Leo tunakumbuka siku muhimu na adhimu katika historia ya kisiasa ya nchi yetu. Mnamo Julai 31, 2010, wananchi wa Zanzibar walijitokeza kwa wingi kupiga kura ya maoni iliyoleta mwelekeo mpya wa kisiasa — wakipitisha kwa asilimia 66.4 mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kama njia ya kuondoa mivutano ya kisiasa na kuleta mshikamano wa kitaifa.
Kura ile ya maoni haikuwa jambo la kawaida. Ilikuwa ni matokeo ya maamuzi magumu, busara za viongozi, na ujasiri wa kisiasa uliochochewa na hamu ya kuona Zanzibar mpya — iliyotulia, iliyoungana, na yenye mwelekeo wa pamoja.
Hatua hii ilifikiwa baada ya makubaliano ya maridhiano kati ya Rais wa wakati huo, Dk Amani Abeid Karume, na Maalim Seif Sharif Hamad, waliokutana Novemba 5, 2009, huko Ikulu ya Zanzibar na kupeana mikono kama ishara ya kufungua ukurasa mpya katika siasa za Zanzibar, tukio lililoashiria mwanzo wa zama mpya.
Nyuma ya viongozi hawa walikuwepo Wazanzibari sita waliounda Kamati ya Maridhiano (maarufu kama Kamati ya Watu Sita), chini ya uenyekiti wa Mzee Hassan Nassor Moyo, Makamu wake akiwa Mheshimiwa Abubakar Khamis Bakary, na sisi wawili — Ismail Jussa na Mansoor Yussuf Himid —pamoja na Mohamed Ahmed Al Mugheiry (Eddy Riyami) na Salim Bimani — tukiwa ni wajumbe. Kamati hii iliendesha mazungumzo ya kina kwa faragha, kwa hekima na kwa moyo wa uzalendo.
Matunda ya kazi hii yalizaa Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, yaliyoweka misingi ya kikatiba ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hatua hiyo iliweka alama ya matumaini katika historia ya Zanzibar baada ya chaguzi zilizojaa mivutano na migawanyiko kwa miongo kadhaa.
Fakhari na masikitiko
Leo, tunapotimiza miaka 15 ya Maridhiano, tunajifakharisha na uamuzi ule wa mwaka 2010, lakini pia tunasikitishwa na mwelekeo unaotishia msingi ule uliojengwa na Wazanzibari kwa umoja wetu. Dalili ziko wazi kuwa dhamira ya Maridhiano imetikiswa.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Imefeli?
Viongozi wa kisiasa hawasikilizani kama zamani, nafasi ya upinzani katika mfumo wa uongozi wa nchi imekuwa finyu, na sauti za wananchi zinazotafuta haki na usawa zinapuuzwa.
Tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba 29, 2025, tunapaswa kujikumbusha kwa dhati kuwa Maridhiano yalilenga kuepusha uchaguzi wa mivutano na machafuko, na kuweka utaratibu wa haki, ushirikishwaji, na utulivu wa kudumu.
Hatujachelewa. Tunayo nafasi na fursa ya kufanikisha malengo hayo kwa kurutubisha upya dhamira ya Maridhiano na kuimarisha Umoja wa Kitaifa.
Wito
Kwa msingi huo, sisi ambao tulikuwa sehemu ya kazi hii tukufu ya kihistoria tangu awali, tunaitumia siku ya leo kutoa wito kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa kwamba tubadilike na tuoneshe ukomavu wa kisiasa kwa kuweka mbele uzalendo na maslahi ya taifa kuliko maslahi binafsi.
Pia, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) itekeleze majukumu yake kwa uwazi, uadilifu na bila upendeleo na wananchi wote wapewe fursa na haki sawa ya kushiriki kwenye shughuli za kisiasa bila vitisho, bughudha wala vikwazo.
SOMA ZAIDI: ACT-Wazalendo Isiipatie CCM Inachotaka kwa Kujitoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Vilevile, misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa iheshimiwe, ilindwe, na iimarishwe, kama ilivyokusudiwa na waasisi wa Maridhiano.
Maridhiano hayakuwa tu makubaliano ya viongozi wawili. Yalikuwa ni sawa na Azimio la Kitaifa, lililotokana na matumaini na matarajio halali ya Wazanzibari kuona mustakabali wa amani, haki, na mshikamano. Azimio hili haliwezi kudumu kwa kumbukumbu tu — linahitaji kufanyiwa kazi, kila siku, na vizazi vyote.
Wito wetu kwa vizazi vya sasa ni huu: tusirudi nyuma. Tusiruhusu hofu, ubinafsi, au chuki za kisiasa kufuta mafanikio yaliyopatikana kwa jasho na hekima ya viongozi wetu. Badala yake, tufufue tena ari ya Maridhiano, tuendeleze misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na tujenge Zanzibar yenye maridhiano ya kweli — kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.
Mansoor Yussuf Himid ni mwanasiasa mkongwe na alikuwa mjumbe wa Kamati ya Maridhiano, pamoja na kushika nyadhifa mbalimbali za Uwaziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ismail Jussa naye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Maridhiano na kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) wa Chama cha ACT Wazalendo. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.