Mpendwa mzazi, ili uweze kuwalea watoto wako vizuri, inakubidi pia ujitunze wewe mwenyewe kwa kuilinda afya yako, ya mwili na ile ya akili. Leo tutaongelea zaidi namna gani unaweza kuilinda afya yako ya akili.
Kwanza kabisa, tambua vitu vinavyokutatiza, au kukupa msongo wa mawazo. Fanya uhakiki binafsi kwa kujitafakari wewe mwenyewe, kisha viorodheshe vitu hivyo ili uweze kuvishughulikia kwa ufanisi.
Kama kuna mambo, au majukumu, ambayo si ya lazima na yanachangia kukupa msongo wa mawazo, basi jaribu kuvipunguza, au kuviondoa. Pia, chunguza hisia zako, tambua ni hisia gani unazopitia na chanzo chake ni nini.
Ikiwa unahisi msongo wa mawazo ni mzito sana, unaweza kuzungumza na mtaalamu wa masuala ya afya ya akili, au mshauri. Watu hawa wanaweza kukupa mwongozo na mbinu za kukusaidia kushughulikia hisia zako.
SOMA ZAIDI: Vitu Muhimu vya Kufanya Kwa Ajili ya Mtoto Wako Akiwa Shuleni
Kitaalamu, kila binadamu anapaswa kupata muda wa kupumzika wa kutosha walau masaa saba au nane ya kulala kwa siku. Unaweza pia kupumzika kwa kufanya shughuli zinazokupa furaha kama vile kusoma kitabu, kusikiliza muziki, kuangalia filamu, kutembea nje, nakadhalika.
Mazoezi ya mara kwa mara pia huimarisha afya ya akili kwa kiwango kikubwa. Mazoezi huchangia katika uzalishaji wa endorphins, au homoni ya furaha. Unaweza kufanya mazoezi kwa kutembea, kukimbia, kucheza mpira au muziki, yaani zoezi lolote ambalo litachangamsha mwili.
Ni kweli tunapitia changamoto nyingi kila siku na ni rahisi kupata msongo wa mawazo, au sonona na magonjwa mengine ya afya ya akili. Hivyo, ni muhimu mno kuwa na mtazamo chanya wa maisha.
Kuwa na mtazamo chanya wa maisha kutaathiri mawazo yako na kukusaidia kuyapa kipaumbelea yale mambo mazuri yaliyopo katika maisha yako kuliko yale mabaya na kujifunza kupitia changamoto za maisha kwa ujasiri.
SOMA ZAIDI: Maarifa 6 ya Jamii Ambayo Mtoto Anaweza Kujifunza Wakati Huu wa Likizo
Ukiwa nyumbani, jitahidi kupata muda wa kucheza na watoto wako, hii ni njia nzuri ya kuimarisha afya yako ya akili na kujenga uhusiano mzuri kati yako na watoto. Hakikisha unapata muda wa kucheza na kuwa na mazungumzo nao.
Vivyo hivyo, tenga na thamini muda wa familia. Muda huo haupaswi kuwa na vikwazo vya kazi au majukumu mengine. Muda huo ni wa kufanya shughuli za pamoja kama familia: kula chakula cha jioni pamoja, kuwa na matembezi ya jioni, kusoma vitabu pamoja, nakadhalika.
Jitahidi kupata muda peke yako au na mwenza wako bila watoto. Kuna muda unahitaji kuwa peke yako. Huu mda ni muhimu kwa kila binadamu. Unaweza kuutumia ukiwa mwenyewe au na mwenza au mzazi mwenzako kutafakari maisha na kuyafurahia pia.
Usijitenge, wasiliana na watu wako wa karibu mara kwa mara. Kuwa na mahusiano mema na familia, marafiki, pamoja na jamii inayokuzunguka ni muhimu kwa afya yako ya akili maana hao ndiyo msaada wako wa kwanza. Kumbuka, kilio huanza na mfiwa!
SOMA ZAIDI: Msimu Huu wa Sikukuu, Tukumbashane Umuhimu wa Kuimarisha Ulinzi wa Watoto
Afya yako ya akili inahitaji kupewa kipaumbele sawa na afya yako ya mwili. Huwezi kuendesha gari kama gari lenyewe halina mafuta, hivyo huwezi ukaendesha familia yako kama inavyopaswa kama afya yako imedhoofika.
Jipende, jihudumie, ili uweze kuwapenda na kuwahudumia watoto na familia yako kwa ujumla.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.