The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Utendi wa Fumo Liyongo: Kama Watawala Hawataacha Kutengeneza Hila, Nasi Tuendelee Kubuni Mbinu za Ukombozi

Simulizi ya kale ya Fumo Liyongo ina mafunzo mengi kwa muktadha wetu wa sasa, ikiwemo ukweli kwamba tabia za watawala hufanana, na hivyo wanaopambania haki hutumia mbinu ambazo watawala huzidharau

subscribe to our newsletter!

Nasikia kuna makampuni huko Marekani hutengeneza maudhui ya filamu yanayotokana na mashujaa tu. Fumo Liyongo angewafaaa sana kwa kuwa ni mtu mwenye nguvu za mwili, werevu na anapendwa sana na watu. 

Pata picha watoto wetu wanaanza kuimba na wazazi wanasimulia tena kwa Kiswahili kisa cha Fumo Liyongo. Hii inawezekana kwa sababu japo ni simulizi ya kale, Fumo Liyongo imekataa kupotea katika utamaduni wa Waswahili. Hivyo ni wakati wetu kujinasibisha na shujaa aliyeishi kwenye tendi za Kiswahili kwa karne nyingi.  

Kuna simulizi nyingi za Fumo Liyongo. Simulizi kuu zaidi iliyo katika maandishi ni ya 1531. Nakala ya utendi ninayotumia hapa ni mmoja kati ya Tenzi Tatu za Kale zilizohaririwa na M.M. Mulokozi (1999). Iliandikwa mwaka 1913 na mwenyeji wa Lamu, Kenya, Muhamad Aboubakar bin omari al-Bakry, almaarufu Muhamad Kijumwa. 

Ni muhimu kuzingatia muktadha wa kihistoria anaotoa mhariri M.M. Mulokozi ili kuelewa vizuri kwa nini tenzi za Fumo Liyongo ziliendelea kuhifadhiwa hadi karne ya 20 wakati kisa chenyewe kikisadikiwa kutokea kati ya karne ya 13 na 14.

Kama ilivyokawaida ya tendi, mhusika mkuu Fumo Liyongo ni mtu mwenye nguvu na maarifa mengi. Kwa sababu hiyo anajulikana na kupendwa na watu. Mfalme wa Pate naye anajua ushujaa wa Fumo Liyongo. 

SOMA ZAIDI: Inkishafi ya Sayyid Abdallah Bin Ali Bin Nasiri: Kutoka Utajiri Hadi Ufukara

Wagala walipomtembelea, wakamuomba Mfalme wa Pate kuwa Fumo Liyongo aoe mwanamke wa kwao ili waipate mbegu yake (ubeti wa 41). Lakini umaarufu wa Fumo Liyongo ulipoendelea japo aliondoka kwenda kuishi kwa Wagala, Mfalme anaogopa kuwa atafika mahali aje kutwaa kiti chake. 

Ili kujilinda, Mfalme anabuni hila nyingi na kutafuta washirika wengi ili kumuua Fumo Liyongo. Kila Fumo Liyongo alipoweza kukikwepa kifo ndivyo Mfalme alivyopandisha dau kwa atakayeweza kumuua.  

Kuelewa historia

Utendi huu ni muhimu kwetu katika kuelewa historia ya pwani ya Afrika ya Mashariki. Unatujengea taswira ya maisha ya Waswahili kwa wakati huo. Miji ilitawaliwa na wafalme, lakini wakazi wa mijini na vijijini waliendelea kuwa na mahusiano. 

Ndiyo maana Fumo Liyongo aliamua kukimbilia mwituni ambapo jamii za Wasanye na Wadahalo wanampokea na kuishi naye mpaka wanapojaribu kumuua kwa ahadi ya riale mia moja kutoka kwa Mfalme. 

Uhusiano wa mjini na kijijini unaendelea kuwa sehemu ya historia yetu ambapo wale wa mijini hutegemea kazi za vibarua na biashara; walio wa vijijini hutegemea kilimo na shughuli nyingine.

SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu

Japo pamekuwa na mjadala mkali siku za nyuma juu ya nani haswa ni Mswahili, hata katika utenzi huu tunaona kuwa watu wanaoishi nje ya Pate huitwa kwa makabila. Japo watu hawa sio Waswahili bado ni sehemu ya maisha ya miji ya Waswahili. 

