The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Mfumo Dume Bado Watajwa Kuwa Kikwazo Wanawake Kushiriki Kwenye Uongozi

Hali hii ya kutokuwepo na uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume kwenye nafasi mbalimbali za uongozi imeelezwa na wadau mbalimbali kuwa chimbuko lake ni mfumo dume uliopo licha ya sera, sheria na maazimio mbalimbali ya kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia ambayo Tanzania na Zanzibar zimeridhia.

subscribe to our newsletter!

Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa upande wa Zanzibar  inaonyesha kuwa idadi ya wanawake ni wengi zaidi kuliko wanaume. Japo wanawake ni asilimia 51.6 ya wakazi wote 1,889,773 waliohesabiwa, uwiano huu hauendani na uhalisia uliopo kwenye nafasi za uongozi.

Takwimu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka 2024 zinaonyesha wanawake wanaoshikilia nafasi za uongozi kitaifa ni asilimia 30 pekee, ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 70. Hii inapingana na lengo la kufikia uwakilishi sawa wa 50 kwa 50 kama lilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP 2021/2026).

Hali hii ya kutokuwepo na uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume kwenye nafasi mbalimbali za uongozi imeelezwa na wadau mbalimbali kuwa chimbuko lake ni mfumo dume uliopo licha ya sera, sheria na maazimio mbalimbali ya kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia ambayo Tanzania na Zanzibar zimeridhia.

Hii inaweza kuonekana dhahiri kipindi cha uchaguzi ambapo wanawake wachache zaidi ndiyo wamekuwa wakijitokeza kugombea nafasi mbalimbali kama vile za uwakilishi kwenye majimbo, na badala yake wamekuwa wakienda kwenye vyombo vya maamuzi kama Baraza au Bunge kwa mgongo wa viti maalum.

Hali hii imenisukuma kuzungumza na baadhi ya wanawake ambao wamewahi kujitosa katika chaguzi mbalimbali kuelewa ni nini hasa kinachokwamisha wanawake wengi kujitokeza kugombea katika nafasi hizo ili kushiriki kwenye uongozi.

Mazungumzo yalianza na Bi. Asha Suleiman, 38, mwanachama wa chama cha ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar na mmoja wa wanawake wachache waliothubutu kugombea nafasi ya uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

SOMA ZAIDI: ZEC Yapunguza Gharama za Fomu za Uchaguzi kwa Wanawake Kuhamasisha Ushiriki

Asha anasema alipojitosa kugombea nafasi ya udiwani katika moja ya wadi alikumbana na ukinzani mkubwa kutoka kwa wanaume na wanawake wenzake kwa misingi ya mfumo dume ndani na nje ya chama chake.

“Nilipogombea nafasi ya udiwani kwa mara ya kwanza, sikukutana na changamoto ya wapinzani pekee, bali nilipambana na dhana iliyojengeka kwenye jamii kwamba siasa ni kazi ya wanaume. Wengi waliniambia, wanawake ni wa jikoni, siyo wa majukwaani,” amesema Asha.

Lakini yeye anaamini kuwa kila mwanamke ana uwezo wa kuongoza, lakini anaona changamoto kubwa ni vikwazo vinavyotokana na mila, mitazamo ya kijinsia, na mgawanyo wa majukumu ya kifamilia unaowafanya wanawake wengi wasijione katika nafasi ya kushiriki kwenye siasa.

“Mfumo dume bado ni tatizo katika jamii na  ndani ya vyama vya siasa ambapo mara nyingine unagombea katika uchaguzi wa ndani  wajumbe wanakupitisha anakuja mtu anakwambia  usigombee nafasi hiyo hutoiweza mwachie mwanaume agombee,” amesisitiza Asha.

Kwa upande Bi. Bahati  Ali Rashid mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mgombea udiwani wadi ya Kihinani jimbo la Mfenesini  Unguja katika uchaguzi wa mwaka huu, amekiri  kwamba bado nafasi za uongozi zimejaa wanaume hivyo kutaka wagombea wanawake wanaojitokeza waungwe mkono.

 ‘’Wanawake tuko wengi, takribani nusu ya wanachama wa chama chetu ni wanawake, lakini unapokuja kwenye maamuzi makubwa, bado mfumo dume unatawala,” amesema Bahati.

 Amewataka wanawake mwaka  huu wa uchaguzi kuwaunga mkono wanawake wenzao ambao wamepitishwa na vyama vyao  vya siasa, kugombea nafasi mbali mbali  za uongozi  ili washinde na kuongeza ushiriki wao kwenye nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi. 

Changamoto hii ya mfumo dume imewaibua wadau wa usawa wa kijinsia ambao wanatahadharisha endapo hali hii itaendelea ni ngumu sana kufikia usawa wa kijinsia.

Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ), ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya uchechemuzi juu ya masuala ya usawa wa kijisnia na kuhimiza ushiriki wa wananwake kwenye nafasi za uongozi kusisitiza kuwa ili kuweza kufikia 50 kwa 50 kwenye uongozi inahitajika kukataa mfumo dume.

 “Iwapo tutakubali mfumo dume ututawale, hatutafika,” amesisitiza Dkt Mzuri.

Sheria  ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992  ambayo imeongezwa  Kifungu cha 10C, inavitaka vyama  vyote kuwa na sera ya jinsia na kuhakikisha wanawake wanashiriki ipasavyo katika siasa na uongozi. 

SOMA ZAIDI: Je, Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024 Utaongeza Wanawake Wenyeviti wa Vijiji?

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Zanzibar, Mohamed Ali Ahmed, amesema kifungu hicho ni jitihada muhimu ya kuvunja mfumo dume ndani ya vyama vya siasa nchini Tanzania. 

“Vyama sasa  vinatakiwa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa na wanaume,” amesema Mohamed.

Hata hivyo, bado changamoto kubwa ni utekelezaji wa sera na sheria hizo ambapo Machavu Bakar Juma ambaye anakaimu nafasi ya  Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa ACT-Wazalendo anaona  changamoto kubwa ni namna vyama vyenyewe vinavyoendeshwa.

 “Vyama vingi bado vinaongozwa kwa misingi ya mfumo dume. Wanawake wanapopewa nafasi mara nyingi huwaza heshima au kusaidia kampeni, badala ya kusimama kwenye nafasi za maamuzi,” amesema Machavu.

Maryam Nassor ni mwandishi Zenjipost kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho anapatikana kupitia baruapepe maryamnassorsuleiman781@gmail.com.  

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×