The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Yanayokera Kuhusu Katiba ya 1977 na Haja Yakuwa na Katiba Mpya Sasa

Mamlaka ya kifalme ambayo Katiba hiyo inampa Rais ni moja kati ya mengi yanayofanya watu wadai Katiba Mpya.

subscribe to our newsletter!

Mjadala wa Katiba si mgeni katika masikio ya Watanzania walio wengi, ni mjadala ambao umekuwepo kwa miongo mingi, na kila wakati umekuwa ukichukua sura mpya, ukiambatana na mabishano na malumbano yasiyokwisha. 

Kwa siku za hivi karibuni, mjadala mkali kuhusiana na umuhimu wa Katiba Mpya umekuwa ukiendelea nchini kwetu, wengi wakionekana kuwa na matamanio na nyaraka hiyo muhimu ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwapatia Watanzania.

Wapo miongoni mwa Watanzania, hata hivyo, wanaohoji baadhi ya wenzao wanaotaka Katiba Mpya, wakiwauliza kwani ni vifungu gani kwenye Katiba ya sasa ya mwaka 1977 vinawakera? 

Swali hili, kwa mfano, liliulizwa kwenye mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika mnamo Septemba 11, 2023, jijini Dar es Salaam.

Nikiwa mmoja wa Watanzania wanaotaka Katiba Mpya, lazima nikiri kwamba yapo mengi kwenye Katiba ya sasa yanayokera na hivyo kutengeneza umuhimu, au haja, ya kuwa na Katiba Mpya haraka iwezekanavyo hapa nchini kwetu.

Kwenye tafakuri hii fupi, nakusudia kuwashirikisha wasomaji kwenye mambo hayo yanayokera ambapo ni pamoja na namna yenyewe Katiba hii ya sasa ilivyopatikana, ambapo, kama tunavyofahamu, Watanzania hatukushiriki kwenye kuitengeneza hii Katiba, kitu ambacho kinaiondolea uhalali wa kutumika.

Ninaamini kuwa ni muhimu kwa Watanzania kushirikishwa kuandika Katiba yao wao wenyewe, waamue aina ya jamii ambayo wanataka kuijenga. Je, tunataka kujenga jamii ya namna gani na inayozingatia nini? 

Rais-Mfalme

Mbali na kukosa uhalali wa kisiasa, Katiba hii ya mwaka 1977 pia ina tatizo kubwa ambalo nadhani ni la msingi na ndiyo linalochochea wengi wetu kutaka mabadiliko ya haraka kufanyika ili kulitatua, na hili si jingine bali ni lile linalohusika na kumpa Rais wa nchi mamlaka ya kifalme.

Hili ni tatizo kubwa sana na tungetamani kuona katika Katiba Mpya dosari hii inarekebishwa. Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema kuwa angetaka, angeweza kuwa dikteta kwa Katiba hii. 

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu Ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Tanzania

Maana yake ni kwamba kwa Katiba hii, Rais wa Tanzania anaweza kuwa dikteta, akiamua, na bado akawa hajaikiuka Katiba hiyo. Madaraka makubwa ya Rais ni suala linalokera sana. 

Hali hii inapelekea kukosekana kwa uwajibikaji, ufanisi, na zaidi linawakosesha wananchi kuwa na uchaguzi huru na wa haki na fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Rais ana msururu mkubwa wa uteuzi; anaowateua wanakuwa na tabia ya kujipendekeza na kuwajibika kwake badala ya kuwajibika kwa wananchi. Madaraka makubwa ya Rais yanawanyima Watanzania uchaguzi ulio wa haki na huru. 

Rais, ambaye mara nyingi huwa ndiyo mgombea wa nafasi ya Urais na Mwenyekiti wa chama tawala, amepewa mamlaka ya kuchagua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Makamu wake, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, na Makamishna wote wa Tume ya Uchaguzi.

Muundo huu wa Tume ya Uchaguzi hautupi tume huru inayoweza kusimamia uchaguzi kwa haki na bila upendeleo. Wateuzi hawa ni lazima watakuwa watiifu kwa yule aliyewateua. Hali hii inakwenda hadi chini kabisa kwa maofisa wa kusimamia uchaguzi ambao ni Wakurugenzi ambao pia ni wateule wa Rais. 

Hivyo basi, ili tuweze kuwa na uchaguzi huru na wa haki, hatuna budi kufanya marekebisho ya Katiba na sheria za uchaguzi; marekebisho ambayo yatatupa vyombo huru vya kusimamia uchaguzi, vyombo huru vitakavyosimamia uchaguzi kwa haki na uhuru.

Kitu kingine kinachokera kwenye Katiba ya sasa, na kinachohusiana na hali hii ya Urais-Ufalme, ni vifungu vinavyozuia matokeo ya kura za Urais, mara yanapotangazwa, kutokuhojiwa na chombo chochote kile. Hili ni suala ambalo limekwishasemwa mara nyingi sana na kulalamikiwa sana.

SOMA ZAIDI: Nia Ovu ya Wanasiasa Yahatarisha Kuwanyima Watanzania Katiba Mpya

Ripoti za waangalizi wa uchaguzi toka mwaka 1995 hadi sasa zimekuwa zikisema na kutoa mapendekezo kuwa kifungu hiki hakifai na mabadiliko yanahitajika ili kutoa nafasi kwa matokea ya Urais kuhojiwa Mahakamani kama yale ya ubunge na udiwani. Mantiki ya kuzuia kuhoji matokea ya Urais ni nini hasa?

Mgombea binafsi

Kama Mtanzania, kifungu kingine kinachonikera ni kile ambacho kinazuia mgombea binafsi. Kifungu hiki kimepingwa sana. Hayati Christopher Mtikila alikwenda mahakamani kupinga kifungu hiki na Mahakama ilitoa hukumu kuwa kifungu hiki kinaminya haki za raia kugombea kwenye uchaguzi. 

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliitaka Serikali ya Tanzania kurekebisha kifungu hiki ili kutoa haki kwa raia, lakini pia kuheshimu mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imesaini. Hadi leo hii, Serikali yetu imekaidi kuyafanyia kazi maamuzi haya.

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, akihutubia katika kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Mbeya, aliwahi kusema kuwa Serikali haina mamlaka ya kuwanyang’anya raia haki yao ya uraia ya kuomba kuchaguliwa bila ya kulazimishwa kuwa wanachama wa chama cha siasa. 

Jambo la kusikitisha zaidi, wanachama wa vyama vyote vya siasa siyo wengi sana. Yawezekana wote, kwa ujumla wao, hawazidi hata milioni kumi. Iweje kuwanyima nafasi ya kuomba kuchaguliwa Watanzania mamilioni ambao si wanachama wa chama chochote kile cha siasa?

SOMA ZAIDI: Mchakato wa Katiba Mpya Tanzania: Yajayo Yanafurahisha

Timu ya waangalizi kutoka Jumuia ya Ulaya, katika ripoti yao ya uchaguzi wa mwaka 2015, wanatoa mapendekezo kadhaa ya kuboresha mfumo wa uchaguzi wa Tanzania. 

Moja ya pendekezo lao ni kuwa haki ya kuomba kuchaguliwa isiwe tu kwa wanachama wa vyama vya siasa, bali iwe pia kwa raia wote wenye sifa za kuomba kuchaguliwa. 

Ripoti inashauri kuwa ni wakati muafaka sasa wa kutekeleza amri ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na kuruhusu wagombea binafsi.

Katiba Mpya sasa

Tunahitaji Katiba bora sasa ambayo Watanzania wameshiriki katika kutoa mawazo yao na maono yao; Katiba ambayo inatupa utaratibu wa taasisi na vyombo kuchungana na kusimamiana; Katiba ambayo itatupa mgawanyo wa madaraka ulio wazi kabisa kati ya mihimili mitatu ya Serikali, Bunge na Mahakama.

Kwa sasa, mhimili mmoja wa Serikali una nguvu kubwa kuliko mihimili mingine. Tunahitaji Katiba ambayo itatupa vyombo na taasisi huru ambazo zitatenda wajibu wao kwa weledi, haki, na uwazi. 

Baadhi ya vyombo na taasisi hizi ni kama vile Bunge, Jeshi la Polisi, Mahakama, Tume ya Uchaguzi, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), nakadhalika.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Serikali Haitekelezi Maamuzi Yanayotolewa na Mahakama?

Tunahitaji Katiba Mpya kwani ndiyo itaweka mazingira sawia katika ushindani wa kisiasa, na hasa tunapokumbuka funzo kubwa tulilopata katika uchaguzi uliopita ambapo tulishuhudia wagombea wengi kutoka upinzani wakienguliwa katika hatua za mwanzo. 

Katiba bora itatupa sababu Watanzania kujitokeza kupiga kura na kuwachagua viongozi wetu; itatupa uchaguzi unaoaminika, wa haki na huru; itatupa fursa ya kuchagua viongozi tunaowataka; na hilo litatupa sababu ya kushiriki kikamilifu katika chaguzi mbalimbali. 

Je, tutakwenda katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 kwa kutumia Katiba hii ya sasa, na je, kama itakuwa hivyo, matokeo yake yatakuwa ni yapi?

Tutafakari kwa pamoja!

Selemani Rehani ni mchambuzi wa masuala ya siasa na demokrasia. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia selemani.rehani.gac@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *