The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Zanzibar Yaweka Walimu wa Saikolojia Shuleni Kusaidia Wanafunzi Wanaokabiliwa na Changamoto za Afya ya Akili

Msongo wa mawazo, changamoto za kifamilia na shinikizo la makundi rika ni miongoni mwa mambo yanayowaathiri wanafunzi.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar – Kumekuwa na baadhi ya matukio katika baadhi ya skuli za msingi na sekondari Zanzibar ambapo wanafunzi wa kike na wa kiume huripotiwa kupiga kelele, kulia au hata kuanguka ghafla wakiwa shuleni. Matukio kama haya mara nyingi yamekuwa yakihusishwa na masuala ya kiimani, ikiwemo imani kwamba mwanafunzi anaweza kuwa amesumbuliwa na mashetani.

Hata hivyo, nyuma ya matukio hayo huenda kukawa na sababu nyingine zinazohitaji kuangaliwa kwa mtazamo mpana zaidi, ikiwemo changamoto za afya ya akili zinazowakabili baadhi ya wanafunzi.

Afya ya akili ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanafunzi kwa sababu huathiri namna anavyofikiri, anavyojisikia, anavyojifunza na anavyoshirikiana na watu wengine. Msongo wa mawazo, wasiwasi, huzuni na changamoto nyingine za kihisia zinaweza kujitokeza kwa namna tofauti, ikiwemo mabadiliko ya tabia, kujitenga, kushuka kwa ufaulu au kutopenda tena kwenda skuli.

Utafiti uliofanywa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), ulioangazia hali ya afya ya akili miongoni mwa wanafunzi, ulibainisha kuwepo kwa changamoto za kisaikolojia, hususani msongo wa mawazo, miongoni mwa wanafunzi wa sekondari.

Kwa baadhi ya wanafunzi, changamoto hizi hazianzi skuli. Huanzia nyumbani, katika mahusiano na wenzao au kutokana na shinikizo la masomo. Kwa wengine, huenda zikajengwa taratibu kutokana na kejeli na unyanyapaa ambao huonekana kama mzaha na watu walioko karibu nao.

“Wananiita bonge nyanya”

Isha Isha* ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika moja ya skuli za sekondari zilizopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Kisiwani Unguja.

Akiwa na umri wa miaka 17 na mtoto wa pili katika familia yao, Isha kwa miaka kadhaa amekuwa akikabiliwa na changamoto ya kudhihakiwa na baadhi ya wanafunzi wenzake kutokana na mwonekano wa mwili wake.

Kauli ya kumuita “bonge nyanya” imekuwa sehemu ya maisha yake ya skuli, jambo ambalo anasema limemfanya kukosa raha na kuathiri namna anavyoshiriki katika masomo na maisha ya kila siku shuleni.

“Wananiita bonge nyanya, na jambo hilo linaniumiza sana. Sina raha, naogopa hata kushirikiana nao. Sijui najionaje, yaani. Nimeshamuambia mama yangu anihamishe skuli, ila mama hata hajali kuhusu hilo,”

Anasema Isha huku akiwa ameinamia chini wakati akizungumza na The Chanzo.

Kwa mujibu wa Isha, kejeli hizo zimekuwa zikijirudia kwa muda mrefu na kumfanya ajisikie kutengwa. Wakati mwingine, anasema, hata suala dogo la kutofautiana na wenzake darasani hugeuka kuwa nafasi ya yeye kudhihakiwa kwa kutumia mwonekano wake kama silaha ya maneno.

“Mara nyingi naumia sana. Nataka kuacha kabisa kuja skuli, maana hata wanafunzi wa madarasa mengine wanajua kuwa naitwa hilo jina,”anasema.

SOMA ZAIDI: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Yaendelea Kujidhatiti Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali 2025/26

Kisa cha Isha kinaonyesha namna unyanyasaji wa maneno na kejeli unavyoweza kuathiri hali ya kihisia ya mwanafunzi. Kinachoonekana kwa wengine kuwa mzaha, kwa mwanafunzi anayelengwa kinaweza kuwa chanzo cha hofu, kujitenga na hata kutotaka tena kwenda skuli.

Ujana na afya ya akili

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa kipindi cha ujana ni hatua muhimu katika ukuaji wa kihisia na kijamii. Kwa mujibu wa WHO, takribani kijana mmoja kati ya kila vijana saba wenye umri wa miaka 10 hadi 19 duniani anaishi na tatizo la afya ya akili.

