Dar es Salaam-Shauri la Kikatiba lililofunguliwa na mawakili wa Tundu Lissu, juu ya kunyimwa haki ya faragha na mteja wao limeendelea Julai 22, 2026, ikiwa ni siku ya tatu ya shauri hili. Tundu Lissu amemhoji Mkuu wa Gereza la Ukonga, Andrew Shabani Ntamamiro. Sehemu kubwa ya mahojiano ni juu ya taratibu anazozi simamia ikiwemo kuruhusu au kutoruhusu baadhi ya watu kumtembelea Tundu Lissu.
Shauri hilo la kikatiba namba 7300/2026 limefunguliwa na mawakili William Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo ambapo linasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu Amir Mruma ambaye ni mwenyekiti wa jopo hilo, Dkt. Angelo Rumisha na Dkt. Evaristo Longopa. Wajibu maombi katika shauri hili wako wanne, ambapo wa kwanza ni Mwanasheria Mkuu, wa pili ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, wa tatu ni Mkuu wa Gereza Ukonga, wa nne ni Tundu Lissu na wa tano ni Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Mahojiano kati ya Lissu na Mkuu wa Magereza Ukonga yalianza kwa Lissu kuhoji juu ya misingi ya kisheria ya utendaji wa Maofisa wa Magereza ambapo Lissu alianza kuhoji juu ya kanuni zinazotumika kuamua taratibu za Magereza, ambapo kupitia Kifungu cha 105 cha Sheria ya Magereza alionesha mwenye Mamlaka ya kutunga kanuni ni Waziri na pia kupitia kifungu cha 5 cha sheria hiyo hiyo Lissu alionesha Kamishna wa Magereza anaweza kuamua taratibu mbalimbali kwa muongozo wa kanuni zinazoundwa na Waziri.
Baada ya Lissu kuonesha msingi wa utaratibu wa Magereza huwekwa kikanuni, akaendelea kuhoji juu ya matukio na uzoefu wake wa moja kwa moja.
Lissu: Kwa kanuni hizo wafungwa wamegawanywa kwa makundi matatu? Au unataka nikutajie?
Ntamamiro: Nitajie
Lissu: Wapo watoto, wapo wafungwa wanaoitwa star prisoners, na kundi la tatu ni wafungwa wa kawaida?
Ntamamiro: Ni kweli kabisa.
Mhe. Lissu: Hao wanaoitwa young prisoners ni wenye chini ya miaka 21.
Ntamamiro : Ni kweli
Mhe. Lissu: Wanaoitwa wafungwa nyota ni wale first offenders? Wamefanya kosa kwa mara ya kwanza?
Ntamamiro : Kweli
Lissu: Oridinary ni wale wafungwa wengine wanaobaki wote wasio kundi la kwanza na la pili?
Ntamamiro : Ni kweli.
Lissu: Jana ulimsikia Kalokola wakili wa serikali akisema kuna wafungwa wa umuhimu wa kisiasa au alisema Prisoners of Security Importance, je kwa kanuni hizo wapo?
Lissu aliendelea kumuuliza shahidi kama Mkuu yeyote wa gereza au Kamishna wa Magereza ana uwezo wa kubadili kanuni, ikiwemo kubadili makundi ya wafungwa ambapo Ntamiro alijibu kuwa hakuna mwenye mamlaka ya kufanya hivyo.
Sehemu kubwa ya mahojiano ya Lissu amekuwa akijaribu kuonesha namna ambavyo kanuni hazifuatwi katika uzoefu wake Magerezani, huku Mawakili wa serikali wakijaribu kuonesha kanuni zinafuatwa. Akimhoji shahidi, Lissu alianza kwa kuufungua zaidi ushahidi uliotolewa na Mawakili wake kwa kutaja majina ya maofisa mbalimbali, akiwahusisha na kuhudhuria na kusikiliza alipokutana na mawakili wake.
Katika ushahidi wa mawakili wa Lissu walieleza kuwa maeneo wanayokutana na Lissu huwa hayana faragha na Maofisa wa Magereza husikiliza kila kitu, ikiwemo kunakili kumbukumbu.
Lissu: Shahidi tuambie Mkuu wa Gereza la Ukonga una matatizo ya kusikia au hauna?
Ntamamiro: Niko vizuri mimi. Nasikia.
