The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Shauri Lafunguliwa Mahakama Kuu Kuipinga Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29 na Kuendelea

Wanaeleza kuwa tume hiyo inakosa uhalali wa kisheria

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam-Watanzania watatu wamewasilisha maombi ya dharura katika Mahakama Kuu, masijala ya Dar es Salaam, kupinga uhalali na muundo wa Tume ya Uchunguzi ya Rais, ambayo iliundwa kuchunguza matukio yaliyotokea siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, na kuendelea. 

Waleta maombi hao ni pamoja na  Rosemary Mwakitwange, Edward Heche, na Deogratius Mahinyila, wanaiomba Mahakama kutoa amri ya kufuta uteuzi huo wa tume na kuizuia tume kuendelea na kazi.Pia, Wameiomba Mahakama itoe amri ya muda ya kusitisha shughuli kwa haraka, ambayo itawazuia mara moja wajibu maombi, wakiwemo wajumbe wa Tume na Mwanasheria Mkuu, kuendelea na uchunguzi hadi usikilizwaji na uamuzi wa maombi ya msingi utakapofanyika.

Maombi ya watatu hao yanadai kuwa uteuzi wa tume hiyo uliofanywa na Rais tarehe 18 Novemba 2025 una dosari za msingi, wakieleza kuwa kuna kuvunjwa kwa sheria, pia kukiuka misingi ya haki ya asili, matumizi mabaya ya mamlaka, na nia ovu (mala fide).

Waleta maombi hao wamebainisha masuala kadhaa wanayoeleza kuwa yanafanya kuwa uundaji wa tume hiyo ugubikwe na ukiukwaji wa sheria. Kwanza, hoja kwamba Rais aliunda tume huru ya uchunguzi, chombo ambacho kinadaiwa hakijatambuliwa wala kuelezwa katika Sheria ya Tume za Uchunguzi inayotumika. 

SOMA PIA: Hotuba Kamili ya Rais Samia Akizindua Tume ya Uchunguzi Matukio ya Oktoba 29, 2025: ‘Nina Matumaini Makubwa na Tume Hii’

Waombaji wanadai pia kwamba uteuzi huo haukutangazwa kwenye Gazeti la Serikali, na kwamba sharti la lazima la kubainisha kwa uwazi madhumuni ya tume hiyo halikuzingatiwa.

Hoja kuhusu upendeleo na uundaji wa Tume kukosa mantiki ni suala lililosisitizwa na waleta maombi.Waombaji wanaeleza kwamba wajumbe wa tume ni wastaafu wa serikali na waliowahi kuteuliwa na Rais, jambo linalowafanya kuwa na mgongano wa kimasilahi, jambo litakalochochea wao kukosa uwezo wa kuchunguza matendo ya watumishi wa umma wa sasa au waliopita, ikiwemo mamlaka iliyowateua.

Katika kujenga zaidi msingi wa hoja, waleta maombi hao wamemtaja Dkt. Stergomena Lawrence Tax, ambaye alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati wa matukio ya Oktoba 29 na kuendelea, ambapo wamesisitiza kuwa ana mgongano wa kimasilahi na hawezi kuchunguza mwenendo wa Wizara aliyokuwa akiiongoza.

Kesi hiyo pia imeainisha pia kauli za awali za Rais, zilizowataka wanajeshi kujiandaa kukabiliana na uwezekano wa vurugu za uchaguzi katika mwaka wa uchaguzi, jambo ambalo waleta maombi wamelieleza linaibua wasiwasi, kwamba mamlaka iliyotea tume inawezekana vipi kuchunguza masuala ambayo tayari mamlaka hiyo iliwahi kutolea maagizo.

SOMA: Tume Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, 2025: Serikali Iepuke Vishawishi vya Kutaka Kujistiri na Badala Yake Ijikite Kwenye Kuliponya Taifa

Maombi hayo pia yanadai kwamba mchakato mzima hauna mantiki kwa sababu suala liloainishwa kuwa rasmi la kuchunguza yaani, “matukio ya uvunjifu wa amani,” linadogosha masuala makubwa yanayolalamikiwa na watu, yaani vifo vya Watanzania, watu kupotea, na vitendo vya mateso vilivyosababishwa na matukio hayo.

Waombaji wanalalamika kuwa tume haina kabisa uwakilishi wa vijana (Gen-Z) ambao ndiyo kundi lililoathirika zaidi, bali imeundwa na watumishi wa zamani wa serikali, waliostaafu na wanaooendelea kupokea pensheni zao.

Waleta maombi pia wanaeleza kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, na mjumbe Jaji Mkuu mstaafu Ibrahim Hamis Juma, pamoja na Inspekta Jenerali wa Polisi mstaafu Said Ally Mwema, wametajwa kuwa waliwahi kuhudumu katika tume nyingine ambayo ilitoa mapendekezo ya kufanya mageuzi katika mfumo wa haki ya jinai, ikijumuisha kulivunja Jeshi la Polisi, lakini mapendekezo hayo hayakuwahi kutekelezwa.

Hoja nyingine iliyotolewa ni kuwa Tume hiyo imeundwa kukiwa na nia ovu (mala fide), ambapo sehemu ya maelekezo yaliyotolewa siku ya kuzindua Tume, ilielezwa kuwa Tume hiyo inaundwa kufanya uchunguzi na kama kutakuwa na Tume nyingine kutoka nje, basi itafanya kazi na tume hiyo.

SOMA: Bila Ushirikishwaji Mpana na Uhalali wa Kijamii, Wananchi Lazima Waione Tume Kama Chombo cha Serikali Badala ya Taifa

Waleta maombi wanaibua hoja hizi kwa kujaribu kujenga hoja kuwa kuna uwezekano mkubwa matokeo ya tume hiyo yamekwisha amuliwa kabla ya kazi ya uchunguzi kuanza, hasa ikizingatiwa baadhi ya maagizo ya kuchunguza vyama vya upinzani. Shauri hili limefikishwa Mahakamani wakati ambapo tayari kuna hoja kutoka kwa vyama vya upinzani, Azaki na taasisi mbalimbali za ndani na za kimataifa juu ya uchunguzi huru wa kimataifa.

Wajibu maombi katika shauri hili ni pamoja na Mwanasheria Mkuu, wajumbe wote wanane wa tume walioteuliwa, na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Kesi hii imewasilishwa mahakamani kwa mara ya pili, baada ya kuondolewa mara ya kwanza kutokana na kile kilichoelezwa kuwa “makosa ya uandishi,” na sasa imepangiwa kusikilizwa kwa dharura.

Uharaka wa kusikiliza shauri hili unatokana na imani kwamba wajibu maombi wataendelea na uchunguzi endapo Mahakama haitachukua hatua, hali ambayo itakuwa ni kutotendewa haki kwa Watanzania wanaotaka kufahamu nini hasa kilichotokea.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×