The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mambo Muhimu Ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Tanzania

Kalenda nzima ya nini kitaanza, na nini kitafuata, hatua kwa hatua hadi kupata Katiba Mpya, itapaswa kuandikwa katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Katiba.

subscribe to our newsletter!

Nilibahatika kualikwa, kuhudhuria, na kuhutubia Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa ulioandaliwa wiki iliyopita kujadili utekelezaji wa taarifa ya Kikosi Kazi na kutathmini afya ya demokrasia nchini. 

Mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ulifunguliwa na kuhutubiwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, huku ukipokea mada na mawasilisho kutoka kwa maprofesa, viongozi, na watafiti kadhaa wa masuala ya siasa na demokrasia nchini. 

Katika mada yangu, nilijikita kuzungumzia eneo la Katiba Mpya ambalo, kwa maoni yangu, halikuwa limepata mjadala wa kutosha wakati wa mkutano huo. 

Kwa vile nilipewa dakika 15 pekee kuwasilisha mada yangu ya uchokozi, na kwa kuwa ni Watanzania takribani 700 tu waliokuwepo ukumbini kunisikiliza, nimeona nitumie fursa hii kujadili hoja nilizowasilisha mkutanoni kwa kina zaidi kimaandishi kwa lengo la kuwafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi yetu.

Kwa ujumla, mkutano ulilenga kujadili hali ya demokrasia nchini kama sehemu ya ujenzi wa Tanzania Mpya kama inavyonuiwa na Rais Samia. Kwa bahati nzuri, Rais mwenyewe alianza kwa kueleza ndoto zake kwa Tanzania anayoiongoza, akitaja haja yakujenga taifa la watu wanaozungumza juu ya matatizo ya nchi yao. 

Katika hotuba yake, Rais alikemea vikali sana tabia inayozidi kukua ya baadhi ya wanasiasa kuendekeza siasa za matusi, kejeli, na vitisho, akisema hakuna mtu mmoja au kundi fulani dogo ambao wao ndiyo Watanzania zaidi kuliko wengine. 

Katika hali iliyoonesha wito wa Rais kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kusikilizana, Rais alitumia muda wake wa hotuba kurejea R zake nne ambazo amekuwa akizitumia kama kauli mbiu yake ya maono aliyonayo kuelekea Tanzania Mpya.

Kwa upande wangu, niliona haja ya kuanzia katika ‘R’ inayohusu ujenzi wa Tanzania Mpya kama sehemu muhimu ya malengo ambayo, kama taifa, tunapaswa tuyatekeleze. 

Katiba Mpya

Katika hilo, nilitoa hoja kuwa ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Mpya ndiyo namna bora kuliko zote ya ujenzi wa Tanzania Mpya kuanzia hapa tulipo. Kwa bahati nzuri, Rais alikuwa amegusia awali katika hotuba yake mambo kadhaa kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya Tanzania. 

Kwa maoni yangu, Rais alikuwa ana maono na nia thabiti ya kutaka Mchakato wa Katiba Mpya ukamilike na nchi yetu ipate Katiba Mpya. Hata hivyo, nilitoa hoja kuwa kitu ambacho Rais alikuwa hajafanikiwa kueleweka, hata miongoni mwa wasaidizi wake wa Karibu, ni suala la muda. 

Je, Mchakato wa Katiba Mpya unaanza sasa au lini? Pia, je, kama taifa, tunaanza na hatua gani?

Kwa mawazo yangu, nilisema, na ninarudia kusema, kwamba Rais anaonesha nia ya kuongoza ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Mpya sasa, hata leo. Kiukweli, nilieleza kuwa Rais alitoa ahadi ya Katiba Mpya tangu alipoapishwa kushika hatamu za uongozi kama Rais kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli mapema mwaka 2021. 

Ndani ya mwaka mmoja tu akiwa Ikulu, Rais aliongoza vikao vya Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwa Mwenyekiti wake, ambapo chama hicho tawala kiliagiza, mnamo mwezi Juni 2022, kuwa Mchakato wa Katiba Mpya uanze sasa na ukamilishwe ili kuzaa Katiba Mpya. 

