The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Instagram Kuchukua Nafasi ya ‘Jamhuri ya X (Twitter)’?- Namna Mijadala ya Kisiasa Tanzania Ilivyohamia Instagram

Kufuatiwa kufungiwa kwa mtandao wa X, Instagram imeonekana kuibuka kama kiota kipya cha mijadala moto ya kisiasa, ikibadilisha namna watu walivyokuwa wakiichukulia.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la maudhui ya kisiasa, ikihusisha mijadala na kampeni, katika mtandao wa Instagram, jambo ambalo lilizoeleka zaidi katika mtandao wa X, zamani Twitter, hadi kupelekea kutambulika kama ‘Jamhuri ya Twitter.’

Hali hii imewalazimisha baadhi ya watumiaji maarufu wa mtandao wa Instagram kujikuta ni sehemu ya kampeni, au kulazimika kufanya marekebisho ya mpangilio wa kurasa zao ili kudhibiti maudhui yanayohusiana na kampeni na mijadala ya kisiasa kwa ujumla.

Kampeni mbili maarufu zinazochagiza hali hiyo ni ile ya msimamo wa chama cha upinzani CHADEMA wa No Reforms, No Election na ile ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Oktoba Tunatiki

Kampeni hizi mbili, kwa kiasi kikubwa, zimechangia kubadilika kwa mtandao huo uliozoeleka kwa sehemu kubwa kwa maudhui ya picha na video zinazohusu maisha binafsi ya watumiaji, burudani na michezo.

Miaka kadhaa nyuma ilitegemewa kwamba kampeni hizi na mijadala mikali iliyotokana nayo kuwa zaidi katika mtandao wa X ambao kimuundo ni mahususi kwa ajili ya mijadala.

SOMA ZAIDI: No Reforms, No Election Yarindima Mitandaoni

Hapa Tanzania umekuwa hivyo, kwani mijadala mingi ya kitaifa ya kisiasa kwa muda mrefu imekuwa ikianzia huko na kisha kusambaa kwenye mitandao mingine kama vile WhatsApp, Instagram, TikTok na Facebook.

Kwa hali ilivyokuwa hapo nyuma mtandao wa X, ambao watumiaji wake walijitambulisha kama ‘Jamhuri ya Twitter,’ ulipata kutambuliwa hata na viongozi wa kisiasa kama ni tanuru la mijadala la kisiasa inayokwenda mbali.

Kwa mfano, Julai 5, 2022, wakati wa hafla ya kuwapongeza timu ya mpira wa miguu ya wanawake chini ya miaka 17 ya Serengeti, Rais Samia alinukuliwa akisema: “Huko kwenye mitandao kuna Jamhuri ya Twitter.”

Wakati akitambua hali hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Tech & Media Convergency (TMC), Asha Abinallah, amesema Instagram haiwezi kuchukua nafasi ya X, na badala yake hili wimbi la maudhui ya kisiasa yanayoendelea hivi sasa linasaidia tu kuwasilisha hisia za wananchi ya mambo yanayoendelea.

Njia rahisi

“Kuna namna mtandao wa X ni rahisi kufikisha ujumbe na ajenda kwa upana wa kufikisha ile inaitwa citizen agency kunapokuwa na ajenda ya kianaharakati na ya kijamii,” amesema Asha ambaye shirika lake hilo lisilo la kiserikali linashughulika na  masuala ya kidijiti na uchechemuzi wa haki za kidijiti.

SOMA ZAIDI: Twitter: ‘Jamhuri’ Inayoitingisha Jamhuri ya Tanzania?

Hoja hii ya urahisi wa mtandao wa X imetolewa pia na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa Thomas Kibwana, ambaye yeye anaona kuwa muundo wa Instagram hauwezi kuziba nafasi ya mtandao wa X katika kuendesha mijadala mizito ya kisiasa.

“X iliundwa kwa ajili ya mijadala wakati Instagram iliundwa kwa ajili ya kutuma picha,  na mtu kusasisha taarifa binafsi za maisha,” amesema Kibwana ambaye ni mtumiaji mzuri pia wa X. 

“Kwa hiyo, unaweza kuona kwamba kwenye mfumo wa Twitter inaruhusu majadiliano, mtu anaweza akatazama yale maudhui ya mtu ‘aka-retweet,’” aliongeza Kibwana. “Sasa hivi Instagram imeleta masuala ya  ‘ku-repost,’ lakini Instagram huwezi kuandika chochote bila picha, na hata ukiandika bila picha mfumo wake hauhamasishi mijadala bali inahamasisha maoni mafupi.” 

Hata hivyo, zipo sababu mbalimbali zinazoelezwa na kuchagiza ongezeko la maudhui ya kisiasa Instagram, ikiwemo ukweli kwamba maudhui hayo yameongezeka katika kipindi Serikali imefungia mtandao wa X kwa kile ilichoeleza kuwa ni kuwepo kwa “maudhui yasiyofaa kimaadili na utamaduni wa Kitanzania.”

Njia mbadala

Mkurugenzi wa Shirika la Zaina Foundation, Zaituni Njovu, anaona kuwa hali ya kuongezeka kwa maudhui ya kisiasa Instagram inafaa kutazamwa kama mwendelezo wa wananchi kutafuta njia mbadala kila wanapozuiwa na mamlaka katika masuala yanayowahusu.

SOMA ZAIDI: Kelele Zinazoshinikiza Kufungwa kwa Mitandao ya Kijamii Zinadhihirisha Uwezo Mdogo wa Kufikiria wa Watu Wetu

“Siku zote unapozuia watu, ukiwazuia wasipite mlango A, watu wanatafuta namna ya kupita mlango B,” alisema Zaina ambaye shirika lake limejikita kwenye utetezi wa haki za kiraia za kidijiti. “Watu wengi wametafuta mtandao mbadala na hii imepelekea Instagram kuendelea kuwa maarufu Tanzania.”

Hoja hii inaendana na mtazamo wa Asha ambaye yeye anaamini kuwa kwa kiasi kikubwa kumeibuka kundi la watoa maoni ambao wamekuwa wakitumia kurasa mbalimbali zilizopo instagram kuelezea kuridhishwa na masuala katika jamii na haswa ya kisiasa.

Lakini kwa upande wake Kibwana yeye anaona kuwa ongezeko hilo la maudhui ya kisiasa Instagram limetokana na ukweli kwamba huu ni mwaka wa uchaguzi na kwamba baada ya uchaguzi mambo yatarudi kama kawaida.

Uchaguzi

“Ni mwaka wa uchaguzi kuliko suala la Twitter [X] kufungiwa,” alisema mchambuzi huyo. “Kwa hiyo, sitashangaa baada ya uchaguzi kuisha masuala ya kisiasa Instagram yatapoa na mtandao ukarudi katika mijadala yake ya kawaida.”

Takwimu za mwaka 2022 zilionesha kuwa watumiaji takribani milioni 2.6 walikuwa wanaingia kila siku kwenye mtandao wa Instagram ukilinganisha na watumiaji laki sita kwenye mtandao wa X. 

SOMA ZAIDI: Mashahidi wa Maji Washauriwa Kutumia Mitandao ya Kijamii Kuibua Masuala 

Hata hivyo, pamoja na kwamba mtandao wa Twitter ulionekana kuwa na watumiaji wachache ukilinganisha na Instagram, bado ulikuwa ndio kitovu cha mijadala ya kitaifa iliyosambaa kwenye mitandao mingine.

Kabla ya Serikali kuufungia mtandao wa X mwaka 2024 kuliibuka kampeni iliyoongozwa na viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) pamoja na baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa watetezi wa masuala mbalimbali ya Serikali, wakitaka mtandao huo ufungiwe. 

Watu wengi, hususan watumiaje, waliikosoa hatua hii kama mkakati wa kudhibiti ukosoaji mitandaoni ambao kitovu chake kilikuwa mtandao wa X. 

Hata hivyo, kukithiri kwa mijadala ya kisiasa Instagram wachambuzi wanaona itakuwa vigumu kwa mtandao huo kufungiwa kama ilivyokuwa kwa mtandao wa X. 

Haiwezi kufungiwa

“Muundo wa Instagram, hata kuongezeka kwa mjadala wa kampeni, hakuwezi kusababisha hadi ikafungwa,” amesema Asha.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Wanasiasa Wanawake Wanaikimbia Mitandao ya Kijamii?

Naye Kibwana anaona kuwa sababu zilizoelezwa na mamlaka kufungia mtandao wa X hazihusiani na mijadala ya kisiasa, na hivyo haoni uwezekano wa mtandao wa Instagram kufungiwa kama ilivyokuwa kwa mtandao wa X.

Wanaharakati wengi wa mtandaoni waliokuwa wamejikita katika mtandao wa X hivi sasa wamejikita kutuma maoni yao pia katika mtandao wa Instagram wakiungana na mwanaharakati Mange Kimambi. 

Mange, kama wafuasi wake wanavyomwita, kwa muda mrefu amekuwa akitumia mtandao huo na kujulikana zaidi kwa aina yake ya uwasilishaji hoja za utetezi na ukusoaji  kwa lugha kali na wakati mwingine ikitafsiriwa ya kuudhi. 

Mpaka kufikia Juni 2025, takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zilionesha kuwa zaidi ya kadi za mitandao ya simu na kadi za mawasiliano milioni 54 zimeweza kuingia, au kutumika, katika mtandao wa intaneti katika kipindi cha miezi mitatu, huku idadi ya simu janja zikifikia takribani milioni 25.

Habari hii imechangiwa na Victoria Kavishe ambaye ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×