Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi jijini hapa wameelezea sifa za wagombea wanaowataka kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 29, 2025, wengi wao wakisema wangependa kupata wagombea wanaoweka maslahi ya wanaowawakilisha mbele na kuwajali.
Kwa mujibu wa ratiba ilioyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Julai 26, 2025, Agosti 9, 2025 hadi Agosti 27 zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi wa wagombea Urais na Makamu wa Rais litafanyika, ambapo jumla ya vyama vya siasa 14 vinategemewa kushiriki zoezi hilo.
Kwa mujibu wa INEC, Agosti 14, 2025 hadi 27 itakuwa ni utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani, wakati Agosti 27, 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa Urais na Makamu wa Rais, ubunge na udiwani.
Kampeni zitafanyika kati ya Agosti 28 hadi Oktoba 28 kwa Tanzania bara, huku Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 27 zitafanyika kampeni za uchaguzi Zanzibar ili kupisha kura ya mapema visiwani humo. Kura itapigwa Oktoba 29, 2025.
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam wameieleza The Chanzo wanasubiri kwa hamu kuona wagombea watakaoteuliwa na INEC kwa ajili ya nafasi hizo, huku wakionesha maarifa ya juu kuhusu aina za wagombea wanaowataka wao kama wapiga kura.
SOMA ZAIDI: Uchaguzi Mkuu 2025: Fursa ya Kubadili Maisha ya Vijana Tanzania
Abdurahman Hamdi Hakiamriyangu, mkazi wa Tabata jijini hapa, anasema kwamba kiongozi bora ni yule anayetenda mazuri, haijalishi kiwango chake cha elimu, au amesoma nchi gani.
“Yaani, uongozi ni wewe mwenyewe, katika muonekano wako,” anasema Hakiamriyangu. “Sifa ya kiongozi aliyekuwa bora ni kufanya mazuri ambayo wananchi wanayahitaji, yaani, sifa ya kiongozi ni kiongozi anayekuwepo watu wakimhitaji.”
Kusikiliza wananchi
Kwa upande wake, Fadhili Dadi Athumani, mwenyeji wa Mtwara ambaye kwa sasa anaishi Dar es Salaam, anaamini kwamba kiongozi bora ni yule mwenye kusikiliza maoni ya wananchi baada ya kuchaguliwa kama mwakilishi wao.
“Kwenye kura za maoni wengi wanakuja na sera nyingi, lakini kutekeleza inakuwa ni suala jingine,” alibainisha mwananchi huyo. “Kwa hiyo, kupata kiongozi ambaye ataweza kutekeleza sera zake na matakwa ya wananchi, hata kama siyo kwa asilimia kubwa, lakini ajue wajibu wake ni nini kwa wananchi, ndiyo kitu bora zaidi.”
Adeya Isaya, mkazi wa Kinondoni jijini hapa, anasema sifa moja kubwa ya mwakilishi mzuri ni yule anayejali wananchi wake na kuyapa kipaumbele maslahi ya wale anaowawakilisha.
SOMA ZAIDI: Polisi: Hatuendi Vitani Lakini Tunaenda Kusimamia Usalama, Amani, Utulivu Kabla, Wakati na Baada ya Uchaguzi
Adeya alibainisha kwamba ingawaje ni ngumu kupata wawakilishi wenye sifa hizo, bado wanaweza kupatikana endapo kama kila mwananchi atatumia haki yake ya kupiga kura vizuri, akitahadharisha dhidi ya kuchagua wawakilishi kwa ushawishi wa fedha na zawadi wanazotoa.
“Usichague kiongozi kwa kulaghaiwa,” alishauri mwananchi huyo. “Kura yako wewe moja ina thamani sana, unaweza ukachagua mtu, kwa leo, kwa ajili ya Shilingi 10,000 uliyopewa, au Shilingi 15,000, ikakugharimu ndani ya miaka mitano na kuendelea.”
Kwa upande wake, Gisendi Monday, mkazi wa Mikocheni, Dar es Salaam, anatamani kuona wagombea ambao ni wawajibikaji, akiongeza: “Yaani, mgombea anayesimama na kile anachokisema, ambaye matendo yake siyo tu kwa mdomo, yaani mtu wa maneno tu bila vitendo.”
Kujitambua
Said Haasan, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam, anasema mwakilishi anayemuhitaji ni yule anayejitambua na anayetambua majukumu yake, na anayetambua kwamba yupo pale kwa ajili ya watu, si kwamba kaenda kujiweka yeye.