SOMA ZAIDI: Nia Ovu ya Wanasiasa Yahatarisha Kuwanyima Watanzania Katiba Mpya

Baadaye, Rais alisikika akiagiza Serikali yake kuandaa utaratibu ili Mchakato wa Katiba Mpya uanze kukamilishwa. 

Kwa kuwa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa na vyombo vinavyomsaidia, Rais alilazimika kutumia hotuba yake kwa taifa kupitia mkutano na vyama vya siasa kuagiza tena kuwa Serikali iandae utaratibu ili Mchakato wa Katiba Mpya ukamilishwe. 

Safari hii, Rais alienda mbali zaidi na kuahidi kuunda kamati ya wataalamu itakayoturatibu, kama taifa, katika kukamilisha Mchakato wa Katiba Mpya. 

Katiba Inayopendekezwa 

Kwa wachambuzi wa masuala ya siasa na katiba kama mimi, ilionekana dhahiri kuwa Rais alikuwa ameridhia mapendekezo ya wananchi, wanasheria, na wanaharakati kuwa itafaa kutoanzia ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba kutoka kwenye Katiba Inayopendekezwa kutokana na waraka huo kukosa kiwango cha uhalali kinachofaa kuiwezesha kupitishwa kuwa Katiba ya Tanzania.

Kwa wasiokumbuka vema, Katiba Inayopendekezwa ilitokana na Bunge Maalum la Katiba lililoketi kwa zaidi ya miezi sita mwaka 2014, likihusisha wanasiasa – wabunge wote, wawakilishi wote kutoka Zanzibar, na wanasiasa wengine kutoka vyama vyote vya siasa – pamoja na wajumbe wengine waliowakilisha wananchi kupitia Asasi za Kiraia na taasisi za dini.

SOMA ZAIDI: Mchakato wa Katiba Mpya Tanzania: Yajayo Yanafurahisha

Ingawa Bunge Maalum lilianzishwa rasmi kisheria, kukosekana kwa mfumo, utaratibu, na vyombo vya kushughulikia tofauti na migogoro ambayo ingejitokeza wakati wa Bunge Maalum la Katiba, kulipelekea kushindwa kutatua mgogoro kati ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na uongozi wa Bunge Maalum la Katiba hadi kusababisha kuondoka barazani kwa wajumbe wote wa UKAWA, wakisusia kile walichokiita uendeshaji wa kibabe wa Bunge hilo. 

Katika hali iliyoonesha ugeni wetu kama taifa kwenye uandishi wa Katiba Mpya, wajumbe waliobaki ukumbini, wengi wao wakiwa CCM, walishindwa kutumia busara ya kutafuta maridhiano kwa kuwaita waliosusia ili kutafuta muafaka na badala yake walisikika wakisema, ‘Zege huwa halilali.’

Kwa kuendelea na kukamilisha mchakato wa kuzalisha Katiba Inayopendekezwa pasipo wajumbe wa vyama vya upinzani vinavyounda UKAWA, ikiwa ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ambaye sheria ilimtambua kama kiongozi wa timu ya uandishi wa Katiba kutoka huko, zao la Bunge Maalum lililokuwa chini ya uenyekiti wa Marehemu Samuel Sitta linakosa uhalali kuifanya iwe ndiyo mahali pa kuanzia ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Mpya.

Rasimu ya Warioba

Kwa upande mwingine, mada yangu ilijikita katika kujadili Usheria wa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, maarufu kama Rasimu ya Warioba, ambayo Watanzania wengi wamekuwa wakisikika kuipigia chapuo kuwa iwe ndiyo mahali pa kuanzia. 

Kilichowashangaza wengi ukumbini ni pale niliposema kuwa hiyo nayo haiwezi kuwa mahali halali pa kuanzia kwa vile kisheria, hii ilishapitwa na wakati baada ya kuwasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba. 