Mhe.Lissu: Assistant Commisioner of Prison, Recha. Ana matatizo ya kuona na kusikia au hana?
Ntamamiro : Sijui.
Lissu: Je ACP Mumbii nae ana matatizo ya kusikia?
Ntamamiro : Mimi sio Daktari sijui.
Lissu: Je ACP Mohamed nae?
Ntamamiro : Nae pia sijui kama ana matatizo ya kusikia.
Lissu: SGT. Hamisi vipi nae anasikia au hasikii?
Ntamamiro: Sijui.
Lissu : Inspector Stima legal officer nae vipi anasikia?
Ntamamiro: Nae pia sijui.
Mhe. Lissu: Wale akina mama watatu wanaofanya kazi admission office wana matatizo ya kusikia na kuona au hawana?
Ntamamiro : Sijui.
Lissu: Koplo Dani mtunza fedha nae vipi ana matatizo ya kusikia au vipi? Maana na yeye mara zote huwa yuko ofisi ya admission?
Ntamamiro: Sijui.
Lissu: Wale maaskari ambao huwa wanatoka na mimi ninakolala na kunileta kwako Insp. Kaisi na Mwingia nao pia huwa wanatatizo la kusikia?
Ntamamiro : Sijui.
Lissu: Je kwa uzoefu wako Jeshi la Magereza linaweza kuajiri askari haoni au hasikii?
Ntamamiro : Haliwezi kuajiri. Lakini unaweza kuumwa ukiwa kazini.
Lissu: Akiajiriwa akapofuka ataendelea kuwa Askari Magereza.
Ntamamiro: Mimi sio daktari
Lissu: Kama atakuwa hasikii je ataendelea kuwa askari magereza?
Ntamamiro : Sina jibu.
Lissu: Hata kutokuwa na jibu ni jibu pia.

Katika maswali aliyoyajibu Ntamamiro aliweza kuonesha kuwa alianza kazi katika gereza la Ukonga mnamo Septemba 2025, hii ni baada ya kupata uhamisho. Ubishani wa hoja ulitokea kati ya Lissu na Ntamamiro pale alipokataa juu ya uwepo wa maofisa wake katika mazungumzo mbalimbali ya Lissu na mawakili, ambapo Lissu aliweza kumpitisha mkuu huyo wa gereza katika nyaraka mbalimbali akijaribu kuonesha matobo katika maelezo ya shahidi huyo.
Lissu: Waeleze majaji kama kuna sharti lolote la kisheria kwamba mfungwa yeyote mwenye wakili aa mawakili anapaswa kuwasilisha orodha ya mawakili wake kwa Bwana Jela?
Ntamamiro : Halipo kisheria. Lakini mfungwa ana haki ya kuchagua nani amtembelee.
Lissu: Nilichagua kuwa Kulwa William Maduhu na umemkatalia?
Ntamamiro : Hakuwepo kwenye orodha.
Lissu: Andrea Chima alikuja kuniona yupo kwenye orodha gani?
Ntamamiro : Hayupo.
Lissu: SUPP 5 twende sasa tarehe 24/12/2025 angalia kwenye entry kuna Nashon Nkungu na Paul Kisabo?
Lissu: Mazungumzo na Nashon ulisema asimamiwe kwa Makamu mkuu wa gereza na kuwataka wasaidizi wako wanne wasimamie? Na mazungumzo ya Kisabo pia ulisema yasimamiwe kwenye ofisi ya Kaimu Mkuu wa Gereza.
Ntamamiro : Ndio
Lissu: Na tunakubaliana wale watu wote akina Mumbii, legal officer Stima, Koplo Dani, na akina mama watatu. Je hawa watu wanakuwemo humo?
Ntamamiro : Si kweli. Huwa wanatoka. Wanaacha mazungumzo yafanyike.
Jaji: Lissu umeridhika na majibu ya shahidi.
Lissu: Ngoja nataka kukamata watu waongo.
Lissu: Kumbe maafisa wote mle chumbani wanatoka nje, sasa soma kiapo chenu ndugu yangu. Nakusomea kwenye kiapo chako. Kiapo kinasomeka kuwa walikuwepo.
Ntamamiro: Kuna ambao walikuwepo na kuna ambao walitoka.
Mhe. Lissu: Waliokuwepo ni akina nani?
Ntamamiro: Waliosindikiza
Mhe. Lissu: Akina nani?
Ntamamiro : Sikumbuki
Katika ushahidi wake Ntamamiro alipinga baadhi ya hoja zilizotolewa na Lissu na Mawakili wake ikiwemo uwepo wa CCTV kwenye chumba cha mawasiliano ya simu aliyokuwa akitumia kuongea na mawakili wake kwenye kioo, na pia alipinga kuwa kuna Askari wanaosikiliza simu hizo kwenye chumba maalum.
Lissu alitumia muda kuhoji juu ya kuzuiwa kwa viongozi na CHADEMA kuweza kumtembelea na kuzungumza naye, jambo lililofanya katikati ya mahojiano, Mwenyekiti wa Jopo la Majaji kuhoji juu ya utaratibu huo, huku Mkuu wa Gereza Ukonga akiishia kuomba radhi.
Lissu: Je ni kweli kwamba baada ya matukio ya Oktoba 29 uliniita ofisini kwako?
Ntamamiro: Sio kweli
Lissu:Ulivyoniita ukaniambia kuanzia sasa ni marufuku viongozi wa CHADEMA na wanachama kuja kukutembelea.
Ntamamiro : Sio kweli
Lissu: Na ukasema mazungumzo yako na mawakili yatakuwa kwa mambo ya kisheria tu?
Ntamamiro : Sio kweli.
Lissu: Wakili Gaston Garubindi alikuwa anakuja kunitembelea Gerezani kabla ya tarehe 14/11/2025
Ntamamiro: Kweli
Lissu: Kuanzia hiyo tarehe hajawahi kuruhusiwa?
Ntamamiro: Simpangii.
Lissu: Kuanzia niingie Gerezani Wakili Dickson Matata na Deogratias Mahinyila hujawahi kuwaruhusu waingie gerezani. Huyu Matata ni Mwenyekiti Kanda ya Magharibi na Mahinyila ni Mwenyekiti wa Vijana Taifa hawajawahi kuruhusiwa?
Ntamamiro: Siwalazimishi waje au wasije.
Lissu: Kumbe ndio hivyo. Haya Mahinyila na Matata kesho njooni Ukonga.
Ntamamiro: Kesi iko Mahakamani sitawaruhusu
Mhe. Lissu: John Heche, Amani Golugwa, Katibu Mkuu Mnyika wakiwa kama mashahidi wangu kwenye kesi ya uhaini wamezuiwa kuingia?
Ntamamiro: Hawawezi kuingia
Jaji: Hilo la kwamba huwezi kuruhusu umelitoa wapi? Kuna amri yoyote ya Mahakama?
Ntamamiro: Siwezi kuwaruhusu.
Jaji Mruma: Tumefikia huko. Unaiambia Mahakama kuwa huwezi kuruhusu na hauna amri yoyote ya Mahakama? Uko serious kweli au hujaelewa ili tufanye maamuzi na sisi sasa?
Ntamamiro: Waheshimiwa majaji naomba radhi.
Katika dodoso lake Lissu alijaribu kuonesha utofauti unaokuwa pale mawakili wa serikali wanapotembelea magereza na mawakili binafsi, ambapo ameonesha kwa mawakili binafsi kumekuwa na upekuzi na kufuatiliwa kwa karibu huku kwa mawakili wa serikali jambo hilo likiwa halipo, hoja ambayo Mkuu wa Gereza aliikanusha.
Lissu alimshutumu Mkuu huyo wa Gereza kuendeshwa na rimoti ya wanasiasa na Kamishana wa Magereza akitoa mifano alipokuja mumbe wa Jumuiya ya Madola, Rais Lazarus Chakwera, Lissu alieleza kuwa alichukuliwa na kupelekwa mjini kukutana naye. Vivyo hivyo alivyokuja Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani, Martin Chungong, Lissu alieleza kuwa alipelekwa mjini kwenda kukutana naye. Hata hivyo Mkuu huyo wa Gereza alikanusha kuwa Lissu alipelekwa kuonana na wajumbe hao. Katika taarifa rasmi, Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mabunge Duniani wote wamethibitisha kukutana na Lissu.
Kesi hiyo itaendelea Julai 23, 2026, ambapo kwa upande wa Jamhuri na wajibu maombi wengine watapata wasaa wa kumuuliza maswali shahidi huyo pekee kwa upande wa Jamhuri.