Dar es Salaam – Mnamo Disemba 2, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza na wazee wa Dar es Salaam katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini humo, kuhusiana na maandamano ya Oktoba 29 mwaka huu, na matukio mengine kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo.
Ifuatayo ni hotuba kamili ya takriban saa moja ambayo Kiongozi huyo Mkuu wa Nchi aliitoa kwa wazee hao, ambapo, pamoja na mambo mengine mengi, alielezea mtazamo wake kwa kile kilichotokea, wahusika wakuu anaoamini wako nyuma ya matukio hayo, pamoja na kile anachoamini ni malengo haswa ya vitendo hivyo ambavyo yeye amevipa jina la “vurugu”:
Wazee wangu wa Dar es Salaam, kabla ya Oktoba 29 mwaka huu [wa 2025], siku ambayo ilikuwa ni siku ya uchaguzi kwa nchi yetu, ulikuwa ukitaja msamiati wa kisiwa cha amani kwa nchi nyingi, au maeneo mingi ya ulimwengu, moja kwa moja mtu anaiona Tanzania ni moja katika nchi ambazo ni visiwa vya amani.
Sifa hii ndiyo utambulisho wa nchi yetu hii, ya kwanza duniani, pamoja na hulka yetu ya upole na ukarimu. Hiyo ndiyo inafanya Tanzania. Amani, hulka ya upole, na ukarimu. Hiyo ndiyo ilikuwa sifa yetu kubwa Tanzania. Amani, umoja na utu wetu ndiyo vilitutambulisha siku zote, hata tukiwa nje, wakiwa wanafunzi wanasoma huko, na tulipokuwa wanafunzi tunasoma huko.
Ukisema wewe ni Mtanzania ndani ya ukumbi, kuna Mtanzania atakuja kukufuata, bila kujali umetoka wapi, dini yako nini, kabila lako gani. Anakuja kukufuata, mnachapa Kiswahili chenu, mnaendelea, na udugu unaanza hapo. Hiyo ndiyo sifa yetu.
Lakini kila siku zinavyokwenda sifa yetu inaporomoka. Wengi wasioitakiwa mema nchi yetu wanakereka na tambo zetu hizo, za kwamba Watanzania sisi tuna umoja, tunapendana, na popote tunapokutana la kwanza ni udugu kuliko mengine yeyote. Wanakereka na sifa zetu hizo, na kwamba Tanzania ni nchi ya amani, inawakera sana.
Nakumbuka wakati mmoja katika ukumbi huu, nimesahau ilikuwa ni shughuli gani, lakini nikiwa kwenye kiriri hapahapa, nilizungumza, nikisema kwamba kuna watu wanakuja kutuchafulia amani, wameshaharibu wanakotoka, sasa wanataka kuchafua huku. Hilo nalo liliwakera. Liliwakera sana, na labda pengine ndiyo hii kutuonesha hata na nyinyi siyo wasafi pia.
Sasa, niseme tu kwa ufupi, kwamba vurugu zilizotokea tarehe 29, zikaendelea na 30, si desturi wala utamaduni wa Watanzania. Si desturi wala utamaduni wa nchi yetu, wala watu wetu. Kila aliyeumia, au kupoteza maisha, ni Mtanzania mwenzetu, mwenye haki sawa na mwingine. Hakuna mtu aliyejuu ya mwingine. Haki ya kuishi, na haki ya kuwa huru, ni tunu zetu sote Watanzania. Kwa hiyo, hakuna sababu ya Watanzania kuumizana na kunyimana uhuru.
Inatia uchungu kuona wachache walioratibu fujo zile, wakitaka Watanzania wawe kafara kwa malengo yao ya kisiasa, yaliyojaa ubinafsi, tofauti na siasa. Yaani, malengo yao ni tofauti na siasa iliyopo. Lakini kwa sababu zozote zile, hatukupaswa kuvuruga amani ya nchi yetu, wala kusababisha vifo kwa watu wetu. Sasa, kwa wale walioondokewa na ndugu zao, na watoto wao, na jamaa zao, natoa tena pole kwa sote. [Huu] siyo msiba wao peke yao, ni wetu sote, kwani damu ya Watanzania ni damu yetu sote. Mtanzania mmoja akiumia, tumeumia sote. Kuondokewa kwa Mtanzania mmoja ni kuondokewa wote. Kwa hiyo, tuwe pole wote.
SOMA ZAIDI: Shauri Lafunguliwa Mahakama Kuu Kuipinga Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29 na Kuendelea
Kama alivyosema kaka yangu Salim Matimbwa [Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam] hapa kwamba katika kipindi hiki ambacho mmeniamini kuongoza nchi nimeshazungumza na wazee mara mbili. Mara ya kwanza niliongea na wazee wa Dar es Salaam mwanzo mwanzo, nadhani ilikuwa 2021 mwisho au 2022. Lakini mara ya pili niliongea na wazee wote wa Tanzania, wawakilishi wao, pale Dodoma, muda mfupi kabla ya uchaguzi. Leo ni mara yangu ya tatu, na ya kwanza katika muhula wa pili wa awamu ya sita.
Nimeona niongee nanyi kutokana na yaliyotokea katika nchi yetu. Kwa hiyo, nikaona ni vyema kuendeleza utamaduni wa viongozi wetu waliotutangulia, kwamba yakitokea mambo makubwa ndani ya nchi, [viongozi] hupita na kuongea na wazee. Kwa hiyo, na mimi nataka niendeleze utamaduni huo kwa kupitia wazee wa Dar es Salaam nizungumze na taifa.
Na hii ni kutokana na upekee wa jiji la Dar es Salaam. Dar es Salaam, kama lango kuu la kuunganisha Tanzania na nchi zingine tunazopakana nazo, lakini hata Afrika, kati na kusini, ni rahisi kufikiwa kwa kupitia Dar es Salaam. Lakini vilevile nimekuja kuzungumza nanyi kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, nikiwa mdogo wenu, wengine dada yenu, [kwa] vyeo vyovyote vile, nimeona nije nizungumze [nanyi], na wengine ni mwanafunzi wenu. Kuna walimu wangu kati ya wazee hapa. Walimu wetu kwenye Serikali waliokuwa wakiongoza na sisi tukifuata, walimu kwenye maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, mliyoyafanya na sisi tumefuata hatua zenu. Lengo ni kusikia ushauri wenu, lakini pia mnisikie na mimi.
