Moja ya changamoto kubwa katika malezi ni pale wazazi tunapokuwa na mtazamo tofauti kuhusu namna ya kumlea mtoto. Inaweza kuwa kuhusu nidhamu; mmoja anaamini adhabu kali ndo njia sahihi ya kuadabisha, mwingine anaamini katika mazungumzo ya upole.
Au labda ni kuhusu majukumu ya nyumbani, masuala ya shule, matumizi ya simu, au hata muda wa kulala. Kwa jicho la nje maswala haya yanaweza kuonekana kama ni madogo, lakini ndani ya familia yanaweza kuleta mkanganyiko na msongo wa mawazo kwa mtoto.
Lakini jambo moja la muhimu tunapaswa kujua ni hili: kutofautiana ni kawaida. Hakuna wazazi wawili waliokuzwa kwa njia moja au waliopitia malezi sawa utotoni. Tofauti hizi mara nyingi hutokana na misingi tuliyokulia, hofu tunazobeba, na maadili tunayothamini.
Hata hivyo, mtoto anahitaji utaratibu. Anahitaji kujua mipaka, anahitaji kuona wazazi wake wakiwa upande mmoja, na anahitaji kuhisi kwamba yuko salama hata wazazi wanapokuwa na mitazamo tofauti.
Tufanyeje?
Tukae na kuzungumza kwa utulivu. Tukigundua tumetofautiana kuhusu jambo fulani, tujipe muda wa kukaa chini na kulizungumzia bila haraka. Tuongee kuhusu hisia zetu, hofu zetu, na sababu zinazoathiri maamuzi yetu. Tukiwa na utulivu, tunaelewana zaidi badala ya kushindana.
SOMA ZAIDI: Mwalimu v Mzazi: Tunavyoweza Kushirikiana Kutatua Migogoro ya Watoto Bila Upendeleo
Tujikumbushe kuweka maslahi ya mtoto kwanza. Tukumbuke kuulizana swali hili muhimu: Uamuzi huu unamsaidiaje mtoto wetu? Tukiwa na swali hili mbele, mazungumzo yanakuwa mepesi zaidi, hasira zinapungua, na tunaanza kuona mantiki ya mawazo ya mwenzetu na kupata suluhisho linalomsaidia.
Tusigombane mbele ya mtoto. Hata kama bado hatujamaliza majadiliano yetu, tujitahidi kutokumuonyesha mtoto kuwa tunapinzana. Watoto husoma mfumo wetu wa mawasiliano, hivyo tuwe na utaratibu wa kuzungumza faraghani kwanza, halafu turudi kwao tukiwa tumefikia msimamo mmoja.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwasaidia Watoto Wetu Wanapohisi Hofu Katika Kipindi Hiki?
Tukubali kuwa sio lazima mzazi mmoja kuwa sahihi. Kuna wakati ambao suluhisho halitakua limetoka kwa mzazi mmoja au wazo la mzazi mmoja.
Ni jambo la kawaida, Ikitokea hivyo basi itatubidi tutafute suluhisho ambalo litakua ni mchanganyiko wa mawazo ya wazazi wote. Hapa tunamfundisha mtoto kuwa katika familia kuna kutokuelewana lakini tunaweza kuzungumza kwa kuheshimiana bila kushindana.
Hakuna wazazi wanaofanana na hakuna haja ya kufanana. Kilicho muhimu ni kuunda daraja kati ya tofauti zetu ili mtoto apate utulivu, mwongozo, na upendo. Tofauti zetu zisiwe tatizo bali ni nafasi ya kukua pamoja. Tujifunze, tujirekebishe, na tusonge mbele tukishakamana pamoja.