WHO inataja wasiwasi, msongo wa mawazo na matatizo ya kitabia miongoni mwa changamoto zinazoweza kuwapata vijana. Shirika hilo pia linaeleza kuwa mazingira salama na yenye msaada katika familia na shuleni ni muhimu katika kulinda na kukuza afya ya akili ya vijana.

Elimu kuhusu afya ya akili shuleni inaweza pia kusaidia kupunguza dhana potofu na unyanyapaa unaohusishwa na changamoto za kisaikolojia.

Hata hivyo, kwa mwanafunzi kama Isha, mazingira ya skuli yanaweza kuwa chanzo cha changamoto hiyo hiyo ambayo elimu ya afya ya akili inalenga kuikabili.

Baada ya kufeli, Hassan alijitenga

Maisha ya Isha yanafanana kwa kiasi fulani na yale ya Hassan Simai Othman, mwenye umri wa miaka 18, mwanafunzi wa Skuli ya Sekondari Chukwani.

Mwaka 2024, Hassan alipitia kipindi kigumu baada ya kufeli mitihani ya kidato cha tatu. Anasema hali hiyo ilimfanya kukosa usingizi, kujitenga na watu na hata kufikia hatua ya kujiona hana maana katika jamii.

Msaada ulianza baada ya kusikia tangazo wakati wa paredi ya asubuhi skuli kwake kwamba mwanafunzi anayepitia changamoto kama upweke, kukata tamaa au hali nyingine za kihisia angeweza kwenda katika chumba maalum na kuzungumza na mwalimu.

Hassan Simai akiwa na mwanafunzi mwenzake wakiwa chumba cha Komputa . Picha/ Najjat Omar

“Niliposikia kuhusu huduma hiyo, nilikwenda kuonana na mwalimu ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa napitia changamoto ya msongo wa mawazo. Mwalimu alinisaidia na kunielekeza namna ya kukabiliana na hali hiyo. Aliniambia kufeli si kwamba mimi ni mvivu au nimekosea; ni changamoto inayoweza kutokea,” anasema Hassan wakati akizungumza na mwandishi wa The Chanzo katika moja ya vyumba vya skuli hiyo.

Baada ya kukutana na mwalimu, Hassan alipangiwa ratiba ya kwenda kwenye vipindi vya mazungumzo mara mbili kwa wiki. Anasema vikao hivyo vilimsaidia kurejea katika hali nzuri ya kihisia na kupata hamu ya kuendelea na masomo.

Mwaka huu, Hassan amerudia mitihani na kufaulu kuingia kidato cha tano.

“Vipindi hivyo vilinisaidia sana kwa sababu nilipata nafasi ya kuzungumza na kueleza mambo yaliyokuwa yananisumbua, anasema Hassan, “Tunawashukuru walimu na Serikali kwa kutusikiliza, kutuelewa na kutusaidia pale tunapokuwa na changamoto hizi, maana si wengi wanaojua kuwa haya ni masuala ya afya ya akili,”

Shinikizo la masomo, familia na mazingira ya kijamii

Tafiti za kisayansi zinaonyesha kuwa afya ya akili ya wanafunzi inaweza kuathiriwa na mchanganyiko wa sababu za kielimu, kifamilia na kijamii.

Utafiti wa mapitio ya kisayansi uliochapishwa kupitia PubMed, uliopitia tafiti 52 kuhusu shinikizo la masomo na afya ya akili ya vijana, ulibaini kuwa tafiti 48 kati ya hizo 52 zilionyesha uhusiano kati ya shinikizo la kitaaluma au kipindi cha masomo na angalau changamoto moja ya afya ya akili, hasa dalili za wasiwasi au huzuni.

WHO pia inataja umaskini, unyanyasaji, vurugu, kutengwa kijamii, unyanyapaa, shinikizo la marafiki na changamoto za kifamilia miongoni mwa mazingira yanayoweza kuongeza hatari ya matatizo ya afya ya akili kwa vijana.

Kwa baadhi ya wanafunzi, changamoto hizo huja kwa wakati mmoja.

Kwa kuzingatia faragha ya familia yake, Raya Juma* ni msichana mwenye umri wa miaka 18 na mwanafunzi wa Skuli ya Sekondari Chukwani.

Hadi sasa anaendelea na vipindi vya mazungumzo na walimu wa saikolojia kila wiki kutokana na changamoto za kihisia alizopitia baada ya wazazi wake kutalikiana.

“Baada ya wazazi wangu kutalikiana, nilianza kuwa na mawazo mengi na wakati mwingine nilishindwa kuelewa namna ya kukabiliana na hali hiyo. Maana huko nyumbani mama alikuwa analia na kutukana asubuhi hadi jioni. Ile hali ilikuwa inaniumiza sana, na baadaye nikaanza kuzungumza na mwalimu wa saikolojia,”

anasema Raya huku akionekana kuwa na aibu anapozungumzia hali hiyo.