SOMA ZAIDI: Othman Masoud Ataka Haya Yazingatiwe Kwenye Mchakato wa Katiba Mpya

Ili kuiweka vema hoja yangu, nilihitimisha kwa kusema kuwa ndiyo maana ni busara kubwa kwa mchakato huu wa Katiba Mpya kuanza na kamati ndogo ya wataalam wa masuala ya Katiba ili wakafanye kazi ya kuchukua nyaraka zote hizi, kuziweka mezani na kuangalia mambo muhimu yanayokosekana ili yaingizwe ndipo tuelekee kwenye Kura ya Maamuzi, yaani referendum ili kupata Katiba Mpya. 

Kuhusu swali la je, hiyo itawezekana vipi katika hali ya sasa? Nilieleza kuwa hatua ya kwanza itapaswa kuwa ni kuandaa na kupeleka muswada wa kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Bungeni ili kuchora ramani nzima ya kazi ya Ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Mpya. 

Kwa lugha nyepesi, kalenda nzima ya nini kitaanza, na nini kitafuata, hatua kwa hatua hadi kupata Katiba Mpya, itapaswa kuandikwa katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Katiba na si vinginevyo. 

Kwa msisitizo, nilieleza kuwa hata kamati ya wataalamu, ambayo Rais alionekana yuko tayari kuiteua, hata leo isingeweza kuteuliwa bila hadidu rejea ambazo zitatokana na sheria. 

Kwa hapa tulipo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyotungwa mwaka 2011 imepitwa na wakati kiasi kwamba haiwezi kutoa mwongozo wowote katika ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Mpya unaopangwa hivi sasa.

Mwongozo makini

Nionavyo mimi, Mchakato wa Katiba Mpya unahitaji mwongozo makini wa namna ya kuukamilisha ili tupate Katiba Mpya. Wakati wa Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa, nilieleza kuwa sayansi ya utengenezaji wa Katiba Mpya inatuambia kuwa ingawa Katiba ni siasa, siasa za Katiba huongozwa na maridhiano, na siyo mashindano. 

SOMA ZAIDI: Twaha Mwaipaya: Rais Samia Hawezi Kukwepa Hitaji la Katiba Mpya

Hapa tulipofika, kuna makosa mawili yanaendelea kutendeka kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya. Kwanza, wanasiasa wanadhani kuwa Katiba ni mali yao. Hili lilikemewa sana na Rais na kwa hilo ninampongeza sana. 

Pili, na kutokana na imani ya wanasiasa kuwa Katiba Mpya ni kwa ajili yao, siasa za Katiba zinaendeshwa kwa mtindo wa kuvutana na kushindana kana kwamba kuna chama kinapaswa kishinde Katiba. Kwa uzoefu wa kidunia, mivutano haizai Katiba Mpya na ikizaa, huzaa Katiba Mbovu!

Katika mada yangu nilieleza uzoefu wangu katika kushiriki na kutazama michakato ya Katiba Mpya duniani ambapo nilisema jambo moja la hatari sana katika uandishi wa Katiba ni mgongano wa maslahi, jambo ambalo limekuwa chanzo cha mivutano isiyoisha kuhusu Katiba. 

Kwa Tanzania, vile tu kwamba wanasiasa wanaogombea waliruhusiwa kujaza ukumbi wa Bunge Maalum la Katiba kulisababisha kuhitilafiana kulikojitokeza. Panapokuwa na mgongano wa maslahi wa dhahiri, kuaminiana kunatoweka na kila mtu anahisi mwenzake anataka kutumia Katiba Mpya kufaidika. 

Katika nchi zilizofanikiwa kuandika Katiba kwa utulivu, wanasiasa wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali walizuiwa kushiriki katika vyombo na michakato inayoandika Katiba. 

SOMA ZAIDI: Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania

Kwingineko, liliwekwa sharti katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuwa yeyote anayeshiriki katika vyombo kama vile Tume, Kamati au Bunge la Katiba la nchi husika kutogombea, au kuteuliwa, katika nafasi yoyote ya uongozi wa nchi kwa kipindi cha kama miaka kumi tangu kupatikana kwa Katiba Mpya.