Kuzungumza na wazee wa Dar
Ndugu zangu wazee wa Dar es Salaam, baada ya kuapishwa nimezungumza na wananchi, hii [ikiwa] ni mara yangu ya nne. Nimezungumza kupitia hotuba ya siku ya kuapishwa. Nimezungumza kupitia hotuba yangu Bungeni. Nimezungumza kupitia siku ya kuapisha mawaziri wa Serikali hii. Lakini pia nilizungumza siku ya kuzindua Tume niliyounda kufanya uchunguzi wa haya yaliyotokea. Hotuba zote hizo haziwezi kuondoa, wala kukwepa, umuhimu wa kuzungumza nanyi wazee wa Dar es Salaam, na ndiyo maana niko hapa leo.
Dar es Salaam yetu ni kitovu cha biashara na moyo wa utamaduni wetu. Dar es Salaam hii, kupitia vurugu zilizopotea, imepitia kipindi kigumu sana, na wote hapa ni mashahidi. Kuna wengi ambao riziki zao ziko mikononi kwao. Mtu mpaka aamke asubuhi, atoke, akajishughulishe, apate cha kupeleka nyumbani, cha kula na watoto. Vurugu zile ziliifanya Dar es Salaam isimame. Wafanyabiashara ndogondogo walisimama. Wenye magenge walisimama. Kariakoo ilisimama. Shughuli zetu zote zilisimama, na ilitulazimu tubaki ndani, na kwa hadithi tunazozipata bei za bidhaa zilipanda sana, sana, sana.
Kwa hiyo, machungu ya siku chache tuliyaona ndani ya Dar es Salaam, mbali na maeneo mengine yote nchini. Maeneo mengine, baada ya vurugu kutulia, shughuli ziliendelea, watu walikula, walitoka kufanya yao, lakini Dar es Salaam tulionja kidogo, vijana wanasema, joto ya jiwe. Kwa hiyo, nikasema tuzungumze kidogo.
Kwa hiyo, kwa muktadha huu, nakuja kuzungumza nanyi kwa kuwa natambua takriban asilimia 10 ya Watanzania wote wanaishi hapa Dar es Salaam. Dar es Salaam ni jiji la watu takriban milioni sita na kitu. Hiyo ni idadi kubwa ya watu kuishi kwenye jiji moja, na ndiyo inaonesha umuhimu wa jiji hili kwa nchi yetu ya Tanzania.
Dar es Salaam inachangia takriban asilimia 17 ya pato la taifa, na asilimia kubwa ya biashara inafanyika hapa, ndani ya jiji hili la Dar es Salaam. Isitoshe, Dar es Salaam ndiyo jiji la kibiashara na taswira ya nchi yetu nje. Kwa hiyo, ina umuhimu wa peke yake. Ikiunguzwa Dar es Salaam, Tanzania yote inaungua. Kwa sababu Dar es Salaam ndiyo Tanzania.
SOMA ZAIDI: Serikali Yapinga Idadi ya Vifo Vinavyotajwa Kufuatia Oktoba 29. Yatoa Sababu Mbalimbali za Kutototoa Takwimu za Vifo
Hakuna kabila lolote ambalo haliko hapa Dar es Salaam. Watu wa mikoa yote wa nchi hii wako hapa Dar es Salaam. Watu wa dini zote wako hapa Dar es Salaam. Kwa hiyo, Dar es Salaam ndiyo Tanzania. Ikidhurika, ikipata madhara Dar es Salaam, hii ndiyo inabeba sura, au taswira, ya nchi yetu. Chochote kitakachoripotiwa vibaya kinachukuliwa Tanzania iko katika hali hiyo. Kwa hiyo, kuna kila umuhimu wa kuzungumza nanyi wazee wa Dar es Salaam.
Tukio la Okt. 29
Ndugu zangu, lililotokea ni tukio la kutengenezwa, na waliolitengeneza walidhamiria makubwa, walidhamiria kuangusha dola ya nchi hii, au ya nchi yetu. Ukiangalia clips za nyuma zilizotokea vijana wetu walifanywa kasuku na kuimbishwa kabisa, [kwamba] yaliyotokea Madgascar yatokee na hapa. Lakini ukimvuta kijana yule, [umuulize], “hebu niambie, Madagascar kumetokea nini?” Hajuwi. “Unataka hapa kitokee nini?” Hajuwi. Lakini waliimbishwa wimbo huo.
Kwa hiyo, lile lilikuwa ni jambo la kupangwa, na vurugu zile zilidhamiria makubwa. Vurugu zile ni mradi mpana sana wenye nia kuu ya uovu, ulio na wafadhili, washitiri na watekelezaji. Katika vurugu ile, waliingia waliokuwemo na wasiokuwemo. Wengine kwa kutokujua. Wengine kwa kufuata mkumbo. Wengine kwa hadaa za maisha bora baadaye. Lakini wengine kwa kulipwa tu. Tunaambiwa kuna vijana walikuwa wanalipwa kwa fedha, kisha kuchukua pesa zao [na] kuingia barabarani. Kwa hiyo, waliingia bila madhumuni maalumu ya nini wanakwenda kukifanya.
Inaumiza sana kuona madhara yaliyotolewa. Nadhani takwimu zinatolewa sasa hivi na [nyingine] baadaye. Kuna majengo kadhaa ya Serikali yameunguzwa. Kuna miradi kadhaa iliyojengwa kwa manufaa ya wananchi imeunguzwa. Vituo vya mafuta, biashara binafsi za watu, vimeunguzwa. Magari ya Serikali yameunguzwa. Vituo vya polisi, vingi tu, vimeunguzwa.
Maandamano au vurugu?
Sasa, nataka tuwe na jina la hayo, ni maandamano au ni vurugu? Maandamano tuliyoyazoea, na tuliyoyakubali ndani ya Katiba yetu, ni yale watu wanaudhika na kitu, tunaomba tuandamane tujieleze, tutatoka pointi moja, tutakwenda zetu mpaka Mnazi Mmoja, au popote pengine, na mabango yetu yanaeleza maudhi tuliyoudhika nayo, na polisi wanawasindikiza vizuri mpaka wanafika wanapofika. Wanaeleza wanayoyataka, wanatawanyika kwa salama, wanakwenda zao.
Lakini haya, ya kuunguza miradi ya Serikali, vituo vya polisi – na kwenye kituo cha polisi unakwenda kufanya nini? Ni kwenda kuvamia na wapate silaha. Madhumuni ya kuwa na silaha mkononi ni nini? Lakini unaunguza biashara za watu binafsi, lengo ni nini? Kwa hiyo, haya hayakuwa maandamano; zilikuwa ni vurugu zilizoandaliwa kwa madhumuni maalumu.
Lakini tujiulize [swali] jingine, kwa nini siku ile ya uchaguzi? Katika hali hiyo, Serikali ina wajibu, tunaapa kulinda nchi hii na mipaka yake, kulinda usalama wa raia na mali zao, na katika hali hiyo, nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo.
Sasa, tunapoambiwa kwamba tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ni ipi? Ilikuwa tuwaangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe? Hapo patakuwa pana dola kweli? Dola haiko hivyo, na hayapo Tanzania peke yake. Tulishashuhudia kwa wenzetu. Waandamanaji wengi wanaingia njiani, na wakiingia njiani Serikali ikiona huo uandamanaji unakwenda pasipo, wanaweka nguvu kubwa. Wanaweka nguvu kubwa. Yameshafanyika kwenye mataifa huko na tumeyaona.
Sasa wanaporudi kutulaumu kwamba tumetumia nguvu kubwa, wao walitaka nini? Tujiulize, je, hao ndiyo wafadhili wa kile kilichofanyika? Walitaka tuangalie ile mob mpaka ifanikiwe walichowapa fedha, walichowatuma? Hapana. Tuliapa kulinda nchi hii na mipaka yake, [na] usalama wa raia na mali zao. Kwa hiyo, katika kufanya hivyo, kama wanavyofanya wao, na sisi tutafanya vilevile kuilinda nchi yetu.
Waratibu
Kwa nini siku ya uchaguzi? Siku ya uchaguzi kwa sababu walishajua kuna ushindi mkubwa wa Chama cha Mapinduzi. Kuna ushindi mkubwa wa Chama cha Mapinduzi. Waangalie kampeni zetu tulizozifanya. Waangalie watu walivyotuitikia. Waangalie kazi tuliyoifanya kwenye miaka mitano iliyopita. Walijua, na wapinzani wetu walikataa kuingia [kwenye uchaguzi]. Hawakuzuiliwa na mtu. Walikataa wenyewe kuingia kwa sababu walishajua wasingefanikiwa. Walishajua aibu ingewapata. Kwa kazi iliyofanyika na mwitikio wa wananchi kwa Chama cha Mapinduzi, aibu ingewapata, na ndiyo maana wakakataa kuingia kwenye uchaguzi.
Lakini wanayageuza, [wakisema] Serikali imewazuia kuingia ndani ya uchaguzi. Lini tuliwazuia? Nayafafanua haya ndugu zangu wazee wa Dar es Salaam muijuwe hali halisi. Inawezekana katika vikao huko mnayasema ambayo hamna taarifa nayo iliyokamili. Hatujawazuia, na katika taarifa zinazotolewa, na waliokuwa huko lakini wakaamua kurudi, kwamba hawaridhishwi na yanayotokea, wanatwambia, walikaa vikao, na wakaamua tusiingie tutakwenda kupata aibu.
Lakini kwa kuficha aibu ambayo wangeipata, wameshusha hili lililotokea. Kwa nini siku ya uchaguzi? Haki gani inadaiwa siku ya uchaguzi? Kama kuna haki yoyote inadaiwa, hakuna siku nyingine? Hakuna njia nyingine ya kudai hiyo haki mpaka yafanywe yale yaliyofanywa? Ni maswali ya kujiuliza.
Lakini katika hili tunaambiwa kuna waratibu ambao wanaishi nje ya nchi. Wengine tunawajua, wengine hatuwajuwi. Tunaendelea kujifunza na kuwatafuta tuwajuwe ni akina nani. Sasa, hebu watu wote hapa chini ya miaka 50 wasimame. Watu chini ya miaka 50 wasimame. Anha, kwa hiyo wengi waliosimama hapa naona ni mawaziri wengu, wengi chini ya miaka 50, haya kaeni. Viongozi wa dini wachache na vijana wa jiji la Dar es Salaam, na wafanyakazi wa Serikali wachache.
Sasa, hili jambo lina waratibu kutoka nje. Lakini kwa nini waratibu kutoka nje? Wale waratibu wa Tanzania tunaowajua, wale ni shida za maisha. Ni shida za maisha. Akisukuma na kusukuma maandamano, umbea na nini kuhusu Tanzania, Watanzania walewale ambao wanadai ugumu wa maisha, wanatumia fedha zao kununua bundle kuangalia na kuwasoma wanasukuma nini. Lakini yeye ukisoma, yeye kule anatiliwa fedha. Kwa hiyo, kimoja kinachowasukuma ni shida ya maisha. Kule waliko hawako sawa, wana shida ya maisha.
Sasa, kuna wale ambao hawana shida ya maisha, wako pazuri, wanalipwa na hao wanaotaka hayo yatokee. Lakini wamekosa uzalendo tu. Wamekosa uzalendo tu, na ukiwatazama vizuri si Watanzania kamili kamili. Kwa hiyo, kwao haijalishi, Tanzania inaungua au haiungui. Yeye ana nafasi ya kuwa nje, si Mtanzania kamili kamili, hana shida hizo. Hana shida hizo.
Kwa hiyo, hili jambo lilipangwa kwa uratibu mzuri. Lakini hebu tuangalie sasa wale waliolipanga na kudai wana madai kwenye hili. Nianze na wenzetu wa vyama vya upinzani. Kama nilivyosema kwamba hawa watu waliishiwa nguvu. Maneno ya vijana waliishiwa pawa, na waliona kabisa mbele kwao siyo kuzuri, na kuingia kwenda …
Hawa watu wana frustrations zao huko nyumbani kwao, lakini wanataka kujificha na kusukuma lile dude kwa watu. Huko waliko hawako sawa. Wanapambana wao kwa wao ndani. Wamemeguka wao kwa wao ndani. Wamemeguka, wanasiasa wakaenda vyama vingine, wanaharakati wakabaki. Kwa hiyo, wenyewe kwa wenyewe huko ndani hakuko sawa. Wasitulaumu sisi, ni wao wenyewe huko ndani.
Mkono wa rehema
Kwa hiyo, kasoro walizonazo huko wanataka kuzisukuma huku kwetu. Hawakuzuiliwa kuingia kwenye chochote. Ni hawa hawa ambao mwaka 2020 mpaka 2023 nilifanya kazi kubwa ya kuzungumza nao, nikanyoosha mkono wa rehema, njooni nyinyi Watanzania, njooni tukae, tuzungumze yetu, twende vile tunavyotaka, nikidhani nawanyooshea watu, Watanzania, ule mkono wa rehema, na wataupokea, watakuja, tukae vizuri.
Ni hawa hawa niliowakuta nje [ya nchi] wanasumbuka hawana shilingi mkononi. Wakaomba sana kuja kuniona, nikawapokea, tukazungumza, hawana hata shilingi, nikatoa kiposho changu nilichogaiwa cha safari, nikawapa, waendelee na maisha, wakiwa nje. Ni hawa hawa walioniambia sawa tutarudi lakini tuna kesi. Nikawaambia kesi nitazifuta, njooni. Njooni tukae, tuzungumze, tujenge nchi. Na wamekuja, baadhi yao wamekuja mikono mitupu, hawana kitu, tukatoa fedha zetu kuwapa waanzie maisha hapahapa Tanzania.
Sasa, nataka mumpe cheo mtu wa namna hiyo, aliyenyooshewa mkono wote huo, wa rehema na mkono wa upatanishi, yeye kaja, yule aliyemnyooshea ndiyo wa kwanza kumkashifu, kumtukana, na kugeuza mambo kuichafua nchi. Huyo mtu anaitwaje? Huyo mtu anaitwaje? Hii si tabia ya Watanzania. Wakati ule nafanya yote nilijua naongea na Watanzania waliotimia, wenye akili timamu. Nikajua watarudi, tukae, tuzungumze, twende.
Na niliwapa fursa zote nyinyi ni mashahidi. Niliwafungulia, walitaka kufanya maandamano, wakafanya maandamano, tukawasindikiza mpaka walipofika. Wakasema yao, wakatawanyika. Yale ndiyo maandamano, ambayo yameruhusiwa kikatiba, na ukiomba [kibali] polisi watakwambia nenda kaandamane, tuambieni njia [mtakazotumia] tuwalinde mpaka mfike sehemu yenu. Yale ndiyo maandamano. Haya yaliyofanyika siyo maandamano.
Ni hawa hawa niliowapa fursa ya kufanya shughuli zao za kisiasa. Sasa, siasa si kutukanana. Siasa si kubezana. Si kuharibu nchi. Hiyo siyo siasa. Wazee wetu wa zamani, ukiwa na harakati hizo, wanasema “Huyu hajuwi siasa.” “Hafanyi mambo yake kwa siasa.” Ina maana siasa maana yake ni usalama. Siasa maana yake ni uungwana. Hiyo ndiyo maana ya siasa. Sasa kama mtu unampa ruhusa afanye siasa za kisiasa, anakwenda kufanya siasa anazozijua yeye za kuvuruga nchi, hiyo siyo siasa. Hiyo siyo siasa.
Kwa hiyo ndugu zangu, niseme kwamba madai yoyote waliokuwa nayo, chama hiki cha siasa, au vyama hivi vya siasa, hawakupaswa kutumia njia ile kudai kwamba sasa tukae, na kwa masharti, tuzungumze ili na wenyewe warudi. Hapana. Haikuwa hivyo.
Vijana na ugumu wa maisha
Lakini kundi la pili tuangalie vijana. Vijana wetu hawa wameingizwa njiani, wakaimbishwa wimbo wasioujua. Wanadai haki, haki gani? Hebu avutwe tu kijana pembeni, [aulizwe], “Wewe uliingia barabarani unadai haki, hivi ni haki gani unadai?” Na hiyo haki hawakuweza kuidai kwa njia nyingine mpaka waingie njiani, wakafanye vurugu, walipwe wakachome vituo [vya polisi na mafuta], walipwe wakafanye vurugu walizozifanya? Hiyo ni haki gani?
Lakini jingine walilobebeshwa wameingia njiani eti kwa ugumu wa maisha. Astaghfirullah! Turudi kwa Mungu tuombe msamaha. Ningekuwa na uwezo ningebeba vijana wa Tanzania nikawatupa kwenye nchi tofauti tu hapa Afrika, pamoja na majirani zetu, wakaone ugumu wa maisha uliokuwepo kule, halafu waseme kwamba kwao Tanzania ni pahala pema.
Hawana sababu, hawana. Mwenye ugumu wa maisha, kwa raha zake kabisa, ataingia njiani akaimbe oyoo oyoo? Huo ni ugumu wa maisha? Mwenye ugumu wa maisha anahangaika kutafuta chakula chake cha leo, na wengi walikuwa kwenye kazi zao, wale wana ugumu wa maisha. Hawa wengine hawakuwa na ugumu wa maisha, walikuwa wana sababu zao zingine.
Kwa wale watafiti, wafanye utafiti ndani ya Afrika Mashariki na nje, labda kusini mwa Afrika. Waangalie nafasi ya Tanzania kwenye ugumu wa maisha. Kwa hiyo, vijana wetu wasimezeshwe tu na wenyewe wakameza, hapana.
Lakini kwa nini yote yanatokea haya tumejifunza kwamba vijana wetu tumewaacha wanakuwa wenyewe. Wanakuwa hawana mwelekeo. Wanakuwa hawana watu wa kuwaongoza vizuri, na kwa maana hiyo hawana elimu ya uzalendo. Hayo ndiyo tuliyojifunza. Vijana wazalendo, hata kutoka vyama vya upinzani, hawakukubaliana na hali ile. Walikuja kutwambia jamani kaeni vizuri, kuna hili inapangwa huku. Vijana wenye uzalendo, kutoka vyama vya upinzani.
SOMA ZAIDI: Oktoba 29, 2025: Tulichoka Hekima na Busara, Tukajaribu Ujinga, Tumeona Matunda Yake
Lakini vijana wetu wengi wa Tanzania hawana uzalendo, na hilo Serikali tumejifunza, na tutakwenda kulifanyia kazi, na ndiyo maana nikasema niunde wizara nzima ya vijana ili kushughulikia vijana kwa upeo mpana badala ya kuwa na kitengo ndani ya wizara kubwa. Kwa hiyo, kwa upande wa vijana wetu hawakuwa na sababu yoyote ya kuingia njiani ila kutumwa na kuimbishwa mambo yasiyowahusu.
Taasisi za dini
Tuangalie taasisi zetu za dini ambazo nazo, kwa namna moja au nyingine, wamejiingiza kwenye mkumbo huu. Hapa, unajua unapokuwa kiongozi lazima ukubali wakati fulani kukosa umaarufu. Lazima ukubali, na kama kukosa umaarufu kipindi hiki kuelekea kampeni, kuelekea uchaguzi na baada ya uchaguzi, utaondoka tu, lakini uondoke, turekebishe, tuseme ukweli.
Taasisi zetu za dini, tunasema Tanzania haina dini, si ndiyo? Lakini watu wetu wa Tanzania tuna dini, na tuna dini na madhehebu mbalimbali. Tuna dini kuu sijuwi nne, sijuwi tano. Tuna Wakiristo, tuna Waislamu, tuna Mabaniani, tuna Budha, na nyingine ambazo ziko huko. Lakini kubwa ni hizo nne au tano. Na hizi nne au tano zina madhehebu mbalimbali. Kwa Waislamu kuna Sunni, kuna Ibadhi, kuna Bohora, kuna sijuwi nani, mambo mengi, tupo. Lakini na Wakiristo na wenyewe wana madhehebu yao tofauti tofauti.
Kikatiba na sheria za nchi hakuna madhehebu hata moja ya dini yeyote imepewa uwezo kikatiba na kisheria kutoa matamko ya kufunika madhehebu mengine yote ya dini, hakuna. Hakuna. Wasijitokeze watu wakajibebesha hilo. Siku zote nasema Tanzania hii haina mwenyewe, wenyewe ni sisi sote. Hakuna mwenye cheti anayeweza kusema Tanzania ni yangu, na itaongozwa ninavyotaka mimi. Hakuna. Tuna sheria zetu, tuna Katiba yetu, tumeamua kuwa nchi ya kidemokrasia, tutaendesha demokrasia yetu kwa njia tulizokubaliana.
Lakini viongozi wa dini msijivishe majoho ya kwamba nyinyi ndiyo mnaweza overrun nchi hii. Hakuna. Hakuna. Tutakwenda kwa Katiba na sheria za nchi. Hatutaendeshwa na madhehebu yoyote ya dini. Madhehebu ya dini [yabaki] na wafuasi wao. Ubora wa dini uko mioyoni kwetu. Wale wanaoamini ndiyo wanaojua ubora wa dini yao. Hakuna overiding hapa. Kwamba mimi dini yangu ndiyo ita-overide Tanzania, na tamko nikilitoa ndiyo hilohilo.
Hata wenyewe wanatofautiana. Mimi toka nimekaa matamko manane yametolewa na [Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania] TEC. Manane. Lakini ukienda chini chini, wenyewe kwa wenyewe wanapingana, [kwamba] matamko hayafanyi kazi vizuri. Wenyewe kwa wenyewe wanapingana. Kwa sababu waliosimama kwenye mstari wa haki, wanaona ile ni batili inayofanyika. Kwa hiyo, waliosimama kwenye mstari wa haki, hawaungani nao, wanaona ni batili iliyofanyika.
Kwa hiyo, niseme kwamba Tanzania yetu ni nchi ya umoja, nchi ya mshikamano, amani na utulivu ndiyo ngao zetu. Tusivurugwe ndugu zangu kupitia mirengo yetu ya dini, ya siasa, mirengo yoyote ile. Hatupaswi kuivuruga nchi hii. Hatupaswi.
Hata kama aliyepo juu ya Serikali humtaki, kuna muda, hii ni nchi ya kidemokrasia, huyu mtu ataendesha mpaka wakati huu, akifanya makosa afanye makosa yake. Ni kosa la [Serikali ya] awamu ya sita kueneza huduma za afya Tanzania, hilo ndo kosa letu? Kosa letu kueneza huduma bora, shule nzuri, mpaka kule vijijini, hilo ndo kosa letu? Kosa letu kukuza uchumi wa Tanzania, ukakua mpaka tukasifiwa duniani, hilo ndo kosa letu? Kosa letu ni kuifanya Tanzania iwe nchi salama, ikalike, na watu wafurahi, hilo ndo kosa letu? Kosa letu ni nini?
Kama mtu hampendi anayeoongoza, tustahamili tu. Demokrasia ipo, ataoongoza, ataondoka. Kwani wote walioongoza kutoka mwanzo mpaka leo awamu ya sita walipendwa na kila mtu? Nchi ilivurugwa? Sasa kama humpendi Samia, huna sababu ya kuvuruga nchi. Kama humpendi kwa alivyo, humpendi kwa dini yake, humpendi kwa alikotoka, hakuna sababu ya kuvuruga nchi. Katiba yetu, sheria zetu, zipo. Nchi hii inaongozwa kwa Katiba na sheria zetu. Hakuna sababu ya kuvuruga nchi ndugu zangu.
SOMA ZAIDI: Tanzania Baada ya Oktoba 29, 2025: Tunarejeshaje Kisiwa cha Amani?
Kwa hiyo, niwaombe sana zile sumu zinazotiwa huko, mnakotiwa sumu, tumieni akili zenu. Najua hakuna eneo baya la kumpata mtu kama dini. Unapomkamata mtu kwenye dini, na ukamlisha ubaya wa mtu kwenye dini, unajenga chuki ya ndani ya moyo, kuliko wanasiasa. Wanasiasa wakimharibu mtu, wanamuharibu mtu kichwani. Akija mwingine na zuri lile baya litaondoka na zuri litaingia. Lakini ndani ya moyo likiingia, limeingia. Kwa hiyo viongozi wetu wa dini, kaeni kwenye mstari wenu.
Dini zetu zote zinasema kila mamlaka imeletwa na Mungu, kila mamlaka imeletwa na Mungu. Iwe kwenye mamlaka kuna mwanamke, iwe kwenye mamlaka kuna mwanaume, kila mamlaka imeletwa na Mungu na sababu ya Mungu kuleta mamlaka hayo, hakuna anayeijua duniani. Hakuna. Mungu peke yake ndiyo anayejua kwa nini Samia leo yuko hapa. Kwa hiyo, niwaombe sana viongozi wa dini mvae majoho, yale majoho yetu yaoneshe sura halisi [ya dini zetu]. Hakuna kitabu chochote cha dini kimesema tutazitumia dini zetu kuvuruga nchi zetu. Hakuna. Ni utashi binafsi wa watu. Kwa ubaya wa nafsi zao.
Kwa hiyo, msivae majoho ya dini mkatengeneza utashi wenu binafsi kwa kupitia vivuli vya dini. Niwaombe sana viongozi wa dini tusimame, tusivuruge nchi yetu. Tusivuruge nchi yetu. Kama kuna lolote, njia sahihi za mazungumzo zipo, njia sahihi za kukaa na kujadiliana zipo. Hakuna sababu yoyote kufika tulikofika ndugu zangu, hakuna.
Nilikuja na falsafa ya 4Rs, nikaifanyia kazi vizuri sana, ikaleta mwanga mzuri sana, mpaka wale nisiowajua jina lao wakaenda kubadilisha, nchi ikachukua mwelekeo mwingine. Lakini nataka niwaambie, tutasimama, na kuilinda nchi hii kwa nguvu zote. Nasema yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.
Madai ya Katiba
Kama madai ya wenzetu ni Katiba, hakuna aliyekataa kurekebisha Katiba ya nchi hii, hakuna. Mnakumbuka, niliunda Tume ya Haki Jinai, ikaenda Tanzania nzima na ikaniletea, [na kuniambia] haya ndiyo wanayoyaona Watanzania. Na katika kuyatekeleza kuna ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Na ya muda mfupi na muda wa kati, mengi, asilimia 90, tumeyatekeleza. Lililobaki la muda mrefu lilikuwa ni la Katiba, marekebisho ya Katiba, na lenyewe nikasema tutalitekeleza, na mkisoma Ilani ya Uchaguzi [wa 2025] ya Chama cha Mapinduzi, nimesema ndani ya siku mia nitaunda Tume ambayo itafanya kwanza maridhiano, halafu tuingie kwenye mchakato wa Katiba.
Mnaendaje kwenye kurekebisha sheria za nchi wakati huku mko vipande vipande? Lazima mrudi kwanza muelewane, mtambue huko mbele tunalenga kitu gani, njia yetu ni ipi, ndiyo mnatunga Katiba yenu. Kutokana na haya tuliyokubaliana sasa Katiba iseme moja, mbili, tatu, iseme nne. Lakini mtakwenda moja kwa moja kila mtu kavimba mashavu mnaunda Katiba, Katiba gani itaundwa hapo?
Nimesema kwanza turidhiane, na kwa sababu wamechafua nchi nilichofanya mwanzo ni kuunda Tume ya kuangalia undani wa hili jambo. Nimewapa miezi mitatu, waangalie kwa undani, watuletee taarifa, yaliyojiri ni haya, sauti ziko hapa, hapa palitokea si haki, hapa palikuwa na haki.
Tukishayajua hayo, tunasema haya, tuliyoletewa ni haya, njooni sasa Kamati ya Maridhiano, leteni sasa tofauti ni hizi, matatizo ni haya. Iteni sasa wa makundi mbalimbali wakwambieni haya tunakwenda nayo vipi. Hiyo sasa ndiyo Tume ya Maridhiano. Baada ya hapo, tunakaa na kuunda Katiba yetu. Hakuna aliyekataa.
Leo wanasema wameingia njiani, wameharibu nchi, wamedai Katiba, Katiba iko wapi? Inaning’inia wapi tuipachue tuwape? Katiba ni mchakato. Tunaanza hili, tunakwenda hili. Sasa katika vile visingizio vya kuepukana na aibu ya kushindwa kwenye uchaguzi, wanaweka visingizio.
Mataifa ya nje
Visingizio vyote hivi vinaungwa mkono na [mataifa ya] nje. Hawana hata aibu. Nje huko wanakaa [wanasema], “Ooh, Tanzania ifanye moja, ifanye mbili, ifanye tatu halafu ndiyo itakuwa hivi.” Who are you? Niwaulize ndugu zangu, niwaulize, kwao hayatokei?
Kwao hayatokei? Tumenyanyua sauti sisi kusema ya kwao? Wanadhani wao bado ni masters wetu, ni wakoloni wetu? Kitu gani [kinawafanya wafanye hivi], ni pesa chache wanayotugaia? Ni fedha chache wanayotugaia? Na fedha yenyewe saivi haipo. Tunafanya biashara wao wapate, na sisi tupate. Ndipo tunaposimamia.
Nataka niwaambie ndugu zangu Watanzania, kawaida, mwanamke mzuri ndiyo anayepiganiwa, uongo kweli? Utakuta watu wanafokeana, wanapigana, wanafanya nini, ukicheki, wanaume wawili watatu wanapigana, katikati kuna mwanamke mzuri.
Sasa nchi yetu hii, alhamdulillahh, Mungu katuumba vizuri. Katuumba vizuri sana. Katuweka pahala pazuri sana. Kama nnavyowaambia, Tanzania ni lango la kuingia Afrika. Tanzania inaweza ikatumika vizuri sana kibiashara. Inaweza ikatumika vizuri sana kisiasa za dunia. Inaweza ikatumika.
Tatizo ni siasa tuliyonayo. Siasa ya kutofungamana na upande wowote. Wengine wanakuja mlango huu kushughulika na sisi, wengine wanakuja mlango huu. Lakini pia mali Mungu alizotuumba nazo [kama vile] madini. Tanzania sisi tuna bahari, ambayo kwa kupitia bahari unaweza kwenda popote ulimwenguni. Tanzania tuna maziwa, makubwa, ambayo kwa kutumia hayo unaweza ukufanya biashara yoyote na nchi jirani, na ukasafirisha vyovyote vile kwenda nchi jirani. Tanzania tuna ardhi nzuri ya kilimo, na ndiyo maana tunajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128. Tunakula na tunauza.
Kubwa zaidi Serikali tumejua kwamba kilimo ndiyo kila kitu. Kwa hiyo, tunatoa ruzuku kwa wakulima wetu ili wazalishe zaidi, mazao ya chakula na biashara. Tanzania sisi tuna hayo madini, kuna madini yanaitwa madini adimu duniani, ndiyo dunia yote imetoa macho hapo, pamoja na kwamba yapo kwengine duniani, lakini Tanzania ni moja wapo ya nchi ambazo hayo madini yapo, na watu wanayatolea macho.