Anasema mazungumzo hayo yalimpa nafasi ya kueleza changamoto alizokuwa akipitia na kupata ushauri ambao umekuwa msaada kwake.

“Mwalimu amenisaidia kuelewa kuwa changamoto ninazopitia si sababu ya kuacha masomo, bali ni muhimu kuzungumza na kupata msaada ili niweze kuendelea na maisha yangu ya kimasomo,”anasema.

SOMA ZAIDI: Elimu ya Zanzibar Inavyowaacha Nyuma Wanafunzi Wenye Ulemavu Kwenye Masuala ya Teknolojia

Kwa mujibu wa Raya, skuli pia ilimshirikisha mama yake katika baadhi ya vikao, jambo ambalo anasema limekuwa msaada kwake na kwa familia kwa ujumla.

Walimu wanakuwa mstari wa kwanza

Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Chukwani, Asha Muhidin Khamis, anasema skuli hiyo ina walimu wawili wanaowasaidia wanafunzi katika masuala ya kisaikolojia.

Muonekano wa mbele wa Skuli ya Sekondari Chukwani Zanzibar- Picha/Najjat Omar

Anasema hatua hiyo imekuja baada ya Wizara kuwapa walimu nafasi ya kushiriki katika semina na mafunzo mbalimbali yanayohusiana na namna ya kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto za kisaikolojia.

“Kwa sasa tuna walimu wawili ambao wanashughulikia masuala ya kisaikolojia kwa wanafunzi. Wizara pia imekuwa ikiwapa nafasi walimu wengine ambao hawajasomea moja kwa moja masuala haya kushiriki katika semina na mafunzo mbalimbali, ili nao waweze kupata ujuzi wa namna ya kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto za kisaikolojia,”anasema Mwalimu Asha.

Anasema wanafunzi wa sekondari wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri afya yao ya akili na mwenendo wao wa masomo.

Miongoni mwa changamoto hizo, kwa mujibu wa Mwalimu Asha, ni ushawishi wa makundi rika, matumizi yasiyodhibitiwa ya simu na mitandao ya kijamii, changamoto za kifamilia na kijamii, pamoja na vishawishi vinavyohusisha matumizi ya shisha, bangi na sigara miongoni mwa baadhi ya wanafunzi.

“Changamoto tunazokutana nazo ni nyingi. Kwa wanafunzi wa kike kuna masuala zaidi ya kifamilia na kijamii, huku kwa wanafunzi wa kiume tukikumbana zaidi na changamoto za makundi rika na matumizi ya dawa za kulevya, ikiwemo bangi, shisha na sigara. Ila tunakaa pamoja na walimu wenzangu, tunawafuatilia na kuwasaidia,” anasema.

Idadi ya wanafunzi inaongezeka

Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi wa msingi na sekondari Zanzibar imeendelea kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

Mwaka 2023, idadi hiyo ilikuwa takribani wanafunzi 344,000, kabla ya kufikia 365,000 mwaka 2024. Mwaka 2025 ilifikia takribani 368,000, huku mwaka 2026 ikikadiriwa kufikia 375,000.

Ongezeko la idadi ya wanafunzi linafanya suala la ustawi wao wa kihisia na kisaikolojia kuwa sehemu muhimu ya mazingira ya elimu.

Baadhi ya skuli binafsi zimeanza kuajiri walimu wenye taaluma ya saikolojia na kutangaza nafasi maalum kwa ajili ya kazi hiyo. Huduma hizo hutolewa kwa wanafunzi kuanzia umri wa miaka sita hadi wanaomaliza elimu ya sekondari, kwa lengo la kuwasaidia kukabiliana na changamoto za kihisia, kijamii na kielimu zinazoweza kujitokeza wakati wa masomo.

Familia nayo ina jukumu

Kwa Lailat Ali, mwalimu mwenye shahada ya uzamili katika masuala ya saikolojia na afya ya akili anayefanya kazi kama mwalimu wa saikolojia, familia ina nafasi kubwa katika kujenga afya ya akili ya mtoto.

Anasema wazazi na walezi wanapaswa kuwapa watoto muda wa kuwasikiliza na kufuatilia mienendo yao.

“Mtoto anapopata nafasi ya kuzungumza na kusikilizwa na mzazi au mlezi, anajenga ujasiri wa kueleza hisia na changamoto anazokutana nazo. Kusikiliza watoto hakumaanishi kukubaliana na kila wanachosema, bali ni kuwapa nafasi ya kueleza wanachohisi na kuwaelekeza kwa njia sahihi,” anasema Lailat.