Elimu ya uraia

Kuhusu umuhimu na nafasi ya elimu ya uraia kuhusu Katiba Mpya, nilieleza kuwa hilo ni jambo zuri likiratibiwa vyema. 

Hata hivyo, msimamo wa Waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, kuwa kunahitajika miaka mitatu ya kuwafundisha Watanzania kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kupoteza muda na fedha za Watanzania!

Katika ziara zangu nyingi vijijini, nimewahi kuulizwa endapo kufuatia elimu hiyo ya Katiba kwa miaka mitatu, je, kila Mtanzania atatunukiwa Shahada ya Elimu ya Katiba (LLB)? Kwa maoni ya Watanzania wengi niliokutana nao, elimu ya Katiba hupatikana na kusambaa pale Mchakato wa Katiba unapokuwa unaendelea. 

SOMA ZAIDI: Ben Ishabakaki: Katiba Mpya Italeta Mageuzi Kwenye Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania

Kwa mujibu wa mwanasiasa mkongwe hapa nchini, John Momose Cheyo, akiongea mkutanoni hapo, kulitokea elimu kubwa sana ya Katiba wakati Mchakato wa Katiba Mpya ulipoanza mwaka 2011 na muda wote wa kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakati wa Mabaraza ya Katiba, Wakati wa Bunge Maalum na baada ya hapo. 

Kusema kwamba Serikali itaandaa mafunzo maalum ya kuwaingiza darasani Watanzania wote kuhusu Katiba ya 1977 ndipo Mchakato wa Katiba Mpya uendelee ni kama maigizo. 

Kwa kauli yangu, elimu ni kitu kizuri na inapaswa kuwa endelevu, lakini haiwezi kupewa kibali kusimamisha mchakato mzima wa Katiba Mpya eti tuelimishe kwanza ndipo tuendelee na hatua za Mchakato.

Mabadiliko ya sheria

Nionavyo, Shilingi bilioni tisa au kumi zinazodaiwa kutengwa na Serikali kwa ajili ya Mchakato wa Katiba ni bora zingetumika kuandaa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maamuzi.

Pia, fedha hizo zingesaidia kuundwa na kuendesha Kamati ya Wataalam itakayoratibu Mchakato mzima wa ukamilishaji Katiba Mpya na zitumike kwa zoezi la upitishaji wa Katiba kupitia Kura ya Maamuzi ya Watanzania wote. 

SOMA ZAIDI: Ismail Jussa: Sikubaliani na Hoja Kwamba Mchakato wa Katiba Mpya Uanze Baada ya 2025

Sehemu ya bajeti ya utoaji na upashanaji wa elimu ya Katiba igawiwe kwa vyombo vya habari ili viweze kujiimarisha kuhabarisha, kuchambua, na kudadavua kuhusu Mchakato wa Katiba pamoja na maudhui yake, ikiwemo Rasimu ya Warioba, Katiba Inayopendekezwa, na maoni mapya yaliyoibuka tangu mchakato usimame mwaka 2014.

Niliunga mkono, na ninarudia kuunga mkono, haja ya kufanya marekebisho madogo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuweka msingi wa Kikatiba wa Maboresho ya Kisheria yanayopangwa ili kuondoa au japo kupunguza kasoro za kiusimamizi katika Uchaguzi Mkuu ujao 2025 na ule wa Serikali za Mitaa mwakani, 2024. 

Binafsi, nimekuwa muumini wa hoja kwamba chaguzi zote za Tanzania, ukiwemo ule wa Serikali za Mitaa, zisimamiwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na siyo TAMISEMI. 

Aidha, nimekuwa nikipigia chapuo kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu yote ifanyike kwa pamoja mwaka 2025 badala ya kupoteza pesa za walipakodi kufanya ule wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka mmoja baadaye, yaani 2025. 

Kikwazo cha hili kinakuwa nini wakati hata Madiwani zamani walichaguliwa mwaka mmoja kabla ya Rais hadi ilipoonekana busara kuwa wahamishiwe kwenye Uchaguzi Mkuu?

Tuwe na huruma na pesa za Watanzania!

Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *