Takribani wananchi 121 katika kijiji cha Pongwe-Kiona kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani wamelalamikia ucheleweshaji wa fidia wanayopaswa kulipwa na Serikali ili waweze kuhama kwenye eneo la makazi na mashamba yao ili kupisha shughuli za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Wakizungumza na The Chanzo, wananchi hao wamesema kuwa ni mwaka wa tatu sasa wamekuwa wakiendelea kuishi katika maeneo yao bila kufanya shughuli za msingi za kimaendeleo wakisubiri kulipwa fidia hili waondoke kwenye hayo maeneo wanaliyotakiwa kuhama.
Wananchi hao kutoka katika vitongoji vya Mpakani B na Kwedigongo kijijini hapo Pongwe-Kiona, wanasema kuwa mchakato wa kuhamishwa ulianza mwaka 2021 walipofanya mazungumzo na watu wa Jeshi, ambapo tangu mwaka 2022 walistahili kulipwa fidia kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.
The Chanzo imemtafuta Mwenyekiti wa kijiji cha Pongwe-Kiona, Rashid Ali Salum ambaye amekiri kuwa ni kweli kuna wananchi kutoka vitongoji viwili katika kijiji chake walitakiwa kulipwa fidia kwa ajili ya kupisha kwenye maeneo yao.
“Sisi kama viongozi tunafuatilia na tumekuwa tukihimizwa na Serikali ngazi ya Halmashauri kuwa tusubiri wanashughulikia,” amesema Rashid, “kwa hiyo, tunawaambia wananchi wasubiri ila kama unavyojua nao wananchi wanataka stahiki yao kwa wakati ili waendelee na maisha mengine.”
SOMA ZAIDI: ‘Maendeleo ya Watu’ Lazima Yahusishe Ulipaji Fidia wa Haraka Kwa Watanzania
Mwenyekiti huyo amesema kuwa madai ya fidia ya wananchi hao yanafika mwaka wa tatu sasa na hata walipopata taarifa kuwa kuna wenzao wa kijiji cha Mandera walishaanza kulipwa, walipofuatilia kwa upande wao waliambiwa kuwa kuna changamoto zilitokea kupelekea zoezi hilo kukwama.
“Madai yao yanafika kama mwaka wa tatu sasa, sababu walidai kuwa Jeshi wanachukua kule ng’ambo ya mto wananchi wahamishwe huko na wafanyiwe malipo ya fidia, lakini kulingana na mambo ya hapa na pale ambayo wenyewe Serikali wanayajua ndio fidia imechelewa mpaka hivi sasa.”
Zuberi Mdoe* ambaye ni mmoja wa wananchi wanaodai fidia amesema kwa sasa imekuwa kama mchezo kuahidiwa tarehe ya malipo ya fidia. Amedai kuwa suala hilo linakiuka haki zao na sheria za nchi zinazotaka mtu kulipwa fidia katika kipindi kinachotakiwa baada ya kufanyiwa tathimini.
“Mwaka 2023 tulienda Halmashauri [ya Wilaya] Chalinze, tulikuwa tunaahidiwa kuwa baada ya wiki mbili tatu itakuwa tayari, tukasema hili jambo linakuwa la kisiasa kwa sababu baadhi wenzetu wa kijiji jirani wameshalipwa,” amesema Mdoe.
Wananchi hawa wameiomba Serikali kupitia kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kupatiwa fidia ili waweze kuendelea na shughuli nyingine za kimaendeleo maeneo mapya watakayohamia.
SOMA ZAIDI: Ucheleweshaji Ulipaji Fidia Mbeya Wahofiwa Kuchochea Migogoro Kati ya Wananchi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Ramadhani Possi ameiambia The Chanzo kuwa wameshafanya mikutano na wananchi hao na wanajua kwamba malipo yao yatafanyika hivi karibuni.
“Tumefanya tathimini, na tathimini zao zimeshapitishwa, tumepeleka Wizara ya Ulinzi,” amesema Possi, “Wizara ya Ulinzi wamekwisha omba hazina hela zao zinakuja hivi karibuni.”
Kuhusu suala la fidia hiyo kuchelewa kwa muda wa miaka mitatu, Possi amesema hafahamu jambo hilo, na kusisitiza kuwa mchakato umefanyiwa kazi mwaka huu na wananchi hao watarajie kupata fidia zao hivi karibuni.
*Sio jina halisi