“[Afahamu kwamba] amesimama anawakilisha watu wengi, yaani kuna watu nyuma, ambao wanamfuata,” anasema Said. “Kwa hiyo, kule kutambua tu kwamba nipo hapa kwa ajili ya watu, mimi ni mwakilishi wa watu, inaonesha kwamba huyo ni mwakilishi mzuri.”
SOMA ZAIDI: Tume ya Taifa ya Uchaguzi Yamkabidhi Samia Fomu ya Ugombea Urais 2025
Pia, Said anasema mwakilishi mzuri ni yule anayezifahamu kero za wananchi wake, kero za mtaa wake, au maeneo yake ambayo anayaongoza.
Kwa upande wake, Rashid Muhsin Makumuli, mkazi wa Kinondoni, anasema mwakilishi anayemtaka yeye ni yule mwenye sifa ya utendaji kazi atakayewasaidia wananchi kutatua kero zao na kujiletea maendeleo.
“Atutengenezee mitaa yetu ambayo imekaa vibaya kama Kinondoni mjini, hata ukienda kuna upande wa sokoni kama humu sehemu za jamii nazo zimekaa vibaya, hapajakaa kama mjini,” alibainisha mwananchi huyo.
Beatrice Ndambo, mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam, anasema mgombea lazima awe mzalendo, kitu ambacho amedai siku hizi ni nadra kukikuta kwa mgombea.
“Kwa hiyo, awe mzalendo, awe anajituma, ni mchapakazi,” anasema Beatrice. “Lakini pia awe na wito wa kuwatumikia wananchi wake kwa sababu tukiachana na mambo ya pesa na ubadhirifu, lakini anapokuwa na wito wa kutumika, basi tuna imani atafanya kazi iliyo njema.”
Mwenye huruma
Deogratias Agustino Mogela, mkazi wa Kinondoni, anataka mwakilishi mwenye huruma, kuchapa kazi, na anayejali shida za wananchi.
SOMA ZAIDI: Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Yatoa Ufafanuzi Takwimu za Wapiga Kura
“Kabla ya kwenda bungeni, arudi kwa wananchi, kukaa nao vikao, kuona wananchi wana changamoto zipi, ili yeye sasa atakapokwenda kule bungeni, aende akawasemee wananchi,” anasema mwananchi huyo.
“Hatuhitaji mbunge kwamba tunamchagua, halafu hata kuja kwetu, kurudi kwetu, kutuuliza jamani kuna changamoto gani, haji; kwamba yeye anakwenda tu bungeni kuongea ya kwake.”
Hoja hii pia ilitiliwa mkazo na Mohammed Fabian Chilemba, mkazi wa Kinondoni, aliyebainisha kwamba kuwa karibu na wananchi ndiyo kigezo kikubwa anachotumia kuamua kama mgombea ni mzuri au hapana.
“Mwananchi anavyomuendea na kumtolea shida yake, awe anamsikiliza, awe mpenda watu, anawasikiliza watu ambao wana matatizo yao, unaona?” anasema Chilemba. “Ni kitu kama hicho mimi ndiyo napenda kupitia kwenye madiwani na hawa wabunge.”
Rushwa
Wananchi wanakiri kwamba kwa kiwango kikubwa wawakilishi wao wanakosa sifa hizi wanazozielezea. Hata hivyo, walisisitiza kwamba hiyo isiwe kigezo cha wao kutokwenda kupiga kura, bali kuwa makini kwenye upigaji kura wenyewe, ikiwemo kuepuka suala zima la rushwa.
SOMA ZAIDI: ‘Chujio Lilikuwa na Tundu Nyembamba, Mpana Mimi Sikuweza Kupenya’
Letisia Kitalima, mkazi wa Tabata, kwa mfano, anatahadharisha dhidi ya kuchagua mwakilishi anayehonga wapiga kura, akisema kwamba akishinda, mwakilishi huyo hatafanya kazi ya wananchi kwani atahisi alilipia nafasi hiyo ya uongozi.
“[Mwananchi] akichagua hivyo [kwa rushwa], ina maana kwamba matatizo yakiwa yanajitokeza, yule mtu aliyemchagua kupitia rushwa hatajishughulisha kutatua matatizo hayo, na hiyo itamaanisha kubaki na matatizo yasiyoisha,” alisema Letisia.
Hija Selemani ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia hijaselemani9@gmail.com.