi nyingi za Afrika hawataki hata kusikia neno mabadiliko. Hivi tumewahi kujiuliza ni kwa nini Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakitaki mabadiliko makubwa ya kimfumo? Hivi sababu zao hasa ni zipi za kukataa mabadiliko? Kwa mtazamo wangu hizi ni baadhi ya sababu za CCM kukataa mabadiliko
Kuendeleza ukiritimba wa kisiasa: CCM imekuwa madarakani toka tupate uhuru. Tanzania haijawahi kubadili chama cha siasa kilichopo madarakani tokea tupate uhuru. Aina yoyote ya mabadiliko ambayo yatatengeneza uwanja sawia wa ushindani, yanaweza kuleta hatari kwa chama hiki kuendelea na ukiritimba katika duru za siasa.
Hivyo, kwao mabadiliko ni suala baya sana, ni mkakati wa kuwaondoa madarakani, ni mpango wa kuwafanya wasiendelee kuhodhi Madaraka na kuwaondolea ukiritimba ambao wanaufurahia katika kila taasisi na kila Nyanja. Hili hawawezi kukubali, na wapo tayari kufanya lolote almuradi hili lisitokee.
Sababu nyingine ya CCM kukataa mabadiliko ni ili waweze kulinda maslahi yao ya kiuchumi na kuendelea kujidumisha kisiasa: Wanasiasa wengi Tanzania wana mitandao ambayo inayouwangaisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuhodhi raslimali mbalimbali. Ndio maana si ajabu hivi sasa kuelekea uchaguzi ukikuta wafanyabiashara wengi wakipigana vikumbo na wengine kutumia mamilioni ya pesa ili waweze kupata nafasi fulani ya kisiasa.
Hali hii inawafanya walinde maslahi yao ya kiuchumi kwa gharama yoyote ile. Hivyo hawawezi kukubali mabadiliko makubwa ya kimfumo ambayo, yataleta uwazi zaidi, kuwezesha kugatua madaraka na kuharibu mitandao ya ulaji.
Kama tumedhamiria kuleta maendeleo kwetu sisi na kwa kizazi kiijacho, hatuna budi kufanya mabadiliko makubwa sana katika Katiba yetu, sheria zetu na taasisi zetu ili ziweze kutuondoa katika hali duni tuliyonayo ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea. Tunahitaji sana tuweze kuimarisha utawala bora, uwajibikaji, uwazi, kuheshimu haki za binadamu, kuwa na taasisi ambazo ni huru, makini zenye uwezo wa kiutendaji na zinachungana.
SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Katiba Yatajwa Kuwa Suluhu ya Uchaguzi Huru na wa Haki
Aidha ni muhimu sana tuwe na mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili yetu yaani mahakama, bunge na serikali. Mihimili iwe huru na iweze kuchungana. Tukifanya hivyo, si tu tutatenda haki na kudumisha amani, bali pia tutaweza kuvutia wawekezaji, sekta binafsi itaweza kukua, tutazalisha ajira zenye tija na tutaweza kumkabili adui umaskini.
Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, imeaninisha shabaha za jumla na moja ya shabaha ya jumla ambayo ni ya kumi na tatu (13) ni: “Tanzania kuwa taifa la kidemokrasia, likiongozwa na Katiba imara inayoakisi mwafaka wa kitaifa,, taasisi madhubuti za umma, na mfumo thabiti wa vyama vingi vya siasa.”
Pia shabaha namba kumi tisa (19) inasema “Watanzania wote wanafurahia uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kukusanyika katika mazingira ya amani, usalama na utulivu.”
Mungu Ibariki Tanzania.
Selemani Rehani ni mchambuzi wa masuala ya siasa na demokrasia. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia selemani.rehani.gac@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.