Dar es Salaam-Majira ya saa tatu na dakika 11 asubuhi siku ya Ijumaa ya Novemba 06, 2026, Majaji wanaingia katika chumba cha Mahakama kilichojaa watu pande zote, huku wengine wakiwa wamesimama.
Jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstun Nduguru limekuwa likisikiliza kesi hii, ambapo Majaji wengine ni Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde. Jaji Ndunguru alitumia takribani saa mbili na dakika thelathini kusoma hukumu.
Wakati Jaji Ndunguru akisoma hukumu yake, Tundu Lissu alikuwa amekaa katika kiti chake kwa utulivu, huku mara kwa mara akipitisha vidole vyake katika karatasi kana kwamba kuna ala fulani ya muziki aliyokuwa akiipiga. Alivyokuwa akigeuka na kukutana macho kwa macho na wafuasi, Lissu alikuwa akitoa ishara kwa kutumia kichwa na macho yake, kuonesha anafurahia uwepo wao.
Majaji walipohitimisha kwa kusema kuwa Lissu hana hatia ya uhaini, Lissu aliegemea nyuma kwenye kiti chake na kuendelea kusikiliza kwa makini, hasa kwa kuwa Jaji alionekana bado ana mengi ya kuzungumza: hatimaye Mahakama ikaeleza kumkuta Lissu na hatia ya kosa la uchochezi.
Kwa wengi waliokuwa Mahakamani walishuhudia wakati Jaji Dunstan Ndunguru akisoma hukumu, vikaratasi vilikuwa vikipita kutoka kwa meza ya wanasheria wa Lissu kwenda kwa Askari Magereza, ambao baada ya kusoma kilichoandikwa walimpatia Lissu, na Lissu akarudisha majibu.
Jaji alipomaliza kusoma uamuzi wake, kabla ya kutoa adhabu, upande wa mashtaka na upande wa utetezi waliruhusiwa kuzungumza mbele ya mahakama. Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, uliomba adhabu kali na ulitumia muda kumhusisha Lissu na matukio ya Oktoba 29,2025.
Ilipofika zamu ya Lissu, aliwaomba majaji wamruhusu kushauriana na mawakili wake, ambao walikusanyika kuzunguka kizimba, wakizungumza naye na kumpa vikaratasi. The Chanzo imezungumza na moja ya Wakili wa Lissu, ambaye ameeleza kilichotokea.
SOMA PIA: Kesi ya Uhaini: Mahakama Yasema Lissu Ana Kesi ya Kujibu, Yafafanua Kanuni Ilizotumia Kufikia Uamuzi
“Baada ya kuona ametiwa hatiani, kwenye kesi ya uchochezi. Kwa sababu yupo kwenye kizimba pale hana namna ya kuangalia TanzLII, kuona kesi, hawezi kutoa muongozo pale. Tukamuandikia ujumbe pale aombe kwa Majaji apate mapumziko ya ushauri na mawakili,” anaeleza Wakili Jebra Kambole akiongea na The Chanzo.
“Alivyokuwa anatuandikia sisi anatujibu akasema sawa nitaomba. Na alivyoomba Mawakili wote tulimpelekea kile amabacho tunafikiri anatakiwa akiseme,” aliendelea kufafanua zaidi.
Lissu na mawakili walizungumza kwa takribani dakika saba, ambapo Mawakili wanaeleza Lissu aliwaambia mtazamo wake, hasa kesi ilipofikia na aliwasikiliza Mawakili. Lissu alionesha kuwa ameshajiaandaa kwa yote yatakayotokea katika Mahakama hiyo.
“Mimi nilimtembelea jumatatu kabla ya uamuzi wa Ijumaa na alisema kwamba mimi hata kama watanihukumu kuninyonga haitakuwa kirahisi, lazima nizungumze. Alishajiandaa kuwa kama wakimkuta na hatia lazima aongee kile ambacho yeye anaamini kiko sahihi,” alisema Kambole, akieleza fikra zilizokuwa nyuma ya hotuba ya Lissu ya takriban saa nzima baada ya hukumu.

Lissu akizungumza na Mawakili wake alisisitiza juu ya umuhimu wa kuongea anayoyawaza hasa kuweka kumbukumbu ya kihistoria sawa kwenye upande wa kisiasa. Huku Mawakili wake wakisisitiza umuhimu wa kuchambua vipengele muhimu vya kisheria hasa kuelekea rufaa.
“Alisikiliza mawazo ya kila mtu huyu anatoa zile mitigation fact [hoja juu ya adhabu] ambazo kikawaida Mahakama huwa inazizingatia. Lakini kwa sababu yeye ni mwanasiasa anajua akizungumza zile mitigation [hoja juu ya adhabu] bila kuongea ukweli wa moyoni mwake hatakuwa na amani, kwa hiyo akasema kwamba ngoja nizungumze ninachowaza,” Kambole alifafanua akizunguza na The Chanzo.
Hotuba ya Lissu ilikuwa na sehemu mbili tofauti zilizo onekana wazi wazi: ya kwanza ya kisiasa, ya pili ya kiufundi. Akizungumza, Lissu alikua akitembea kutoka upande mmoja mpaka mwingine kama anavyofanya akihutubia katika mikutano. Hili lilikuwa tofauti na mawasilisho yake ya siku za nyuma, ambapo sehemu kubwa alikuwa akizungumza huku akiwaangalia Majaji na hakua akizunguka zunguka mara nyingi. Safari hii, ilikuwa kana kwamba hadhira iliyokuwa ukumbini ilikuwa na umuhimu sawa na majaji waliokuwa kitini katika kile alichotaka kuwasilisha.
Kwa sehemu kubwa ya hotuba, majaji watatu walikuwa wakiandika bila kumuangalia moja kwa moja. Akizungumza na The Chanzo, mawakili wake walieleza kwa nini walisisitiza sehemu ya kiufundi ya hotuba hiyo.
“Sisi [Mawakili] tukawa tunasisitiza kwamba hizi mitigation [hoja juu ya adhabu], lazima uziweke kwa sababu ya record inapoenda Mahakama ya Rufaa. Ukisema Majaji hawakuzingatia hiki watatuuliza mliwaambia, lazima tuwe tumewaambia. Ndio maana aliongea yale yote halafu akasema ninayoenda kuyaongea yasichukuliwe kama nimekiri makosa,” Wakili Kambole alifafanua.
Tundu Lissu alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela, huku mahakama ikieleza kuwa ana haki ya kukata rufaa. Kwa mujibu wa mawakili wa chama, Lissu amewaruhusu kuendelea na rufaa, itakayoongozwa na Dkt. Rugemeleza Nshala.
Soma hotuba kamili ya Tundu Lissu kama alivyozungumza Novemba 06, 2026, kutoka kwenye kumbukumbu za mwandishi wetu:
Waheshimiwa Majaji, nawashukuru kwa fursa ya kuzungumza, naomba msinisikilize kwa makini kama ambavyo mmenisikiliza kwa makini kwa zaidi ya mwaka mmoja na mrekodi vizuri kama ambavyo mmerekodi proceedings za Mahakama hii.
Waheshimiwa Majaji leo ni siku ya 577 nikiwa gerezani, siku 577 nikiwa gerezani kwa kuitwa Mhaini. Kwa kuitwa Mhaini, kosa ambalo kwa Katiba ya nchi yetu ndio kosa kubwa kuliko yote katika Jamhuri ya Muungano. Ndio kosa pekee lililotamkwa katika Katiba, Uhaini.
Kwa siku 577, nimeitwa Mhaini, kosa ambalo kwa mujibu wa kifungu nilichoshtakiwa nacho cha 39(2)d ya Kanuni ya Adhabu, adhabu yake inaweza kuwa kifo. Baada ya siku 577 za hilo wingu jeusi la adhabu ya kifo kuning’inia juu ya kichwa changu, leo Waheshimiwa Majaji mmeniita mchochezi, kosa ambalo wala halina adhabu, halijapangiwa adhabu.
Mmeniita mchochezi na wakili wa serikali mkuu anahangaika kutafuta hii sasa adhabu yake ni nini. Maana yake ni nini waheshimiwa Majaji? Kosa nililoshtakiwa nalo, halikuwa kosa, na nyie leo mmesema hivyo halikuwa kosa. Halikuwa kosa na leo waheshimiwa Majaji mmesema wenyewe sio kosa.
Kwa hiyo nilikaa [Mahabusu] siku 577 bila kosa lolote. Waheshimiwa Majaji, kauli yenu kwamba halikuwa kosa imekubaliana na msimamo wangu na ushahidi wangu kwamba hakukuwa na kosa lolote mmekubaliana nami.
Kuna kitu kimoja hamjakisema na nitakisema for the record Waheshimiwa Majaji. Nimesema all along, na ushahidi wangu umethibitisha hili, kwamba hii ilikuwa ni kesi ya kisiasa tu. Kugeuza Mahakama kuwa uwanja wa mapambano ya kisiasa, kugeuza Mahakama ya jinai kuwa uwanja wa mapambano ya kisiasa, kwa hukumu yenu imethibitisha hili, ni political persecution.
Kwa sababu ni political persecution, inabidi visababu vitengenezwe vya kumfunga huyu mgomvi wetu wa kisiasa. Visababu, excuses zitafutwe za kumfunga huyu mpinzani wa kisiasa. Na visababu vyenyewe waheshimiwa Majaji ni kosa la uchochezi ambalo nyie waheshimiwa Majaji mmelitengeneza. Sikushtakiwa nalo kabisa, sikushtakiwa kwa uchochezi nilishtakiwa, nje ya uhaini; nilishtakiwa kwa kusambaza taarifa za uongo, hilo lilisahauliwa. Mmetafuta kosa waheshimiwa Majaji ambalo halikuwepo kabisa.
Na waheshimiwa Majaji with all due respect mmefanya hivi kwa sababu za kisiasa. Kwa sababu ya maelekezo ya kisiasa. Hana kosa lakini asiachiwe hivi hivi akaona ameshinda, serikali itaaibika, anayetupa Ujaji ata-aibika, kwa hiyo tafuteni vijisababu. Ndivyo mlivyofanya leo waheshimiwa Majaji. Na ninajua mna hukumu, mmeshakubaliana hukumu, ninajua, I feel it in my heart.
Kwa hiyo, kwa bahati mbaya sana waheshimiwa Majaji, mmefanya kile ambacho Mahakama Kuu ya Kenya ilifanya mwaka 1954, kwenye kesi ya Mzee Jommo Kenyatta na wenzake sita, the Kapenguria Six. Mwaka 1954, Mahakama Kuu ya Kenya kwenye kesi ya Mzee Jomo Kenyatta, na the Kapenguria Six, ilimpata na hatia Mzee Kenyatta pamoja na kwamba ilikuwa inajulikana, historia imethibitisha hakukua na hatia yoyote. Ni katika namna ya kumkomesha huyu mpinzani mkubwa wa serikali ya kikoloni, ndicho ambacho mmefanya leo waheshimiwa Majaji.
Historia haijawa na wema sana kwa Majaji ambao wamegeuza Mahakama zao kuwa mahali pa kuadhibia wasio na hatia ili kuwaridhisha walioko madarakani. History has never been kind to those Judges, kwa sababu ninaamini ni mtu ambaye mnajua hana hatia, na dunia inafahamu hana hatia. Sasa Waheshimiwa Majaji wasiokuwa na hatia kama mimi, huwa hawaombi msamaha; unaomba msamaha kama una hatia, kama umekosa. You don’t beg for mercy when you are innocent; huombi msamaha unapojua huna hatia.
Kwa hiyo waheshimiwa Majaji nataka niwe very clear, kwamba haya nitakayoyasema yasichukuliwe kwa namna yeyote ile kuwa naomba msamaha, siombi msamaha kwa sababu I’am completely innocent. Lakini kwa vile wakili wa serikali Mkuu amezungumza hayo aliyoyazungumza, naomba nimjibu, halafu muangalie kama hiyo ni mitigation au la.
