Kwa Watanzania walio wengi, mitandao ya simu ndio njia pekee iliyo rasmi ya ujumuishi wa kifedha waliyonayo. Tafiti mbalimbali zinaonesha gharama za huduma za fedha kupitia mitandao ya simu zinakabiliwa na changamoto ya mzigo mkubwa wa kodi na tozo, unaoathiri unafuu wa huduma hizi, hasa ukizingatia kwamba benki hazijafanikiwa kuwafikia sehemu kubwa ya Watanzania.
Kwa mujibu wa GSMA, taasisi yenye washirika wa mitandao ya simu zaidi ya 1,000 duniani, nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara zinachangia takribani asilimia 66 ya miamala yote ya fedha kupitia simu duniani.
Kwa Tanzania, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) mpaka kufikia Disemba 2025, akaunti milioni 76.5 za pesa mtandao nchini Tanzania zilifanya miamala takribani bilioni 1.85. Wakati huo huo, bado mabenki ya kibiashara yanaendelea kupata ugumu wa kupenya katika soko na kutoa huduma za kifedha nafuu na zinazofikika kwa wote.
Katika hali hii, huduma za fedha pamoja na miundombinu ya mawasiliano inayowezeshwa kupitia simu zinafanya kazi kama uti wa mgongo katika uchumi wa kidijitali.
Hata hivyo, gharama kubwa za mitandao ya simu zinawatenga wale wanaohitaji huduma hizi zaidi. Mzigo mkubwa wa kodi kwa watoa huduma za simu unaongeza kiasi kikubwa cha gharama kwa mtumiaji wa mwisho. Tathmini ya Innovations for Poverty Action (IPA), iliyochunguza maeneo 41 ya mijini na vijijini Tanzania, ilibaini kuwa gharama za kutoa pesa zipo juu, kwa wastani wa asilimia 8.6, jambo linaloifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye viwango vya juu zaidi vya kodi duniani.
Pigo katika uti wa mgongo hudhoofisha mwili mzima – yaani uchumi wa nchi: mama lishe analazimika kurejea kwenye mtindo hatarishi wa kutunza fedha taslimu chini ya godoro, vijana wabunifu vijijini wanapata ugumu kufikia masoko rasmi, na wajasiriamali wa mijini wanalazimika kutumia mamilioni kwa ajili ya miundombinu ya kidijitali ya kigeni.
Jambo ambalo husahaulika ni kwamba hii pia hudhoofisha uwekezaji wa makampuni ya simu na hurudisha nyuma agenda ya ujumusihi wa kidigitali kupitia miundombinu ya mawasiliano
Gharama kubwa za tozo
Tozo katika huduma za kifedha kwa njia ya simu zimekuwa zikiangaliwa kama kisima kisichokauka, hata hivyo ushahidi unaonesha mzigo mkubwa huleta athari zisizohimilika, kiuchumi na kijamii. Mfano dhahiri ni pale serikali ilipoanzisha tozo za miamala ya kifedha mwaka 2021. Mabadiliko hayo yalisababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa miamala ya mtu kwa mtu na kuathiri utoaji wa fedha kupitia mawakala.
Idadi ya miamala iliporomoka kwa asilimia 38 kati ya Juni na Septemba mwaka huo, huku utoaji wa fedha kwa mawakala ukishuka kwa asilimia 25. Baada ya mabadiliko kadhaa ya tozo, ilichukua takribani miezi 13 kwa miamala ya mtu kwa mtu kurejea katika viwango vya awali kabla ya tozo.
Katika haya yote, mapato ya Serikali yaliathiriwa huku tabia za watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu zikibadilika. Inachukua ushawishi mkubwa kubadili tabia ya mlaji. Ada zinapokuwa nafuu, ushahidi unaonyesha kunakuwa na utayari mkubwa wa kutumia huduma za pesa kwa mtandao. Hata hivyo ada zinapokuwa juu, watu hurejea kwenye tabia za zamani.
Ada ambazo lazima zimfikie mlaji ni pamoja na kodi, tozo na gharama za uendeshaji. Kutokana na mabadiliko ya tozo, yaliyobadili tabia za walaji, mwisho wa siku makampuni ya simu yakaishia kuandika hasara; jambo linaloathiri uwekezaji, biashara na maendeleo ya sekta kwa ujumla.
Kubwa zaidi, athari hizi zinazikumba zaidi kaya zenye kipato cha chini; kaya za wakulima, vijana wabunifu, na wajasiriamali wa mijini, ambao serikali inafanya jitihada kubwa kuwavutia katika mifumo rasmi ya kifedha.
Njia kuelekea unafuu wa gharama
Wataalamu wengi wanaonesha kuna uwezekano wa kufanya huduma kuwa nafuu zaidi, hivyo kuvutia wengi na kuongeza wigo wa kimapato. Ili kuangalia suala la unafuu kwa upana, ni muhimu kuelewa muundo wa ada kwa mtumiaji wa mwisho.
Takwimu za kisekta zinaonyesha kuna aina mbili za gharama zinazounda ada za miamala: Gharama za kiuendeshaji, ambazo ni gharama zisizoepukika zinazowezesha uwekezaji katika kujenga miundombinu inayohudumia akaunti zaidi ya milioni 76 kwa ufanisi. Hizi ni pamoja na mifumo ya usalama wa mtandaoni, upanuzi wa huduma, mishahara ya wafanyakazi na watoa huduma, udhibiti wa ubora, kamisheni za mawakala, na matakwa ya kisheria kama mafunzo ya mawakala, leseni, na mifumo ya kuzuia utapeli.

