The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar: Maadili Kama Mkakati wa Kisiasa

Maadili bila mkakati ni sauti isiyosikika; na mkakati bila maadili ni nguvu hatari kwa taifa.

subscribe to our newsletter!

Katika historia ya siasa za Zanzibar, Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) imekuwa ikitangazwa kama suluhisho la migogoro ya kisiasa na njia ya kudumisha amani. 

Hata hivyo, uzoefu halisi wa Wazanzibari unaonyesha kuwa mara nyingi SUK imekuwa chombo cha kisiasa cha kuzima madai ya haki badala ya kuyatatua. 

Ndiyo maana mjadala wa kujiunga au kutojiunga na SUK haupaswi kuwa wa hisia au presha za muda mfupi, bali uwe wa misingi, maadili, na mustakabali wa taifa.

Mfano hai ni SUK zilizopita, ambapo vyama vilishirikiserikalini, lakini misingi ya uchaguzi haikubadilika. Tume za uchaguzi zilibaki zilezile, taratibu za uchaguzi zilibaki na dosari zilezile, na malalamiko ya uchaguzi hayakutatuliwa kwa haki. 

Mwisho wa siku, wananchi waliendelea kupoteza imani na sanduku la kura. Ushiriki huo haukuzaa haki, bali ulihalalisha mfumo uliokosa uhalali. Hili linatuonyesha wazi kwamba kushiriki madaraka bila kuyabadilisha ni sawa na kushiriki dhuluma kimya kimya.

Ali Muhsin Al-Barwani, mwanasiasa na mwanadiplomasia nguli wa Kizanzibari, aliwahi kusema: “Kile kilicho sahihi kimaadili ni busara kisiasa.”

SOMA ZAIDI: Kwenye Hili la SUK, ACT-Wazalendo Wamekalia Kuti Kavu 

Kauli hii ina uzito mkubwa sana katika muktadha wa Zanzibar. Maamuzi ya kisiasa yanayokiuka maadili huweza kuonekana kuwa ya busara kwa muda mfupi, lakini huishia kugharimu chama, yaani ACT Wazalendo, na taifa kwa muda mrefu. 

Kujiunga na SUK bila masharti ya mageuzi ya kimuundo kunaweza kuleta vyeo leo, lakini huua uaminifu wa chama kesho, na huacha jeraha la kisiasa kwa wananchi.

Kwa mtazamo wangu, dilema ya SUK haiwezi kutatuliwa kwa kusema “ndiyo” au “hapana” tu. Jibu sahihi ni ushiriki wa masharti makali na yanayotekelezeka, au kutojiunga kabisa. 

Ushiriki wowote unaopendekezwa lazima uambatane na ratiba ya wazi ya mageuzi ya uchaguzi, si ahadi zisizo na tarehe. Lazima kuwe na dhamana za kisheria, si maneno ya kisiasa yanayobadilika kulingana na mazingira. 

Vilevile, ni lazima kuwepo kwa mifumo huru ya usimamizi na uangalizi, pamoja na uwajibikaji wa wazi kwa umma endapo makubaliano yatakiukwa. Bila misingi hii, SUK hubaki kuwa mtego wa kisiasa badala ya suluhisho.

READ MORE: Kwa Nini Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Imefeli? 

Wakati huo huo, kukataa SUK bila mkakati mbadala pia ni kosa. Chama hakiwezi kudai haki kwa maneno pekee bila kujenga nguvu za muda mrefu. 

Hii inahitaji kuwekeza katika elimu ya kisiasa kwa wananchi, kuandaa mapambano ya kisheria na kikatiba, na kujijenga kama mbadala halisi wa uongozi unaoaminika. Maadili bila mkakati ni sauti isiyosikika; na mkakati bila maadili ni nguvu hatari kwa taifa.

Zanzibar haihitaji amani ya juu juu inayojengwa juu ya ukimya wa waliodhulumiwa. Inahitaji haki, hata kama haki hiyo ni ngumu, inachukua muda, na inahitaji ujasiri wa kisiasa. Historia imetuonyesha mara nyingi kuwa amani isiyo na haki huvunjika, lakini haki hujenga amani ya kudumu.

Kwa hiyo, kulinda mustakabali wa Zanzibar, mustakabali wa chama, na heshima ya siasa zetu, ni lazima tuchague njia inayounganisha maadili na busara ya kisiasa. Kwa sababu, kama alivyosisitiza Ali Muhsin Al-Barwani, kile kilicho sahihi kimaadili ni busara kisiasa.

Bakran Awadh Ali ni mwanafunzi wa udaktari na mchambuzi chipukizi wa masuala ya kisiasa na sera za umma, mwenye mwelekeo maalum katika utawala bora, demokrasia, na uchumi wa kisiasa wa Zanzibar. Anapatikana kupitia bakranawadh2515@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×