Kwanza kabisa, Wakili wa Serikali Mkuu amesema hivi, kwenye hicho kifungu cha 35 ambacho amekiombea adhabu kali, Wakili wa serikali anasema, adhabu ya juu katika kifungu hicho ni kifungo cha miaka mitano au faini au vyote viwili.
Sasa waheshimiwa Majaji, sheria inapotoa adhabu ya aina hiyo, kifungo au faini au vyote kwa pamoja. Mahakama inatakiwa ifanye nini, Kesi ya Salum Shabani dhidi ya Jamhuri 1985 Tanzania Law Report 71. Na kwenye shauri hilo waheshimiwa Majaji, Mahakama hii ilisema pale ambapo Bunge limetoa option ya faini au kifungo, Mahakama inayotoa hukumu, lazima itoe kwanza adhabu ya faini. Lazima itoe adhabu ya faini kwanza, kwa hiyo mnapotafakari adhabu kali iliyoombwa na Wakili wa Serikali Mkuu, waheshimiwa Majaji msije mkasahau kwamba msimamo wa kisheria unasema mtoe adhabu ya faini kwanza.
Na kesi nyingine zinazosisitiza msimamo huo waheshimiwa Majaji, ni kesi ya Alice Nyawira Nungu Vs Republic, Criminal Appeal No 40/2022, ipo reported kwenye TanzLII ya 2022, 11653. Na kesi ya pili waheshimiwa Majaji, kesi ya Elias Ndikumana dhidi ya Jamhuri Criminal Appeal No. 39/2022 ipo reported 2020 TanzLII 11656, na mashauri mengine mengi waheshimiwa majaji ambayo nina uhakika mnayafahamu. Kwa hiyo ishu ya kwanza ni hiyo option ya fine must be taken first.
Sasa waheshimiwa Majaji kuna maneno yamezungumzwa na Wakili wa Serikali Mkuu, amejigeuza kuwa shahidi badala ya Wakili wa Serikali Mkuu. Amezungumzia kwamba haya makosa ya uchochezi kwa mujibu wake yamekuwa ni makosa mengi sana nchi hii kwa mujibu wa taarifa za polisi, na kwa mujibu wa hotuba ya Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman. Na kama nimemuelewa vizuri Wakili wa Serikali Mkuu, kimsingi anasema kwamba matukio ya vurugu za Oktoba 2025 zilitokana na kauli zangu, kama nimemuelewa sawa sawa.
Waheshimiwa Majaji kwenye kesi hii sina hakika kama mmeletewa ushahidi wa hotuba ya Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, haipo kwenye ushahidi wa kesi hii, Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Chande Othman hajaja kutoa Ushahidi hapa kuthibitisha hizo vurugu zilisababishwa na kauli za wanasiasa gani. Mnaambiwa waheshimiwa Majaji mnitolee adhabu kali kwa kosa ambalo kama lipo, limefanyika takribani miezi sita na ushee baada ya mimi kukamatwa, limefanyika miezi sita na zaidi mimi tayari niko Mahabusu.
Mnaambiwa mniadhibu kwa yaliyotokea miezi sita na nusu baadae, mkikubaliana na mualiko huo waheshimiwa Majaji utakuwa ni uthibitisho mwingine kwamba huu ni uamuzi wa maelekezo. Kesi nyingi, matukio mengi ya uchochezi; mengi mangapi, yametokea wapi, nani ameyafanya. Wakili wa serikali Mkuu anataka muamini porojo za mitandaoni, mkizikubali waheshimiwa Majaji itakuwa ni uthibitisho mwingine kwamba ni maagizo.
Sasa waheshimiwa Majaji wakili wa serikali Mkuu amewaambia vile vile kwamba kwa sasa hawana taarifa zozote kama hili ni kosa langu la kwanza au la. Maana yake anaashiria ninaweza kuwa na previous conviction zingine, waheshimiwa Majaji kwa vile hana uhakika mimi nitawaambieni kitu cha uhakika. I have never ever been convicted of the criminal [offence]…ever in my life. Sijawahi kupatikana na hatia yoyote katika maisha yangu, never.
