The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Buriani Bernard Membe, Mwanasiasa Sungura, Mwanadiplomasia Nguli

Daima nitasimama na mema ya Membe, mwanafamilia mwema, mwanaharakati mahiri, Mkristo safi, mgombea urais mtata na rafiki wa kweli.

subscribe to our newsletter!

Joyner William “Willie” Traynor ni mmoja wa wahusika katika riwaya ya John Grisham The Last Juror. Waliosoma kitabu hiki, wanafahamu sifa kubwa ya Willie ni uandishi wa tanzia.

Katika jamii za kawaida, uandishi wa tanzia siyo fani. Binafsi, ningekuwa mwandishi, hii ingekuwa fani yangu. Sina sababu maalum, pengine ni kutokana na mapenzi yangu kwa Willie.

Leo, nimeketi kwa majonzi, naandika tanzia yangu ya kwanza. Inamhusu mzee wangu, baba yangu, kwani wanaye wamekuwa rafiki zangu kwa muda mrefu kabla sijakutana naye.

Baadaye nilikutana na mzee wangu huyo, nikafanya naye kazi kwa muda mfupi. Ni kipindi kilichokuwa na mafunzo lukuki.

Tanzia yangu inaweza kuwa tofauti na za wengi walioandika. Nimejizuia kusoma za wengine wote ili niandike ya kwangu kwa ukamilifu bila kubebwa na hisia za wanzangu. Baada ya kumaliza yangu, nitasoma za wengine wote.

Namwongelea Membe niliyemfahamu kama BM, uhusiano wake nami pamoja na wengi tuliowahahamu, vilevile mafunzo lukuki tuliyoyapata kutoka kwenye maisha yake.

Kuna mengi nisingeweza kuyazungumza alipokuwa hai, kwani yangeweza kuleta mtafaruku kwenye shughuli zake za kisiasa, ila sasa naweza kuyasema, kazi ameshaimaliza na safari ameshaifikia.

Mwanadiplomasia

Membe huyu nilimfahamu katika vyombo vya habari na kwa watu wake wa karibu. Namkumbuka rafiki yangu (jina namhifadhi), tukiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, tukielekea Zanzibar, alikuwa akizungumza kwa simu na mmoja wa viongozi wa juu wa Jumuiya  ya Madola.

Kiongozi yule wa Jumuiya ya Madola, alimweleza rafiki yangu wasifu mrefu wa Membe. Kilikuwa kipindi cha ushawishi ili Tanzania impendekeze Membe kugombea Ukatibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola. Hata hivyo, pamoja na sifa zote, watawala wa wakati huo hawakutaka Membe awe.

Bado naikumbuka ile simu na sifa nyingi za Membe zilizotajwa kwenye nyanja ya diplomasia.

Membe huyu nilimsikia kutoka kwa Cessy, Richard na baadaye sana Dennis. Mara nyingi tulipokuwa maeneo yetu, Oysterbay, kila Jumamosi, Richard na Cessy, ilipofika mchana walituacha kwenye burudani za ujana na kuelekea nyumbani kuonana na baba yao kwa ajili ya masuala ya kifamilia.

Majukumu mengi ambayo BM alikuwa nayo ya kulitumikia taifa, hayakumzuia kutenga muda maalum wa kukutana na familia yake, hususan kuzungumza na wanaye kuhusu elimu na maisha.

Kwa hili, BM ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine wa leo na hata kesho. Kwa namna yoyote, familia yako ni kipaumbele. Tujifunze hili. Buriani Membe!

Membe huyu nimemfahamu kupitia milango yangu mitano ya ufahamu. Nilikaa naye, niliyaona na kuyatambua maono yake. Niliufahamu ujasiri na uthubutu wake. Membe hakuwa mwoga.

Ni viongozi wachache ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali, kati ya mwaka 2015 hadi 2021, walioweza kumpinga hayati Rais John Magufuli kwa hoja. Membe hakuomba msamaha kama ambavyo wengine wote walifanya baada ya kutofautiana na Magufuli.

Mcheshi

Kwa ambao hawakumfahamu kwa karibu, hawakufahamu hulka ya Membe ya ucheshi. Mara kadhaa aliniita ofisini kwake, pia alifika ofisini kwangu, tunakaa na kuzungumza. Tunacheka tunafurahi.

Tunakunywa kahawa, chai au maji, huku yeye akiniusia mengi kwa ajili ya uzalendo wa nchi, uongozi, ujasiri na uthubutu kama kijana.

Namkumbuka sana akinisisitiza kwa sauti ya taratibu, ‘Sikiliza Venance.’ Halafu ananihadithia matukio kadhaa kati ya mengi, likiwemo la Zimbabwe alipokuwa mwangalizi wa uchaguzi. Uhadithiaji wake ulikuwa na mvuto na uliojaa ucheshi.

Membe alikuwa mwalimu, si wa darasani, bali wa maisha na uongozi. Namkumbuka akiishika kalamu yake yenye wino pande mbili. Mmoja mwembamba mithili ya kalamu ya gololi na wa pili kama marker pen ya rangi ya kijani.

Sikuwahi kumuuliza kwa nini alipenda rangi ya kijani. Najilaumu sikuwahi kumshauri abadili iwe zambarau! Membe alikuwa mwalimu wa wengi, alifundisha namna ya kuwa kiongozi na jinsi ya kuishi na viongozi. Na alisistiza kusimamia unachokiamini hata kama jamii yote itakupinga.

BM alikuwa ni mwenye imani kwa vijana. Katika umri wangu na uzoefu mdogo wa mambo ya uongozi na viongozi, mimi na rafiki yangu (jina nalihifadhi), Membe alituamini, akatutuma moja ya nchi Kusini mwa Afrika, kukutana na kiongozi mkubwa wa taifa hilo na kufikisha ujumbe, pia kumrudishia majibu.