Pili, kuna kodi na tozo. Kwa sasa, aina tatu za kodi zinagusa sekta hii: Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18, Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) wa asilimia 10, na tozo ya miamala ya huduma za kifedha ambayo ni wastani wa asilimia 23. Gharama hizi zikikokotolewa kwa pamoja zinafikia wastani wa asilimia 43 kama gharama za kikodi katika miamala ya simu. Gharama hizi zinawekwa na sera na zinaweza kupunguzwa bila kuathiri utoaji wa huduma yenyewe.
Kwa mfano, kwa kawaida, Serikali huweka ushuru wa bidhaa ili kupunguza matumizi ya bidhaa fulani. Mfano vilevi, sigara au bidhaa zenye athari hasi kwa jamii. Hata hivyo, kutokana na urahisi wa kukusanya mapato kupitia akaunti za pesa za simu, serikali imechagua kuweka ushuru kwenye huduma za kifedha pia.
Kwa kuweka kodi hii, gharama zinaongezeka kwa mlaji wa mwisho, hali inayopunguza kasi ya matumizi ya fedha kidijitali, kuathiri ajenda ya miamala ya kimtandao (cashless economy), na kuathiri uwezo wa makampuni haya kuendeleza uwekezaji wenye tija.
Mbaya zaidi ni kuwa muundo wa sasa wa makato ya kikodi unawaumiza zaidi watumiaji wa kipato cha chini. Mtumiaji anayetoa kiasi kidogo kati ya Sh 500 na 10,000 analipa gharama ambazo ni takribani asilimia 35 ya thamani ya muamala, wakati mteja anayetoa Sh 500,000 analipa asilimia 2 pekee.
Madaraja ya sasa ya miamala, ambayo ndiyo msingi wa muundo wa ada, yanaweka mzigo usiostahimilika kwa kundi la kipato cha chini. Kuondoa tozo kwa miamala isiyozidi Sh 20,000 kunaweza kusaidia kufikia lengo la ujumuishi wa kifedha, kwani kiwango hiki kinawahusu zaidi watu wa kipato cha chini.
Mabadiliko zaidi katika muundo wa ada, kwa mfano kwa kuiga mifumo kama ya Uganda, yanaweza kurahisisha zaidi ukokotoaji na kuondoa mzigo usio wa lazima kwa watu wanaotegemea miamala ya viwango vidogo.
Muelekeo uwe kuondoa tozo, sio kuleta tozo mpya
Hoja ya kupunguza tozo zinaungwa mkono na tafiti za kitaalamu, kwa mfano, uchambuzi wa kampuni ya mahesabu na uhasibu ya PwC unapendekeza kuondolewa kwa tozo ya kutoa fedha kwenye huduma za simu; marekebisho muhimu kuleta msawazo juu ya tofauti iliyopo sasa ya kisheria kati ya sekta ya kibenki na sekta ya huduma za fedha kupitia simu.
Hii inaonekana zaidi katika miamala midogo; kwa mfano, kutoa fedha kwenye ATM chini ya Sh 30,000 kwa sasa kumesamehewa tozo ya huduma za kifedha, lakini ahueni hii haijafika kwa mamilioni ya watu wanaotegemea miamala ya simu pekee.

Kundi la kijamii linalofanya miamala midogo kupitia mitandao ya simu ndilo linalostahili ahueni inayopatikana kwa watumiaji wa benki ili kuongeza ujumuishi wa kifedha. Wengi wao katika kundi hili hawajafikiwa na benki, na njia pekee ya wao kupata ahueni hiyo ni kama urahisishaji wa kodi uliopo kwenye benki ungetumika pia kwenye mitandao ya simu.
Ubaguzi huu hauongezi tu gharama za ujumuishi wa kifedha, bali pia unashindwa kutambua kuwa watoa huduma za simu huwekeza mamilioni katika kujenga minara na kupanua mawasiliano, wakati mabenki na watoa huduma wengine wa kifedha hawana jukumu la uwekezaji wa miundombinu hii muhimu kwa umma.
Katika Bunge la Bajeti linaloendelea, tayari kumeanza minong’ono ya tozo nyingine. Akichangia mnamo Aprili 13, 2026, Mbunge wa Tanganyika, amependekeza kuanzishwa kwa chanzo kipya cha mapato kwa kuweka tozo ya Sh 100 kwenye muda wa maongezi kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Anadai mpango huu unaweza kukusanya hadi shilingi trilioni 1, fedha ambazo zingegawiwa kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ajili ya matengenezo ya barabara.
Hata hivyo, tunapofikiria kujenga na kukarabati barabara za lami, ni lazima tujiulize kuwa ni busara kubomoa miundombinu yetu ya kidijitali kwa kuitoza kodi kupita kiasi? Sera yoyote ya kodi inapaswa kutazamwa kama mfumo mzima ambapo kila kiungo kinategemea kingine.
Ndipo hapa pia tunakuja kwenye hoja nyingine iliyotolewa leo Aprili 27, 2026, na Mbunge Abbas Tarimba kwamba kuna umuhimu wa serikali ifikirie kuondoa tozo, kwa maneno yake, “ili fedha ziweze kuzunguka na kuwasaidia ndugu zetu wananchi kuwaondolea mzigo.”
Ni wakati wa kupunguza mzigo wa tozo na sio kuweka tozo mpya.
Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamao wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kwa maelezo yetu kupitia editor@thechanzo.com.