The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Upande wa Pili Usiozungumzwa wa Michezo ya Kubashiri ‘Kubeti’ Tanzania

Uraibu, kupoteza fedha na kuvunjika kwa familia ni baadhi ya maswahibu yanaowakuta wadau waliojikita katika michezo ya kubashiri Tanzania

subscribe to our newsletter!

Kwa kila dakika moja ya kila siku kati ya shilingi milioni 20 mpaka milioni 50 za Kitanzania zinazunguka katika  michezo ya kubashiri. Zaidi ya nusu zya fedha hizi zinatokana na ubashiri wa michezo hasa hasa mpira wa miguu.

Kwa serikali, michezo ya kubashiri imekuwa moja ya njia ya kukusanya kodi ambapo mapato ya kikodi yameongezeka kutoka Bilioni 33 mwaka wa fedha 2016/17, mpaka kufikia Bilioni 261 kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Utafiti wa Geopoll wa Aprili 2025, ulionesha sehemu kubwa ya wanaoshiriki michezo hii Tanzania, hutumia chini ya dola 10 ambayo ni takribani 25,000 kwa siku; hata hivyo katika nchi ziliangaliwa katika utafiti huo, Watanzania walionesha kucheza mara kwa mara.

Tumezungumza na baadhi ya wadau wanaocheza michezo ya kubashiri, ambapo ukiacha picha za ushindi, jumbe za motisha katika redio na kwenye mitandao ya kijamii; kuna upande wa michezo ya kubashiri unaonekana kujificha au kufichwa mbele ya kadamnasi, wengi wakiugulia chini chini, na hata wengine kupoteza dira.

Upande wa pili

Ni siku nyingine tena kwa Joachim Joseph, imekuwa kawaida kwake kuwa anapomaliza kazi zake za uchomeleaji ratiba ya kwanza aliyoipanga ni kwenda kwenya mashine ya dubwi, kutumia chochote alichopata kwenye uchomeleaji,  kucheza na kuangalia kama anaweza kupata chochote cha ziada.

Ni ratiba ambayo Joachim anaifuatiliza kama dini na amekuwa akifanya hivyo toka mwaka 2023. Joachim ambaye ni baba wa watoto wanne anaeleza kuwa alivutiwa kucheza baada ya kuona watu wakicheza na kupata zaidi ya kiwango walichoweka.

Hata hivyo hali hii ya Joachim, imeanza kuathiri familia yake, hasa baada ya kuonekana kuna mabadiliko ya mara kwa mara juu ya bajeti ya kifamilia. Kwa kawaida Joachim hutumia takribani shilingi 20,000, kiwango ambacho kinakaribiana na pesa yote anayoipata kwa wastani kila siku kwa kazi zake za uchomeleaji.

Vijana wanaojihusisha na michezo ya ubashiri wakiongea na mwandishi

Baada ya athari kubwa kuonekana katika familia, mke wa Joachim akamtaka aache michezo hiyo, jambo ambalo limeshindikana, na kwa sasa anacheza kwa kificho.

“Hii michezo inashusha sana maendeleo, kwa sababu mwenzio anahitaji mfanye jambo fulani. Mnaweza mkakubaliana sawa, kwa sababu kuna pesa sehemu fulani utakapo ipata unasema ngoja naweza kuongeza. Ile kusema kuongeza sasa, unaenda kutupa kule,” anaeleza Joachim akiongea na The Chanzo.

“Kwa kuwa ninapocheza yeye haoni inakuwa ni vigumu kujua. Kwa hiyo unakuta udanganyifu ule unakuwepo lakini sasa unafanyaje? Lakini hakuna kitu kitakuwa na siri katika dunia hii. Vitu kama hivi vinaathiri sana ndoa,” Joachim anafafanua kuhusu ahadi yake ya kuacha michezo hiyo na namna ndoa yake ilivyoathirika.

Suala la michezo ya kubashiri limemfanya Joachim amekuwa kama mateka wa mamuzi yake ya kila siku, ambapo anaeleza kuwa suala la kuacha kucheza hataki lakini pia madhara yanaendelea kujikusanya.

“Ukishaliwa, na ulipanga kwamba unaenda nyumbani ukiwa na pesa lazima utawaza je watoto wanaishije. Kwa hiyo ile kuwaza watoto Wataishije, na umesha beti umeliwa hela yote lazima unakuta kichwa chako hakikai sawa,” anaeleza Joachim.

Niko radhi nisile

Silas Bugotabululu (33), ni mmoja wa wadau ambao anajieleza kuwa kama ‘mkamaria’ mwenye uzoefu, na anasema alipofikia hawezi kuacha michezo ya kubashiri, kwa sababu ameshaonja mafanikio yake.

“Mwaka 2021, nilivyojaribu siku ya kwanza nikawa nimekula, kwa hiyo safari yangu ikaanzia hapo. Niliweka 10,000 nikala 600,000,”anasema Silas baba wa watoto wawili alipokuwa akiongea na The Chanzo.

Silas kwa kiwango kikubwa hucheza michezo ya ubashiriki wa mipira wa miguu,ambapo anaeleza ingawa kuna siku za hasara, siku za mafanikio zimemfanya aone suala la kuacha ‘kubet’ kabisa haliwezekani.

“Ni bora niweke Shilingi 500, 200 lakini niwe nimesha beti kwa hiyo siku. Nisipobeti roho inaniuma sana, ni bora nikabeti nikaliwa lakini lazima nibeti kila siku. Niko radhi nisile lakini nibeti,” anasema Silas huku akiwa ameshika simu yake mkononi akiangalia mechi mbalimbali.

Silas anayefanya kazi ya U-DJ, akiwa anaandaa ‘mikeka’ kwa ajili ya kubashiri

Anaendelea kusisisitiza: “Bora nikabeti halafu nikaliwa yaani nikawa na amani, kwamba hapa nimebeti nikaliwa. Yaani kuliko nisibeti kabisa, kuacha itakuwa ngumu sana. Labda nifikie kiwango changu kwamba nimeshakula mkeka mwingi nikawa na vitu vyangu vinaniingizia hela zaidi ya betting naweza nikaacha.”

Katika sehemu kubwa ya mazungumzo na wadau wa ‘kubet’ moja ya jambo ambalo The Chanzo iliweza kuliona katika maongezi ni wengi wa wachezaji wa kubeti husisitiza kuwa wanapata zaidi, hata hivyo baada ya maongezi ya muda hukubali kuna kupoteza zaidi huku wakiamini kesho au baadaye kutakuwa na ahueni.

Fedheha

Paul Dicklucky (34) ni dereva Guta Dodoma, anaeleza kuwa aliingia kwenye michezo ya ubashiri wa mpira wa miguu, baada ya kuona wenzake wanajaribu na kupata fedha.

“Nakumbuka kwa mara ya kwanza nimebeti niliweka Shilingi 1000, halafu nikapata Shilingi 250,000. Ukiangalia hiyo hela sijafanya kazi, nikawa nimepata kwa hiyo nikaingia,” anaeleza Paul.

Hata hivyo, Paul anafafanua kuwa toka wakati huo, tathmini yake inaonesha amekuwa akipoteza zaidi kuliko anavyopata, huku akiwa hawezi kuiacha tabia ya kucheza michezo hiyo.

“Kuliwa ni kwingi kuliko kula, nikaendelea kucheza. Nikajua pengine nitafika sehemu nitaweza kuacha, lakini hiko kitu hakikuwezekana.Unajikuta unaingia kwenye mfumo wa madeni ambayo hayakupaswa kuwepo,” anaeleza Paul.

