Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Wolfgang Pisa, ametangaza marufuku juu ya watumishi wa kanisa hilo kushiriki katika kampeni za siasa. Akiongea leo Septemba 25, 2025, katika misa ya kuadhimisha miaka mia moja ya seminari ya Kipalapala-Tabora, Pisa ameeleza marufuku hiyo ipo kwa mujibu wa kanuni za Kanisa hilo lenye miaka 2000 duniani.
“Mtawa, Padri au kiongozi yeyote wa kanisa hapaswi kushiriki katika kampeni zozote za siasa. Wala hapaswi kutambulishwa na chama chochote kwa kuvalishwa gwanda lolote la chama chochote cha siasa au kiashiria chochote. Ni Marufuku Mapadri, marufuku kwa watawa, marufuku kwenu nyinyi waseminaristi kuonekana kwenye kampeni ya siasa, marufuku kubwa,” alieleza Askofu Pisa.
Tamko hili linakuja ikiwa siku moja baada ya picha iliyosambaa ikiwaonesha Masista wa kituo cha Masista wa Mtakatifu Benedicto wa Msaada wa Kikristo Afrika kutoka Ndanda, wakionekana katika mkutano wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi, huko Masasi, Mtwara wakiwa wameshikilia machapisho mbalimbali ya kampeni.

Katika hotuba yake Pisa ameonya juu ya kuvaa mavazi kama kofia au T-sheti za vyama vya siasa. Na kuwasihi wadau wa siasa kusubiri muda wa kupiga kura ikiwa wanaamini kuna wafuasi wao miongoni mwa watumishi wa kanisa hilo.
“Na ni vibaya watu kurubuni na kuhadaa watu, hao wahusika wakipita kwenye nyumba za kanisa, wakipita kwenye convet za kanisa kuwahadaa na kuwarubuni hiyo ni dhambi haipaswi,” alieleza Pisa.
“Haipaswi kumrubuni mtu kitu ambacho hafahamu, unamkamata Mnovisi, unamkamata Mtawa mmoja Mklara ambaye hata redio hasikilizi, taarifa ya Habari hasomi, unamsomba tu, halafu unamuelekeza, unamfanyisha ile doctrination, hiyo ni dhambi na ni makosa makubwa, marufuku,” alisisitiza zaidi.