Hili ukiliangalia kwa macho ya kawaida, utaliona dogo. Hata hivyo, aina ya ujumbe na mpokeaji, ni wazi alituamini. Ndiyo maana naweza kusimama na kusema Membe aliamini sana vijana.

BM alikuwa mwenye utu na upendo. Kuna hadithi ya kuchekesha kumhusu huyu Membe mwenye utu. Nilikuwa naye Lindi, nyumbani kwa kaka au dada yake, sikumbuki vizuri.

Baada ya uchovu wa siku nzima tukitoka kijijini Lupaso kumzika mzee wetu, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, tuliletewa chakula. Membe alinyanyuka na kutupakulia chakula sisi wote tuliokuwepo.

Pili, nilikutana naye kwenye mgahawa mmoja, Mikocheni, Dar es Salaam. Tuliagiza chakula, kila mmoja cha kwake. Tulipoletewa, akanyanyua sahani, akapunguza chakula chake, akaongeza kwangu. Alifanya hivyo akinipigia hadithi za seminari, namna walivyoishi kwa utu, umoja na upendo.

Kuna siku nikitokea Zanzibar na rafiki yangu kwenye mashindano ya mchezo wa Golf Sea Cliff Resorts, tulisimamishwa uwanja wa ndege na kusumbuliwa sana na askari.

Yule askari alinikagua katika mazingira yasiyo ya kawaida. Mwisho mmoja wa wale wana usalama akasema, “Mbona hawana kitu chochote?”

Binafsi nilifahamu sababu kubwa ya jambo lile ni ukaribu wangu na Membe, hasa kipindi kile cha uchaguzi, yeye akiwa mgombea urais.

Nilipofika Dar es Salaam, nilimfahamisha kilichotokea uwanja wa ndege, siku iliyofuata alikuja ofisini kwangu na kunipa pole. Baadaye tukaendelea na mazungumzo kama ilivyokuwa kawaida yetu. Huu ndiyo urafiki.

Muadilifu

Mengi yaliongelewa kuhusu Membe kuwa mtu tajiri sana. Kweli utajiri siyo dhambi, ila mwanasiasa akiwa tajiri humpunguzia alama za uadilifu.

Wengine walisema alipewa fedha nyingi na aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, vilevile mfanyabiashara Aliko Dangote. Nilikaa naye. Sikuwahi kumwona Membe tajiri. Niliyemfahamu mimi ni mwadilifu na mnyenyekevu.

Membe alikuwa mwanasiasa na nilimfahamu vema. Siasa ina mengi, ukweli na uongo. Ni propaganda, vilevile mchezo wa mawazo yaliyo bora.

Wakati Membe anaondoka CCM na kujiunga na ACT-Wazalendo, alisema kuwa angekula kiapo Uwanja wa Taifa, kisha angesaini kitabu kwa wino mwekundu, na jioni yake angefanya tafrija kubwa Ikulu.

Ulikuwa mfano wa siasa, lazima uwaoneshe watu kwamba huingii kwenye ushindani wa kisiasa kwa unyonge, bali kushinda hata kama wafuasi wako ni wawili.

Rekodi ya Membe kusimama kama mgombea urais ni pale alipobeba tiketi ya ACT-Wazalendo, Uchaguzi Mkuu 2020. Mwaka 2015, alijaribu kuomba tiketi ya CCM lakini hakupata.

Nilifanya mambo mengi na Membe akiwa mgombea urais. Nilisafiri naye, nilishiriki vikao vyake na tulifanya mambo mengi pamoja.

Baadaye, ACT-Wazalendo, kwa ajili ya kukuza nguvu ya upinzani dhidi ya Magufuli, uongozi ulitangaza kumuunga mkono mgombea wa Chadema, Tundu Lissu.

Membe hakupinga kumuunga mkono mgombea mwingine wa upinzani ili kukuza nguvu, ila hakumkubali Lissu. Mimi nilimshauri amkubali kwa sababu ndiye alikuwa chaguo lenye nguvu.

Alisema, nafsi yake haikukubali. Hapo, mimi na yeye tulitofautiana, lakini tofauti hiyo haikuvunja uhusiano wetu. Niliendelea kumnadi Lissu, naye akabaki kung’ang’ania ugombea wake wa ACT-Wazalendo.

Pamoja na yote, tuliendelea kuheshimiana na kuwasiliana. Hili ni jambo muhimu sana, hata mkitofautiana kiitikadi na mitazamo, haitakiwi kuondoa uhusiano wenu kamwe.

Mengi naweza kueleza kuhusu Membe kama mgombea urais. Kikubwa alikuwa mtu wa mipango. Alikuwa na mtandao mzuri wa mawasiliano. Kama mgombea, alikuwa na baraka za viongozi wengi wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Matendo mema

Funzo kubwa ambalo nimelipata kwenye kifo cha Membe ni kuchagua matendo mema. Si kwamba hakuwa na kasoro za kibinadamu, isipokuwa nimeweka uzani sawia wa maisha ya Membe, mema yana uzito mkubwa kuliko mabaya.

Daima nitasimama na mema ya Membe. Mwanasiasa sungura, mwanadiplomasia nguli, mwanafamilia mwema, mwanaharakati mahiri, Mkristo safi, mgombea urais mtata na rafiki wa kweli.

Pole kwa mama Membe, Cessy, Richard na Dennis. Pole kwa familia na marafiki.

Tangulia BM, tangulia Mwamba wa Kusini, Mjanja wa Mtama. Lala ngoxolo tata Membe!

Venance Msebo alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Hamasa ya Kifedha, kampeni za urais za Membe za 2020. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia venance.austin@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *