Siku hizi tunaelezwa sana mambo ya kuupata utajiri kwa uharisi. Lakini hatuambiwi tufanyeje endapo, kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, tutaupoteza utajiri huo. Basi, Sayyid Abdallah Bin Ali Bin Nasiri anauongoza moyo uweze kuendelea kuishi baada ya kupoteza kila kitu. Chapa ya Inkishafi ninayorejea hapa ni ile iliyohaririwa na M.M. Mulokozi kwenye Tenzi Tatu za Kale (1999).
Kati ya miaka ya 1800 na 1802, Bin Nasiri anauandika utenzi huu wakati wa anguko la pili la miji ya pwani ya Afrika Mashariki baada ya kuja kwa watawala wa Omani. Pate, alipoIshi Bin Nasri, kama ilivyo Mombasa, Lamu na Kilwa, ilishadhoofika kwa kuja kwa Wareno kati ya karne ya 16 na 18.
Maanguko haya mawili yalisababisha miji hii kupoteza biashara zilizotegemea Afrika ya kati, kusini, mashariki pamoja na uwanda wote wa bahari ya Hindi.
Japo Bin Nasiri anatusimulia anguko la Pate, hanakili matukio kama yaliyoongozana kutokea. Anatusimulia kama safari ya maisha ya mwanadamu kwa mwili na roho. Hivyo, utenzi wake unaanza kwa kuutuliza moyo ili usihadaike na mambo ya dunia. Kwa maana anavyoonesha kwenye beti zinafuata ustawi wa Pate ulivyokuwa kabla ya maanguko.
Mji ulikuwa na dola, viongozi wa kidini na watu matajiri. Walikuwa na makasri, wake, watumwa na anasa za kila aina. Lakini anguko lilipokuja, walipoteza kila kitu, ikiwemo maisha yao. Miji yao ikageuka kuwa makazi ya wanyama, wakati miili yao ikioza chini ya ardhi.
SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu
Hivyo, Bin Nasiri anahitimisha kwa kuukumbusha tena moyo kutenda yaliyo mema kwa maana baada ya kifo ni wenye matendo mema tu ndio wataishi maisha mazuri.
Ni rahisi kuona kuwa utenzi huu ni wa kidini, wa Kiislamu. Tena mwandishi akatumia herufi zilizo kwenye lugha ya kiarabu kama a’iin, khaa na haa yenye sakna. Lakini, kwa muktadha wa Bin Nasiri, Kiarabu na Uislamu, si vitu ambavyo angeviepuka. Bin Nasiri alizaliwa kwenye familia ya wasomi wa dini na hata ushairi wao wa kale zaidi ukielezea Uislamu kwa Kiswahili, kama Utenzi wa Hamziyya, 1652.
Historia ya Waswahili
Ni kweli kama anavyotuongoza mhariri wa chapisho hili la Inkshafi M. M. Mulokozi, tunapaswa kuangalia utenzi huu kama sehemu ya historia ya Waswahili kwa sababu unatokana na matukio halisi ya nyakati za kuja kwa watawala wa Omani.
Hivyo, Inkishafi inapoanza na kuisha kwa kumtaja Mungu na kuomba rehema zake sio mbali sana na ambayo sisi kwa sasa tunasema Asalaam Aleykum kwa sababu ni sehemu ya utamaduni.
Utenzi huu nashauri usome taratibu sana, ikiwezekana kwa sauti. Beti zake zimesheheni matini mengi. Ni utenzi mzuri sana kwa wenye kutafuta taamuli ya maisha. Binadamu, kama anavyotuonesha Bin Nasri, anaweza akaishi maisha yenye ufahari, hata akawa na wajakazi wa kumkanda na kumpepea usiku.
