Sina umahiri wa msamiati unaotosheleza kuelezea hisia tulizonazo Watanzania sasa hivi. Vilio, machozi na nyuso zilizojaa huzuni, hasira na hofu vyaweza kuwa ni viashiria tu vya hisia hizo. Sisi ni hodari wa kutumia tabasamu na lugha laini kuficha hisia zetu za kweli zinazotutafuna ndani kwa ndani.
Tanzania yetu ambayo tumejivunia kwa miongo mingi kama kisiwa cha amani sasa imebeba doa zito. Uzalendo wetu unatutaka kurejesha na kuimarisha misingi ya amani: Amani ya kudumu kama zao la matumaini, haki, ukweli na uaminifu na sio amani ya muda mfupi itokanayo na nguvu, hofu na ahadi hewa.
Kilichotokea kuanzia mchana wa Oktoba 29 mpaka Novemba 3, 2025, hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi yetu. Ni tukio lililogeuza nchi nzima kuwa uwanja wa taharuki, simanzi, na machozi.
Oktoba 29 ilikuwa siku ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Kulikuwa na tetesi za uwezekano wa kutokea vurugu siku hiyo. Kwa miezi na wiki kadhaa, vyombo vya ulinzi na usalama vilitahadharisha kuhusu uwezekano wa fujo hizo na kwamba vimejipanga kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia alikuwa mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), aliwaahidi Watanzania uchaguzi shwari akisema hakutakuwa na “nywinywi wala nywinywinywi”: yaani, hakuna atakayebughudhiwa kwa kunyukuliwa (bara twasema kufinywa) akitoka kwenda kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kidemokrasia wa kupiga kura na watu wahamasishane kujitokeza kutiki.
Siku ilianza kama kawaida ya siku za chaguzi Tanzania. Watu wachache hujitokeza mapema asubuhi na wengine wakingoja yapite masaa kadhaa kisha waelekee vituoni kupiga kura. Waliojihimu kupiga kura wakaji-selfisha, na kurusha katika mitandao ya kijamii kuhamasisha wengine wajitokeze pia. Hali ilionekana kuwa shwari kwa masaa machache ya asubuhi.
Lakini kuanzia mida ya saa 5 asubuhi hali ilibadilika ghafla. Watu walielekea barabarani badala ya vituo vya kupigia kura. Picha mjongeo na mnato za mwanzo hazikuonesha vurugu. Zilionesha wananchi wakitembea, wakitabasamu na kuimba nyimbo za kizalendo kando ya magari ya jeshi. Kumbe panapofuka moshi, moto u-karibu.
SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Matamanio Yao Binafsi Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Vurugu zilizuka kama moto wa kifuu na kusambaa kama moto wa mabua shambani kipindi cha kiangazi. Nimeelezwa jinsi wasimamizi wa uchaguzi katika baadhi ya vituo walivyovua fulana na kofia zinazowatambulisha na kukimbia. Askari wachache vituoni pia walitoa sare zao na kugeuka askari kanzu kwa hofu ya usalama wao.
Watu wakaongezeka barabarani, tabasamu zikafutika na badala yake hasira na jazba zikawa dhahiri nyusoni pao, mayowe, mbinje na vilio vilisikika, mioto ya magurudumu na magodoro ikawaka, moshi mzito wa kupofusha ukatanda, wananchi wengi, wakiwemo askari, walijeruhiwa na wengine waliuawa, mali na miundombinu vikaharibiwa pia.
Vurugu zikaendelea kwa masaa kadhaa, watu wakikimbia huku na kule kwa miguu na vipando mbalimbali wakijaribu kurejea majumbani kuwa karibu na wapendwa wao. Siyo wote waliofanikiwa kurejea makwao siku hiyo au kesho yake.
Hatimaye mida ya jioni barabara nyingi zikawa tupu, maduka yakafungwa, lakini mioto ikiendelea kuangaza baadhi ya mitaa, moshi wa kutoa kamasi ukitapakaa, na mirindimo ya mabomu ya machozi na milio ya risasi ikisikika kwa ukaribu kuliko ngurumo za radi za masika.
Baadhi ya watoto walishangilia wakidhani ni baruti zipigwazo wakati wa sherehe za Diwali au mwaka mpya. Watoto wakaanza kuchanganyikiwa kuona wazazi wakiharakisha kufunga milango, kuhimizana kujificha ndani na wakiongea kwenye simu kwa sauti zilosheheni wasiwasi mkubwa.
Jua lilipozama hata kunguru hawakuweza kutulia kwenye matawi ya miti au nyaya za umeme kama ilivyo kawaida yao: waliruka kila mara risasi na mabomu ya machozi yaliporindima. Nikatambua asili ya ile methali ya kunguru mwoga hukimbiza ubawa wake. Ngedere wa maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nao hawakuachwa salama: mirindimo iliwachanganya wasijue pa kukimbilia. Alimuradi hekaheka na tafrani kwa binadamu, ndege na wanyama!
