Takribani asilimia 80 ya mazungumzo yaliyofanyika kutafuta suluhu ya migogoro kati ya mataifa barani Afrika kati ya mwaka 1989 na 2019 hayakuzaa makubaliano ya amani wala usitishaji mapigano, kwa mujibu wa takwimu za African Peace Processes (APP) Dataset. Takwimu hizi zinaibua swali muhimu: kwa nini juhudi za upatanishi zimeendelea kushindwa kuleta suluhu ya kudumu katika baadhi ya migogoro barani Afrika?
Licha ya kuwepo kwa Umoja wa Afrika (AU) na taasisi za kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), migogoro imeendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya bara hili, ikiwemo Ukanda wa Maziwa Makuu.
Changamoto ya kupata amani ya kudumu ilikuwa miongoni mwa hoja kuu zilizojadiliwa katika Mkutano wa Amani na Usalama Afrika Mashariki, uliofanyika Novemba 19–20, 2026, jijini Dar es Salaam, uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya taasisi ya Konrad-Adenauer-Stiftung Tanzania (KAS) na Kigoda na Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katika mkutano huo, wadau wa siasa, diplomasia na ujenzi wa amani walijadili sababu zinazozuia juhudi za upatanishi kuzaa matunda na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kupata suluhu za kudumu.
Rasilimali na udhaifu wa uongozi
Miongoni mwa sababu zilizotajwa ni namna rasilimali za asili zinavyosimamiwa katika maeneo yenye migogoro, pamoja na udhaifu wa mifumo ya uongozi na utawala.
Dkt. Christian Manahl, aliyewahi kuwa Naibu Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, balozi na mpatanishi, amesema upatikanaji wa rasilimali za asili katika maeneo yenye migogoro unaweza kuvutia wadau kutoka nje ya maeneo hayo, hali inayochochea ushindani wa kiuchumi na kisiasa. Kwa mujibu wake, fedha zinazotokana na rasilimali hizo zinaweza kutumika kufadhili ununuzi wa silaha na kuendeleza mapigano.
Akitolea mfano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Manahl amesema ukubwa wa nchi hiyo na uwezo mdogo wa serikali kufika katika baadhi ya maeneo yake huacha mwanya unaoweza kutumiwa na makundi yenye silaha pamoja na wadau wa nje kuingilia masuala ya ndani.
Hata hivyo, amesema changamoto za upatanishi haziishii katika masuala ya rasilimali na usalama pekee, bali zinahusisha pia namna michakato ya amani inavyoongozwa na wadau wanaoshirikishwa.
“Kuna haja ya uongozi bora katika upatanishi. Haisemi tu kuhusu nani anahusishwa katika mchakato wa amani. Bila shaka, wadau wote lazima wahusishwe,” amesema Manahl.
SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiwango Gani Waafrika Wanaweza Kujitatulia Matatizo Yao Wenyewe?
Kauli hiyo inaonesha kuwa mafanikio ya mchakato wa amani yanategemea si tu uwepo wa wadau mbalimbali, bali pia ubora wa uongozi unaoratibu mazungumzo na kuhakikisha maslahi yao yanazingatiwa.
Viashiria vya migogoro vinapaswa kushughulikiwa mapema
Mbali na changamoto za rasilimali na uongozi, washiriki wa mkutano huo wameeleza umuhimu wa kutambua na kushughulikia viashiria vya migogoro kabla havijageuka kuwa vurugu.
Dkt. Petro Protas, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema Afrika inahitaji kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema ili kubaini na kutatua matatizo yanayoweza kuchochea migogoro kabla hayajafikia hatua kubwa.
Ametaja migawanyiko ya kikabila, migogoro ya ardhi na malalamiko ya vijana kuhusu ukosefu wa ajira kuwa miongoni mwa changamoto zinazoweza kuchochea migogoro ikiwa hazitashughulikiwa kwa wakati.
Pia ameeleza kuwa harakati za vijana wa Generation Z katika nchi mbalimbali za Afrika ni miongoni mwa ishara zinazopaswa kuchukuliwa kwa uzito na viongozi. Kwa mtazamo wake, viongozi wanapaswa kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyafanyia kazi badala ya kusubiri hadi yafikie hatua ya kusababisha vurugu.
“Matatizo mengi ya Afrika yanatokea pale ambapo vile viashiria, warning signs, havitibiwi mapema. Kama tungeweza kutibu visababishi mapema, pengine bara la Afrika lingeweza kuwa na amani katika sehemu kubwa,” amesema Protas.
Taasisi za kikanda zinahitaji kupitia upya mifumo yake
Pamoja na kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, Protas amesema taasisi za kikanda zinapaswa kupitia upya mifumo na mikataba yake ili iendane na mabadiliko ya mazingira ya kisiasa na kiusalama.
Ametolea mfano Itifaki ya Amani na Usalama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliyosainiwa mwaka 2013, wakati jumuiya hiyo ikiwa na nchi wanachama watano, tofauti na sasa ambapo ina wanachama wanane.