Anaongeza kuwa watoto wanaokulia katika mazingira ya familia yenye migogoro ya mara kwa mara, ikiwemo wazazi kugombana, kutukanana au kuwa na ugomvi, wanaweza kuathirika kihisia na kuishi katika hali ya msongo wa mawazo na woga.

Hali hiyo, anasema, inaweza kufanya mtoto ashindwe kuzingatia masomo vizuri na kuanza kuiona skuli na masomo kama mzigo badala ya kuwa sehemu ya kujifunza na kujenga maisha yake.

“Mtoto anapokua katika mazingira yenye ugomvi na hofu mara kwa mara, mawazo yake yanaweza kubaki kwenye matatizo ya nyumbani badala ya masomo. Ndiyo maana kama mwalimu unatakiwa kujua hali za wanafunzi kwa ujumla ili utoe msaada pale unapoona mabadiliko yanayoashiria changamoto,”anasema.

Serikali yaweka walimu wa saikolojia

Zanzibar ina takribani skuli 1,200 za msingi na sekondari, huku skuli za msingi za Serikali zikiwa takribani 600 na za sekondari takribani 250.

The Chanzo ilimtafuta Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdulla Said, ambaye anasema Serikali iliona umuhimu wa kuimarisha huduma za kisaikolojia katika skuli baada ya kubaini changamoto mbalimbali miongoni mwa wanafunzi, hususan wanafunzi wa sekondari.

Khamis Abdulla Said Katibu wa Wizara ya Elimu na Ufundi Stadi Zanzibar. Picha/ Najjat Omar

“Serikali iliona kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi, hususan wa skuli za sekondari, ambazo wakati mwingine huonekana kupitia mabadiliko ya tabia na mwenendo wao. Ndipo ikaona umuhimu wa kuweka utaratibu wa kuwepo kwa walimu wa saikolojia katika skuli zote,”anasema Khamis wakati akizungumza na mwandishi wa The Chanzo ofisini kwake Mazizini, Zanzibar.

Khamis anaongeza kuwa pamoja na wanafunzi kupewa elimu kuhusu saikolojia na afya ya akili, Serikali imekuwa ikitoa mafunzo na semina kwa walimu ili kuwawezesha kutambua changamoto za kisaikolojia zinazowakabili wanafunzi na hata wao wenyewe.

Picha ya familia ofisi ya Wizara ya Elimu Zanzibar- Picha Najjat Omar/ Zanzibar

“Si wanafunzi pekee wanaohitaji elimu ya afya ya akili, hata walimu wanahitaji kufahamu masuala haya. Serikali imekuwa ikitoa mafunzo na semina mbalimbali kwa walimu ili tujue namna ya kutambua changamoto za wanafunzi, kuwasikiliza na kuwasaidia kwa njia inayofaa,”amesema Khamis.

Zaidi ya “mashetani”

Katika jamii ambayo baadhi ya matukio ya wanafunzi kupiga kelele, kulia au kuanguka ghafla yanaweza kutafsiriwa kwa mtazamo wa kiimani, simulizi za Isha, Hassan na Raya zinaongeza sura nyingine ya jambo hilo: uwezekano wa kuwepo kwa changamoto za kihisia na kisaikolojia zinazohitaji kusikilizwa.

Hii haimaanishi kwamba kila tukio la aina hiyo lina sababu ya afya ya akili. Badala yake, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kutazama hali ya mwanafunzi kwa upana, kusikiliza anachopitia na kutafuta msaada unaofaa pale dalili za changamoto zinapoonekana.

Kwa Isha, kuitwa jina linalomdhalilisha kumemfanya atamani kuacha skuli.

Kwa Hassan, kufeli mtihani kulimpeleka katika kipindi cha kujitenga na kukata tamaa, lakini mazungumzo na mwalimu yakamsaidia kurejea kwenye masomo.

Na kwa Raya, kuvunjika kwa familia kulimwacha akiwa na “mawazo mengi”, lakini kupata mtu wa kuzungumza naye kulimsaidia kuanza kukabiliana na hali hiyo.

Hadithi zao zinaonyesha kwamba wakati mwingine ishara ya kwanza ya changamoto ya mwanafunzi inaweza isiwe alama mbaya kwenye mtihani. Inaweza kuwa kimya, kujitenga, kulia, kukosa usingizi, kuogopa kwenda skuli au kubadilika kwa tabia.

Najjat Omar ni mhariri na mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Anapatikana kupitiaa najjatomar@gmail.com 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×