Msimu wa mpira wa miguu unahitimishwa wiki hii wakati klabu za Yanga na Simba zitakapokutana kwenye Uwanja wa Mkapa kumalizia kiporo chao kilichocheleweshwa na mgogoro uliodumu kwa miezi mitatu kutokana na uahirishaji mechi kiholela.
Wakati mgogoro huo ulianika dosari kubwa katika mfumo wa utawala bora na ufanyaji maamuzi, mechi iliyopangiwa tarehe mpya kutoka Machi 8, kwenda Juni 15 na hatimaye Juni 25, imebariki kile kilichozungumzwa msimu mzima: uamuzi mbovu.
Mechi ya Machi 8 iliahirishwa kimazingaombwe baada ya Simba kutishia kutocheza kwa hoja kwamba ilizuiwa kuingia uwanjani Machi 7 kufanya mazoezi ya mwisho kama kanuni zinavyotaka. Awali, Bodi ya Ligi (TPLB) ilisema mechi ingechezwa kama ilivyopangwa na waliofanya vurugu wangeshughulikiwa kwa mujibu wa kanuni.
Saa chache baadaye, TPLB ikatangaza kuahirisha mechi hiyo kwa madai kuwa kulikuwa na matukio yaliyohitaji uchunguzi ambao ungechukua muda mrefu na kwamba ilipokea ripoti ya ofisa usalama iliyoashiria vurugu, kwa hiyo ikatumia kanuni inayoipa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi mamlaka ya kuahirisha mchezo “kwa kadiri itakavyoona inafaa.”
Yanga ilipinga vikali uamuzi huo na hapo ndipo mgogoro huo ulipoanza kuchukua sura mpya kila kulipokucha, Yanga ikitaka viongozi wa TPLB wajiuzulu, huku rais wa TFF, Wallace Karia, akihoji unadhifu wa watoaji shinikizo hilo na kuwataka waende kucheza sinema zao.
Hakuna mfumo mzuri
Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mguto, naye akajikuta akitoboa siri ya sababu iliyosababisha kuahirisha mechi, akisema ni kuokoa mpira wa Tanzania kwa kuwa moja ya timu hizo mbili ingeshushwa daraja. Hayo yaliendelea hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, alipoingilia kati. Mgogoro ulionyesha hakuna mfumo mzuri wa kuwajibishana, ufanyaji maamuzi na uwajibikaji kwa viongozi.
SOMA ZAIDI: Ni Fursa kwa Klabu Kuunda Upya Bodi ya Ligi
Zaidi ilionekana kulindana ndio jambo kubwa. Haieleweki katika mkutano na Rais Samia kilizungumzwa nini, lakini kitendo cha Mguto kujiuzulu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB kusimamishwa baada ya mkutano huo kilimaanisha kulindana kungeendelea kama mkuu wa nchi asingeita pande zote kujadili sakata.
Hata hivyo, sakata hilo lilikuwa ni majumuisho ya mijadala ya muda mrefu kuhusu uendeshaji mbovu wa ligi, huku suala la uamuzi mbovu likijadiliwa takriban kila wiki baada ya mechi za raundi moja.
Ilikuwa ajabu kwamba ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe, ambaye alitaka mamlaka zichukulie kwa uzito mijadala hiyo ya uamuzi mbovu, hasa tuhuma kwamba ulinufaisha timu moja, alipelekwa Kamati ya Maadili siku chache kabla ya Machi 8, na hukumu yake kusomwa wiki chache baada ya mechi hiyo kuahirishwa.
Ungetegemea hoja ya Kamwe na mijadala ya vyombo vya habari ingewalazimisha watawala kuchukua hatua kushughhulikia mapungufu yaliyokuwa yanajadiliwa kila kukicha, mamlaka zikakaa kimya na kuridhika na adhabu ya Shilingi milioni 6 aliyotozwa Kamwe kana kwamba ingerekebisha matatizo ya uamuzi, kumbe ilijenga kiburi zaidi.
Wakati fulani zikaibuliwa hoja kwamba marefa wanaochezesha mchi za Yanga, hawachezeshi za Simba na hali kadhalika kinyume chake. Yaani, klabu hizo mbili zilikuwa na waamuzi wake zinaowataka, kitu kilichozidisha mijadala.
Kunajisiwa kwa soka
Utamu wa mchezo wa soka uliopachikwa jina la “our beautiful game (mchezo wetu mzuri)”, ulinajisiwa na uamuzi mbovu wa marefa na kusababisha ubora wa mechi, ubora wa wachezaji, mbinu za walimu na mambo mengine yasitawale ajenda kuu za mijadala ya kila baada ya mechi za raundi moja. Mijadala ikalenga zaidi uamuzi mbovu na tuhuma za kuinufaisha timu moja.
SOMA ZAIDI: TFF Ijiepusha na Chaguzi za Wilaya
Haikuwahi kutokea mamlaka za soka, Kamati ya Utendaji ya TFF wala TPLB kujitokeza na kulaani uamuzi huo mbovu na kuahidi kuutafutia ufumbuzi. Kilichofanyika ni kuiachia Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kuwachukulia hatua waamuzi waliofanya makossa, ambayo mengine yalionekana ya kudhamiria.
Adhabu zikawa mazoea na utamaduni. Marefa wanapewa mechi, wanavurunda halafu wanapotezwa. Baada ya muda wanarejea. Marefa wakazizoea. Hakuna wakati ilifikia mamlaka zikasema zifanyie uchunguzi tatizo hilo ili kujua kama ni makosa ya makusudi au ya kutojua vizuri tafsiri ya sheria au basi hata kutetea kama waamuzi walikuwa sahihi.
Ilifikia wakati refa aliongeza dakika 15 za majeruhi mwishoni mwa mchezo licha ya kutokuwepo kwa mchezaji aliyepata jeraha kubwa kama kuumia kichwani, wala kusubiri picha za marudio za Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R). Alitumia muda uliokuwa unapotezwa, kuongeza dakika hizo 15, kitu ambacho ni nadra sana labda kuwepo kwa matukio kama hayo ya kuumia kichwa, taa kuzima, V.A.R na mengine.
Hadi leo si TFF wala Bodi ya Ligi iliyoonyesha kuchukizwa na uamuzi mbovu uliotawala msimu mzima wa 2024/25 na waamuzi wanaongezeka kiburi kwa kuwa wanaona hatua hazichukuliwi. Hisia zinaibuka kwamba labda wenye mamlaka wanahusika katika dosari hizo.
Mfupa mgumu
Lakini uamuzi wa Bodi ya Ligi kuteua waamuzi kutoka Misri kuchezesha pambano la watani hao wa jadi la Juni 25, ni uthibitisho tosha kwamba chombo hicho pamoja na TFF wamethibitisha kuwa tatizo la uamuzi lipo na hawajaweza kulishughulikia na sasa vinatumia msaada kutoka nje.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Msimu wa Ligi Uwe Miezi 12 Badala ya Tisa ya Kawaida?
Hadi sasa ni mwamuzi mmoja tu, Ahmed Arajiga ndiye anaonekana kuaminiwa na asilimia kubwa ya viongozi na mashabiki wa mpira wa miguu, jambo ambalo ni aibu kwa mpira wa Tanzania.
Hata huko Misri, ambako klabu za Al Ahly na Zamalek zimekuwa zikishinikiza mechi zao zichezeshwe na waamuzi kutoka nje, bado Chama cha Soka na Ligi Kuu vimekuwa vikisita kutekeleza makubaliano hayo kwa kuwa ni aibu au ni kukiri mapungufu ya kushindwa kuzalisha waamuzi wanaoaminika.
Kwa kuwa TFF na Bodi ya Ligi wamekiri waziwazi kuwa waamuzi wetu hawaaminiki, ni muda muafaka sasa wa kuchukua hatua stahiki kumaliza tatizo hilo ili msimu ujao uwe wa kufurahia mpira mzuri unaochezwa uwanjani na si uamuzi mbovu.
Na hili tumekuwa tukilisema wakati wote kuwa kozi za kufuzu kuwa mwamuzi wa daraja fulani, hazitoshi kumfanya refa awe na kiwango kizuri. Anapata cheti tu kutokana na kujiandaa vizuri kupita majaribio lakini baada ya hapo hana programu yoyote nyingine ya kumuwezesha kumudu mechi katika mazingira magumu.
Mafunzo
Uzoefu wa muda mrefu na programu za mara kwa mara zinazobuniwa baada ya uchunguzi wa kina wa aina ya makossa yanayofanywa na waamuzi, ndio zinaweza kutupunguzia doa hili la maamuzi mabovu.
SOMA ZAIDI: Sakata la Yanga, Simba Haliwezi Kuisha Kama Kidonda. Viongozi Wawajibike
Hatua za viongozi wa juu kujitokeza na kuzungumzia tatizo hilo huwa ni salamu tosha kwa waamuzi kuanza kujitathmini kabla ya kushughulikiwa na mamlaka. Kukaa kimya kunahalalisha makossa ya kizembe na mengine ya makusudi yanayofanywa na waamuzi.
Bila ya kuyakemea, viongozi wanaonekana ni sehemu ya dosari hizo na hivyo kuibua hisia za kutoaminiwa kama hizi zilizosababisha waamuzi kutoka Misri waje kuchezesha pambano la Simba na Yanga.
Matarajio yetu ni kwamba uamuzi huu wa kubariki malalamiko ya msimu mzima kuhusu marefa, yatawazindua wahusika wafikirie nini cha kufanya kuanzia msimu ujao na hatimaye mchezo wetu pendwa urudie burudani yake safi.
Kwa kutumia Wamisri, tumeshabariki tuhuma kwamba waamuzi wetu hawaaminiki. Ni jambo zuri kujua tatizo na hivyo kinachotakiwa sasa ni kuchukua hatua.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.