Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeeleza katika ripoti yake ya mwezi Julai 2025 kuwa takribani wafanyakazi 20,000 waliokuwa wakifanya kazi kwenye sekta ya afya Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) pamoja na wafanyakazi 30,000 kwenye sekta ya afya waliokuwa wakipata malipo ya ziada kwa kazi nje ya majukumu ya kawaida wataathirika kutokana na kusitishwa kwa misada ya Shirika hilo.
Ripoti hiyo iliyotolewa mnamo Julai 03, 2025, ni ya tathmini ya maendeleo ya Tanzania chini ya program maalum ya uangalizi wa kiuchumi ya IMF ambayo imekuwepo toka mwaka 2021.
Taarifa hiyo ya IMF inaeleza: “Kusitishwa kwa misaada kutoka nje kumeiathiri sekta ya afya, kwa pande zote yaani vifaa tiba, madawa pamoja na wafanyakazi. Kwa mfano, USAID ilikuwa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 20,000 moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja (ikiwemo mashirika ya kiraia na watendaji wa jamii) waliokuwa wakihusika kwenye huduma zinazolenga magonjwa kama UKIMWI, Malaria pia uzazi wa mpango na huduma za matibabu kwa Watoto,” inaeleza ripoti hiyo.
“Pia watoa huduma za afya takribani 30,000 waliokuwa wakilipwa na USAID kutoa huduma za ziada nje ya majukumu yao ya kawaida [nao wataathirika],” imeendelea kueleza ripoti hiyo.
IMF imeonyesha Tanzania ni kati ya nchi tisa kusini mwa Jangwa la Sahara zilizopokea misaada zaidi kutoka USAID, ambapo Tanzania imepokea Dola milioni 400 (Takribani Trilioni 1) sawa na asilimia 0.5 ya pato la taifa kwa mwaka 2024. Misaada hiyo ni takribani asilimia 40 ya fedha zote zilizotumika katika sekta ya afya. Ripoti hiyo inaonesha kuwa maeneo muhimu ya sekta ya afya ambayo ni takribani asilimia 0.2 ya pato la taifa yataathirika kwa kusitishwa kwa misaada hiyo.
Kama sehemu ya hatua za awali baada ya kusitishwa kwa misaada, Tanzania ilitenga bajeti ya ziada kwa mwaka wa fedha 2024/25. Ambapo kwa mujibu wa Wizara ya Afya, takribani Shilingi Bilioni 93 zilitolewa kwa ajili ya mpango wa dharura hatua za awali.
“Kupitia uratibu wa ofisi ya Waziri Mkuu, tumefanya tathmini ya kina. Tumeangalia tulicho nacho, tulichokiagiza, tunacho tarajia kukipata. Na tayari tumeshaweka mpango mkakati wa muda mfupi, wa muda wa kati ,na wa muda mrefu,” alieleza Waziri wa Afya, Jenista Mhagama akiongea na waadishi wa Habari mnamo Aprili 25, 2025.
“Kwa dawa za Malaria na vitendanishi tunavyo vya kututosheleza mpaka mwezi wa pili mwaka 2026. Kwa dawa nyingine kama dawa za Ukimwi, na dawa nyingine tayari tumeshachukua hatua. Mpaka sasa tunao utoshelevu wa kutupelekea mpaka mwezi wa sita,” aliongeza Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama pia alieleza kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya Utumishi wanategemea kuangalia baadhi ya nafasi zilizokuwa zikiwezeshwa na misada kuweza kuwa chini ya mipango ya utekelezaji kupitia bajeti ya serikali.
“Tumekwisha kupata fedha kutoka serikalini katika mpango wetu wa muda mfupi, tulishafanya tathmini ya mahitaji yetu. Na tayari tumekwisha kupokea Bilioni 93 kutoka serikalini. Na tumekwisha kuagiza dawa za magonjwa mengine yote ambayo yalikuwa yanafadhiliwa na miradi hiyo,” alifafanua zaidi Mhagama.
Katika bajeti ya mwaka 2025/26, Tanzania imeanzisha vyanzo vipya vya mapato kukabiliana na upungufu uliojitokeza. Vyanzo hivyo vinatokana na ushuru kutoka kwenye vinywaji vya kilevi
vinavyozalishwa na vinavyoingizwa kutoka nje, mawasiliano ya kielektroniki, mafuta, madini, michezo ya Kubahatisha, ushuru kwenye magari na mashine zinazoingizwa kutoka nje ya nchi. Pamoja na tozo kwenye tiketi za treni na anga.
Serikali inategemea kukusanya Zaidi ya Bilioni 500 kupitia vyanzo hivi, ambapo asilimia 70 itapelekwa kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) na asilimia 30 itapelekwa kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.