The Chanzo imefanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Africa, Maxence Melo, kuhusiana na kufungiwa kwa mtandao wa Jamii Forums na athari zake. Unaweza kuangalia mahojiano yote hapa chini, au ukaendelea kusoma katika ukurasa huu.
Habari gani mtazamaji wa The Chanzo, tunakukaribisha tena kwenye mfululizo wa vipindi na mazungumzo ambayo tumekuwa tukiyafanya hapaThe Chanzo na wadau mbalimbali.
Leo tutakuwa na mazungumzo maalum na Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forums, jukwaa mashuhuri kabisa nchini Tanzania, ambalo Watanzania wengi wamelizoea kwa ajili ya kwenda kupata taarifa na mambo mengine mbalimbali kuhusiana yanayoendelea nchini mwao.
Lakini Jamii Forum zinajihusisha na vitu vingi zaidi kuliko tu ku-host jukwaa la watu kuzungumza kupiga soga na kupashana habari kuhusiana na yanayoendelea na tunazungumza haya katika muktadha wa zuio la siku tisini. Ambalo kama utakuwa unafuatilia, utakuwa unafahamu kwamba lilitolewa Septemba 06, [2025]. Na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ilisema kwamba inaifungia Jamii Forums kwa siku tisini.
Kwa hiyo kufahamu kuhusiana na zuio hili,limetokanaje, lina athari gani na lina maanisha nini kwa upana wake, tutakuwa na mazungumzo hapa na Maxence Melo kama nilivyomtambulisha ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forums.
Na ambaye nitakuwa nakuendeshea mazungumzo haya ni wako wa kawaida Khalifa Said, kwa niaba ya mwenzangu aliyeko nyuma ya Camera, Shafii Hamis, tunawakaribisha sana. Max shukrani sana bwana kwa kukubali mwaliko wetu.
Max: Nashukuru sana kaka khalifa.
Khalifa: Sasa labda pengine kitu cha kwanza ambacho watu, wadau wenu wangependa kufahamu tangu zuio hili la TCRA ni mnaendeleaje tangu zuio hili litangazwe? How are you holding up wanasema kwa kiingereza?
Max: Sisi tuko salama na tunaendelea na shughuli zetu nyingine kwa sababu hatukuwa tunategemea shughuli moja kwa ajili ya shughuli zetu,lakini ni kwamba kusitishwa kwa leseni ya jukwaa la Jamii Forums somehow kulikuwa na sintofahamu kubwa lakini hakujazuia maisha yetu mengine kuendelea kwa hiyo kimsingi tunaendelea vizuri,tunamshukuru Mwenyezi Mungu.
Khalifa: Ulipokea vipi hii taarifa ya TCRA kufungia Jamii Forums?
Max: Labda niseme kwamba ni kitu tulikiona kwamba kinakuja,unajua kuna dalili za mvua, wanasema ni mawingu, kulikuwa na mawingu kulikuwa na rasha rasha,halafu mvua yenyewe ikaja kunyesha. Kulikuwa na dalili za awali, mwanzoni niliambiwa kwamba naitwa nahitajika mimi wenyewe,baadaye nikaambiwa kwa sababu nilikuwa niko nje kwa matibabu nikaambiwa kwamba sasa kama haupo, tulikuwa tunakuhitaji wewe mwenyewe.
Ilikuwa ni jumatano hiyo kabla ya siku ya Alhamisi ambayo walikuwa wananihitaji nikamwambia basi naweza nikatafuta hata flight ya haraka kama kweli kuna issue binafsi wakaniambia sio binafsi sana basi tutumie hata watu na watu wangu wakaenda siku ya Alhamisi kwenda kuongea nao walikaa kikao na TCRA hii kilichokuwa dakika zisizozidi tano wakawaambia yaani hakukuwa na kitu cha ziada.
Lakini Ijumaa ambayo ilikuwa ni sikukuu ukafanyika kama uvamizi ofisini kwetu ambao niliuripoti lakini tayari kulikuwa na chanzo ambacho kilinifahamisha kwamba lengo lilikuwa ni mimi na walikwazika kwa kutokutokea kwangu.
Lakini sasa mwisho wa siku haya mambo unaelewa yanavyokwenda naelewa kwamba tuko kwenye msimu wa uchaguzi na tulijua tangu awali, tangu mwezi wa kwanza wa pili wa tatu wa mwaka 2025 kwamba tunaingia mwaka wa uchaguzi, na hata wenzetu wote tuliwafahamisha kwamba kipindi hiki hakiwezi kuwa rahisi.
Kwa hiyo nafahamu si kwetu tu lakini kwa wote walio kwenye space hii watakuwa wanaelewa kwamba kipindi hiki cha uchaguzi si kama vipindi vingine. Lakini niseme ukweli kwamba tayari kulikuwa na barua kadhaa za kutaka baadhi ya maudhui kuondolewa ndani ya mtandao wa Jamii Forums.
Ambapo tulishiriki kwenda kutoa ufafanuzi kwa nini baadhi ya maudhui hayawezi kuondoka na kwa nini utaratibu uliyotakiwa na Kamati ya Maudhui haukuwa sahihi. Lakini pia kulikuwa kuna simu nyingi kutoka kwa wenye Mamlaka, kutaka baadhi ya vitu visifanyike kama tunavyovifanya,tukikumbushwa huu ni wakati wa uchaguzi hivyo hamna sababu ya kuvifanya.
Baadhi ya vitu tunajua tunawajibu kwa Umma. Kwa hiyo mwisho wa siku unawaambia hilo hatuwezi kulifanya, Na unajua ukishakataa kuna watu unakuwa umewakwaza, kwa hiyo kulikuwa na dalili za awali na tuliziona.Lakini mwisho wa siku kikatokea kilichotokea.
Khalifa: Ni vizuri uligusia hapo kwamba walikuja kwenu kuomba msushe baadhi ya maudhui fulani swali langu ilikuwa ni kwamba,kulikuwa na jitihada zozote au mazungumzo yoyote kati yenu na TCRA kabla ya huu uamuzi? Kwa sababu unafahamu kwamba hivyo ndivyo wanafanya mara nyingi watakuja watawaambia shusheni hii, na uzuri umesema kwamba kulikuwa na hicho kitu. Lakini nilikuwa nataka kufahamu…..
Max: Labda Khalifa niseme kitu kimoja, haya mengine ninayoyasema ya awali hayana uhusiano na hicho kilichotokea. Kwa sababu maudhui ya awali niliyoyasema yanahusu watu wengine, ambao kwa kweli kwenye mashtaka au yale madai ya kutoka kwa mamlaka hayakuwa yanawahusu.
Ila kwa haya ambayo yalikuja yalitokea siku hiyo ya ijumaa, siku hiyo hiyo tukapewa masaa mawili tuwe tumeripoti TCRA, siku hiyo hiyo tukapewa dakika thelathini kila kitu kiwe kimeondoka na siku hiyo hiyo tukaadhibiwa.