READ MORE: Kwaheri Amir Sudi Andanenga, Tanzania Itakukumbuka Daima
Inakuwaje siku akiwa amelala na vibao kaburini, wakati mbwa tu asiyekuwa na mali wala kazi anabaki hai? Na ndio maana haswa ya kichwa cha utenzi: Inkishafi, neno la Kiarabu linalotafsiriwa kama zinduko au ufunuo.
Ukisoma haraka haraka unaweza usione utajiri wa watu wa Pate wakati huo. Bin Nasiri anaelezea majumba, mapambo, samani na anasa zilizokuwa zikifanyika humo. Hadhi, vyeo na watu maarufu wa nyakati hizo. Hutuwezi kubaki tunalalama kwamba hatuijui historia ya Waafrika nje ya utawala wa Wazungu wakati Bin Nasri ametupa upenyo la kuchungulia na kuiona Afrika ya zamani.
Uwezo wa mtunzi
Nadhani uwezo wa Bin Nasiri kuelezea hali ya nyakati zile kwa kuongea na moyo wake, bila kuelezea tukio moja baada ya lingine, ni sababu kwa nini utenzi huu ni maarufu sana. Inkishafi husoma, hunukuliwa na imepigwa chapa nyingi.
Natumaini wahariri wa chapa za siku za mbeleni wataweza pia kuangalia uwezekano wa kurekebisha, ama kutoa ufafanuzi, wa baadhi maandishi ili kumuongoza msomaji. Kwa mfano, kwenye ubeti wa 58, neno tunaloliita giza limeandikwa jiza.
Nadhani ni kutonaka na mwandishi mwenyewe kuchagua herufi Jiim (Ja) badala ya Gha’iin (Gha) ya Kiarabu. Je, herufi ‘ga’ ya Kiswahili ilianikwaje kwa Ajami (Hati inayotumia msingi wa uandishi wa Kiarabu, lakini ikiwa na herufi ambazo haziko kwenye matamshi ya kiarabu kama ‘pa’)?
Katika mambo aliyoyaona Bin Nasiri ni jinsi wanawake walivyokuwa sehemu ya utajiri. Anaandika kwenye ubeti wa 63:
“Aimi! Wawapi wake zidiwa,
Zituzo za mato, wasiwa ngowa?
Wasiriye wote kuwa mahuwa,
Sasa ni waushi waliushiye.”
Yaani Pate palikuwa na wanawake wazuri mno, lakini nao wameota mbawa na kutoweka! Inavyoonekana wanawake, kama walivyokuwa watumwa, walikuwa wanakuwa wengi kulingana na hadhi ya mwenye nao. Hivyo, kama uzuri wa Pate ulivyopotea na sura nzuri za wanawake hawa waliowastarehesha mabwana zao ulipotea.
SOMA ZAIDI: Zainab Burhani Anavyouchora Mchango Chanya wa Baba Katika Malezi ya Watoto Kwenye ‘Mali ya Maskini’
Inskishafi ni kitabu kidogo tu chenye beti 79. Tangu nilipokisoma kwa mara ya kwanza, na hata sasa, ni kama vile kinakuita tena ukisome. Kwa mtu anayependa kujifunza ushairi wa Kiswahili, hiki ni kitabu kizuri kwa sababu lugha yake ni ya ufupisho haswa.
Kwa wengine wanaopenda kujifunza kuhusu mambo ya kale ya Waswahili, maneno ya Bin Nasiri yanakusaidia kuiona ni nini mabwana na watwana walifanya ndani ya makasri kabla ya karne ya 20.
Kwa wanaotafuta taamuli, jinsi Bin Nasiri anavyokiwasilisha kifo na kaburi, inakusaidia kuitafuta thamani ya maisha ya mwanadamu. Binafsi naishi na ubeti huu:
65. Moyo, Taadabu, sipeketeke,
Ata ya jauri, haki ushike,
Wendo wachokoka nawe wokoke,
Moto wa Jahimu usikutwaye.
Diana Kamara hupenda kujitambulisha kama binti wa Adria Kokulengya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia dianakkamara@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.