The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kampeni Maalum Yazinduliwa Kuhamasisha Ujenzi wa Vituo vya Huduma za Utambuzi na Upimaji wa Mahitaji Maalum ya Ujifunzaji wa Watoto

Kampeni hiyo imeandaliwa na shirika la HakiElimu kwa kushirikiana na Child Support Tanzania (CST), ikiwa na lengo la kuhamasisha halmashauri pamoja na Serikali Kuu kuwekeza zaidi katika huduma za utambuzi wa awali kwa watoto wenye changamoto za ujifunzaji na maendeleo.

subscribe to our newsletter!

Licha ya Serikali kutoa mwongozo mwaka 2022 kuhusu uanzishaji na uendeshaji wa Vituo vya Utambuzi  na Upimaji wa Awali wa Watoto (ESRACs), utekelezaji wake bado ni mdogo huku maelfu ya watoto nchini wakikosa huduma muhimu za utambuzi wa mapema zinazoweza kubadili mwelekeo wa maisha yao ya elimu.

Hali hiyo imebainishwa mkoani Mbeya, Juni 3, 2026, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Kuhamasisha Uanzishaji na Uimarishaji wa Vituo vya ESRACs uliofanyika katika Shule ya Msingi Mwenge. Wadau wa elimu waliohudhuria hafla hiyo wamesema bado kuna pengo kubwa kati ya mwongozo uliowekwa a na utekelezaji.

Kampeni hiyo imeandaliwa na shirika la HakiElimu kwa kushirikiana na Child Support Tanzania (CST), ikiwa na lengo la kuhamasisha halmashauri pamoja na Serikali Kuu kuwekeza zaidi katika huduma za utambuzi wa awali kwa watoto wenye changamoto za ujifunzaji na maendeleo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa HakiElimu, Mary Ndaro, amesema utambuzi wa mapema ni nguzo muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata elimu jumuishi na yenye usawa, lakini utekelezaji wa mwongozo wa Serikali bado haujafikia kiwango kinachotarajiwa.

“Watoto wengi wana changamoto za ujifunzaji ambazo hazitambuliki mapema,” amesema Ndaro, ‘Bila utambuzi wa mapema, mtoto anaweza kuonekana hana uwezo au ni mvivu, wakati ukweli ni kwamba anahitaji mbinu maalumu za ufundishaji.”

Ameongeza kuwa kuchelewa kwa utambuzi kunawaathiri watoto kielimu na kisaikolojia, huku walimu wakikumbana na changamoto ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji tofauti bila mwongozo sahihi.

Takwimu zilizowasilishwa katika hafla hiyo zinaonesha kuwa kati ya halmashauri 184 nchini, ni halmashauri 36 pekee zenye vituo vya ESRACs. Aidha, kati ya vituo hivyo, 34 havijakidhi vigezo vya kutoa huduma kikamilifu, huku vituo viwili pekee vikifanya kazi kwa viwango vinavyokubalika.

SOMA ZAIDI: Elimu ya Zanzibar Inavyowaacha Nyuma Wanafunzi Wenye Ulemavu Kwenye Masuala ya Teknolojia

Kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali wa mwaka 2022, vituo vya ESRACs vilianzishwa ili kusogeza huduma za upimaji na utambuzi wa awali karibu na jamii, kwa lengo la kuhakikisha watoto wanabainika mapema na kupatiwa huduma stahiki bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda ngazi za mikoa au taifa kutafuta huduma hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Child Support Tanzania (CST), Noelah Msuya Shawa, amesema utambuzi wa mapema huwasaidia walimu na wataalamu kuelewa mahitaji halisi ya mtoto pamoja na mbinu sahihi za kumsaidia darasani.

Ametoa mfano wa changamoto ya dyscalculia, hali inayosababisha ugumu wa kujifunza hesabu, akieleza kuwa watoto wengi hupewa sifa za uvivu au kutokuwa na uwezo, wakati kiuhalisia wanahitaji mbinu maalumu za ufundishaji.

“Mimi ni miongoni mwa watoto wa wakati huo ambao hawakufanyiwa upimaji mapema,” amesema Shawa, “Huenda walimu wangu hawakugundua kuwa nilikuwa na changamoto ya dyscalculia.”

Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Mwenge, Agnes Asalile Mwakaje, amesema shule hiyo ina wanafunzi 115 wenye mahitaji maalumu, wakiwemo wavulana 75 na wasichana 40, ambao wanapata huduma kupitia kituo cha ESRAC kilichopo shuleni hapo.

Ameeleza kuwa kituo hicho kina wataalamu watatu wanaoshughulikia huduma za usikivu, ufahamu wa akili, pamoja na watoto wenye uoni hafifu na wasioona kabisa.

Mmoja wa wazazi wenye mtoto wa mahitaji maalumu, Angela Charles, amesema awali hakuwa akielewa chanzo cha changamoto ya mtoto wake, lakini baada ya kufanyiwa tathmini alipata mwongozo sahihi wa namna ya kumsaidia jambo ambalo limempa matumaini.

“Mtoto wangu ana ulemavu wa akili,” alisema mama wa mtoto, “Awali sikuwa naelewa kabisa tatizo lake, lakini baada ya kupata utambuzi nilielekezwa namna ya kumsaidia na kumpeleka katika shule hii ya Child Support.”

Uzinduzi wa kampeni hiyo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wadau wa elimu. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Brigedia Jenerali Salum Hassan Sulumbu, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za utambuzi wa mapema ili kuhakikisha watoto wote wanapata haki sawa ya elimu.

SOMA ZAIDI: Wadau Wataka Kutungwa Sheria Mpya ya Elimu Itakayoakisi Mabadiliko ya Sera

Wadau wa elimu wamesema mafanikio ya baadhi ya vituo vilivyopo yanaonesha uwezekano mkubwa wa kupanua huduma hizo iwapo kutakuwa na uwekezaji wa kutosha pamoja na ushirikiano kati ya Serikali, halmashauri na wadau wa maendeleo.

Hata hivyo, pengo kubwa la utekelezaji wa mwongozo wa ESRACs linaendelea kuibua maswali kuhusu kasi ya Serikali katika kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kutambuliwa mapema na kupata msaada unaostahili kabla changamoto hazijawa kubwa zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×