Khalifa: Samahani kama labda pengine haya maudhui ambayo yaliwaweka kwenye hali hii ni maudhui gani haswa kwa sababu taarifa yake, taarifa ya Dokta Jabir, haitaji haya maudhui, inasema tu kupitia jukwaa lake na akaunti zake ilipandisha maudhui ya kupotosha umma, kukashifu na kudhalilisha serikali na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kinyume na kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka elfu mbili na… unajali kutuambia haya maudhui yalikuwa yanahusu nini kama hutojali.
Max: Sidhani kama kutokusema ni sahihi kwa sababu jukwaa ambalo limesitishiwa leseni wala siyo kurasa za mitandao ya kijamii, Jukwaa la Jamii Forums watumiaji wake ni wananchi kwa hiyo wana haki ya kufahamu, haswa maudhui hayo yalikuwa ni yapi. Tuliyaweka kwa kwa umma.
Moja ilikuwa inamhusu Rostam Aziz mfanyabiashara na mwanasiasa wa zamani ambaye aliwahi kuwa Mbunge ambapo yalikuwa ni maudhui ambayo yalisemwa na ndugu Humphrey Polepole, tuliandikiwa barua kwamba tuondoe maudhui yale,kwamba Rostam ameuziwa mgodi kwa shilingi Bilioni Tano tukaambiwa tulitakiwa kuweka mizania, kwa kuwa na maoni ya upande wa pili.
Katika hali ya kawaida sheria inavyotaka, kifungu cha ishirini cha kanuni za maudhui ya mtandaoni ukisoma vizuri,affected party ina maana hapa anakuwa ni Rostam Aziz, sasa sijajua sisi tulishindwa kuelewa kwa nini Mamlaka iwe ya kwanza kuja kwetu na tena itupe saa mbili wakati sheria inataka saa kumi na mbili.
Ukishaondoa maudhui, kwa mfano mamlaka zikikucompel au zikikulazimisha kwamba uondoe maudhui basi maudhui unatakiwa kuwa umeyaondoa ndani ya saa kumi na mbili ukishayaondoa, kwa kwa forums, hii siyo media hii ni forum, maudhui yakiondolewa you were compliant; yaani wewe ulitii sheria kama ulivyoagizwa. Lakini ni bahati mbaya kwamba pamoja na kwamba walitaka baadhi ya maudhui hayo yaondoke; moja hakukuwa na sababu ya kuyaondoa, kwa sababu kilichosemwa na Humphrey Polepole ni upande mmoja, tulitarajia upande wa pili ungejibu.
Kama utakuwa ulifuatilia kaka Khalifa, kulikuwa na kituo cha runinga ambacho kilimhoji Rostam, hao wenzetu sasa hawakuambiwa nyinyi hamkuweka mizania. Ila sisi tukaambiwa hamkuweka mizania. Sasa sisi tulibakia tunasema haa! sasa hapa sheria imetumika,kwa kuegemea upande mmoja kwa kimombo wanasema impunity. Lakini sasa wakati mwingine unayaacha haya mambo yaende maudhui ya pili….
Khalifa: Ngoja, haya mliyashusha?
Max: Hatukuyashusha, hatukuyatoa kwa sababu tulikuwa na maelezo ya wazi na tuliwaandikia TCRA kwamba haya moja yamesemwa na Humphrey Polepole. Lazima nieleweke kitu kimoja na wenye mamlaka hapa ndiyo tunapoweza kuwa tunatofautiana kila mara. Tulikuwa na kesi Mahakama ya Kisutu. Kulikuwa na Afisa wa Ardhi Halmashauri ya Mji wa Moshi, Kilimanjaro, afisa huyu alitufungulia mashtaka,akidai Jamii Forum imemchafua kwa kudai amembaka mtoto, nasema hivi kwa sababu hii kesi imeshaisha na ni vizuri ikafanyiwa reference na baadhi ya watu.
Huyu alikuwa anatulaumu kwamba sisi tunamchafua, Jamii Forum imetumika kumchafua na baadhi ya watu ambao alidai kwamba wao ndio walio-upload, Youtube content. Forums ni sehemu ambako watu wana-aggregate maudhui, ni vizuri watu waelewe, siyo kwamba sisi ndio tunaoandika ni wananchi wanaandika. Sisi kama wamiliki wa platform tunajukumu moja, maudhui yakilalamikiwa na mtu yeyote hata Khalifa akisema aah, haya maudhui siyo, kabla ya kuyaondoa tunamfahamisha mchapisha maudhui na ndio maana tuna saa kumi na mbili, kwamba kuna maudhui uliyowaweka haya si sahihi.
Lakini kama maudhui haya aliyoyaleta ameweka hadi chanzo,ameona youtube kuyaondoa ni kumwonea. Kwa sababu hata aliyeleta maudhui Jamii Forums aliyatoa kwa Huphrey Polepole kwenye account ya youtube. Kama mamlaka zilikuwa zinataka maudhui hayo yasije public sehemu ya kwenda kuyaondoa ilikuwa ni wapi, Youtube, kwa hiyo wanajulikana youtube wanapatikanaje sio sisi.
Kimsingi Jamii Forums isingeruhusu mjadala usiokuwa na chanzo wenye tuhuma ambazo hazina source, source ilikuwa iko so clear kesi yetu ya kisutu tulishinda, ukienda ukairejelea tulishinda hiyo kesi, Hakimu alisema Jamii Forums, hii ni sawa na kuzima wananchi kwamba kule maudhui yapo ila nyinyi msiongee.
Ambayo si sahihi kwa wananchi na kufanya hivi ni kuvunja Katiba ya nchi, sasa ndio hivi karibuni nilisema, wakati mwingine kwa vyombo vya habari au wanahabari ni hatari sana kuwa uko sahihi pale wenye mamlaka au walioshika mpini wakiwa wamekosea.
Lakini kimsingi kesi ile ya kisutu tulishinda na ni reference moja nzuri sana kwa wanahabari kuweza kujua kwa kuwa chanzo kilikuwepo aidha ni Meta au kokote maudhui hayo yalikuwepo kuwazuia wananchi kwamba kaeni kimya si sahihi. Ni jukumu la mamlaka kwenda kwenye platform husika kuondoa maudhui.
Ambayo inanipeleka sehemu ya pili, mahitaji ya pili ambayo mamlaka zilitaka yaondolewe yalikuwa ni maudhui yanahusiana na sijui nimuite mfanyabiashara, jamaa mmoja kutoka Zimbabwe. Kwanza nilikuwa niko Zimbabwe kwa siku takribani kumi mwezi Julai. Ambapo nilikuwa na wenzangu kadhaa tulitembelea vyombo vya habari vya umma vya uchunguzi, lakini pia tulikutana na private sector na asasi za kiraia mbalimbali. Lakini katika kuongea miongoni mwa watu ambao walitukumbusha, kwamba huyu mtu ameanza kuingiza miguu kwenu, kuweni makini naye anaitwa Wicknell Chivayo.
