Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza leo Januari 29, 2026, kumteua Dkt. Rahma Salim Mahfoudh kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ambapo atasimamia masuala ya utawala na udhibiti wa ndani wa Benki Kuu. Kabla ya uteuzi huo Dkt Rahma Mahfoudh alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ikiwa ni takribani miezi miwili toka ateuliwe na Rais Hussein Mwinyi.
Dkt Mahfoudh anakuwa mwanamke wa tatu kushika wadhifa wa Naibu Gavana katika historia ya BOT, ambapo uteuzi wake umefuata uteuzi wa Sauda Msemo aliyeteuliwa na Rais Samia kuwa Naibu Gavana mnamo Juni 01, 2022.
Naibu Gavana ni wasaidizi wa Gavana, ambapo huwa wanne. Hawa ni sehemu muhimu ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu pamoja na Gavana. Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ndio chombo cha juu zaidi cha maamuzi katika taasisi hiyo nyeti Tanzania.
Wajumbe wengine wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ni pamoja na Mwakilishi wa Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Pia kuna Wakurugenzi wanne wasio watendaji na Katibu wa Bodi. Wakurugenzi hawa ni pamoja na Nassor S. Ameir ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), pia Ngosha S. Magonya Mtendaji wa muda mrefu wa Wizara ya Fedha, pia Profesa Esther Ishengoma, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na Esther Manyesha.