Jeshi la Polisi Tanzania limemtaka Humphrey Polepole kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoa maelezo na ushahidi wa tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa kupitia mitandao ya kijamii.
Katika taarifa yake Polisi imeeleza kuwa ilifungua jalada la uchunguzi na linaendelea na uchunguzi wa tuhuma mbalimbali ambazo Polepole amekuwa akizitoa kuanzia mwezi Julai mwaka huu.
Polepole ambaye amewahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Itikadi, Mafunzo na Uenezi, na mbunge wa Bunge la Tanzania, alijiuzulu nafasi ya Ubalozi wa Cuba, Julai 13, 2025 nafasi ambayo aliteuliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Tangu kujiuzulu katika nafasi hiyo ya Ubalozi, Polepole amekuwa akifanya mikutano ya wazi kwa njia ya mitandao ya kijamii akikosoa mwelekeo wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuibua tuhuma mbalimbali.
“Jeshi la Polisi mbali ya kukusanya ushahidi, limekuwa likifanya jitihada za kumpata ili aweze kutoa maelezo/ushahidi na vielelezo vitakavyothibitisha tuhuma hizo ili kuwezesha hatua zingine za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na ndivyo utaratibu wa kisheria unavyokuwa,” imeeleza taarifa ya Polisi.