Sasa katika hali ambayo isiyo ya kawaida baadaye Balozi Polepole akamgusia sasa alipomgusia wananchi wakaona wakaweka kwenye platform ya Jamii Forums wanahoji. Tukaambiwa ondoeni hayo maudhui, narudia ukijerejelea kesi ambayo tulishinda Kisutu, maudhui haya aliyeyaleta kayaona kwenye mtandao wa Instagram na wa Facebook wa mhusika mwenyewe.Mamlaka zilipokuja kwetu tukawaambia mwambieni Wicknell afute kwake kimsingi hata kwetu kutakuwa hakuna cha kujadili,badala yake tukaambiwa hatuna maadili,tunachafua watu; lakini mwisho wa siku hii ni kuzima wananchi kwamba hata kama wanaona kitu wasithubutu kuongea na hata tunavyoongea mpaka sasa maudhui hayo yapo Instagram, na yako Facebook kwenye account ambayo ni verified ya Bwana Chivayo. Kwa hiyo haya ndiyo alipelekea sisi kusitishiwa leseni.
Khalifa: Asante sana Max nilikuwa nataka ufafanue kidogo na utueleze kwa undani kidogo kuhusiana na kile ulikisema Septemba 5, ambapo uliripoti kuhusiana na ule uvamizi kwenye ofisi zenu za Mikocheni. Utakumbuka kwamba Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa hakukubaliana na your characterization tunasema,alisema kwamba hakukuwa na uvamizi, lakini namnukuu: Utaratibu wa kawaida kati ya mamlaka za serikali na wadau wake Msigwa pia alisema waliofika ofisini kwako walikuwa Maafisa wa Serikali.
Max: Neno maafisa ulizingatie, naomba uzingatie neno Maafisa.
Khalifa: Walikuja kuwasilisha barua ya wito ofisini hapo, wewe Septemba 5 ile ulisema kwamba umma utaujua ukweli hivi karibuni, tunaweza kuujua ukweli?
Max: Ukweli haukuchukua hata saa ishirini na nne, kesho yake mambo yalibadilika tukajua waliofika ni kina nani. Kimsingi ngoja nikueleweshe kaka Khalifa, utaratibu uko wazi, ndiyo maana walipoleta barua rasmi siku nyingine ya kufungiwa ililetwa kistaarabu, alikuja mtu mmoja na gari la serikali na nampongeza huyo dada ali-handle vizuri alifanya kama Afisa wa Serikali. Sasa wale wengine waliokuja na gari isiyokuwa la serikali walio lazimisha kuingia ndani ya jengo bila kufuata utaratibu, kwa nguvu kwa kumlazimisha mlinzi, ni bahati mbaya hawajui kwamba kila kitu kiko recorded pale. Kwa hiyo mimi nilikuwa nasikia na nilikuwa naona, na niliwaambia nawaona mnakosea.
Khalifa: Lakini nini kilitokea exactly?
Max: Kimsingi ni kwamba waliforce entry, kuingia kwenye jengo la mtu yeyote bila kufuata utaratibu tena sikukuu haikuwa sahihi lakini pia maneno ambayo si ya kistaarabu kwa afisa yeyote au mtumishi wa umma ambaye yawezekana anaenda kwa mdau kuanza kusema aah wewe tunaweza kufanya lolote si lugha sahihi
Mambo kama haya yanapelekea watu kutokuaminiana lakini mwisho wa siku watu wangu walisema kama mnataka kuingia ingieni na nadhani walikuwa wanatarajia labda watakuta ndani ya ofisi kutakuwa kuna labda kuna kompyuta au servers sijui. Lakini waliingia, hawakukuta kitu kwa sababu mwisho wa siku sisi lile ni jengo tu, halina kitu chochote ndani yake. Lakini niseme nilikwazika kwa sababu utaratibu haukufuatwa na sivyo mamlaka zinavyofanya kazi.
Na nashauri hata wadau wengine wakija kwa mtindo huo tusikubali na ndiyo maana neno nililiwekea mabano uvamizi kwa sababu haukuwa utaratibu wa kawaida.
Khalifa: Max tuzungumze kuhusiana na athari za hili zuio la siku tisini pale mwanzo ulisema kwamba
Jamii Forums mna vitu vingine vingi mnavyofanya na kuna mambo mengine yanaenda,lakini utakubaliana na mimi kwamba lazima kutakuwa kuna athari kubwa sana.Kwa mfano athari moja ambayo naiona ni kwangu mimi kwa sababu mimi nilikuwa mtumiaji mkubwa sana wa Jamii Forums, mimi mwanahabari nataka kujua nini kinaendelea kwenye nchi yangu kwa ajili ya kuchapisha habari kwa ajili ya kuverify vitu kudhibitisha. Nilikuwa natumia sana Jamii Forums kupata habari nadhani hiyo ni athari moja.
Lakini wewe kama kama kama mtu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forums ambaye sasa mnapambana na hili zuio la siku tisini unaweza ukatuambia kwa mtazamo wako ni athari gani haswa mtakabiliana nazo kutokana na hili zuio?
Max: Kwanza niseme athari kubwa sana ambayo sisi tumeiona kwanza kumbuka leseni ya Jamii Forums kama platform ni ya kampuni inaitwa Vaper ambayo ilikuwa ina makubaliano na sisi kwenye kuendesha kazi zetu.
Kusitishwa kwa leseni yake kwa Tanzania kumesababisha kudrop kwa traffic kwenye platform kwa kiwango kikubwa, asilimia zaidi ya hamsini ilishuka kabisa. Unaona wateja wote wa Tanzania hawawezi ku-access platform. Wengine wa nje ya Tanzania wanaendelea kuaccess platform na wanaendelea kutumia kadiri wanavyoweza, lakini wateja wetu wa Tanzania wamenyimwa haki yao ambalo sisi actually ndio lengo kuu la kutumia platform kama ile. Kwa hiyo athari kubwa tunaona kwa wateja wetu wa Tanzania kunyimwa haki yao ya kikatiba ambayo wamepewa ya kupata na kusambaza taarifa bila kujali mipaka ya nchi, Ibara ya kumi na nane ya Katiba. Kibaya zaidi kuna baadhi ya wanachama wameshatutishia watatufungulia mashtaka tumewazuia isivyo halali lakini tumewaambia wana haki hatuwezi kuwazuia kwa sababu mwisho wa siku hata sisi tulikuwa tunatekeleza wajibu wetu.
Khalifa: Hawa ni members wenu?