Severine Mwasisi (36) anakumbuka akiwa jijini Dar es salaam mwaka 2019 alikuta marafiki zake wakicheza michezo ya kubahatisha kwa kutumia mashine ya dubwi. Mmoja wa marafiki zake alishinda kiasi cha Shilingi 50,000 hali iliyomvutia kucheza. Anasema alicheza kwa miaka mitatu, ni mara nne pekee alibahatika kupata fedha kwenye michezo hiyo.

“Fedha niliyokuwa nikipata haikuizidi Shilingi 100,000. Nilijikuta natumia kiasi kikubwa kuliko ninachokipata nikaona ni hasara. Kwa maumivu niliyoyapata wakati nacheza, nilipoteza hela hata Shilingi 1,000,000 inafika. Hela hiyo ningekuwa nayo mkononi ningekuwa nimepiga hatua, lakini sasa nimesha ichezea kamari, haiwezi kurudi,” anaeleza Severine kwa huzuni.

Ester Joseph (23) ni muhudumu wa baa na mkazi wa kata ya Mkonze mkoani Dodoma, amekuwa akicheza michezo ya kubahatisha kwa kutumia mashine ya dubwi toka 2021. Anaeleza changamoto kubwa anayokutana nayo ni kushindwa kuacha michezo hiyo ingawa tayari amesha amua kuacha.

Esther akiwa amesimama mbele ya mashine ya Dubwi

“Unaweza ukakuta umecheza, umetumia hata 10,000 umeliwa, ukatamani ukachukue hata hela nyumbani uje ucheze,” anasema Ester. “Kwa hiyo kuna muda kweli uchumi unapungua, nina mpango wa kuacha. Kwa sasa hivi naona nikicheza naliwa sana, mambo yangu hayaendi. Nikipata hela nawaza kucheza, kwa hiyo natamani kuacha.”

Uraibu

Daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dkt Kenneth Majolo, anafafanua kuwa hali kama inayowakabili Severine, Paul na Esther ni uraibu.

“Ikishaingia kwenye mfumo wa saikolojia ya mtu, inaenda kumuharibu, kwa sababu hata akipata hela kidogo yeye anawaza kwenda kubeti. Na hii michezo ya kubeti huwa inaleta furaha ya muda mfupi, unakutaka anapata siku moja, siku nyingine hapati. Hiyo inamfanya aone kuna uwezekano wa kupata hela kwa njia ya urahisi,” anafafanua Majolo.

Majolo anaeleza kuwa hatua za juu za uraibu huathiri zaidi mfumo wa kawaida wa maisha ikiwemo ufanyaji maamuzi.

“Kama ni mwanafunzi unakuta anatumia hela ya ada, au wakati mwingine anafanya namna yoyote apate tu hela akabeti. Wakati mwingine inatokea huyu mtu anaingiza hela nyingi sana kwenye kubeti, akikosa ndiyo wale wanaenda kujiua au kuua watu wengine,” anasisitiza zaidi.

Mtaalamu huyu ambaye pia amehusika kwenye kutoa msaada wa kitabibu kwa waraibu wa kubeti, anafafanua kuwa waathirika wa michezo ya kubahatisha kwa sasa si vijana peke yake bali ni watu wa rika zote.

“Elimu haitolewi kwa watu, kiuhalisia michezo hii, ilikuwa inachezwa na watu matajiri. Ila wametuletea nchi zetu za kimasikini za Afrika na mabara mengine. Kwa sababu ndiyo kuna vijana hawana kazi,” anaongeza.

Kuna changamoto pia zinazoonekana katika mifumo ya kiuchumi, kwa mfano katika baadhi ya maeneo kama ya vijijini ambapo kuna misimu ya kilimo, kuamini kuwa kuna kupata hela kupitia ‘kubet’ kunawaondoa au kuendelea kuwapunguza vijana wengi katika shughuli za uzalishaji.

The Chanzo ilifika katika moja ya Wilaya ya pembezoni ya Jiji la Dodoma, Wilaya ya Bahi na kuongea na wadau mbalimbali, ambao walizungumzia namna michezo ya kubashiri inavyoathiri uzalishaji katika jamii.