Wamenishitaki kama nilivyosema kwenye ushahidi wangu, wamenishtaki waheshimiwa majaji, wamenishtaki kwa miaka 24 tangu 2002, hawajawahi kunipata na hatia hata mara moja. Kwa hiyo mnapofikiria adhabu ya kutoa kwa hili ambalo mnaliita kosa, mtakapokuwa mnatafakari adhabu gani, msije mkasahau kwamba, mnatoa adhabu kwa mtu ambaye hajawahi kupatikana na hatia ever.
Waheshimiwa Majaji, natumaini mnafahamu kwamba nina msiba mkubwa sana. Nina msiba mkubwa sana wa mtu ambaye amenifanya mimi mwanasheria, mtu ambaye amenifanya the person I’am, wa mtu aliyenilea. Nilikuwa natumaini kwamba kwa sababu sikupata nafasi ya kumuuguza, nilikuwa natumaini Mahakama itaona ukweli hii kesi hakuna kitu iniache nikamzike Mzee Alute, nilikuwa natumaini hivyo. Nikamzike kaka yangu, I was hoping that.
Inaelekea waheshimiwa Majaji hiyo haipo kwenye mahesabu zenu. Ninaomba mtakapokuwa mnafikiria hiyo adhabu kali mfikirie na hilo, family obligation is a factor kwenye kuamua adhabu. Huyu mtu amefiwa; actually dunia nzima inafahamu, magazeti yanaandika every day. I was hoping, and I hope you will consider that, kwamba ninahitaji kwenda kutimiza wajibu wa kumzika huyo ambaye sikuweza kumuuguza, na ndiye aliyenilea.
Kwa hiyo leo ni mwaka na miezi saba, siku 577 niko gerezani. Mnapofikiria adhabu kali ya kuitoa msije mkasahau kwamba mimi nimeshakaa gerezani kwa mwaka na miezi saba kwa kosa ambalo mmelisema wenyewe sio kosa. Na wala waheshimiwa Majaji msije mkasahau walichokisema Jopo la Majaji watatu wenzenu: Jaji Mruma, Jaji Dr. Longopa, Jaji Dr. Rumisha, kuhusiana na mambo ambayo nimetendewa nikiwa gerezani, kwa mwaka na miezi saba nimenyimwa fursa ya kuwasiliana na Mawakili wangu.
Nimenyimwa fursa ya kuwasiliana na wanachama na viongozi wenzangu wa chama kinaitwa CHADEMA, nimenyimwa fursa hata ya kuomba Mungu, hata ya kuabudu. Kwa kipindi fulani nimewekwa pamoja na wafungwa wenye adhabu ya kifo wakati mimi ni Mahabusu na Majaji wenzangu hao niliowataja wamesema hayo yaliyotendeka gerezani yameninyima haki ya kujiandaa sawa sawa ili kupambana na huu uongo ulioletwa na serikali Mahakamani. Wamesema nimenyimwa fursa ya kujitetea, haki ya kikatiba ya kujitetea, msije mkasahau hiyo mnapofikiria adhabu kali mnayoombwa.
Waheshimiwa Majaji mimi ni raia mwema wa nchi hii, mzalendo wa nchi hii. Nimetumikia nchi hii kama Mbunge wa kuchaguliwa na wananchi mara mbili, nimetumikia taifa hili, nimekwenda Jeshini, nimekuwa Rais wa chama cha Mawakili wa nchi hii. Mimi sio mpiga kelele kama huyo anayesemwa na hawa Mawakili wa Serikali, mimi sio mpiga kelele, mchochezi chochezi, mimi I’am a solid patriot. Na ndiyo maana na mabalozi mnawaona leo, na wamekuwepo kila siku na dunia nzima huko inazungumza hiki kinachoendelea ni travesty of justice, the entire world is saying that, kwa sababu wanajua, I’am a true patriot they have seen in this country. Na hilo waheshimiwa Majaji mnapofikiria adhabu iliyoombwa ambayo ni kali, msije mkasahau.