Max: Ni wanachama wa platform na wamekuja kadhaa wakinipigia simu fungueni tutafanya lolote tutaenda Mahakamani mwisho ya siku tunawaambia mna haki ya kuenda mahakamani na unawakumbusha ni haki yao kabisa ya kikatiba. Lakini wanatakiwa kuelewa kwamba kulikuwa na tangazo la wazi la Mamlaka la kutaka tufanye hivyo lakini niseme hilo ndio tatizo kubwa tuliloliona. Lakini pili kwa wafanyakazi ambao walikuwa wako based Tanzania wakitegemea platform na kuingiza kipato ni wazi kwamba kwa siku tisini tulisitisha utendaji kazi wao. Tuliwaambia kwa kwa sasa nyie wafanyakazi mlio based Dar es Salaam au Tanzania kwa ujumla shughuli zenu kubwa ambao mlikuwa mnasimama kwenye platform zimesitishwa mpaka further notice. Kwa hivyo wamebakia wengine ndio wanaosimamia maswala yanayohusiana na the global platform. Na hapo lakini madhara yake ni kwamba kipato cha watu kimeathirika.
Khalifa: Na hapo unazungumzia kama watu wangapi? kwa sababu hilo lilikuwa ni swali langu lingine
Max: Hao ni watu takribani thelathini na wanne
Khalifa: Na pengine kwa kwa muktadha hiyo ni kama shilingi ngapi labda.
Max: Sasa we chukulia kwa wastani chukulia kama mmoja analipa shilingi milioni mbili na laki moja.
Khalifa: Ambayo sasa hiyo itasimama kwa siku hizi zote….
Max: Naam
Khalifa: Jamii Forums mtakuwa mnalipa kodi?
Max: Sisi ni walipwa kodi wakubwa, wakubwa tu kwa sababu mwisho wa siku ukishakuwa na wafanyakazi zaidi ya hao thelathini nilivyosema ina maana kuna kodi kadhaa kuna nani kadhaa mapato kadhaa ya serikali yanayolipwa.
Khalifa: Kwa hiyo wapo pia serikali itapoteza mapato fulani?
Max: Sasa sisi haya yatakuwa ni maongezi baina yetu na Mamlaka husika hasaTRA lakini nadhani wa kutakuwa kuna kuna gap kubwa kwa sababu pia kusitishwa kwa kazi za baadhi ya watu Pay as You Earn kuna workers compensation fund kuna kuna NSSF kuna mapato yataondoka.
Na hiki si kitu rafiki mimi niseme moja kati ya vitu ambavyo mi naona kama athari ya pili kubwa sana achana na mambo ya ajira tunajenga fear kwa vijana wa Kitanzania kuwa na uthubutu wa kufanya vitu kama hiki cha kwetu tunatamani watu wenye uwezo wa kufanya kitu kama hiki kikakuwa nje ya mipaka ya tanzania na kikaweza kufanya zaidi na zaidi. Badala yake tunaona Mamlaka zinadhibiti vitu vilivyotengenezwa nyumbani lakini inashindwa kudhibiti Tiktok, inashindwa kudhibiti Meta.
Maudhui yale yale yanaendelea kwingine, kwa msingi tunaua local content, tunaruhusu global platforms kuja kutawala kwetu tunaua innovation za asilia za kwetu. Kitu hiki si kizuri sana kina-paint picha mbaya kwa nchi yetu lakini kinafanya vijana wengine kukosa uthubutu huko tunakoelekea.
Khalifa: Max kwa mtu ambaye hafanyi kazi kwenye eneo unalofanya kazi wewe unaweza kusema kuna urahisi kiasi gani au ugumu kiasi gani wa kufanya kazi kwenye sector ambayo wewe unafanyia kazi?
Max: Information ecosystem au tuseme watu wote wanao deal na uchakataji wa taarifa au wanatoa access to information, changamoto kubwa ni kwamba ni vizuri kwanza tuanze na picha hii. Mwananchi katika maisha yake saa ishirini na nne anategemea taarifa ili aweze kufanya maamuzi sahihi ubora wa taarifa anazozipokea unatengeneza ubora wa maamuzi anayofanya mwananchi anapolishwa matongopori au taarifa za upande mmoja zenye kusifia au kusifu na kuabudu wengine wanasema au uchawa aidha unaegemea upinzani au unaegemea chama kilicho madarakani au unaegemea hata serikali unakuwa hujamsaidia mwananchi kuweza kufanya maamuzi.
Sahihi kwamba aidha wapinzani wanakosea au watawala wetu wanakosean a ni jukumu la wenye kusimama aidha vyombo vya habari au wenye platforms kama za kwetu ni jukumu letu kuhakikisha kwamba sehemu zetu au maudhui yanayokuwa wanalishwa wananchi yanakuwa yako sound.
Sasa ni bahati mbaya baadhi ya watu wangependa maudhui yaegemee upande fulani kwa wale ambao tunakuwa tunasema hapana hapo ndio changamoto inapoanzia tunalia na kusaga meno na wananchi mnaelewa. Si rahisi na ni bahati mbaya kuna baadhi ya watu wakiona kakitu fulani hakijafanyika kidogo tu, vijana wanasema wanakuwashia moto watakutukana watasema nini hawajui kuna simu yawezekana hata hamsini sitini zinazokuwa zikikutishia wengine wanatufuata physically wanakwambia kwamba nitashughulika na wewe.
Tangu mwezi Mei nilikuwa natishiwa maisha nafanywa nini lakini yote ye tunayaishi lakini niseme pale unapotoa aidha taarifa ambayo iko detailed ya kumsaidia mwananchi kujua hapa una unaingizwa chaka au hapa yawezekana ni wapinzani kuna wakati ya kipindi kimoja mimi nawapongeza wakati mwingine wapinzani kwa mfano kulikuwa na taarifa ambayo ya ilifanya na watu wenzetu upande wa Jamii Check ya kufact-check taarifa yaliyokuwa inamhusu Ndugu Godbless Lema kuna picha alipost kwenye mtandaohalafu bahati mbaya hatutakiwi kuegemea kumsaidia yeye tukasema kapotosha.
Kuna vijana wa CHADEMA walituvaa mmenunuliwa maneno kibao lakini bahati nzuri ilivyokutana na Lema mwenyewe akasema mmetusaidia sasa hivi tunawaambia hadi vijana wetu kabla hamjafanya hivyo mjue kunaJamii Check sitaki kuwa fact checked. Kimsingi unaona kwamba kuna watu wanaelewa na pia hata viongozi wa CCM kuna baadhi ya kero zikiwekwa wanasema mmetusaidia tunaenda tunazifix mamlaka nyingi zimejitahidi kuwa zinajibu hizo kero ndani ya Jamii Forums.
Lakini unaweza usiamini kaka yangu kuna mtu akatupigia simu kutoka Mamlaka mojawapo, wakitaka mimi nitawatajia na nitawapata details, akitaka kwa sasa ni wakati wa kampeni haya mambo ya kero za wananchi achaneni nayo kwanza mambo makubwa mama anafanya. Tukamwambia pamoja ni kwamba mama yawezekana anafanya mambo makubwa kama mnavyoona ninyi, lakini kuna kero hizi anapokuwa anapita kufanya kampeni aidha aziaddress au kabla hajaenda eneo fulani awe anajua kuna changamoto za wananchi nikaambiwa bwana we, ondoa ukishindwa tunajua namna ya kuja na ndiyo maana wamekuja.
Khalifa: Hapo mwanzo hapo umegusia kuhusu matishio ya maisha na hayo huwa yanatoka wapi?
Max: Matishio ya maisha yanatoka kwa wasiojulikana ambao sisi tunawajua na hata we kaka unawajua lakini tunaamua kuwasisitiri kwa sasa lakini wajue everything is documented yana mwisho haya. Kwa hiyo hawa wanaofanyanga hivi hawasemi moja kwa moja. Ingawa at one point kuna mmoja alinipigia simu na mpaka sasa iko kwenye rekodi akiniambia kwamba tunaweza kukufanya chochote wakati wowote watu watapiga kelele kwa mwezi mmoja miezi mitatu sita na utasahaulika.
Kauli hii huwa inanirudia lakini sidhani tunatakiwa kuwa tuna watu wenye mamlaka wenye kuwa na uwezo wa kutoa kauli kama hizi si rafiki hazikubaliki na bahati mbaya wakati anipigia hivyo simu, alivyoanza kutoa vitisho hivi niliamua kumweka loudspeaker na wenzangu wakarekodi kuhakishika ya kwamba in the near future iko siku tutaweka ushahidi mezani.
Khalifa: Hauogopi?
Max: Nimwogope nani? Namwogopa Mungu pekee
Khalifa: Nataka kukuuliza hili swali, so unaripoti polisi
Max: Unasema?
[Wote Wanacheka]
Khalifa: Hizo taarifa unaripoti Polisi?
Max: [Anacheka kidogo], Una swali lingine?
Khalifa: Nilikuwa nataka kuuliza , is it worth it? [ni jambo linalostahili kuendelea nalo]
Max: Ngoja niulize kaka yangu, The Chanzo inachokifanya kuna watu wanafika point wanasema kuna kwa nini muendelee kama mambo ni magumu hivi lakini kuna watu wanakuja wanasema kazi mnayoifanya ni nzuri na mwenyezi mungu azidi kuwabariki it’s worth it. Tuna watu wengi ambao wamerejea kwetu wanakuambia nimepata kazi baada ya Jamii forums kuweka moja mbili tatu. Tuna watu wengi wanaosema nisingeingia kwenye siasa kama nisingepata skills hizi kutoka kwa wana Jamii Forums wenzangu.
Kuna watu ambao walishakata tamaa hadi wameandika wanatamani kujiua lakini wamepata ushauri na hawajajiua. Kuna watu walikuwa na changamoto za kiafya lakini hawakujua waende hospitali gani na wamepata madaktari,pale pale wameweza kuhudumiwa.
Kwa sababu Jamii Forums siyo jukwaa la siasa peke yake kuna watu ambao walikuwa wana changamoto au tunaita kero za wananchi zipo zaidi elfu nne ambazo zimetatuliwa na wenye mamlaka. Sio kwamba watu wote walikuwa kwenye mamlaka ni wabaya, tuna watu wazuri sana serikalini, wazuri mno wengine natamani hata niwataje majina, tuna watu wazuri mno.
Na ni watendaji wanaotumia weledi mkubwa ndani ya serikali ila tuna wahuni wachache na hawazidi hata kumi. Ila wahuni hawa wakipata nafasi wanaumiza wananchi, lakini hatuwezi kukata tamaa kwa sababu ya watu wawili,watatu wanne ambao wanakuja kutumia mamlaka yao vibaya.
Kwa hiyo kwa namna moja ama nyingine niseme it’s worth it,kwa sababu tuna watumishi wa umma wazuri wanaosaidia kutatua kero za wananchi lakini wanaoleta solutions ambazo wanajifunza kutoka kwa wananchi. Lakini tuna professionals kama madaktari, wataalam wa masuala ya uchumi wanaotumia platforms kama hizi kuweza kujengea wananchi uwezo.
Naelewa changamoto kama hizi haziepukiki issue ni kwamba tutatokaje kwenye changamoto kama hizi kuendelea mbele ndiyo muhimu zaidi lakini niseme ukweli it’s worth it. Imesaidia wengi, imesaidia wanafunzi wengi vuoni ambao baadhi mikopo walikuwa wanakosa lakini baadaye wanarejea kutuambia amepata mikopo ni sehemu ya wananchi kupaza sauti na wala hatukomi.
Khalifa: Kwa hiyo maanayake unataka kusema kwamba ukilinganisha contribution ambayo Jamii Forums inafanya kwenye jamii na magumu ambayo wewe unalazimika kuyavumilia unaona it’s worth it?
Max: Asilimia mia moja yaani kama kuna changamoto nazichukua kama ni asilimia tano they are individual ingawa zinaweza ziakaathiri hadi platform lakini kwa asilimia kubwa sana imekuwa ni ya msaada kwa wadau wengi. Wananchi, taasisi mbali mbali, Asasi za kiraia zinatumia Jamii Forum kwa ajili ya kufanya uchechemuzi ni kwamba kwa kuizima hujamkomoa Max umekomoa wananchi kitu ambacho si sahihi.
Khalifa: Zungumzia athari za kuzimwa kwa Jamii Forum sasa hivi tukiwa tupo kwenye msimu wa uchaguzi kwa sababu, nadhani uchaguzi, ni suala ambalo tunaweza tukalijadili kwa upekee kulingana na attention ambayo wananchi wana-invest kwenye hilo jambo na Jamii Forum lile ni jukwaa ambalo lina taarifa nyingi sana kuna mambo mengi sana yanatokea nchini. Mtu akitaka kufahamu, mimi nakumbuka, kuna mtu alisema mimi bwana nikitaka kujua kama kitu ni cha kweli sio cha kweli na naingia Jamii Forum. Sasa hilo hilo jukwaa sasa hivi halipo unaweza kuzungumzia athari ya kufungwa kwa Jamii Forum kwenye muktadha wa uchaguzi ambao tunaenda kupiga kura Oktoba 29.
Max: Kaka yangu ni kwamba kwa kwa kiwango kikubwa wananchi wamekuwa denied haki yao ambayo wamepewa na katiba ya kupata taarifa kuchakata taarifa na kuweza kushirikishana taarifa na kwa sababu sisi tulishaona kwamba traffic ya Jamii Forum ilikuwa inafikia hadi milioni nne kwa siku na unapoona inarudi milioni mbili milioni moja na laki nane kwa siku inakupa ishara kwamba wananchi wengi wamekosa pa kwenda kuweza kuchakata maudhui,sasa kwa wale wenye mamlaka labda nitoe ushauri tu.