Diwani wa Kata ya Bahi Ugustino Ndonu ameieleza The Chanzo kuwa athari ya michezo ya kubahatisha katika kata ya Bahi, halmashauri ya wilaya ya Bahi zimeshamiri kwa namna ya kipekee.

“Kuna watu wameshapigana visu kwa ajili ya michezo hii ya kubeti, mmoja amepigwa majuzi wamegombaniana hela. Yule aliyetoa hela hakukubali hela yake iondoke, akachomoa kisu akampiga mwenzake,” anasema Diwani huyu.

Anasema, vijana wilayani humo wameona kubeti ni sehemu ya kujipatia fedha, hali ambayo inawafanya washindwe kufanya kazi za mikono.

“Unamkuta kijana anaamka asubuhi anaenda kubeti, anaona hafanyi kazi anapata fedha kirahisi. Wakati mwingine unamtuma kijana kwa ajili ya shughuli za kijamii, aende akachukue mchele anakuja kukwambia hela imepotea kumbe ameenda kubeti. Tunaona kesho ya vijana ambao hawajitambui.”

Uvurugaji wa namna yeyote wa nguvukazi, hasa maeneo ya kijijini una uwezekano mkubwa wa kuathiri kwa ukubwa ukuaji wa kiuchumi, hasa kwa kuwa tayari maeneo ya kijijini yanaathiriwa na shinikizo kutokana na vijana kuhamia mijini.

Elimu, matangazo

Akizungumza na The Chanzo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, James B. Mbalwe, ameieleza The Chanzo kwa njia ya simu kuwa bodi hiyo imeendelea kutoa elimu kwa Watanzania juu ya athari zinaweza kujitokeza kwa uraibu wa michezo ya kubahatisha.

“Kwa hiyo tumekuwa tukitoa elimu kwa umma, hasa vijana kwamba wahakikishe wanaposhiriki katika michezo hii wanacheza kwa kiasi ama kwa busara. Ili wasije wakaingia katika madhara ambayo yanaweza yakajitokeza kuhusiana na kujihusisha kwao na michezo ya kubahatisha,” ameeleza Mbalwe.

Baadhi ya wadau wanashauri kuwa kuna umuhimu wa kuratibu utitiri wa matangazo yanayofanyika juu ya ‘betting’ ambayo kwa sasa yameshamiri katika vyombo vyote vya habari nchini.

“Leo hii vyombo vya habari matangazo mengi kama sio soka, ni kubeti. Kubeti, kubeti, kubeti, mkeka, kubeti ama sijui nini?,Tunamleaje Mtanzania wa kesho, [tunatengeneza] jamii ya watu wavivu kufikiri, watu wanaopenda njia fupi ni matapeli wa kitaifa,” alitahadharisha mwanahabari  Elizabeth Riziki kwenye kikao cha wadau wa habari mnamo Februari 12, 2026

Hoja hiyo iliungwa pia mkono na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile ambapo alitolea mfano wa nchini Kenya na hatua zilizochukuliwa ikiwemo kuongeza kiwango cha chini cha watu kutumia ili kuzuia wanafuzi.

“Kwenye ‘betting’ tukiacha hivi taifa linaingia kichakani. Miaka minne mitano iliyopita Kenya walikuwa na majibu haya haya. Lakini Agosti 26, 2025 wakapitisha Sheria ya ‘betting’ kwenye ‘Gambling’. Kuanzia sasa nchini Kenya hakuna redio, TV wala mtandao wa kijamii unapaswa kuonesha matangazo ya ‘betting’ kati ya saa kumi na mbili asubuhi mpaka saa nne usiku,” alieleza Balile.

“Tusipolinda watoto wetu tukadhani tunapata bilioni 394 kupitia ile Bahati Nasibu ya Taifa, tutazalisha wezi.Tutajenga taifa lililoharibika,” alitahadharisha zaidi.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×