Tangazo likatoka la nchi kufungwa (curfew), na ikafungiwa kwa siku sita. Hatukutakiwa kutoka usiku, na hata mchana kuingia mitaani ilihitaji sababu maalum na kitambulisho. Polisi na wanajeshi wakaijaza mitaa: wakisimama imara kwenye vizuizi vilivyoibuka kama uyoga na wakizunguka mitaani kwa macho ya umakini na mitutu mikononi. Magari ambayo hatukuzoea kuyaona yakapita barabarani mara kwa mara.
Ving’ora vya magari ya wagonjwa (ambulance) vikisikika kama muziki wa huzuni masikioni pa wengi: tukijiuliza kama yamebeba majeruhi au maiti. Milio ya mabomu ya machozi na risasi ikaendelea kurindima kwenye vitongoji. Mitetemo yake “sabwufa” (wub-woofer speakers) zinangoja.
Mioyo ikitudunda kwa kasi. Matumbo yakitucheza: chango si chango, kuhara si kuhara. Tukihema juu juu kama kuku alokimbizwa mchana wa jua kali. Taharuki! Jakamoyo! Patashika nguo kuchanika ikawa sio msemo tu bali uhalisia kwa siku sita mfululizo.
Mitandao ya intaneti ilizimwa. Mawasiliano yakawa magumu. Watu hawakuweza kuwasiliana na wapendwa wao; hofu ikatawala. Taifa zima likawa gizani—si giza la umeme, bali giza la kiakili na kiroho. Watoto walilia kwa hofu na kuchanganyikiwa. Wazazi waliongea kwenye simu kwa hofu kuu.
Vijana walijificha. Tulitetemeka kila milio ya risasi na mabomu iliposikika karibu kabisa na makazi yetu. Vyakula na maji vikaanza kutuishia majumbani. Taarifa sahihi na zisizokuwa sahihi zilisambazwa haraka sana. Sintofahamu na taharuki ikatawala kama wingu zito juu ya bahari tulivu.
Tafrani hii imesababisha majeraha mengi na makubwa. Majeraha haya si ya mwili pekee. Ni ya nafsi. Ni ya roho ya taifa. Na hayataisha mapema. Tutahitaji uponyaji wa kweli—uponyaji wa busara, wa ukweli, na wa uadilifu. Si ule uponyaji wa “funika kombe mwanaharamu apite.”
Angalau sasa hali imeanza kutulia — shukran kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi. Wakati tukipangusa machozi kwa viganja na kuanza kushusha pumzi, ni wajibu wetu kukaa kitako na kuanza kutafakari mustakabali wetu kwa siku zijazo. Nini kimetokea? Tumefikaje hapa? Tunatokaje hapa? Twenda wapi?
Mchawi ni nani?
Wakati taifa linatafuta nani wa kulaumiwa, tunapaswa kujiuliza: hali hii iliibukaje? Haya hayakutokea kwa bahati mbaya wala kwa ghafla. Yamekuwa yakitokota taratibu, kama moto unaofukuta chini ya majivu. Ni matokeo ya miaka mingi ya raia kujihisi kutelekezwa, ahadi zisizotekelezwa, na vijana waliokata tamaa. Mchawi ni ahadi hewa. Mganga ni kutimiza ahadi.
SOMA ZAIDI: Wananchi Wachambua Usahihi Zawadi za Wagombea Kipindi cha Uchaguzi
Tanzania ya leo ina kizazi kikubwa cha vijana kilichojaa elimu lakini hakina ajira. Kizazi kinachoshuhudia viongozi wakijitapa kwa kupaa kwa uchumi wakati wao wakihangaika kupata mlo mmoja. Ni ukweli usiopingika kuwa viashiria kama pato la taifa (GDP) na thamani ya bidhaa tunazouza nje imeongezeka maradufu kuashiria kukua kwa uchumi wetu. Lakini ni ukweli usiopingika pia kuwa bado kuna Watanzania wengi sana wanaelemewa na kuongezeka kwa gharama za maisha.
Vijana wengi wa bodaboda, kwa mfano, humeza Panadol na kunywa energy drink kukabiliana na njaa wakiwa katika shughuli zao. Tumesikia visa mkasa pia vya watoto kunyweshwa pombe, au piritoni, ili walale wasilie kwa njaa mpaka muda wa mlo mmoja utakapowadia. Wananchi, hasa vijana, wanaambiwa kila mara “subirini,” wakati njaa na hasira vimekuwa sehemu ya maisha yao.
Wanasiasa wetu wamegeuza ahadi kuwa mtindo wa kisiasa, si mkataba wa utumishi na uadilifu. Kila uchaguzi unapokuja, vijana wanapewa tena ahadi tamu kama asali. Wanaahidiwa ajira, mikopo, huduma bora za afya, maji na umeme. Mwananchi anapoahidiwa maendeleo, halafu akaachwa katika umaskini uleule, anajiona ametupwa. Vijana wanapoona kila nafasi ya ajira ikihusishwa na upendeleo au hongo, wanakata tamaa. Ndipo vijana wanapouliza: “Kwa nini tuliamini?”
Waangalizi wa uchaguzi kutoka SADC na Umoja wa Afrika (AU) wamesema uchaguzi wetu haukukidhi sifa za chaguzi za kidemokrasia. Matokeo hayalingani na matakwa ya wananchi. Hapo ndipo vijana wanapohisi kuwa hata njia ya amani ya kupaza sauti—kupiga kura—imefungwa. Hata tukiwaambia “subirini uchaguzi ujao,” wanauliza: “kwa nini tuamini tena?”
Na pale ambapo matumaini yanapokufa, hasira huzaliwa. Wakati mwingine, fujo siyo chaguo—ni kilio cha watu wasiokuwa na njia nyingine ya kusikika. Tukumbuke ya kwamba: “fukara hana ustaarabu.”
Je, tuwalaumu ‘wachochezi’?
Vurugu sio namna nzuri ya mawasiliano. Vurugu hutumika pale lugha inaposhindwa. Hakuna mshindi katika vurugu. Kila tukio la vurugu, viongozi husema kwa haraka na ukali “wachochezi wanawachonganisha wananchi na Serikali yao pendwa.” Nionavyo mimi, sio rahisi kumchochea mtu mwenye furaha na tumbo lililoshiba. Hata akichochewa, atacheka na kupuuza.
Vurugu hizi hazingeweza kutokea kama Watanzania wangekuwa na imani na Serikali yao, kama wangeona matokeo ya juhudi zao, kama wangehisi sauti zao zinasikika na kama Serikali yao ingekuwa na unyenyekevu wa kukiri pale inaposhindwa kushughulikia kero zao.
SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Sifa za Mwakilishi Wanayemtaka Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Tumeshuhudia mara kadhaa namna ambavyo ziara za kusikiliza wananchi zinavyosaidia kurejesha imani baina ya wananchi na Serikali yao. Serikali isichoke kufanya mazungumzo na wananchi wake.
Amani ya kweli haiwezi kulindwa kwa makaripio, virungu, bunduki na mabomu ya machozi. Inalindwa kwa imani, haki na uaminifu. Serikali ikitumia nguvu badala ya busara, inazalisha chuki na visasi, si utulivu. Na chuki hiyo ndiyo mbegu ya vurugu.
Nguvu ni moto uwashao moto. Katika hotuba ya uapisho, Rais Samia amekumbusha umuhimu wa kutopimana mabavu. Watanzania hatuna desturi ya kupimana mabavu. Tujiulize, tumefikaje hapa?
Wakati wa vurugu, tuliona risasi na mabomu ya machozi vikutumika kukabiliana na walioitwa wafanya fujo. Tuliona vijana, watoto na wanawake wakikimbia, wengine wakianguka, wengine wakipoteza maisha. Wengine wakipigwa risasi miguuni, wengine mabegani.
Na wengine—ambao hawakuwa hata sehemu ya maandamano—walijeruhiwa na kupoteza maisha wakiwa majumbani kwao au maeneo yao ya biashara. Ni dhahiri matumizi ya nguvu yanasababisha hasara kubwa.
Matumizi ya nguvu hayawezi kuleta amani. Yanazidisha maumivu. Kila risasi iliyolia imeacha jeraha lisiloonekana, ndani ya mioyo ya maelfu. Kila aliyeshuhudia majeruhi, au vifo, hawezi kusahau. Vijana walioona marafiki zao wakianguka hawataamini tena kauli za “amani na utulivu.”
Leo tunaweza kusema hali imetulia, lakini ukweli ni kwamba mioyo haijatulia. Chuki inatulia kimyakimya kama lava chini ya mlima. Na kama hatutatafuta uponyaji wa kweli, mlipuko mwingine unaweza kutokea. Busara na unyenyekevu vinahitajika sana kuleta uponyaji wa kweli.
Hawajaanguka, wameangushwa
Mara kadhaa tumesikia viongozi wakisema “vijana wetu ni wavivu,” “hawajitumi,” “wanapenda starehe,” “vijana wetu ni wa hovyo.” Watu husema “maneno huumba”: kwa nini hatutoi kauli chanya juu ya vijana wetu na badala yake tunawakejeli kila uchao? Na tujiulize, ni nani aliyeunda mfumo huu unaowafanya vijana kuwa hivyo tunavyowaona?