Kwa hiyo, tunapigwa, tunalembewa mawe, kwa vile Mungu alivyotuumba. Sasa nataka niwaambie, maumbile yetu na utajiri wetu isiwe laana, tukauana sisi kwa sisi kwa kushawishiwa na wanaoitolea macho nchi yetu, hapana. Mjenga nchi ni mwananchi.
Huu ni wakati wa Watanzania kushikana ndugu zangu, na kujua kwamba yaliyoumbwa na Mungu hapa kwetu ni yetu, ni yetu, na haya Mungu alitupa makusudi kuinyanyua nchi yetu. Nyuma hatukuwa tunapigwa mawe sana, tulikuwa tunahesabika tu ni nchi masikini, inayoendelea polepole. Lakini tulivyoufungua utajiri, tukatumia rasilimali zetu kwa utalii, tukatumia madini yetu kibiashara, tukatumia bahari yetu na maziwa yetu kujenga uchumi wetu, hili sasa ndiyo linaloumiza watu huko ulimwenguni.
Kwa hiyo, huu si wakati wa kukaa tukanyoosheana vidole sisi kwa sisi Tanzania; ni wakati wa Watanzania kushikana tukasema Tanzania ni yetu, Mungu aliiumba hapa kwetu, na ni lazima itufaidishe sisi Watanzania.
Uhuru
Tunaposema tunalinda sovereignty, tunalinda uhuru wetu, tunalinda nchi yetu, lazima tuseme kwa moyo, sisi wazee ambao tunakwenda zetu, na vijana mlioinuka hapa wa chini ya [umri wa miaka] 50, sisi tunaondoka, tunawaachia [nchi] nyinyi. Hatujui kati ya nyinyi nani atakuja kuwa Rais hapa, lakini hilo mlijue vizuri sana. Mlijue vizuri sana. Na kwa bahati mbaya maumbile ya mwanadamu ni ya kushawishika.
Wemeweza kuwashawishi watu wetu wengine, na ndiyo hao wanaotekeleza [hizi vurugu], na ndiyo maana nikasema mradi huu uliotokea una walioupanga, kuna washitiri, kuna watekelezaji. Kwa hiyo, kuna washitiri na watekelezaji ndani ya nchi yetu ambao hatupaswi, kwa namna yoyote ile, kuwaachia watuvuruge.
Ndugu zangu, nilisema yaliyopitwa si ndwele tugange yajayo. Hili lililopita limepita, kwa maneno tunasikia liko jingine linapagwa, lakini, inshallah, Mungu hatosimama nao, litapeperuka. Lakini nataka niseme, nilimsikia mmoja kati ya waandaaji wa nje, anasema hebu tarehe 9 [Disemba] ahirisheni, subirini Krismasi, kwa sababu sasa hivi wamejipanga. Nataka niwaambie, wakati wowote wakija tumejipanga. Wakati wowote wakija tumejipanga.
Kwa ujumla, niseme, kama binaadamu, wanadamu hukosana, wakaelewana. Hatusemi labda Serikali tuko safi, hatuna makosa, hapana. Inawezekana kabisa kuna mapungufu, na hakuna Serikali yoyote duniani isiyo na mapungufu. Lakini wanakaa, wanazungumza, na kuondoa mapungufu yaliyopo. Kwa hiyo, na sisi hatuna budi kukaa, kuzungumza na kuondoa mapungufu yaliyopo.
Nimepata salamu, wanasema tutakubali tu kukaa na Serikali ikiwa watafanya moja, mbili, tatu. Serikali hii siyo ya kuamrishwa wala kupewa maelekezo. Tunawataka wenzetu tuzungumze, waje kwenye meza tuzungumze, na nimepata salamu za wengine wanaowapa nguvu, hakuna mazungumzo mpaka mumwachie huyu, mufanye hili, mufanye hili. Hiyo inatokea ndani ya nyumba tu, ndani ya nyumba tu. Baba ukishamkera mama, ukimrudia jioni anakwambia sitaki mpaka ufanye hili, na utafanya ili maridhiano yaende, uongo au kweli?
Sasa Serikali haipewi masharti hayo. Serikali haipewi masharti hayo. Labda Serikali ya wanafunzi kwa walimu wao, hilo linawezekana. Serikali ya wanafunzi hamtapa hili au lile mpaka mufanye hili. Wanafunzi watafanya. Lakini nchi huru, yenye kujielewa na kuendesha mambo yake, [hapana]. Kama ni Watanzania wa kweli, na wanaumwa na Watanzania kama wanavyosema, maana yake mara nyingi wanasema “tunasema kwa ajili wa wananchi.” Unajiuliza [wananchi] wepi?
Ushindi wa asilimia 97
Kama ni kwa ajili ya wananchi, wananchi walishasema, walishatoa maamuzi. Wameipa CCM asilimia 97, hayo ndiyo maamuzi ya wananchi. Wananchi wanaowasemea wao ni wepi? Halafu wanahoji, “Kwa nini asilimia 97?” Kwa nini isiwe? Waswahili wanasema paukwa, pakawa. Wao hawakuwepo, na wale 16 waliokuwepo ni wadogo sana, wao ambao wangeitingisha CCM hawakuwepo. Hakukuwa na CHADEMA, hakukua na ACT [Wazalendo], ndiyo ambao tungekwenda nao, na sisi tulijitayarisha kwamba tunakwenda kupambana na vyema wenzetu vikubwa. Hawakuwepo, mwananchi afanyeje?
Tunataka kuwaambia hata hao wafuasi wao walipigia Chama cha Mapinduzi, walipigia Chama cha Mapinduzi. Wale wanaohoji “kwa nini asilimia 97,” hicho ndicho kilichotokea. Ni asilimia 97 ya waliopiga kura, siyo ya Watanzania wote, ya waliopiga kura ni asilimia 97. Kazi imefanyika, kampeni imefanyika, na watu wameelewa, na wamepiga kura. Na Mungu ni mkubwa kwamba lile balaa lao walilianza saa tano sijuwi sita, watu walishajipeleka mapema asubuhi, wakapiga kura, wakaondoka. Mungu ni mkubwa, hasa kwenye miji, [watu walishapiga kura kabla ya vurugu].
