Dodoma. Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imekutana na wadau mbalimbali wa elimu jijini Dodoma kwa siku mbili lengo la kuwasilisha taarifa ya awali ya Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu Sura 353, na kujadili mapitio ya Sheria hiyo.
Uchambuzi wa taarifa hii ya awali ya Mei 2026 kuhusu mapitio ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353, ni kwamba inahitajika kuhuisha au kutunga sheria mpya itakayoendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023.
Akiongea Mei 21, 2026 kwenye ufunguzi wa kikao hicho, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Sera ya Elimu tayari imeshapita na utekelezaji wake unahitaji muelekeo wa kisheria.
“Sisi elimu ya lazima nchini kiutekelezaji sasa hivi ni miaka saba. Lakini Sera sasa inasema elimu ya lazima Tanzania itakuwa ni miaka 10, mpaka kidato cha nne. Kwa hiyo lazima Sheria sasa ibadilike iakisi mabadiliko hayo, ili tuwe na nyenzo ya kutekeleza Sera yetu,” amesema Prof. Mkenda.
Mwezi Februari mwaka 2026, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 – Toleo la 2023 kufuatia kipindi kirefu cha majadiliano ya wadau wa elimu.
“Kwa hivyo leo tunakutana hapa kwa ajili ya kupitia mapendekezo ambayo yameshafanyiwa kazi ya Sheria. Suala lilikoko mbele yetu ni je, tutahitaji Sheria mpya? Au tutafanya marekebisho tu ya Sheria hii iliyopo,” ameongeza Prof. Mkenda.
Wadau wazungumza
Makumba Mwemezi Mkuu wa Idara ya Utafiti, Ubunifu na Uchambuzi wa Sera kutoka Shirika la Hakielimu amesema, miongoni mwa maeneo ambayo wangependa yajitokeze kwenye Sheria ya Elimu ni kuhakikisha inazingatia mabadiliko ambayo yametokea ya kumrejesha mtoto shule baada ya kuacha shule.
“Tunatambua na tunafurahi kwamba Serikali imetengeneza miongozo kwenye eneo hilo, lakini mabadiliko haya ni lazima yapewa nguvu za kisheria.”
Kwa upande wa mabadiliko ya Sera ya Elimu ya lazima ya miaka 10, Mwemezi ameungana na Waziri Mkenda kuwa mabadiliko hayo yanapaswa kupewa nguvu ya kisheria na pia ametaka suala la adhabu za kikatili dhidi ya wanafunzi kuzuiwa kisheria.
“Mambo mengine ambayo tungependa yajitokeze kwa wazi kabisa ni kuhusu adhabu za kikatili, ambazo zimekuwa zikitolewa mashuleni,” amesema Mwemezi, “Kwamba kanuni zinazoruhusu uchapaji zina mianya ambayo zinaleta madhara kwa watoto hasa unyanyasaji kwa watoto”
SOMA ZAIDI: Tujifunze Tunavyoweza Kuwasaidia Watoto Wetu Kwenye Safari Yao ya Elimu
Kwa upande wa Awadhi Mbogo ambaye ni mdau wa elimu amesema, katika Sheria hiyo matamanio yake ni kuona watoto wenye mahitaji maalum hasa wale wa shule nyumbani wanazingatiwa.
“Hawa wanashindwa kufika shuleni, Sheria yake tuone namna gani tunaweza tukaiweka vizuri ili waweze kupata elimu kama watoto wengine,” amesema.
Kwa upande wa Abdulaziz Seleman amesema, kwenye Sheria hii anatamani kuona elimu inakuwa ya vitendo zaidi na si nadharia, ili watakao ipata elimu hiyo iweze kuwasaidia katika shughuli zao za uzalishaji.
“Katika kuboresha pia Sheria, iangalie na maslahi zaidi ya watendaji wa elimu, kwa maana ya walimu. Iandae mazingira rafiki itakayo wezesha walimu ili waweze kutimiza wajibu wao, katika namna iliyokuwa bora zaidi ili waweze kuleta ufanisi katika elimu,” amesisitiza.
Uchambuzi wa taarifa ya mapitio yabainishwa
Akieleza kuhusu uchambuzi wa taarifa hii ya awali ya kuhusu mapitio ya Sheria hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Innocent Mgeta ameeleza masuala ya msingi yaliyochambuliwa kutoka kwenye vyanzo ikiwemo maboresho ya Mfumo na Muundo wa Elimu
“Taarifa inapendekeza kutambuliwa kwa muundo mpya wa elimu ambao ni 1+6+4+2/3+3+ Muundo huu unajumuisha mwaka mmoja wa elimu ya awali na miaka sita ya elimu ya msingi. Miaka minne ya sekondari ya chini ambapo mfumo utagawanyika katika mikondo miwili. Mkondo wa Elimu ya Jumla na Mkondo wa Elimu ya Amali (Ujuzi). Elimu ya Lazima sasa itakuwa ni ya miaka 10 na itatolewa bila ada kwa shule za Serikali.”
Kwa upande wa usimamizi na uendeshaji wa sekta ya elimu, amesema kamati ya mapitio ya Sheria hiyo imebaini mapungufu katika muundo wa sasa wa uongozi.
“Ofisi ya Kamishna wa Elimu inapendekezwa kuanzishwa kisheria na Kamishna awe mteule wa Rais. Kamishna atakuwa kiungo cha uratibu wa masuala yote ya kisera kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu,” amesema.
SOMA ZAIDI: Elimu ya Zanzibar Inavyowaacha Nyuma Wanafunzi Wenye Ulemavu Kwenye Masuala ya Teknolojia
Kwa upande wa fursa sawa, elimu jumuishi na haki za mwanafunzi, taarifa inasisitiza kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa elimu.
“Urejeshwaji wa wanafunzi (Re-entry), Sheria itatambua haki ya wanafunzi waliokatiza masomo kurejea shuleni.”
Kwenye eneo la matumizi ya teknolojia, amesema Sheria inapendekezwa kutambua rasmi matumizi ya TEHAMA katika kujifunzia na kufundishia. Hii ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kielektroniki katika usajili wa shule na utunzaji wa takwimu za walimu na wanafunzi..
Hata hivyo, kutokana na mabadiliko yanayogusa karibu kila sehemu ya sheria ya sasa, kamati inapendekeza kufutwa kabisa kwa Sheria ya Elimu ya sasa (Sura ya 353) na badala yake itungwe Sheria Mpya ya Elimu itakayobeba maono mapya.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com