Moja ya changamoto kubwa katika jamii yetu ni kwamba wafanyakazi wengi wanapopatwa na majanga kazini hawachukui hatua za haraka za kuomba fidia kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF). Hali hii husababisha familia nyingi kubaki kwenye matatizo makubwa ya kifedha, kisaikolojia na kijamii, ilhali kuna haki zao za msingi zinazolindwa na sheria.
Mara nyingi, ukosefu wa uelewa ndiyo sababu kuu inayowafanya baadhi ya wafanyakazi kushindwa kuchukua hatua za kudai fidia. Wengi wao hudhani changamoto zao zinapaswa kushughulikiwa na mwajiri pekee, bila kufahamu kwamba mfuko maalum wa kisheria upo kwa ajili ya kulinda maslahi yao.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263]. Lengo kuu la mfuko ni kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara ambao wataumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira.
Uchangiaji katika WCF unaohusisha waajiri pekee. Kila mwajiri katika sekta ya umma na binafsi anatakiwa kuchangia asilimia 0.5 ya mshahara wa kila mfanyakazi kwa mwezi. Ni muhimu kufahamu kuwa mchango huu haulipwi na mfanyakazi na wala haikatwi kutoka kwenye mshahara wake, bali hulipwa na mwajiri kwa niaba yake.
SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu ya Kuzingatia Usipoteze Mafao Yako Kutoka kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Ni mafao Yepi Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Hutoa?
WCF hulipa fidia kwa matukio ya ajali, ugonjwa au kifo yaliyotokana na kazi. Ili WCF iweze kulipa fidia, maombi ya fidia hiyo yanapaswa kuwasilishwa ndani ya kipindi kisichozidi miezi kumi na mbili (12) tokea tukio husika lilipotokea au kugundulika. Fidia zifuatazo hutolewa na WCF: –
Fidia ya Matibabu
Fao hili linajumuisha gharama zote za matibabu kwa mfanyakazi aliyeumia kazini au kuugua kutokana na kazi yake.
Huduma atakazopatiwa mfanyakazi zinajumuisha gharama za hospitali, dawa, vifaa tiba, upasuaji, uuguzi, usafiri wa gari la wagonjwa, uchunguzi na vipimo mbalimbali, pamoja na kurudi hospitali iwapo matibabu ya ufuatiliaji yanahitajika.
Pia mfuko hufidia upatikanaji wa viungo bandia, vifaa vya ukarabati wa mwili na huduma za urekebishaji ili kumsaidia mfanyakazi kurejea kwenye hali ya kawaida ya maisha na kazi. Huduma hizi hutolewa kwa kipindi cha miezi 24 tangu tukio litokee au ugonjwa kugundulika.
Fidia ya Ulemavu
Kwa ulemavu wa muda mfupi fidia inayolipwa kwa mfanyakazi ambaye amepata madhara kazini kiasi cha kumfanya ashindwe kufanya kazi kwa muda fulani lakini bado anaweza kupona. Mfuko humlipa mfanyakazi sehemu ya mshahara wake (wastani wa asilimia 70 ya mshahara) kwa kipindi chote ambacho hatoweza kufanya kazi, mpaka atakaporejea kwenye hali ya kawaida ya kiafya.
Kwa ulemavu wa kudumu mafao hulipwa kwa mfanyakazi aliyepata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali au ugonjwa wa kikazi. WCF hulipa fidia kulingana na kiwango cha ulemavu uliojitokeza.
SOMA ZAIDI: Unataka Kuomba Fao la Urithi Kutoka NSSF? Soma Hapa Kufahamu Zaidi
Kwa ulemavu wa kudumu kuanzia asilimia 1 hadi asilimia 30, mfanyakazi hulipwa fidia kwa mfumo wa mkupuo. Iwapo ulemavu utazidi asilimia 30, mfuko humlipa mfanyakazi pensheni ya kila mwezi ili kumpa uhakika wa kipato cha muda mrefu.
Malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki
Iwapo mfanyakazi atafariki kutokana na ajali au ugonjwa wa kikazi, wategemezi wake wanastahili kulipwa fidia. Malipo haya hufanywa kwa familia ya marehemu kwa lengo la kusaidia maisha yao baada ya kupoteza chanzo chao kikuu cha kipato. Malipo ya fidia hutolewa aidha kwa mfumo wa pensheni ya kila mwezi kwa wategemezi au kwa mkupuo, kulingana na taratibu zilizowekwa na mfuko.
Thomas Ndipo Mwakibuja ni mtaalamu wa hifadhi ya jamii. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thomasmwakibuja@gmail.com au +255 767 879 281.