Dodoma. Shauri la Kufungiwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima limeendelea leo Julai 14, 2025, Mahakama Kuu Dodoma, ambapo Mawakili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima wameomba shauri hilo kuondolewa ili kuanzishwa upya baada ya barua yenye jina sahihi la kufungiwa kwa kanisa hilo kupatikana.
Itakumbukwa kuwa barua ya kanisa hilo kufungwa ilisambaa katika mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari mnamo Juni 02, 2025. Baada ya barua hiyo kusambaa polisi walilizingira kanisa hilo na kuzuia shughuli zote za kiimani kuendelea katika kanisa hilo nchi nzima.
Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo kupitia Wakili wake Peter Kibata ilifungua kesi kwa hati ya dharura mnamo Juni 04, 2025, ikiiomba Mahakama kuondoa zuio la kufanya shughuli za kiibada wakati mchakato wa kukata rufaa ndani ya serikali unaendelea.
Shauri hili likakutana na kiunzi kipya Mahakamani, baada ya barua iliyowasilishwa kama kielelezo kuonekana iliandikwa kwa kanisa linaloitwa Glory of Christ Church badala ya Glory of Christ Tanzania Church. Ambapo Mawakili wa Serikali walikazia kuwa majina ya barua kutofanana na kanisa husika, inamaanisha hakukua na uamuzi wowote uliofanyika wa kulifungia kanisa hilo. Na pia kusisitiza barua hiyo namna ilivyopatikana kupitia mitandao ya kijamii, inaifanya iwe uzushi tu, na jambo ambalo halipo.
Kutokana na changamoto hiyo ya jina hata Mahakama chini ya jaji Juliana Masabo haikuweza kutoa ahueni yeyote au kufanya maamuzi juu ya kufungiwa kwa kanisa hilo.Suala hilo liliendelea kuzunguka katika Mahakama toka ilivyopelekwa changamoto ya msingi ikiwa ni uhalali wa barua na makosa ya barua.
Hata hivyo, Mawakili wa Kanisa hilo wameweza kupata barua nyingine, ambayo ndio wanategemea kuitumia upya.
“Tulifika Mahakamani kutokana na barua ambayo tuliipata mtandaoni. Barua ile kila mtu aliiona sisi kama mawakili tuliona ina mapungufu kwa sababu ni barua ambayo haikuwa imesainiwa. Ni barua ambayo ilikuwa haimtaji mteja wetu kwa maana ya Glory of Christ Tanzania Church, barua ilikuwa na jina ambayo ni Glory of Christ Church ambayo siyo kanisa la Ufufuo na Uzima,” ameeleza Wakili Alphonce Nachipyangu akielezea shauri hilo.
Wakili Nachipyangu anaeleza baada ya kupata barua nyingine imewabidi kuiomba Mahakama shauri kuanza upya, hasa kwa kuwa wana uhakika na barua ya sasa ilipotoka na uhalali wake.
“Wakati tuko Mahakamani tukapata barua nyingine sasa ambayo ilikua inamtaja mteja wetu vile ambavyo sisi tunamtambua, hata kama barua hiyo haikufika rasmi ofisini au sehemu rasmi ya wateja wetu. Tulifanikiwa kuipata na sisi tukajiridhisha kwamba barua hii sasa ni halali,” aliongeza Nachipyangu.
Itakumbukwa pia hata mnamo Juni 13, 2025, Wakili wa Kanisa hilo, Peter Kibatala alieleza alipokea barua kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, ikieleza kuwa barua iliyosambaa mtandaoni haikua ikitambulika.
“Suala la kwamba ile barua ya kwanza ilitoka wapi, bado sisi kama Wanasheria bado hatufahamu na bado hatujapata taarifa yeyote kutoka kwa vyombo ambavyo vinahusika,” alifafanua Wakili Nachipyangu.
Mawakili hao wanaeleza tayari wameshafanya mchakato wa kurudisha shauri hilo na wanategemea litapangiwa siku ya kusikilizwa.