The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Wazazi Walalamikia Wanafunzi Kwenda Shule Wakati wa Likizo: ‘Mtoto Ana Maisha Zaidi ya Shule’

Wadau wa elimu wasisitiza ni muhimu mwanafunzi kupumzika ili kuweza kufikia malengo ya ukuaji na elimu

subscribe to our newsletter!

Dodoma Aprili mwaka 2025, Serikali ilipiga marufuku tabia ya Taasisi za Elimu, hususani shule binafsi kwenda kinyume na kalenda ya ufundishaji kwa kuongeza muda na kuendelea kufundisha wakati wa likizo. Ilieleza hali hiyo inaathiri maendeleo ya ukuaji na ujifunzaji kwa wanafunzi.

Mbali na katazo hilo, wanafunzi wameendelea kwenda shule wakati wa likizo hali ambayo imesababisha malalamiko kwa wazazi.

Eliabu Mazengo (42),  baba wa watoto wanne anayejishughulisha na kilimo mkoani Dodoma anasikitishwa na suala hilo ambapo anaeleza kuwa wanafunzi hawana muda wa kupumzika hata wakati wa likizo.

“Sasa nini maana ya kufunga shule? Kufunga shule ni kupumzisha akili,” alisema Mazengo wakati akiongea na The Chanzo Juni 24, 2026. Mazengo aliulalamikia mfumo uliopo sasa kuwa ni tofauti na zamani walivyokuwa wakisoma.

“Kama mwanafunzi hajui kusoma hii likizo hamsaidii kitu,” aliongeza Mazengo. “Kwa sababu mwalimu hawezi kumfundisha mwanafunzi likizo ya mwezi mmoja akajua kusoma anavyofikiria yeye. Wito wangu wanafunzi wapewe muda wa kupumzika wakati wa kufunga. Itawasaidia kupumzisha akili, kwa sababu kazi ukifanya sana akili inafeli.”

Mazengo si mzazi pekee mwenye malalamiko hayo, Aidan Ndulu (67), mkazi wa Dodoma na baba wa watoto watatu alisema, ni jambo la kushangaza kuona wanafunzi wanaendelea kwenda shule licha ya kufunga shule. Alisema mwanafunzi anapaswa kupumzisha akili, ili akifungua shule aweze kufanya vizuri kwenye masomo yake. Mbali na mapumziko, Aidan alisema mwanafunzi atajifunza kazi za nyumbani.

“Atajifunza kazi zingine kama kulima, au kuchota maji. Ninaona anakosa muda wa kufanya kazi zingine inakuwa ni masomo tu,” alisema wakati akiongea na The Chanzo Juni 24, 2026. Kazi zingine anakuwa hajui kwa mfano, kulima anakuwa hajui, kufua hajui.”

Kwa upande wa Christina Yoram (58), mama wa watoto wanne anayejihusisha na ujasiriamali alisema, haridhishwi na kitendo cha wanafunzi kwenda shule wakati wa likizo.

“Mara nyingine nataka mwanafunzi akae nyumbani anisaidie kazi ndogondogo za nyumbani. Kuosha vyombo, kufua nguo, kulima. Na yeye pia anakuwa anapata maarifa fulani nyumbani,” alisema mama huyo.

Muongozo wa Serikali

Waraka wa Elimu Na 05 wa Mwaka 2025 unaeleza kuhusu kalenda ya mihula ya masomo kwa shule za awali, msingi na sekondari mwaka 2026. Waraka huo unasisitiza umuhimu wa kuzingatia utekelezaji wa kalenda husika kama ilivyopanga, ili kuepuka changamoto ya kutokamilisha ufundishaji na ujifunzaji wa mada zote kwa wakati. Waraka huu pia unaonesha siku za masomo kwa mwaka ambayo ni 194.

Wakati haya yakiendelea wadau wa elimu wanaonya kuwa shule kufungwa na watoto kuendelea kuwepo kwenye mazingira ya shule, ni kukinzana na madhumuni halisi ya ujifunzaji shuleni.

Ochola Wayoga ambaye ni mdau wa elimu alisema, hakuna kitu kinachomtatiza kama kuona mtoto akiendelea kwenda shule, wakati zimefungwa. Akijitolea mfano yeye mwenyewe alisema, kwa shule nyingi ambazo watoto wake wamesoma na zilikuwa na utaratibu huo aliwahamisha.

“Nilikuwa naenda walimu wananichukia, lakini ninawaambia mtoto ana maisha zaidi ya shule,” alisema Ochola wakati akiongea na The Chanzo kwa njia ya simu Juni 23, 2026.

Ochola aliendelea kusema, siku za mwanafunzi kukaa shuleni zinatosha, kwa kuwa zimepangwa kulingana na mitaala na silabasi husika.

“Ndiyo maana kuna muda wa mapumziko, kuna muda wa kucheza wakati wa shule, kuna muda wa mitihani, kuna muda wa vipindi vya walimu. Mimi huyu mtoto nina muhitaji nyumbani aje anisaidie kufagia, kupika. Na ndivyo mtoto anapata ile dozi ya makuzi.”

Utaratibu wa watoto kusoma wakati wa likizo, Ochola alisema ulikuwa zaidi kwenye shule binafsi, sasa umeingia mpaka kwenye shule za Serikali.

“Inaonekana Serikali nayo wameshindwa kulisimamia hilo. Miongozo iko wazi, na hizi shule ambazo ni za binafsi sehemu kubwa ni katika utafutaji. Wanajaribu kutafuta kipato zaidi kuhakikisha watoto hawa wanapata A.”

Akitoa rai kwa Serikali Ochola alisema, shule zikifungwa watoto wote iwe shule binafsi au Serikali wapumzike nyumbani.

“Warudi nyumbani wakakae na wazazi wao na walezi. Wajifunze mambo ya nyumbani kazi za mikono, nidhamu. Mtoto anakuwa na maadili tunayoyategemea. Kwa sababu hata shule akitoka mzazi ukiwa haufuatilii anakuwa siyo mtoto tena.”

Mratibu wa Elimu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Agnes Mwingira akiongea na The Chanzo Juni 24, 2026 alisema, wao wanaangalia mihula yao shuleni. Ambapo mwanafunzi anaenda shule kusoma, na anapofunga shule anarudi nyumbani kwa ajili ya mapumziko. Alifafanua, mwanafunzi anaporudi likizo anakuwa kwenye utawala mwingine.

“Tunachoamini kwamba tumewaajiri walimu kwa ajili ya kuwapa elimu wanafunzi, masomo ya ziada sisi hatusimamii zaidi. Sisi tunachoamini kwamba, mwanafunzi anapopelekwa pale ni kwamba anapewa masomo kama wanafunzi wengine katika shule zetu za Serikali.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmai.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×