Akizungumza na The Chanzo katika mahojiano ya ana kwa ana, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta Tanzania (TAOMAC), ameeleza kuwa tathmini ya awali iliyofanywa na waagizaji, inaonesha kuwa mshtuko wa bei ya mafuta duniani unaweza kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea kutokana na vita inayoendelea Mashariki ya Kati.
“Tathmini ya wanachama [waagizaji mafuta] na maoni ya wadau katika sekta hii ni kwamba mshtuko wa bei wa sasa, labda ni haijawahi kutokea; hata mgomo wa kuuza mafuta wa mwaka 1973 haifanani na hii,” ameeleza Mgaya mnamo Machi 21, 2026.
“Kwa sababu ndani ya wiki mbili mafuta yamepanda bei kwa zaidi ya asilimia sabini. Haijawahi kutokea ndani ya wiki mbili mafuta kupanda bei kwa zaidi ya asilimia sabini,” aliongeza zaidi.
Mgaya pia ameeleza kuwa baada ya eneo la Mlango wa Bahari wa Hormuz kufungwa, eneo ambalo zaidi ya asilimia 20 ya mafuta ya dunia yanapita; inafanya hali ya sasa kuwa mbaya zaidi kuliko hata wakati wa COVID na vita vya Ukraine.
Mlango wa Homuz unapitisha mafuta kutoka katika chi mbalimbali ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Kuwait, Iraq, Iran na Saudia Arabia. Toka vita hiyo ianze lango hilo limefungwa, ambapo Mgaya anafafanua hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania ambapo sehemu kubwa ya mafuta yanatokea ukanda huo.
“Lakini pia tumeshuhudia kwamba ile Strait of Hormuz imefungwa. Haijawahi kufungwa, ndiyo mara ya kwanza na kama ulivyosema kwamba 20% ya mafuta yanayokwenda katika soko la dunia yanapita pale. Lakini nadhani kwetu sisi ni zaidi ya hiyo kwa sababu unakuta kwamba mafuta mengi yanayokuja upande wa Afrika Mashariki, yanatoka kwenye maeneo ya jirani yaani viwanda vya kusafisha mafuta vilivyopo Singapore na India,” anafafanua Mgaya.
“Lakini ukiangalia viwanda vingi vya kule vya kusafishia mafuta vinachukua mafuta ghafi kutoka kule Ghuba ya Mashariki ya Kati. Kwa hiyo ina maana kwamba vile vikikosa mafuta ghafi moja kwa moja hata uzalishaji utapungua na hivyo hata patikanaji utapungua,” anaendele kufafanua.
Moja ya athari inayotegemewa kuonekana moja kwa moja ni kupanda kwa bei ya mafuta Tanzania na nchi zingine.
“Mfumo wa uingizaji mafuta Tanzania, tunaingiza mafuta miezi miwili kabla. Kwa sasa tunavyo ongea hakuna athari, kwa sababu mafuta yanauzwa sasa hivi ni mafuta ambayo yalikuwa tayari yameshanunuliwa na yameshaingizwa nchini au yako njiani yanakuja kabla ya ile vita,” anafafanua Mgaya.
Hata hivyo Mgaya ametahadharisha kuwa mafuta yaliyoagizwa baada ya vita kuanza yataenda kushuhudia kupanda kwa bei kutokana na mshtuko uliojitokeza.
“Sisi kutokana na bei zinavyopanda huku duniani tumejaribu kufanya uchambuzi wa haraka haraka na kugundua kwamba bei itapanda kwa karibu shilingi 1,800 kwa lita kwa hiyo unazungumzia zaidi ya shilingi 4,000 na kitu huko kwa lita,” aliongeza.
Mgaya amefafanua kuwa tayari wao kama Waagizaji Mafuta wameshafanya mazungumzo kadhaa na serikali na hatua zimeanza kuchukuliwa katika kukabiliana na hali hiyo inayotegemewa.