Katika siasa, heshima ya kihistoria si kinga dhidi ya tathmini ya sasa. Freeman Mbowe, ambaye kwa miaka mingi aliinuliwa kama nembo ya mapambano ya kidemokrasia nchini Tanzania, leo anakumbana na maswali yanayohitaji majibu ya dhati kuhusu nafasi yake katika harakati za mabadiliko ya kweli.
Mnamo Januari 2025, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Uenyekiti wa Taifa wa CHADEMA dhidi ya Tundu Lissu, Mbowe alimpongeza mshindi kwa maneno mazito ya busara, akihimiza mshikamano na kuonyesha ukomavu wa kisiasa. Hata hivyo, matendo yake ya baadaye hayajaendana na maneno hayo.
Tangu wakati huo, Mbowe hajajitokeza hadharani hata mara moja kushiriki au kuonyesha mshikamano na Lissu anayekabiliwa na mashtaka mazito ya kisiasa. Wapo wanaotafsiri ukimya huu kama uhuru wa kibinafsi wa kutofautiana au kupumzika kisiasa. Hata hivyo, kwa kiongozi wa ngazi ya juu ndani ya chama kikuu cha upinzani, kutokuwapo kwa kauli ya wazi katika wakati mgumu kama huu kunazua maswali ya msingi kuhusu wajibu wa uongozi wa kisiasa.
Katika mazingira haya, hata kushiriki kwake katika shughuli za serikali au kuonekana karibu na viongozi wa serikali ya CCM kumekuwa kukionekana na baadhi ya watu kama ishara ya kujitenga polepole na msimamo wa kisiasa wa chama chake. Iwe ni juhudi za kuhimiza maridhiano au uamuzi wa binafsi, athari kwa taswira ya chama na harakati za upinzani ni kubwa.
Zaidi ya hayo, Mbowe bado ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CHADEMA — chombo chenye dhamana ya kutoa mwelekeo wa kisiasa wa chama. Hili linazua hoja pana zaidi: Je, uanachama wa mtu kwenye chombo hicho cha juu, ambaye hana tena ushiriki wa wazi au mchango wa kisiasa unaoendana na misingi ya harakati, unaendelea kuwa na uhalali wa kisiasa na kimaadili?
Wakati huu ambapo Taifa linakabiliwa na changamoto za kisiasa na kiu ya mabadiliko inaongezeka, siasa za ukimya zinaweza kuwa mzigo. Katika mazingira ya mfumo mgumu wa vyama vingi, ukimya wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele unaweza kuathiri morali ya wafuasi na kuharibu mshikamano wa ndani wa vyama.
Ni muhimu kutofautisha kati ya uhuru wa mtu binafsi na wajibu wa hadhara wa kisiasa. Wakati haki ya kimya ni halali kikatiba, wajibu wa kisiasa huambatana na uongozi wa dhamira, uwazi na uwajibikaji. Mbowe, kama mwanasiasa mwenye historia kubwa, analo jukumu la kuweka wazi msimamo wake kwa njia ambayo haitoi taswira ya mkanganyiko au usaliti wa kimya.
Kwa hiyo, hoja kuu hapa si kumhukumu Mbowe kama mtu, bali kuhoji nafasi ya kimkakati ya uongozi wa aina hii katika harakati za mabadiliko. CHADEMA na watanzania wanaoamini katika demokrasia wana kila sababu ya kuanzisha mjadala huu kwa uangalifu, busara na ujasiri.
Maoni haya ni ya mwandishi binafsi na hayaakisi msimamo rasmi wa chama chake.
John Kitoka ni Mchambuzi wa Siasa na Masuala ya Kimataifa. Vilevile ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.