Kwa mujibu wake, mabadiliko hayo yanaonesha umuhimu wa kutathmini upya mifumo iliyopo ili kuhakikisha inatoa majibu yanayolingana na mazingira na changamoto za sasa.
“Ni wakati mwafaka wa kuweza kupitia upya mkataba na kuona jinsi gani tunaweza tukapata majibu sahihi,” amesema.
Hata hivyo, rekodi za kisheria za EAC zinaonesha kuwa Itifaki hiyo, iliyosainiwa jijini Dar es Salaam Februari 15, 2013 utekelezaji wake una changamoto kwani za kisheria na kiutawala.
SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?
Hali hiyo inaibua swali kuhusu utayari na kasi ya nchi wanachama katika kukamilisha taratibu za kisheria zinazohitajika ili mifumo ya kikanda iweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Wananchi walioathirika washirikishwe katika maamuzi
Pamoja na umuhimu wa mifumo imara ya kisiasa na taasisi za kikanda, washiriki wa mkutano huo wameeleza kuwa juhudi za kutafuta amani haziwezi kuwa na mafanikio ya kudumu bila kuwashirikisha wananchi wanaoathiriwa moja kwa moja na migogoro.
Vianney Bisimwa kutoka taasisi ya Centre for Civilians in Conflict amesema wananchi hao wanapaswa kupewa nafasi ya kueleza madhara waliyopata, hasara walizopata na matarajio yao kuhusu mustakabali wa jamii zao.
Amesema michakato ya amani haipaswi kuendeshwa na viongozi na wapatanishi pekee, bali inapaswa kuwapa nafasi pia wananchi ambao wamebeba madhara ya migogoro.
“Lakini jambo la muhimu zaidi katika mchakato wa amani ni kwamba lazima ujumuishe jamii ili ziweze kuleta mateso yao wenyewe mezani, ziweze kujadili jinsi zilivyoathirika, kile walichoweza kupoteza, na jinsi wanavyotazama siku zijazo,” amesema Bisimwa.
Kwa mujibu wake, juhudi za kukomesha migogoro zinapaswa kwenda sambamba na kuboresha maisha ya jamii zilizoathirika, ikiwemo kuhakikisha zinapata msaada unaohitajika ili kurejesha hali ya kawaida.
Hoja hii inaonesha kuwa amani haiwezi kupimwa kwa kusitishwa kwa mapigano pekee, bali pia kwa uwezo wa jamii zilizoathirika kurejesha maisha yao na kushiriki katika kujenga mustakabali wao.
Ushirikishwaji wa wananchi katika michakato ya amani unahusisha pia kuhakikisha makundi ambayo mara nyingi hukosa nafasi katika maamuzi yanapata uwakilishi wa kutosha. Miongoni mwa makundi hayo ni wanawake na vijana.
Balozi wa Finland nchini Tanzania, Anna Merrifield, amesisitiza kuwa amani haiwezi kuwa ya kudumu ikiwa wanawake na vijana hawatashirikishwa katika maamuzi yanayohusu maisha na mustakabali wao.
“Najua kwamba amani si amani ya kudumu ikiwa hatuna wanawake mezani, ikiwa hatuna vijana mezani tukiwa tunazungumza kuhusu mustakabali wao,” amesema Merrifield.
Kwa upande wake, Jackline Msabila, Mkurugenzi wa taasisi ya Sustainable Africa Digital Transformation Initiative (SADTI), amesema mifumo iliyopo bado haijawa rafiki kwa vijana kushiriki kikamilifu katika michakato ya maamuzi.
SOMA ZAIDI: Uhasama Kati Ya Mataifa Ya Afrika Mashariki Unaipeleka Wapi Jumuiya Hiyo?
Akitumia Tanzania kama mfano, amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo inayowapa vijana nafasi halisi ya kutoa maoni na kushiriki katika maamuzi yanayowahusu, badala ya ushiriki wao kubaki katika kauli na ahadi.
“Kuna mifumo ambayo kwa hakika si rafiki kwa vijana ili waweze kushiriki,” amesema Msabila.
Amani ya kudumu inahitaji hatua zaidi ya mazungumzo
Kwa ujumla, hoja zilizojitokeza katika mkutano huo zinaonesha kuwa changamoto ya kupata amani ya kudumu barani Afrika haiwezi kutatuliwa kwa mikutano ya upatanishi na makubaliano ya kisiasa pekee.
Inahitaji kushughulikia visababishi vya migogoro kabla havijazaa vurugu, kuhakikisha rasilimali za asili zinasimamiwa kwa uwazi, kuimarisha mifumo ya uongozi na taasisi za kikanda, pamoja na kuweka mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema.
Vilevile, michakato ya amani inapaswa kuwapa nafasi wananchi walioathirika, wanawake na vijana kushiriki katika maamuzi kuhusu mustakabali wao.
Holyness Mbise ni mwandishi mwandamizi wa habari wa The Chanzo, aliyepo mkoani Dar es Salaam. Anaweza kupatikana kupitia mbiseholyness02@gmail.com.