SOMA ZAIDI: Kama Sera ya Matibabu Bure Haitekelezeki, Basi Serikali Iache Kudanganya Wananchi
Katika kaya zetu tunawajengea vijana nidhamu ya uwoga, kutojiamini na kutosema ukweli wakihofia adhabu pindi wanapokosea. Kisha tunawapitisha katika mfumo wa elimu unaowafundisha kukariri badala ya kufikiri. Wanaingia sokoni bila stadi za kutosha, bila mitaji, bila uelewa wa fursa, bila kujiamini.
Wakijaribu kujiajiri, wanakutana na urasimu usioisha, na msururu wa kodi na tozo. Wakihoji, au kulalamika, wanaitwa “wachochezi” au “wahuni.” Huu ni udhalilishaji. Vijana hawahitaji virungu, wanahitaji nafasi ya kusikilizwa.
Katika miaka ya hivi karibuni, mataifa mengi yameangukia katika machafuko kutokana na hasira za vijana. Kenya, Sri Lanka, Bangladesh, Madagascar—yote yalishuhudia machafuko yaliyochochewa na ukosefu wa ajira na matumaini, huku wakiwaona viongozi wao wakila kuku kwa mrija (msemo wetu wahenga). Tanzania ikichelewa kujifunza, historia itajirudia kwa namna mbaya zaidi.
Badala ya kulaumiana, tuchunguze visababishi. Kwa nini vijana hawana matumaini? Kwa nini kila mara wanahisi hawasikilizwi? Kwa nini kila Serikali inapokuja, matumaini mapya huzaliwa, lakini yanakufa kabla ya kupumua?
Jibu ni moja: hatujawajibika. Ahadi zimekuwa wimbo bila melodi. Tunazungumza zaidi ya tunavyofanya. Maneno ni mengi, vitendo ni haba. Mapendekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mfano, yanabaki kuwa mapendekezo tu mwaka hadi mwaka.
Wananchi wanaendelea kulalamika kuwa vipaumbele vyao havizingatiwi ipasavyo katika mipango ya maendeleo. Wanazuoni kadhaa wamesisitiza umuhimu wa kuleta uwiano wa maendeleo ya vitu na maendeleo ya watu. Turejeshe imani ya Watanzania, hususan vijana, kwa vitendo. Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.
Tunahitaji uponyaji
Kama taifa, tunahitaji uponyaji. Siyo tu wa maneno ya pole kutoka kwa viongozi, bali wa vitendo. Waliopoteza wapendwa wao wapewe fursa ya kuwahifadhi kwa staha. Majeruhi wapewe matibabu na faraja. Taifa lipate ukweli kuhusu kilichotokea. Walioumizwa nafsi zao wasipangiwe namna ya kulia. Bila ukweli, hakutakuwa na uponyaji wa kweli na amani itabaki kuwa ndoto ya Abunuwasi.
SOMA ZAIDI: Wananchi Waibane Serikali Kukithiri Matukio ya Utekaji Tanzania
Chambilecho wahenga “mkubwa ni jaa.” Serikali iwe tayari kukiri makosa, kujifunza, na kujirekebisha. Serikali iwape kumbato wananchi wake na kuwaruhusu kulia kwa mtindo wao. Ukubwa wa Serikali haupimwi kwa mabavu yake, bali kwa uwezo wa kupokea vilio vya wananchi, kuwafariji na kuwatatulia kero zao.
Na wanasiasa wote—wa pande zote—wakumbuke kuwa siasa ni chombo cha kuhudumia watu, si uwanja wa majeraha. Na uponyaji huu siyo wa wanasiasa pekee, bali wa jamii nzima.
Tukitaka kuepuka fujo na machafuko ya aina hii siku zijazo, tusianze na askari barabarani—tuanze na dhamira zetu. Tuanzie kwenye ahadi tulizozitoa na hatukutimiza. Turejeshe imani iliyofifia kwa matendo, si maneno pekee.
Mwananchi akihisi anathaminiwa, ataipenda Serikali yake na atailinda nchi yake. Lakini akihisi anakandamizwa, ataiona Serikali kama adui. Hakuna risasi itakayoua hasira ya dhuluma.
Amani ya kweli ni pale ambapo wananchi wanapewa haki, vijana wanapewa nafasi, na viongozi wanapewa moyo wa kusikiliza na kuwa wanyenyekevu. Tusitafute mchawi wa vurugu; mchawi ni namna tulivyowaangusha vijana wetu.
Na kama kweli tunapenda kuendelea kuwa kisiwa cha amani, basi tuanze kukitengeneza leo—kwa kutimiza tulichoahidi—kabla damu nyingine haijamwagika.
Dk Baruani Mshale ni Mkurugenzi wa Mafunzo na Mikakati kutoka asasi ya kiraia ya Twaweza East Africa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia baruani.mshale@gmail.com au X kama @BMshale. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.