Ofisi ndogo ya Bunge Dodoma, Mtaa wa Shaaban Robert. Nimesimama eneo la mapokezi kusubiri kupanda ngazi kwenda kwenye vikao vya Kamati za Bunge. Mtu mzima mmoja kanisalimia na kuomba kunizungumzisha. Tukakaa kwenye viti vya chuma palepale mapokezi. Akajitambulisha kuwa yeye ni Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini.
Sababu ya kuniomba kuzungumza ni mapato ya gesi asilia kutoka kisiwa cha Songosongo, gesi ambayo ilizalisha umeme katika mitambo ya umeme ya Ubungo, Dar es Salaam. Mbunge huyo wa Kilwa Kusini, ambaye sasa ni marehemu, Selemani Bungara, alinieleza kuhusu changamoto ya kampuni ya Pan Africa Energy inayochimba gesi katika wilaya ya Kilwa kutolipa ushuru wa huduma wilayani humo.
Hivi ndivyo nilivyokutana na ndugu Bungara, al maarufu Bwege. Ilikuwa mwaka 2011 katika kipindi changu cha pili Bungeni, nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC). Ninaamini kuwa alinifuata kutokana na ushauri wa mke wake, mama Mwanawetu Zarafi, ambaye nilihudumu naye Bungeni na kwenye kamati hiyo. Mama Zarafi alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Mkoa wa Lindi kupitia Chama cha Wananchi (CUF).
Baada ya mazungumzo yale nilimuahidi kusaidia kulitafutia ufumbuzi jambo lile. Tuliwaita Shirika la TPDC katika Kamati. Kwa msaada wa aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, tuligundua kuwa kampuni ya PAET ilikuwa inalipa ushuru wa huduma (service levy) kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ambapo kulikuwa na ofisi zao.
Jitihada zilifanyika, tukaboresha sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa, na kutambua kuwa kampuni italipa ushuru wa huduma pale ambapo uzalishaji umefanyika, na sio kule pesa zinakusanywa.
SOMA ZAIDI: Juma Duni Haji: Tafsiri ya Mwanasiasa Mnyenyekevu
Ndugu Bungara ametangulia mbele ya haki. Baada ya kuugua kwa muda mrefu hatimaye amekwenda kwa mola wake. Sisi wanadamu tumefunzwa kumshukuru Mungu kwa kila kitu na kusema hakika sisi wote ni wa mwenyezi mungu na kwake tutarejea.
Mapenzi kwa Kilwa
Selemani alikuwa anaipenda Kilwa. Kilwa ilikuwa kwenye moyo wake. Aliwapenda watu wa Kilwa. Simulizi niliyoitoa hapo juu ni moja ya mfano mmoja tu ya jitihada zake kutafuta haki za watu wa Kilwa.
Ikumbukwe kuwa gesi ya Songosongo ilianza kuchimbwa mwaka 2004, hadi kufika mwaka 2011 mapato yake yalikuwa yanachukuliwa na Manispaa ya Ilala. Kabla yake kulikuwa na Wabunge, tena wasomi zaidi yake. Yeye, kwa namna yake, aliweza kupatia ufumbuzi na jambo kubwa la maendeleo kwa jimbo lake.
Selemani alikuwa mtetezi wa haki. Katika miaka ya 2017 – 2019 kulikuwa na changamoto ya watu kuuwawa katika maeneo ya MKIRU – Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Mauaji yale yalifika mpaka Kilwa ambapo watu walipotea na kuuwawa. Katika msikiti wa Chumo, Kilwa Kaskazini, askari walivamia na kuua watu. Selemani alileta jambo lile Bungeni.
Aliongea kwa uchungu sana. Kufuatia hoja yake ile na kwa msaada wa taasisi mbalimbali, ikiwemo Shura ya Maimamu ya Sheikh Issa Ponda, nilifanikiwa kuwasilisha Bungeni orodha ya watu 348 waliohofiwa kuuwawa katika eneo la MKIRU. Ndugu Bungara aliendelea na utetezi wa haki mpaka mauti yalivyomkuta.
Msimamo usioyumba
Selemani alikuwa na msimamo kwenye jambo analoliamini. Wakati mwingine ni msimamo uliomletea shida na wenzake, lakini alibaki na msimamo wake. Alianza siasa za upinzani akiwa katika chama cha CUF, ambacho ndimo alihudumu kama Mbunge wa Kilwa.
SOMA ZAIDI: Buriani Bernard Membe, Mwanasiasa Sungura, Mwanadiplomasia Nguli
Kutokana na kupishana mitazamo na kundi mojawapo ndani ya chama, alihamia chama chetu cha ACT Wazalendo. Kwetu pia tulipishana kwenye msimamo na hatimaye alitangaza kuhama chama chetu na kujiunga na chama cha CHADEMA. Sio kwamba Selemani alitetea haki za wengine tu, bali pia alisimamia anachoamini ni sahihi.
Selemani alikuwa na namna yake ya kufikisha hoja zake. Wakati mwingine aliweza kuifanya hoja nzito sana kuonekana ni jambo linachochekesha. Namna alivyowasilisha hoja Bungeni ilikuwa ya pekee sana.
Alitumia ucheshi mkali na mtindo wa drama ili kufikisha mambo mazito ya kitaifa. Alizungumza kwa ustadi ambao ulifanya hata wapinzani wake wasikilize kwa makini. Ni sifa hii iliyonifanya nimkumbuke mara moja niliposoma kitabu cha Rais wa zamani wa Marekani, John F. Kennedy, Profiles in Courage.
Katika kitabu hicho, Kennedy anasimulia hadithi za wabunge waliosimama kidete kwa haki hata kinyume na chama chao na shinikizo kubwa. Vivyo hivyo, Selemani Bungara alikuwa “Profile in Courage” halisi wa Bunge la Tanzania — mbunge aliyezidi kufikiria haki ya watu wake kuliko umaarufu au starehe za kisiasa.
Ndugu Bwege, umetutangulia mbele ya haki baada ya kuugua kwa muda. Umetuachia kumbukumbu na somo kubwa la uadilifu, ujasiri na upendo kwa watu. Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama mstaafu wa chama cha upinzani, ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia zruyagwa@icloud.comau X kama@zittokabwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.comkwa ufafanuzi zaidi.