Kwa hiyo ndugu zangu, sisi ni Watanzania. Tanzania itajengwa na Watanzania. Jeraha limetokea, lazima sisi Watanzania tutibu jeraha letu. Na hili siyo la kwanza. Tulipata jeraha kama hili 2001 [kisiwani Pemba]. Ni Watanzania sisi sisi tukatibu jeraha letu. Jeraha hili halitatibiwa na [watu kutoka] nje. Nje tutawekewa masharti, tutafutia misaada, lakini watakaotibu jeraha hili ni sisi Watanzania.
Zungumzeni na vijana
Niwaombe, tukae kwenye majukwaa yetu. Wazee mna majukwaa yenu, na kwenye majukwaa yenu mna dini mbalimbali, makabila mbalimbali, mna vyama mbalimbali, lakini nyote mpo kwenye majukwaa yenu. Kaeni mzungumze. Kaeni mzungumze na vijana wetu, wasitumike walivyotumika.
SOMA ZAIDI: Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Wahimiza Uwajibikaji Juu ya Mauaji ya Oktoba 29
Unaporudi leo mzee, na kulia kijana wako kaumizwa mguu, kijana wako kwa bahati mbaya alikufa, ulishindwa nini kumzuia asitoke? Ulishindwa nini kumwambia maneno ya hekima asiende, tukawaachia? Sisi ndiyo wazee wa nchi hii, tukae tuzungumze na vijana wetu, kwenye mabaraza yetu na kwenye majukwaa mbalimbali.
Viongozi wa dini, kama kweli vizimba vile tunavyoviingia msikitini na [kuita] Allah Akbar, Allah Akbar, na madhabahu yale tunayoyatumia, kama kweli tunayatumia kwa moyo, na kumsabili Mungu, twendeni tukamsabili Mungu. Tuacheni huu uchochezi unaotokea. Tuacheni. Tusiende kumtania Mungu. Huku ni kumtania Mungu. Kuchukua utashi wako binafsi, wa nafsi yako, ukauvisha majoho ya dini. Hapa ni kumtania Mungu. Ni kumtania Mungu. Tuacheni kumtania Mungu.
Ndugu zangu, nimesema kazi yetu sasa ni kuziba jeraha, na hapa nataka nizungumze na watoto wangu pia wanaoangalia mbele, vijana wangu hawa [waliopo hapa ukumbini] na walioko huko nje, wanaoangalia mbele, 2030. Safari hiyo [ya kisiasa] isiende kutuvurugia nchi yetu. Nimezungumza na mawaziri wangu, nikawaambia namwangalia mmoja mmoja. Una maslahi na huko [2030] kaa nje huko, usifanye ukiwa ndani ya Serikali yangu.
Nimekuweka hapo, ukatumikie wananchi. Maslahi yako ya huko mbele, twende utaikuta huko mbele. Mungu ndiyo anajua nani kiongozi wetu wa baadaye, ni Mungu peke yake ndiyo anajua. Kwa hiyo, unaweza ukajipanga, unaweza kuwa na mikakati, na usiwe. Kwani wangapi walipanga, na walikuwa na mikakati, walikuwa? Na walikuwa na nguvu zote mpaka za kifedha, walikuwa? Mungu ndiyo anajua nani huko mbele ndiyo kiongozi wetu. Kwa hiyo, ile safari ya 2030 isiende kutuharibia nchi.
Ndugu zangu, mengine yaliyosemwa na wazee hapa, nimeyapokea. Waziri wao yupo, ambaye atashughulikia shida zao, na mimi katika ziara zangu, kote Tanzania, nikifika ndani ya mkoa la kwanza ni kuonana na wazee wa mkoa ule, kote. Toka niko Makamu wa Rais mpaka nimekuwa Rais, huo ndiyo mtindo wangu, nikifika ni kuonana na wazee wa mkoa.
Tatizo linakuja hapa Dar es Salaam ni mji, kwa hiyo ukiwa Dar es Salaam unajihisi niko Dar es Salaam makao makuu. Ukiwa Dodoma, [unajiambia] niko Dodoma makao makuu. Lakini nikifanya ziara huko mikoani la kwanza kufanya ni kuonana na wazee, nasikiliza shida zao, nasikiliza maoni, yote tunayajua, na tunayapeleka wizarani kwao ili yafanyiwe kazi.
Na katika tunayoyafanyia kazi ni hilo la kujua kwamba kila tunapozeeka na miili yetu nayo inahitaji haja maalumu ya matibabu. Kwa hiyo, hilo nalo tumelishughulikia.
Haki na wajibu
Ndugu zangu baada ya kusema hayo, niseme tena kuna madai ya haki, lakini haki huja baada ya wajibu. Fanya wajibu wako, udai haki. Lakini pia katika kudai haki, tumekubaliana njia za kudai haki. Kwa hiyo, timiza wajibu wako, useme mimi nimetimiza wajibu wangu, lakini haki hii sikuipata.
Kwa hiyo, nenda kwenye vyombo vinavyotoa haki, wende ukadai haki yako. Japo wanasema haki haiombwi, hudaiwa, siyo madai haya waliyofanya wenzetu. Hapana, tumeweka vyombo vya madai ya haki. Kwa hiyo, wale wote wenye madai ya haki tutimize kwanza wajibu wetu, halafu twende tukadai haki zetu.
Nimesema mjenga nchi ni mwananchi, kwa hiyo sisi ndiyo wananchi wa Tanzania, uwe unatambua uwepo wa Serikali hii, uwe hutambui uwepo wa Serikali hii. Serikali ipo, inaendesha Tanzania, na sisi ndiyo wananchi wa Tanzania, tunaotakiwa kusimama, kushikana, kufanya umoja wetu, kuweka nguvu kwenye amani na utulivu wa nchi yetu.
Ndugu zangu, kaka zangu, dada zangu na wadogo zangu, niwashukuru. Niwashukuru sana kwa nafasi hii mlionipa, niwashukuru kwa jukwaa hili mliloliandaa, nimewasikia, mmetusikia.
Nataka niwaambie: wakati wowote mna haja ya kuonana na mimi, basi mimi niko tayari kama Samia, kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii. Niko tayari kuonana nanyi wakati wowote. Kama nina kazi, nitawaambia kipindi hiki nina kazi, tufanye kipindi kingine. Lakini niko tayari kwa mazungumzo.
Asante sana!