Dodoma. Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango amesema kuwa Serikali itayapa kipaumbele maombi ya vifaa tiba vya magonjwa ya figo na saratani yaliyotolewa na Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH) wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kituo cha mafunzo, kituo cha Saratani na kituo cha kupandikiza figo katika hospitali hiyo siku ya Jumatano, Septemba 3, 2025.
Katika maombi yake kwa Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Prof. Abel Makubi alisema kuwa mradi wa ujenzi utakapokamilika vitahitajika vifaa tiba vya huduma za matibabu ya saratani na upandikizaji wa figo vyenye thamani ya shilingi bilioni 13.3 na bilioni 2.3 mtawaliwa.
“Napenda tu niseme kwamba kwa niaba ya Serikali nimepokea maombi hayo tutayapatia kipaumbele ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora hapa nchini,” alisema Mpango.
Ametoa wito kwa Wizara ya Afya kusimamia kwa karibu mradi huo wa ujenzi katika hospitali hiyo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati kwa vifaa tiba kusimikwa na wataalam wa kutosha wanakuwepo.
“Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha iweke utaratibu wa kuwasomesha na kuwaendeleza madaktari hadi kufikia ngazi ya ubingwa na ubobevu katika kutibu magonjwa ya saratani, upandikizaji wa figo na upandikizaji wa uboho,” alisisitiza.
Takwimu zinaonesha kumekuwepo na ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani nchini ambapo inakadiriwa kuwa wagonjwa wapya 40,000 hugunduliwa kila mwaka huku takribani watu 27,000 wenye saratani hufariki dunia.
Kwa sasa matibabu ya kibingwa ya saratani yanapatikana katika Hospitali ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyopo jijini Dar es salaam pamoja na Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.
Ujenzi wa kituo cha tiba ya saratani katika Hospital ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma itawezesha kuhudumia wananchi milioni 14 waliokuwa wanalazimika kwenda umbali mrefu zaidi kufuata huduma hizo.
Naye Prof. Makubi amesema ujenzi wa mradi wa Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Saratani wenye thamani ya shilingi bilioni 30.9 utawezesha wagonjwa wanaopata huduma za saratani nchini kutoka 5,000 hadi 8,500 kwa mwaka sambamba na kupunguza gharama ya kwenda nje ya nchi kupata matibabu.
Kuhusu huduma ya upandikizaji figo, Prof. Makubi amesema tangu hospitali ya BMH ianze kutoa huduma hiyo mwaka 2018 kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na shirika la TOKUSHIKAI hadi sasa wagonjwa 50 wamenufaika na huduma hiyo.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com.