Kilichotokea madhara ambayo yanaenda kutokea baada ya siku tisini au hata wakiongeza ni sawa tu. Lakini ambayo yatakuja kutokea ni kwamba inapotokea information gap, someone is going to feed it, mmh sijui kama nitumia lugha gani ikitokea kuna ombwe la taarifa kuna mtu ataingia kujaza ombwe hilo. Wakati mwingine yawezekana ni unayemjua au usiyemjua mwanzoni nilisema watu wanapoingia aidha redioni magazetini au mitandaoni wanachokitafuta ni taarifa wakikuta hakuna taarifa kwenye mitandao iwe ni The Chanzo iwe ni Jamii Forums ukifungia The Chanzo, ukafungia Jamii forums ukafungia yeyote ambaye yawezekana ni critical voice wananchi wakawa wamekosa taarifa watatengeneza taarifa wananchi wakitengeneza taarifa you have no control over it.
Kwa sababu hawa hawana leseni kwa sababu wewe si ulikua unatoa leseni, unaweza ukaivuta hawa hawatakuwa na leseni mtakamata wa kwanza mtakamata wa pili mtakamata watatu lakini ukizuia wa ndani kuandika au hata kucomment wataacha ila majirani zako wataanza kuwalisha wananchi na kwa sababu kiu ya kula au hamu ya kula maudhui haitaisha wananchi wataanza kula maudhui kutoka Kenya kutoka Uganda kutoka nchi yoyote. Sasa katika ulimwengu wa sasa bidhaa inayotumika kwa ajili ya kufanya espionage sijajua kiswahili nisemeje….
Khalifa: Ujasusi
Max: Ujasusi imegeuka kwenda kwenye taarifa kulisha wananchi taarifa za kuwaaminisha kitu fulani kikifanyika mara ya kwanza ya pili ya tatu ya nne kinaaminika. Kimsingi usishangae wananchi akaanza kuona baadhi ya vitu vinavyotokea kwenye nchi fulani ndivyo vya kuanza kutumia kwetu. Kwa sababu kwetu tumeshazuiliwa na wenzetu wanajua jinsi ya kupush narrative. Labda nikurahisishie zaidi,ndiyo maana ukiingia Tiktok kuna maudhui ya nchi nyingine unaanza kuletewa kwa nguvu baadaye unayazoea na unadhani kwamba ni kawaida ndiyo maana ukiingia Instagram kuna maudhui hujayaomba, kwa sababu ya algorihim wanakusukumia baadhi ya maudhui.
Lakini kwa sababu mamlaka zetu hazitaki sisi tufanye tunawaacha hizi big tech zifanye lakini wajue in the long run katika kwa muda mrefu ujao utaonekana madhara ya kufanya vitu kama hivi.Siombei yawakute wenzetu The Chanzo au wengine wowote walio kwenye space lakini nawashauri wenye mamlaka kufikiria kwa kina kama kuna maudhui yanaweza yakawa yako mtandaoni ni ya kuondoa, kuna approaches za kufuata si kufungia chombo hata aliyekuwa waziri wa habari enzi hizo Nape Nnauye alishasisitiza kuna haja hata mwandishi akikosea tusifungie chombo kizima cha habari.
Sasa walichokifanya unafungia chombo kizima kuna majukwaa thelathini na nane ndani ya mtandao wa Jamii Forums jukwaa moja la siasa linapelekea unafunga majukwaa yote. Kwa sababu tu ulikuwa hutaki hilo jukwaa lionekane kwa wananchi si sahihi na ni uonevu ambao hautavumilika.
Khalifa: Max hapo umetoa onyo au indhari tunasema na wewe kama mi navyofahamu ni kwamba unapata fursa ya kuengage hawa wenzetu walioko kwenye nafasi za mamlaka kazi ambayo umekuwa ukifanya kwa kwa kwa muda mwingi unadhani wao wanafikiria kama hivyo?
Max: Sio kwamba hawajui, wanajua sana kaka yangu
Khalifa: Kwa mfano umezungumzia kwamba, umejaribu kuainisha athari ambazo zinaweza zikatupata kama nchi endapo kama haya mambo yataendelea, hili jambo linawa-concern wao? Kwa sababu wewe unakutana na hawa watu tunaona unapiga picha na nini,tunaona sio? unaengage hawa watu, na nilikuwa nataka kufahamu pengine kwamba kwa mtazamo wako do they care?
Max: Mkiwa mnaongea kaka yangu they seem to care, na mara nyingi mimi nachokifanya,mara nyingi wanakwambia weka kwa maandishi, wanakwambia serikali inaenda kwa maandishi. Nimeshaandika maandiko mengi, nilivyoanza kupush kwa ajili ya data protection nikaambiwa, mtuandikie kwa nini. Ndugu yangu Aidan Eyakuze atakuwa na kumbukumbu,tulifanya hivyo 2019, 2020 tuka-engage tukaandika andiko kwa nini tunadhani tunahitaji sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi na the same applies tuliwaandika watu wa Ofis ya Rais wanajua kwa nini tunadhani kuna haja ya kutenganisha Wizara ya Habari, tukawa na Wizara ya ICT inayojitegemea kwa maandishi.
Na kuelezea tuko tayari hata kutoa mchango kuhakikisha kwamba wizara ya ICT inabadilika kwa hiyo hata maongezi ya namna gani ya kumanage online content, umuhimu wa kupush kuwa na local innovation tunapush tumeongea sana na ukitoka kuongea nao kakangu wanakwambia mawazo mazuri sana, wewe ni mzalendo,ila sasa kunapokuwa na pressure ya uchaguzi kuna haja ya kuweka vitu vingine kapuni kwanza tufanye kazi.
Khalifa: Uamuzi wako wa kujuzulu nafasi yako, kwenye Tume ya Ulinzi wa taarifa binafsi unahusiana na hii hatua ya kufungiwa kwa Jamii Forums?
Max: Hapana hapana kama utaangalia ukirejea nyuma utagundua nilikuwa nimesema sikuwepo hata nchini nilitoa taarifa kwamba kiafya sikuwa niko sawa nilikuwa nashughulikia matibabu yangu.Lakini vikao nilipoona naanza kushiriki vikao vya bodi nashiriki lakini nashiriki kwa njia ya mtandao nikahisi kwamba sitoi mchango wangu inavyotakiwa. Ni bahati mbaya maamuzi yakawa yamegongana na maamuzi ya TCRA, lakini haikuwa na uhusiano wowote,kwa sababu ile ni mamlaka nyingine na hii ni mamlaka nyingine.
Lakini kimsingi nilidhani kwamba ni uungwana nikaachia mtu mwingine ambaye ni mzalendo, ambaye anaweza akaingia pale akatoa mchango wake. Lakini nilijitahidi kuwa wazi kwa sababu kuna watu walikuwa wanapotosha kwamba labda ni nimekula bingo nitakuwa nakula posho. Sikuwahi kupokea posho yoyote gharama zangu za ushiriki zilikuwa zinalipwa na taasisi yangu kwa sababu tulikuwa tunafanya kitu tunachokiamini. Lakini niliona kwamba tunakoelekea, kushiriki kwa njia ya mtandao, wakati mwingine mtandao unakuwa hauko sawa lakini nadhani pia maoni yanayotolewa kwa njia mtandao si sawa na unayoyatoa ukiwa pale physically. Nikadhani ni uungwana kukaa kando.
Khalifa: Maana wengine sisi tunasema aah umeikasirikia serikali
Max: Serikali haikasirikiwi mzee, kuna serikali ,kuna watu. Kimsingi serikali inatambua kwamba kama una mchango wanaujua, lakini nia ni njema na sababu ya kupush kuwepo sheria hiyo inajulikana nikitamani mtu mwingine atakayepewa aelewe haswa lengo la uwepo wa sheria na umuhimu wa kulinda taarifa binafsi za watu.
Khalifa: Jamii Forums mnaenda kuchukua hatua gani, kuhusiana na hii hatua ya TCRA: Mnaenda kufanya maombi?, mtaenda Mahakamani au mtaitisha maandamano, mtachukuwa hatua gani?
Max: Niseme Oktoba tunatiki au nisemeje?
[Wote wanacheka]
Max: Hatua ambazo tunaweza kuzichukua kwanza ni tulipewa siku ishirini na moja kwamba tunaweza kwenda kukata rufaa
Khalifa: Kukata rufaa TCRA?
Max: Ndio maelekezo ya TCRA. Lakini kabla hujakata rufaa lazima ujiulize unakata rufaa kwa nani kwa mantiki hiyo kuna vikao vinaendelea vya wenzangu huko kwa sababu mimi sipo bado niko nje ya nchi kwa ajili ya kuangalia afya yangu lakini nimejitahidi kuhakikisha kwamba nawaelewesha what really happened, na kushauri pale ninapoweza.
Lakini wanafanya vikao kuhakikisha wanachukua maamuzi yaliyo sahihi. Kwa sababu siku ni ishirini na moja na muda bado upo naamini kabla siku ishirini na moja, utaona kitakachotokea. Kama tutakata rufaa tutaenda kwa umma tutawaelezea kwa nini tunakata rufaa na tutakuwa tuko wazi kabisa. Nadhani inatakiwa kuwa ni mchakato wa wazi ili wananchi wajue kwa nini tulichukua hatua hizo.
Khalifa: Max unadhani ni sawa kwa mamlaka ya serikali kwa mfano kama TCRA kuchukua uamuzi wa kufungia chombo cha habari bila kuwepo kwa amri yoyote ya Mahakama.
Max: Wametengeneza mazingira hayo ambapo kwanza hata TCRA watakwambia sio sisi, kwa sababu hata ukiangalia barua ya ya kutufungia, kanuni za maudhui mtandaoni zimetengenezwa na Wizara na TCRA iko chini ya wizara nyingine, kamati ya maudhui iko chini ya Wizara ya Habari. TCRA iko chini ya Wizara ya ICT kuna kanamna fulani hivi,na hata barua ya kutufungia ingawa imetoka TCRA lakini waliosaini ni watu wa kamati ya maudhui.
Kuna kamfumo ambako kuweza kukabiliana nako ni changamoto lakini niseme sidhani na ndiyo maana wanakwambia una haki ya kwenda kukata rufaa. Kabla hujaenda kukata rufaa na wewe ujipime kuna haja ya kukata rufaa au umwachie Mwenyezi Mungu kuna wakati unaweza ukamwachia Mwenyezi Mungu au ukauachia umma wenyewe.Kwa sababu Watanzania siyo wajinga, wakati mwingine ni kuamua kwa busara.
Kwa hiyo sisi unajaribu kuhakikisha kwamba tunaiacha busara ichukue nafasi yake. Lakini niseme katiba ya nchi ndiyo sheria namba moja sheria yoyote kanuni yoyote itakayokuja kutungwa ikiwa inaendana tofauti na ibara ya kumi na nane ya Katiba hiyo ni sheria mfu ni sheria kandamizi ni sheria isiyofaa yawezekana leo sheria hii ukaitumia ukiwa una mamlaka utaenjoy kwa sababu uko upande wa mamlaka siku ukitoka tutakukumbusha at one point ulitufanyia hivyo.
Khalifa: Ni mabadiliko gani unadhani yanapaswa kufanyika kwenye space ambayo wewe unafanyia kazi kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika vizuri zaidi?
Max: Moja mamlaka nadhani tu zikae na wadau usipotembelea wadau likely mnakuwa mnafanya maamuzi kwa sababu mnafikiria upande mmoja. Nawapongeza wasemaji wa serikali waliopita watatu, walitutembelea wakati huo hata Wizara ya ICT haijaanza. Walitutembelea kuweza kuelewa, walikuwa wamejazwa upepo na mtu anakuja anaanza kuongea vitu fulani unamsikiliza unaambia mkuu
hebu tulia kwanza sasa tukuambie nini kinatokea. Wakishasikiliza anakuambia hao wenzangu walinipoteza.
Kwa hiyo cha kwanza tembelea wadau washirikishe sikiliza sio uende kuongea, ukisikiliza kwa sababu mtu akienda The Chanzo akakaa na Khalifa na wenzake akawasikiliza atakuja kubaini kwa nini Khalifa na wenzake wanafanya kazi kwa utaratibu huu na wanafanyaje na kama ana cha kushauri atashauri.
Pili kwa kuwa kuna sheria au kanuni au taratibu mamlaka nadhani na zenyewe ziwe fair wafuate sheria inavyoelekeza badala ya mamlaka at one point kuwa ndiyo inayotangulia kabla mtu hajalalamika inasema tuliona sisi wenyewe. Sisi tuliwauliza sasa kama mmeona ninyi kwanini msimwambie yeye akaja aje yeye tukishindwana sisi ndio aje kwenu tukishindwana kwenu tukutane mahakamani hakuna anayekataa kwenda mahakamani kwa hiyo nadhani kama zinawekwa sheria na taratibu basi zifuatwe na pande zote impunity si kitu sahihi.
Tatu ruhusuni innovation ubunifu ndani ya nchi nchi za wenzetu ukienda na bahati mbaya nimezunguka nchi nyingi nimeenda Ujerumani ninaenda Marekani nimeenda Uchina nimeenda Urusi nimeenda mataifa mengi kujifunza kwa wenzetu wanasaidiaje local solutions yaani zile bunifu za ndani wanazisaidiaaje ziweze kukuwa na kwenda zaidi sisi kwetu tunapambana na zile za ndani unazinyongelea mbali unatamani hata mtu mpige risasi umteke, sio sawa.