Hivyo, Waswahili ni watu wenye asili ya miji ya Pwani ya Afrika ya Mashariki. Ni mazalia ya Waafrika wa mijini na vjijini; na Waafrika na watu wa mabara mengine. Kama tunavyoona nyakati za Fumo Liyongo watu wakioana kutoka pande zote: mijini na vijijini.

Tabia za watawala

Pili, tabia za watawala hufanana, na hivyo wanaopambania haki hutumia mbinu ambazo wanazidharau. Kuna wakati Mfalme alifanikiwa kumfunga gerezani Fumo Liyongo. Mama yake Fumo Liyongo alikuwa akimtumia chakula. 

Siku moja askari alipoona Fumo Liyongo ameletewa mkate wa wishwa hakuukagua. Na tena akaudhihaki kuwa ni chakula cha watwana. Kumbe Liyongo alimuambia kijakazi Saada amuambie mama yake aandae mkate wa wishwa na ndani yake aweke tupa. 

Liyongo akatumia tupa kufungua na kutoroka. Jambo la kujifunza kwa Fumo Liyongo ni kwamba kama watawala hawataacha kutafuta njia za kutukandamiza nasi hatupaswi kuancha kutafuta mianya ya kudhoofisha mipango yao.  

Wanawake kama nyenzo

Tatu, wanawake kutumika kama nyenzo za kutuliza ugomvi wa kisiasa ni jambo la tangu kale. Nionavyo mimi, Mfalme alimuoza Fumo Liyongo binti wa Wagala ili kumpunguzia umaarufu. 

SOMA ZAIDI: Kwaheri Amir Sudi Andanenga, Tanzania Itakukumbuka Daima 

Lakini ushujaa na sifa za Fumo Liyongo zilibaki pale pale. Mbeleni Mfalme anaamua kumuahidi mtoto wa kiume wa Fumo Liyongo cheo cha uwaziri na kumuoza binti yake endapo atafanikiwa kumuua baba yake. 

Ukiachilia mbali kuwa mke wa Liyongo na binti Mfalme hawakushirikishwa kwenye maamuzi ya hizo ndoa, ndoa zenyewe bado zisingetosha kumaliza hofu ya Mfalme. Hivyo, wanawake hawa wanatumiwa kama vidhibiti vya muda. 

Watawala wakiona hatari imezidi wanaendeleza umwagaji damu bila kujali kwa kiasi gani watawaumiza wanawake wanaojikuta wako katikati ya vita za wazazi na wakwe zao.

Matumizi ya lugha

Unapoanza kusoma utendi wa Liyongo unasita na kugugumia kwa sababu ya lugha iliyotumika. Kiswahili cha Lamu mwanzoni mwa karne ya 20, huku kimeandikwa kwa ufupisho ili kiwe ushairi. 

Lakini kwa sababu unajua Kiswahili unavyoendelea tenzi zinazofuata ndivyo utakavyoweza kusoma kwa urahisi zaidi. Labda siku moja na wewe utaweza kusimulia utendi wa Fumo Liyongo kama sio kwa tenzi basi sanaa ya namna nyingine kama hadithi au michoro.

SOMA ZAIDI: Zainab Burhani Anavyouchora Mchango Chanya wa Baba Katika Malezi ya Watoto Kwenye ‘Mali ya Maskini’

Imekuwa ngumu kuthibitisha taarifa za Fumo Liyongo, ikiwemo wakati alioishi.  Pia, haujulikani hasa kama alikuwa tu mhusika au mtu halisi. Lakini tuna uhakika ufundi wa Waswahili katika utunzi wa visa. 

Kisa cha maisha ya Fumo Liyongo kinasisimua sana kiasi kwamba washairi wa nyakati tofauti wamekiandika kwa mitindo tofauti. Kisiasa, utendi huu huwatia moyo watu wenye mapambano. 

Kama watawala hawataacha kutengeneza hila, nasi tuendelee kubuni mbinu za ukombozi. Tukifa kwa mwili, tuishi kwa tenzi kuchochea vizazi vijavyo kama Fumo Liyongo.   

Diana Kamara hupenda kujitambulisha kama binti wa Adria Kokulengya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia dianakkamara@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×