Dodoma. Jeshi la Polisi Tanzania limesema pamoja na kuendelea na uchunguzi wa tuhuma za kutekwa kwa Humphrey Polepole zilizotolewa Oktoba 6, 2025 na aliyejitambulisha kuwa ndugu yake aitwaye Augustino Polepole, Jeshi hilo limesema linamtafuta ndugu huyo wa Polepole ili aweze kuwapatia ushirikiano.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Oktoba 7, 2025, imeeleza kuwa Polisi inamtaka Augustino Polepole aweze kutoa maelezo yake na uthibitisho wa shutuma alizotoa kwamba kuna afisa wa Jeshi la Polisi amehusika katika kumteka ndugu yake.
Mapema siku ya Jumatatu, Oktoba 6, 2025 ilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha Augustino Polepole ambaye alijitambulisha kuwa ni kaka wa Humphrey Polepole akieleza kuwa nyumba aliyokuwa anaishi Humphrey Polepole iliyopo Ununio jijini Dar es Salaam ilivamiwa usiku wa kuamkia siku hiyo na ndugu yake aliyekuwa akiishi humo kutekwa.
Sambamba na hilo Jeshi la Polisi limesema kwamba wanamhitaji Augustino ili kuthibitisha kuwa Humphrey Polepole alikuwa ni mpangaji ama mkazi wa nyumba inayotajwa kuwa utekaji huo umefanyika.
Humphrey Polepole ambaye amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi na Cuba, hivi karibuni baada ya kujiuzulu nafasi ya ubalozi nchini Cuba Julai 13, 2025 alikuwa mkosoaji mkubwa wa mwenendo wa Serikali na chama chake cha CCM.
Katika ukosoaji wake Polepole aliibua tuhuma mbalimbali ambazo Jeshi la Polisi liliwahi kumpa wito Septemba 15, 2025 wa kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoa maelezo na ushahidi wa tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa kupitia mitandao ya kijamii.