Wenzetu hata kama hawakubaliani na mtu fulani lakini wanajitahidi kumvusha mipaka na kusimama naye kwetu wanakunyonga kwa kamba tena wanaangalia kama ushakufa au bado unapumua si sawa tusaidie kuimarisha local innovations. Si kwa sababu zimeegemea aidha kwa serikali au kwa upande wa chama kinachokuwa kiko madarakani leo yawezekana sehemu yawezekana keshokutwa ni ACT yeyote atakayekuwa madarakani, lakini hamasisha local innovations shirikiana nao kama wana makosa waelekeze sio kupambana nao,waelekeze waonyeshe namna gani lakini tengeneza namna ambazo ajira zitakuwa zinazalishwa kila inapowezekana.
Nisisitize kwamba hakuna mtanzania mwenye nia mbaya na nchi yake siyo kweli na haimaanishi unapokuwa aidha umepewa madaraka au umeshika nafasi serikalini we ndio mzalendo namba moja si kweli Khalifa, Max na wengine ambao wako kwenye space kwa namna moja ama nyingine wanatengeneza ajira kwa vijana wenzao au wanatengeneza ajira kwa ajili ya Watanzania lakini wanafundisha wengine namna ya kuwa innovative.
Tena sisi wengine tunatamani aje mwingine awe bora zaidi yetu lakini sasa kwa bahati mbaya au nzuri sijui kama ni nzuri kwa wengine wanadhani kwamba ukiwa na mawazo tofauti na walio kwenye mamlaka wewe ni adui, hapana. Alternative thinking is not a crime, sidhani kwamba yeyote anayefikiria tofauti na yule aliye madarakani au na mwenye mamlaka anakuwa ana nia ovu ni vizuri kuweza kukaa na wadau kukaa na wadau ni kitu muhimu sana na namwambia ndugu yangu Gerson Msigwa tembelea wadau, utakuja kugundua mengi tofauti na unavyodhania.
Lakini pia wale ambao ni watumishi wa umma niwashukuru ambao mmekuwa mkitupa ushirikiano mara zote lakini niwatie moyo kwamba mnachokifanya kusupport hizi initiatives ambazo wakati mwingine zinaweza zikaonekana kwa wengine ni mbaya msiache kufanya hivyo.
Kwa sababu ni kwa kufanya hivi tunatengeneza kizazi kijacho ambacho kina uthubutu lakini kinachoweza kuja na solutions mbadala zinazo endana na dunia ya kwetu. Sisi ndio tumezindua AI ya kiswahili hata tulikuwa tujafika popote tukala za uso. Si jambo zuri sana kutokea kwa Tanzania yetu. Pale ofisi zetu za Nairobi, nilikuwa Nairobi hivi majuzi ofisi zetu za Nairobi na Zimbabwe tuna ofisi na Kampala zinaendelea na kazi.
Lakini sijisikii vizuri kwamba siku moja tulazimike tuseme makao makuu yetu yako nchi jirani natamani tuhamasishe kujenga maongezi baina ya pande zote mbili tukubali kukutokubaliana haiwezekani watu wote tuongee lugha moja ni ngumu. Lakini pale unapo ona kwa wale wenye mamlaka unapoona watu tunakuwa tunakataa jambo fulani au tunalisema sana, sisi sio wapumbavu au sisi sio wajinga kuna kitu tunadhani hakiko sawa. Kama ukubaliani nasi tuite tukae meza moja tuambie kwa nini kitu fulani tunadhani hakiko sahihi.
Khalifa: Neno la mwisho kwa wadau wa Jamii Forums kama mimi hapa ambaye sasa hivi nikifungua Jamii Forums nakutana na ujumbe Ndugu….
Max: Kwa wapenzi wetu wa Jamii Forums moja tunawashukuru sana kwa miaka yote mliokuwa na sisi zaidi ya miaka ishirini wengine wako na sisi hatujawatupa lakini mnajua ni changamoto zimetokea tunajitahidi kuendelea kutoa huduma lakini tunawaahidi baada ya siku zilizowekwa na mamlaka kuweka zuio hilo kama tutakata rufaa ikafunguliwa mapema itakuwa ni jambo jema lakini hatuna namna zaidi ya kuwa compliant au kuhakikisha kwamba tunaendana na sheria za sehemu tunazozihudumia lakini tunawaomba muendelee kutuunga mkono kama ambavyo mmetuunga mkono wa daima lakini mwendelee kutumia huduma zetu pale huduma zitakaporejea.
Lakini wale wanaofuatilia kurasa zetu za mitandao ya kijamii tulisitisha sio kwa sababu tulisitishiwa leseni tulisitisha kwa sababu tunatakia tujipange tuje na approach tofauti kwa sababu hatudhani kwamba tunaweza kupata mabadiliko chanya kwa kuendelea kutumia mbinu zile zile kwa hiyo hatujasitisha huduma kwenye mitandao mingine ya kijamii kwa sababu ya sitisho la forum bali tumelitisha kwa sababu tunadhani tunatakiwa tukae chini tujitafakari na tuje na njia mbadala.
Kwa wadau wa sekta ya habari wale mnaofurahia kwamba labda yamewakuta kina Max, leo kwangu kesho kwako; wale ambao mmeungana nasi mnaoendea kutuombea heri tuko pamoja na nyinyi tutaungana nanyi kwa njia nyingine kwa kisha kwamba na sisi tunawasaidia na nyinyi muweze kufanya vizuri hata kutuzidi sisi. kwa sababu hatudhani kwamba we are the best we believe tunaweza utengeneza wengine wakawa bora zaidi yetu kwa sababu tunania njema kwa ajili ya nchi yetu lakini tunania njema kwa ajili ya space nzima.
Kwa Asasi za Kiraia zilizotoa tamko kwa niaba yetu tunawashukuru kuna wadau wengi ambao alioanza kupiga kelele kwa niaba yetu viongozi wa dini asanteni sana maaskofu ambao mliongea kwa niaba yetu wengine walinitafuta asanteni sana wachungaji, asanteni sana mashehe.
Kuna mashehe walinitafuta nawashukuru sana wazee wangu, mnakumbuka mkutano wetu kule Zanzibar,tuliyaongea haya na yametokea na yalitarajiwa lakini kwa upande wa maaskofu wapande zote wakatoliki na madheebu mengine mnakumbuka vikao vyetu niliwaambia kwamba tunatarajia moja mbili tatu na kimetokea nawashukuru lakini kwamba mmeendea kututia moyo.
kwa Asasi za kiraia hii ambao nimewataja asanteni sana kwa kuongea kwa niaba yetu lakini kwa wadau wa sekta nzima mmeandika X, nimeona, mmeandika Instagram, nimeona mmeandika kila sehemu kututetea tunawashukuru sana kwa sababu wakati mwingine unahitaji kujua kwamba kuna watu wanaona unayoyapitia na wako na wewe. Nawashukuru sana na mwenyezi Mungu awabariki
Khalifa: Asante sana, inatosha utanifanya nilie
[Max anacheka]
Khalifa: Shukrani sana bwana na kila la heri kwenye mapambano