Waheshimiwa Majaji gerezani sio mahali pazuri sana na ninaweza nikasema hivyo kwa sababu naishi gerezani for the past 577 days, nakaa kwenye chumba cha sita kwa sita, mita sita kwa sita, kama hiki kizimba. Hapo ndipo ninapokaa kwa mwaka na miezi saba, sio Sheraton. Unaweza ukasema funga, kama hujui gereza ni nini, sasa waheshimiwa Majaji nasema haya kwa sababu mimi sio mzima sana. Kwenye huu mwili wangu waheshimiwa Majaji nina operesheni 25, visu vya madaktari. Ninatembea na risasi mwilini, katika 16 zilizoingia mwilini, moja walishindwa kuitoa, kwa hiyo ninatembea na risasi mwilini.
Ninatakiwa niwe naenda hospitali Ubelgiji, hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nilipotibiwa. Baada ya yalionikuta miaka tisa iliyopita. Natakiwa niende kila baada ya miezi sita na nimeshamiss appointment nne tayari kwa sababu ya kesi hii. Na juu ya yote hayo waheshimiwa Majaji nina kisukari huu ni mwaka wa sita. Kwa hiyo mtakapokuwa mnatafakari hiyo adhabu kali iliyoombwa na hiyo msije mkasahau kwamba hali yangu ya afya sio nzuri sana.
Waheshimiwa Majaji, kosa la uchochezi mara ya mwisho nilipoangalia ni kosa lenye dhamana, lina dhamana. Kama itawapendeza waheshimiwa Majaji mnipe dhamana ili nikatie uamuzi wenu huu rufaa nikiwa nje kwa dhamana, lakini muhimu zaidi, ili niweze kumzika huyu ambaye amelala. Hilo nawaombeni, nilisema sina mpango wa kuomba [ila] dhamana nawaomba.
Waheshimiwa Majaji, uamuzi huu wa kunitia hatiani kwa kosa ambalo sikushtakiwa nalo, sikujitetea nalo kosa ambalo limetengenezwa ‘kubalansisha’. Effect yake na pengine ndicho kitu ambacho kinatafutwa, inatoa kinga ya aina fulani ya kisiasa kwa watu ambao wamefanya mauaji makubwa ya Watanzania. Mmewapa sababu ya kutoka nje na kusema waliochochea wameshakutwa na hatia, you are covering mass murderers.
Serikali ya nchi hii haijawahi kuua watu wengi kama serikali ya Samia ilivyoua watu wengi mwaka jana. Mara ya mwisho kulikuwa na mass murder ilikuwa miaka 120 iliyopita wakati wa Majimaji. These mass murderers ambao hakuna hata mmoja aliyewajibishwa, watashangilia sana uamuzi huu, kwa sababu mmewapa hadhi ya kusema mkosaji aliyesababisha ya Oktoba amepatikana na hatia. Hiyo wala haitafunika, these mass murderers will be held accountable someday. Kama mnafikiria itawasaidia, haitawasaidia.
Serikali ya Mwalimu Nyerere iliua watu 37 mwaka 1976, Mwinyi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alijiuzulu, Peter Syovelwa alikuwa Waziri wa Usalama wa Taifa alijiuzulu, Elango Shahidi alikuwa IGP alijiuzulu, Peter Kisumo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga alijiuzulu, na Jacob Kasubi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alijiuzulu. Walijiuzulu, serikali iliua watu 37.
Leo serikali imeua watu kwa uchache, watu 518, hakuna hata mmoja amewajibika, uamuzi wenu hautaficha hiyo kashfa. Niwakumbushe waheshimiwa Majaji kwa guideline za Mahakama hilo kosa lenye option ya fine item 1.3.1 ya guideline inataka adhabu ya fine itolewe isipokuwa kama kosa ni kubwa, grave offence. Uchochezi ambalo ninashtakiwa nalo sio grave offence haina hata adhabu kosa lenyewe.
Kwa hiyo waheshimiwa Majaji mimi namaliza kwa kusema hivi: Toeni hukumu ambayo mnayo, ambayo mmeagizwa kutoa. Nawashukuru sana.